JK: Acheni urafiki wa dhambi na wachimbaji wakubwa

Rais Jakaya Kikwete 


Rais Jakaya Kikwete ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuacha urafiki wa dhambi na baadhi ya wachimbaji wakubwa wanaohodhi maeneo makubwa na badala yake wazingatie sheria ili kutoa haki kwa wachimbaji wadogo.

Akizungumza katika siku yake ya mwisho kutembelea Mgodi wa Dhahabu wa Baraka uliopo wilayani Geita katika Kijiji cha Nyaruyeye juzi, Rais Kikwete alisema kilio cha wachimbaji wadogo hivi sasa ni maeneo lakini wanaweza kuchimba sawa na wachimbaji wakubwa hivyo kuitaka wizara hiyo kuzingatia sheria kwa kuwafutia umiliki wenye maeneo ambayo hawayafanyii kazi.

“Mkiyatwaa watapiga kelele, acheni wapige kelele lakini timizeni sheria. Masele (akimwangalia Naibu Waziri Nishati na Madini Stephen Masele) na wenzako lazima mzingatie sheria. Wanyang’anyeni maeneo haya wapeni wachimbaji wadogo wachimbe. Acheni kufanya urafiki wa dhambi na hawa,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete ambaye alieleza kufurahishwa kwake na wachimbaji wadogo kuanza kuchimba kisasa alisema sheria ya umilikaji wa maeneo ya utafiti na uchimbaji wa madini inaelekeza kuwa iwapo mwombaji akija kuomba tena (renewal) leseni ya eneo alilopewa anapaswa kulipunguza kwa asilimia 50 ili wapewe wengine na vivyohivyo anapokuja kwa mara ya pili, pia anapaswa kupunguziwa eneo lake kwa asilimia 50.

“Pamoja na kwamba sheria ipo wazi, ukiwauliza wizara kwa nini hawafanyi hivyo, hawana maelezo wapo kimya, sijui wanaingia kigugumizi gani kutimiza sheria hii. Wanaposhindwa kufanya haya ni hasara kwa taifa maana haya madini hayachimbwi, wangezingatia sheria hii na kuchukua maeneo haya wangewapa wengine wakachimba leo tusingekuwa na kelele za wachimbaji wadogo,” alisema. Rais Kikwete alisema madini yakiwa chini hayana thamani yoyote mpaka yanapochimbwa na kubainisha kwamba iwapo watu waliopewa leseni watazishikilia bila ya kuendeleza maeneo yao, watakwamisha ajira na maendeleo kwa nchi.

Aidha, aliitaka wizara hiyo kuwa makini wakati wa kutimiza matakwa ya sheria hiyo ya umiliki wa maeneo ya uchimbaji, akitahadharisha kuwa wamiliki wengine wanaweza kubadili majina pindi watakaponyang’anywa maeneo yao.

“Wana tabia ya kubadili majina, mkimnyang’anya atakuja upya. Kama alikuwa anaitwa Kikwete & Sons sasa atakuja tena anajiita SK lakini ndiye huyohuyo, tazameni sana. Najua, mnayajua mengi maana na ninyi ni wabia wao lakini ninachotaka ni kuzingatia na kusimamia sheria,” alisema.

Akizungumzia Mgodi wa Mzawa alioutembelea, Rais Kikwete alisema amejionea jambo kubwa na la kushangaza kiasi cha kusema kwamba iwapo angeishia kusimuliwa mambo hayo na watu bila ya kufika, asingeamini kama Watanzania wanaweza kuendesha migodi kama huo.

Alisema Serikali inathamini mchango wao na kuwataka kujiandikisha Tume ya Uwekezaji ili nao waweze kuomba msamaha wa mafuta na zana mbalimbali kama ilivyo kwa wawekezaji wakubwa wa nje.

Awali, Masele alimwomba Rais kuangalia uwezekano wa kuwapatia wachimbaji wadogo msamaha wa kodi akisema vifaa wanavyotumia havina tofauti na vile vya wachimbaji wakubwa.

Kilichomuua Dk Mvungi

Dk Sengondo Mvungi


Hospitali ya Millpark ya Johannesburg, Afrika Kusini, imesema madaktari waliokuwa wakimtibu aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi walibaini kuharibika kwa ubongo wake kutokana na kumwagika kwa maji yanayoutunza ambayo kitaalamu yanaitwa ‘cerebrospinal fluids’ au CCF.

Msemaji wa Hospitali hiyo, Tebogo Nyembezi alisema Dk Mvungi alicheleweshewa tiba baada ya kupata tatizo la maji hayo yanayotunza ubongo kumwagika mara baada ya kujeruhiwa.

