Chadema yamng’ang’ania Kawambwa
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akiongoza maandamano
WAKATI Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameunda tume kuchunguza matokeo mabaya ya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012, Chadema kimesisitiza msimamo wake kwamba kitafanya maandamano kushinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo wajiuzulu.
Mapema wiki iliyopita Pinda alitangaza kuunda tume kuchunguza matokeo hayo, hatua ambayo Rais Jakaya Kikwete alitangaza kuiunga mkono katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi aliyoitoa juzi.
Lakini jana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema watafanya maandamano makubwa aliyoyaita ya kihistoria, katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya na Dar es Salaam ili kushinikiza kutekelezwa kwa hatua hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Mtatatila, Sumbawanga mkoani Rukwa, Mbowe alisema: “Lengo la maandamano ni kuwataka waziri wa elimu na naibu wake wajiuzulu kwani wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kusababisha watoto wa maskini kufanya vibaya kwenye mitihani yao.”
Alisema maandamano hayo yatahusisha wafanyakazi wa Serikali, mama lishe na wafanyabiashara wa usafirishaji wanafunzi wa shule za msingi na sekondari... “Siku hiyo hakutakuwa na masomo wala kazi, kila kitu kitasitishwa.”
Mbowe alisema maandamano hayo yatakuwa ya kihistoria na kwamba Chadema kinataka kuwafungua macho wananchi walio na kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kusomesha watoto wao nje ya nchi ili washinikize Dk Kawambwa na Mulugo waachie ngazi.
“Tunataka shule za sekondari na msingi zisigeuzwe kuwa vituo vya kulelea watoto, bali vifanye kazi za kutoa elimu, kama ilivyokusudiwa,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe aliwataka wananchi kuwa makini na uchochezi unaofanywa na baadhi ya vyama vya siasa, badala yake waangalie chama chenye sera, mtazamo na harakati za kuleta mabadiliko yatakayokuwa na manufaa kwa Watanzania wote.
“Njia sahihi ni kuhakikisha mnajiondoa, kwani ili muweze kujua mustakabali wa maisha yenu ni lazima mhakikishe mnakuwa makini kufanya uamuzi ulio sahihi kwa viongozi mnaowataka, ”alisema Mbowe.
Hii ni mara ya pili katika mwaka huu kwa Chadema kutaka viongozi wajiuzulu. Mwezi uliopita, chama hicho kilimtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai wajiuzulu kwa maelezo kuwa wamekuwa wakiminya demokrasia, kuubana upinzani na kupendelea chama tawala (CCM) bungeni.
Wanaume milioni 3 kuvuliwa ‘soksi za asili’
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Dr Hussein Mwinyi.
SERIKALI imejiwekea lengo la kutahiri wanaume milioni 2.8 ifikapo mwaka 2015, baada ya kufanikiwa kuwatahiri 287,055 kati ya mwaka 2010 na 2012.
Hayo yamebainishwa katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ikifafanua kuwa huduma ya tohara ya kitabibu kwa wanaume ilianzishwa mwaka 2010.
Imetekelezwa zaidi mikoa ambayo ilibainika kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
“Iligundulika kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU ambako kuna kiwango cha chini cha tohara kwa wanaume. Mikoa hiyo ni ya Iringa, Njombe, Simiyu, Geita, Katavi, Mbeya, Rukwa, Tabora, Kagera, Mwanza na Mara,” inaelezwa taarifa hiyo.
Inaelezwa kuwa Serikali ilifanikiwa kuwafanyia tohara wanaume hao kwa kutumia njia ya kuwaelimisha kwa kuwaelezea umuhimu wa tohara na hatari inayowakabili kwa kuendelea kuishi bila kufanyiwa tohara hasa kuambukizwa magonjwa ya zinaa ikiwamo VVU.
Pia, taarifa hiyo inaeleza kuhusu mpango wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa mwaka 2005, wajawazito 11,435 ambayo ni asilimia tisa ya wenye maambukizi ya virusi.
Inasema walipatiwa dawa za ARVs kuzuia maambukizi hayo kwenda kwa mtoto.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, wizara hiyo inaendelea kutoa kupaumbele maeneo ya kudhibiti magonjwa ya ngono, utoaji ushauri nasaha na huduma kwa wagonjwa wa nyumbani, elimu na habari, tiba na matunzo, huduma ya maabara kwa wagonjwa waishio na VVU.
“Hamasa kwa Watanzania imekuwa ikiongezeka hasa baada ya kampeni iliyoongozwa na Rais (Jakaya Kikwete) mwaka 2007, idadi ya vituo vya upimaji iliongezeka kutoka vituo 521 mwaka 2005 hadi 2,200 mwaka jana,” inasema taarifa hiyo na kuongeza:
“Iidadi ya wananchi waliopatiwa huduma hiyo nayo imeongezeka kutoka watu 365,189 mwaka 2005 hadi watu 17,008,475 Machi mwaka jana.” ( R & Ed)
Kondomu feki zaanza kuleta madhara Uingereza
WAKATI kondomu feki zilizopigwa marufuku Uingereza mwaka jana zikiwa katika mzunguko nchini Tanzania, kesi za gonjwa la ngono hatari lisilotibika zimeongezeka kwa asilimia 25 Uingereza, huku wataalamu wakionya kwamba ugonjwa huo umekuwa sugu zaidi katika tiba.
