Lindi. Hali katika Jimbo la
Mtama si shwari baada ya kundi la wananchi kufanya maandamano ya kukataa
matokeo ya kura za maoni yaliyompa ushindi Katibu wa Itikadi na Uenezi
wa CCM, Nape Nnauye huku wakimtaka mpinzani wake achukue uamuzi mgumu.
Katika kura za maoni, Nape alipata kura 9,344 wakati Suleiman Mathew alipata kura 4,766.
Wakiwa
wamebeba mabango yaliyoandikwa ujumbe wa aina mbalimbali kumpinga Nape
na kuonyesha kumkubali Seleman Mathew, ambaye wanaamini ndiye
aliyeshinda, wananchi hao walimtaka mgombea huyo atangaze kujiengua CCM,
kama makada wengine waliochomoka chama hicho kupinga matokeo ya kura za
maoni.
“Karibu Mathew, sisi hatuchaguliwi
kiongozi, tuna imani na Messi wetu,” liliandikwa bango moja la karatasi
la boksi baada ya wananchi hao kumpokea Mathew na baadaye kumsindikiza
kutoka Mnazi Mmoja hadi kijiji cha Mtama, Kata ya Majengo ambako
kulikuwa na watu wamekusanyika kwenye uwanja ulio karibu na ofisi za
mbunge.
Akizungumza katika eneo la Mnazi Mmoja ambako
alipokelewa na wananchi hao waliomtaka ahamie chama chochote cha
upinzani, Mathew, ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa Yanga na timu ya
Taifa, alisema kuwa amesikia wito wa wazee wa jimbo hilo pamoja na
wananchi wengine waliomuita kutoka Dar es Salaam na kumshawishi ahame
chama.
Mathew alidai kuwa kulikuwa na mchezo mchafu
katika kura za maoni na kwamba uongozi wa CCM wa wilaya hiyo ulishiriki
kumuhujumu, akisema katibu wa wilaya hakutangaza matokeo halisi, jambo
ambalo alisema linawakosesha amani wananchi wa Mtama.
Wakati
Mathew akidai kuibiwa kura, katibu wa Wilaya ya Lindi Vijijini,
Christina Bukwi alisema uchaguzi ulifanyika na kumalizika salama kisha
kutangaza matokeo mbele ya mkutano wa waandishi wa habari na wanachama
wote.
Alisema wagombea wengine walioshindwa kwenye uchaguzi huo walikubali na kusaini fomu, isipokuwa Mathew aliyeamua kukataa.
“Kama
alikuwa na malalamiko angekuja ofisini, lakini mpaka sasa sijapokea
taarifa zake ofisini na kila mgombea alikuwa na wakala wake kwa ajili ya
kulinda kura za wagombea wao, kwa hivyo mimi sitambui hayo malalamiko
yake,” alisema Christina.
Lakini Mathew alisema
ameshauriwa kutochukua hatua yoyote hadi vikao vya juu vya chama
vitakapomaliza uchambuzi wa mwisho wa wagombea ubunge na udiwani, huku
akieleza kuwa ana ushahidi kuwa ameporwa haki yake.
Kuhusu
taarifa kwamba alifuatwa kushawishiwa awe na subira, Mathew alidai kuwa
alifuatwa na viongozi wa Serikali, akiwamo mkuu wa mkoa na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, aliyemtaka kuwa mvumilivu mpaka Kamati Kuu itakapotoa
matokeo.
“Ni kweli waliniita nikazungumza nao kwa
sababu hawa ni viongozi wetu na walitambua Mtama kuna tatizo. Nilipoitwa
kuonana na Waziri Mkuu, kubwa nililoambiwa ni kuwa mstahimilivu hadi
Kamati Kuu itakapotangaza matokeo ndiyo maana nimekuja hapa kwa sababu
lengo letu ni moja tusubiri hiyo tarahe,” alisema Mathew.
Akizungumzia
sakata hilo, Nape alisema: “Mimi sizungumzii mambo ya mtu anayepiga
kelele barabarani. Halafu ninyi Mwananchi mbona mnapenda kukuza mambo.
Ni kwa nini niliposhinda kwa kishindo hamkuandika leo mnataka mambo
hayo?”
No comments:
Post a Comment