Dk Mvungi (61), alipata majeraha makubwa baada ya kujeruhiwa na watu waliovamia nyumbani kwake Kibamba, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu. Alifariki dunia jana mchana.

“Maji hayo ambayo ni miligramu 50 tu katika ubongo wa mwanadamu ambayo huufanya ubongo uelee yakimwagika nusu tu, basi mgonjwa yupo hatarini, lakini akiwahishwa na kupata tiba sahihi anaweza kupona,” alisema Nyembezi.

Alisema iwapo mgonjwa atapewa tiba sahihi ndani ya saa 48, ubongo wake unaweza kurudi katika hali ya kawaida, lakini saa hizo zikizidi hawezi kupona kabisa kwa sababu maji hayo yanapomwagika ubongo hujigonga kwenye mifupa ya sakafu yake na kuharibika kabisa.

Mtaalamu wa mishipa na neva za fahamu (neurosurgeon) katika Hospitali ya Regency, Dar es Salaam, Dk Hariff Najin alisema kazi kubwa ya maji hayo ni kuulinda ubongo pindi inapotokea ajali ili usidhurike lakini endapo maji hayo yatamwagika nao huharibika.

“Haya maji yanaufanya ubongo uelee na usielemee kichwa. Hivyo inapotokea maji haya yakaisha au kupungua, ubongo hujigonga na kukosa ukinzani na kuharibika,” alisema.

Alisema maji hayo ambayo hufika hadi kwenye uti wa mgongo yakikosekana katika ubongo, husababisha damu isitembee kwenye eneo hilo jambo ambalo pia linaweza kusababisha mishipa katika sehemu ya nyuma ya ubongo kuharibiwa.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu Muhimbili (Moi), Profesa Lawrence Museru alisema anachofahamu ni kuwa Dk Mvungi alipelekwa Afrika Kusini kwa kuwa alipata madhara makubwa kwenye ubongo na wala si kwa sababu ya kumwagika kwa maji kama ilivyoelezwa Afrika Kusini.

“Majeraha hayo yalisababisha damu kuvilia katika ubongo na kusababisha uvimbe ambao kwa kitaalamu unaitwa ‘traumatic brain injury’ na sisi tulithibitisha vipimo hivyo vya awali na kumsindikiza mpaka huko,” alisema Profesa Maseru.

Profesa Museru alisema Dk Mvungi alipata majeraha makubwa kichwani na sehemu nyingine mwilini ambayo yanaonekana yalisababishwa na kupigwa kwa vitu vyenye ncha kali au magongo na hivyo kuleta madhara katika ubongo.

Alisema hawezi kuthibitisha chanzo hasa cha kifo hicho kwani kinaweza kuwa ni kuharibika kwa ubongo au sababu nyingine zilizotokana na tatizo hilo (secondary causes).

Sekondari ya William Lukuvi wanafunzi walala darasani

Mmoja wa wanafunzi akiwa juu ya godoro hivi karibuni. Picha na Said Ng’amilo 


Wiki iliyopita nilikwenda Morogoro ambako pamoja na mambo mengine nilikuwa na kipindi kwenye televisheni moja mkoani humo, kilicholenga kutoa ushauri kwa jamii kuhusu namna ya kupambana na changamoto za maisha. Baadaye nilikutana na watu waliokuja kwenye hoteli niliyokuwepo kwa lengo la kubadilishana mawazo zaidi kuhusiana na yale ambayo niliyaeleza kwenye televisheni. Mmoja wa watu alikuwa ni Erick Mtengele, kijana wa Kimasai ambaye amekuwa akihangaika huku na kule kutafuta namna ya kuwasaidia wafugaji nchini.

 “Mimi ni kati ya Wamasai wachache nchini walio na elimu ya chuo kikuu, nimehitimu elimu ya maendeleo ya jamii katika Chuo Kikuu cha Tumaini mwaka 2010, kwa bahati mbaya hadi leo sina ajira,” anasema Mtengele ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Luganga, Kata ya Ilala Mpya, mkoani Iringa.

Tulizungumza mengi, yakiwemo matatizo ya sekta ya elimu nchini na harakati zake za kuwasaidia wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya William Lukuvi wapate angalau bweni, akisema kuwa ameandika barua maeneo kadhaa kuomba shule hiyo ijengewe bweni bila mafanikio.

“Shule haina mabweni, wanafunzi wanalala kwenye madarasa,” anasema Mtengele.

Baada ya mazungumzo hayo nililazimika kufuatilia ili kujua ukweli, nilibaini kuwa ni ukweli thabiti kwamba wapo wanafunzi wanalala kwenye madarasa katika shule hiyo, sababu kubwa ni kwamba shule haina uwezo wa kifedha wa kujenga mabweni.

