Waokoaji wanaendelea na shughuli ya kuwasaka mamia ya wahamiaji waliotumbukia baharini baada ya boti walimokuwa wakisafiria kwenda Ulaya kuzama majini katika bahari ya Mediterrania karibu na ufuo wa Libya.
Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa takriban watu 700 walikuwa kwenye mtumbwi huo uliozama baada ya kukumbana na mawimbi makali.
Wanajeshi wa majini kutoka Ireland wanakisia kuwa idadi kubwa ya watu wamekufa maji.
Aidha shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka Medecins Sans Frontieres (MSF) limeonya kuwa huenda kukazuka maafa makubwa kufuatia idadi kubwa ya abiria waliokuwa kwenye mtumbwi huo uliozama.
Inakisiwa kuwa takriban wahamiaji 2,000 walikufa maji kwanza mwanza wa mwaka huu wakijaribu kufika ulaya kupitia bahari hiyo ya Mediterranea
Meli nne za uokozi na ndege tatu zimetumwa huko kujaribu kunusuru maisha ya wahamiaji hao.
Walinzi wa Ufuo wa bahari ya Uitaliano wamesema boti hiyo ya uvuvi iliyokuwa imebeba mamia ya wahamiaji.
Inavyoelekea boti hiyo ilikumbwa na dharuba lakini pia ilipenduka pale watu walipokurupuka upande mmoja walipoona chombo kingine kilichokuwa kikienda kuwasaidia.
Zaidi ya watu 150 wameokolewa lakini wengine wengi wanahofiwa wamekufa maji.
Msemaji wa shirika linalohusika na maswala ya wahamiaji IOM, Leonard Doyle ameiambia BBC kuwa
''Lazima tukumbuke kuwa hawa ni watu ambao hawajazoea usafiri wa baharini kwahivyo waliogopa.''
''Na wakati walipoona chombo kingine kinakuja kuwaokoa wakataharuki na kukurupuka upande mmoja''.
Hilo ndilo tunalokariri kuwa hao walanguzi wa kusafirisha watu hawajali kabisa kuhusu maisha ya wahamiaji hao licha ya kuwa wamewalipa pesa nyingi kwa safari hizo hatari''.
Kwamba mkasa wa aina hii unaweza kutokea wakati ambao hata watu wamepelekewa chombo cha kuwaokoa karibu yao ni jambo la kusikitisha sana.
No comments:
Post a Comment