Zaidi ya kesi 21, 000 za maambukizi mapya zimedaiwa kutambulika kwa mwaka 2011/12.
Kondomu hizo feki aina ya Trojan na Durex zenye vipele vipele ambazo mwishoni mwa mwaka jana serikali ya Uingereza iliingia katika msako mkali kusaka mamilioni ya kondomu hizo bandia zilizokuwa zikiuzwa nchini humo miezi 18 iliyopita.
Kirusi kinachoambukiza ugonjwa huo hatari kimetajwa kuwa ni 'Neisseria' ambacho ni tofauti na vingine ambavyo mara nyingi hutibiwa kwa dozi moja tu ya viuavijasumu (antibiotics) ambayo angalau hufanya kazi kwa asilimia 95 kiufanisi.
Akizungumzia maendeleo ya utafiti wa kondomu hizo nchini , Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Wiwango Tanzania(TBS),Leandri Kinabo alisema shirika hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Ckula na Dawa(TFDA) hivi sasa lipo katika mchakato wa kuhakikisha vipimo halisi vya ubora wa bidhaa hizo vinaangaliwa.
"Hili suala ni nyeti na ni la kiafya na usalama zaidi, hivyo tulikaa kikao na TFDA na tulikubaliana tufanye uchunguzi wa kondom hizi, kwani ni kweli zipo sokoni lakini suala la ubora linatakiwa kuangaliwa," alisema Kinabo.
Aliwataka Watanzania kuwa na subira ili waweze kuchunguza bidhaa hizo kwa umakini zaidi na kwamba baada ya uchunguzi watatoa majibu.
Baada ya gazeti hili kutaka kujua uhalali wa bidhaa hizo sokoni, Kinabo alisema bidhaa zote zinazoingia bandarini hupimwa, lakini kuna baadhi ya bidhaa ambazo huingizwa kwa njia zisizo halali na mara nyingi huwa feki.
"Inetegemea na lebo ya bidhaa husika, kuna wakati bidhaa inaweza kupimwa na kuonekana kuwa ni salama na kisha kuingizwa sokoni, lakini baada ya muda zikaingia bidhaa feki zenye nembo hiyohiyo, hivyo hilo ni suala la kusubiri vipimo kutoka TFDA," alisema Kinabo.
Tatizo hilo sugu Uingereza limesababishwa kuanzishwa kwa kampeni mpya ya kukabiliana na tishio kubwa la kuongezeka kwa kasi kwa magonjwa hayo nchini Uingereza na Wales ambayo yamedaiwa kusambaa kwa wingi nchini humo na nchi zinazoendelea.
Wataalamu wa Afya wana matumaini mapya baada ya kuanzishwa mpango mkakati wa kuzuia ugonjwa wa gono 'Gonorrhoea Resistance Action Plan' ambayo itaongeza ufahamu wa ugonjwa huo.
Mpango huo ulioanzishwa na shirika la Ulinzi wa Afya, utafuatilia tatizo hilo la kimataifa linaloongezeka kwa kasi tangu kupungua miaka 10 iliyopita.
Tatizo hili limeanza kukua kwa kasi mwaka 2011, wagonjwa wengi waliojitokeza wameugua zaidi ya mara tatu magonjwa ya ngono. Zaidi ya theluthi ya kesi hizi ni za wanaume waliokuwa wakifanya mapenzi na wanaume wenzao, kutoka karibu ya robo kwa mwaka 2010.
Profesa Cathy Ison kiongozi wa kampeni hiyo anasema "idadi kubwa ya watu waliougua magonjwa haya wanatamka kuwa walipata kutumia kondom ambazo hata hivyo baadaye zilitambulika kuwa ni feki na kuzuiwa hapa nchini Uingereza.
"Bado hatuwezi kuwahakikishia watu kuwa tunatarajia kupata suluhu ya gono hili hatari, hili bado ni tatizo kubwa kwa afya ya umma na ni kwamba sasa limeanza kusambaa hata nchi zinazoendelea," anasema Ison.
Nchini Uingereza na Wales, kuna hatari kubwa ya kuendelea kwa maambukizi haya ambayo hata hivyo yameonekana kukua kwa kasi kubwa licha ya wagonjwa wengi kudai kuwa hutumia mipira katika tendo la kujamiiana.
Ingawaje kesi za kushindwa kutibu gono hilo zimekuwa ni taarifa za kimataifa, Afisa Mganga Mkuu Uingereza, Profesa Sally Davies, hivi karibuni aliishauri serikali kuongeza nguvu katika dawa za Antibiotics kwa ajili ya dharura kwa wagonjwa watakaopatikana na gonjwa hilo.
Prof esa Davies anasema "tumeona na kuwa na wasiwasi mkubwa katika kesi za dawa sugu za magonjwa ya zinaa kwa muongo uliopita, lakini kuna haja ya kutengeneza dawa hizo kwa ajili ya tatizo hili, labda tutafanikiwa, lakini kazi ya ulinzi wa shirika la afya ni muhimu katika kutafuta suluhu ya tatizo hili" anasema.
Mdhibiti wa dawa na bidhaa za afya nchini humo, alidai kwamba mamilioni ya kondom hizo feki ziliingia nchini humo zikitokea Mashariki ya Mbali na kwamba zimeshatumiwa na watu wengi tangu kuingizwa nchini humo.
Kondom hizo zilidaiwa kutengenezwa kwa vifaa rahisi visivyo na ubora ambavyo vinaweza kuongeza hatari kwa watumiaji kwa kusambaza kwa kasi magonjwa ya zinaa, au kusababisha mimba zisizohitajika, pamoja na kuharibu mikakati ya uzazi wa mpango.(Herrieth Makwetta)
21 mbaroni kwa ujambazi Dar
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Charles Kenyela
Mtuhumiwa wa ujambazi, Omary Said (37), ameuawa kwa
kipigo kutoka kwa wananchi wakati akiwa kwenye tukio la kijambazi na
wengine 21 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, kwa
tuhuma za ujambazi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Charles Kenyela, alisema marehemu, mkazi
wa Tabata Aroma, aliuawa baada yeye na wenzake kumvamia, Abdulrahaman
Mohamed, maeneo ya Mlimani City na kumpora fedha taslimu Sh. milioni 14
alizokuwa amezibeba kwenye mfujo wa rhambo.
Kamanda Kenyela watuhumiwa wengine kumi waliokamatwa kwa
kutumia silaha katika maeneo ya Kawe, Kilima hewa, Boko Yombo Dovya, Tegeta, Mbezi Beach, Kunduki Mtongani na Ununio.
Aliwataja kuwa ni Alex Msale (27), Godfrey Msale (30), Harod Francis
(26), Athuman Athuman (21), Isaya Songo (32), Magret John (30), Emanuel
Thomas (28), Rukia Mohamed(26), Hamisa Mahamood (28) na Kelvin Mwehombe
(24).
Walikamatwa wakiwa na bastola aina ya Browning yenye namba A 558656
iliyokuwa na risasi moja na Aina ya Astra yenye namba 1273826 iliyokuwa
na risasi saba kwenye magazine.
CAG agundua madudu Tanesco
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema uchunguzi alioufanya dhidi ya vigogo watatu wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), unaonyesha kuwa kuna madudu ya kutisha.
Utouh alisema hivi karibuni kuwa alijikita
zaidi katika mikataba yenye thamani ya zaidi ya Sh500 milioni
iliyoingiwa na shirika hilo.
Awali, Ofisi ya CAG ilitoa ripoti ambayo
ilisababisha aliyekuwa Mkurugenzi wa Tanesco, William Mhando
kusimamishwa na baadaye kufukuzwa.
Vigogo wengine waliotajwa katika ripoti hiyo,
Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja
Mwandamizi Ununuzi, Harun Mattambo walisimamishwa kazi ili kupisha
uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kuingia mikataba
mibovu wakati wa ununuzi wa mali za shirika.
Utouh alisema ripoti hiyo imejaa madudu, jambo ambalo lilisababisha kutumia nguvu kubwa wakati wa ukusanyaji wa taarifa zake.
Alisema baada ya kugundua madudu hayo,
walilazimika kuzunguka kwenye ofisi za shirika hilo zilizoko mikoani ili
waweze kuhoji baadhi ya wafanyakazi na kukagua mikataba hiyo.
Alisema
kutokana na hali hiyo, walitumia nguvu kubwa wakati wa ukusanyaji wa
taarifa zake, jambo ambao lilisababisha kuchukua muda wa miezi mitatu
ili kukamilisha.
“Tumefanya kazi kubwa sana katika ripoti hii
ya awamu ya pili. Hii inatokana na kutakiwa kukagua mikataba iliyoingiwa
na Tanesco ya miradi mikubwa, jambo ambalo lilisababisha kwenda hadi
kwenye ofisi za mikoa ili kuhoji na kuchunguza mikataba hiyo,” alisema
Utouh.
Alisema baada ya kubaini madudu hayo walitoa
mapendekezo yao ambayo Serikali inapaswa kuyafanyia kazi ili waweze
kutenda haki pindi wanapotoa uamuzi kuhusu tuhuma zinazowakabili
viongozi hao.
Alisema kutokana na hali hiyo wamekabidhi ripoti hiyo tangu Januari mwaka huu kwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jenerali Robert Mboma ili aipitie na kuiwasilisha kwenye mamlaka nyingine husika.
Mboma alikiri kupokea ripoti hiyo na kudai kuwa wanaanza kuwahoji watuhumiwa hao wiki jayo.
Subscribe to:
Posts (Atom)