“Huogopi kufuatilia shule hii?” anaonya mwandishi mmoja wa habari anayefanyia kazi mkoani Iringa kwa maelezo kuwa kufuatilia shule hiyo kunaweza kuzusha kutokuelewana na baadhi ya watu ambao kwa namna moja ama nyingine wanahusika na shule hiyo.

Mwandishi huyo anaonya kuwa hofu ya kufanyiwa mabaya ndiyo sababu waandishi walio wengi wanaogopa kuandika ukweli kuhusiana na shule hiyo kwamba baadhi ya wanafunzi wanalala katika madarasa tofauti katika shule hiyo.

“Kuna  waandishi waliwahi kufuatilia suala hili na kuhoji kwa nini mabweni hayajengwi, matokeo yake siyo tu kwamba hawakupewa ushirikiano na wale ambao wanahusika kutolea maelezo jambo hilo, bali walionekana kama wanaingilia mambo yasiyowahusu, wengine hata wakajikuta katika hofu kuhusu maisha yao,” alionya mwandishi huyo.

Hata hivyo niliendelea kufuatilia kutokana na ukweli kwamba lengo la makala hii siyo kudhalilisha yeyote, bali kueleza ukweli ili kuangalia namna gani wanafunzi wanaweza kusaidiwa kwa kujengewa mabweni.

Kama yupo mwenye nguvu za kusumbua wale ambao wanaeleza ukweli kuhusiana na hali mbaya ya maisha ya wanafunzi kwa kukosa mabweni, nguvu hizo azielekeze kuhakikisha mabweni yanajengwa, tena ikiwezekana haraka.

Nguvu zake zitakuwa za maana zaidi ikiwa atafikiria namna ya kusaidia kupatikana kwa mabweni kuliko kukasirika kwa sababu ya kuandikwa ukweli kwamba Shule ya Sekondari William Lukuvi haina mabweni kiasi kwamba wanafunzi wanalazimika kulala darasani.

Katika kufuatilia ilibainika kuwa ni kweli kuna ugumu wa kupata ushirikiano, na pia hata baadhi ya waandishi wa habari wana hofu, kwa mfano kuna mwandishi alifanikiwa kupiga picha miezi kadhaa iliyopita wanafunzi wakiwa darasani wamelala, hakuweza kuzitumia, huku ulinzi ukiwekwa kuhakikisha hakuna mwandishi anayefanikiwa kufahamu hali hiyo ya watoto kulala darasani.

 Changamoto

Japokuwa kuna changamoto kadhaa, lakini kutokuwa na mabweni inaonekana ni changamoto kubwa katika Shule ya Sekondari ya William Lukuvi iliyopo Jimbo la Isimani, wilaya ya Iringa.Shule hiyo ipo takribani kilomita 50 kutoka Manispaa ya Iringa.

Shule hiyo imepewa jina hilo kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Isimani, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, anayepongezwa kwa harakati mbalimbali za kuleta maendeleo katika jimbo hilo.

Shule hiyo imejengwa na wananchi wa Kata ya Ilolompya ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa shule ya sekondari katika kila kata ili kuhakikisha watoto wanaomaliza elimu ya msingi wanapata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari.

Sekondari ya William Lukuvi imejengwa na wananchi wa Kata ya Ilolompya kwa lengo la kuwahudumia wananchi wa vijiji vinne vya Magozi, Ilolo, Luganga na Mkombilenga; shule iko mbali na baadhi ya vijiji kiasi kwamba inalazimika baadhi ya wanafunzi kubaki shuleni kutokana na kushindwa kurudi nyumbani kwao kutokana na umbali na pia usalama kwani baadhi ya maeneo wanayopita ni mapori yanaonekana kutokuwa salama hasa nyakati za usiku.

Shule ina zaidi ya wanafunzi 251 wakiwemo wavulana 145 na wasichana 106 ambapo kidato cha kwanza kuna wanafunzi 100 wavulana 52 na wasichana 49, kidato cha pili 74 wavulana 49 na wasichana 25.

Kidato cha tatu 39 wanafunzi wakiwemo wavulana 26 na wasichana 13, kidato cha nne ni 36 ambapo wavulana 22 na wasichana 14. Tatizo la bweni ni kubwa hali inayosababisha wanafunzi wavulana kutumia chumba cha darasa kwa ajili ya matumizi ya kulala wakati wasichana wakitumia jengo ambalo linatumika kwa muda mfupi wakisubiri kukamilika kwa bweni lao.

Wengi wa wanafunzi wanatoka umbali wa kati ya kilomita moja hadi nne kufika shule na kuwa kwa wale wanaotoka umbali wa kilomita nne, maana yake ni kuwa wanatembea kilomita nane kwenda shule na kurudi nyumbani.

Umbali huo wa zaidi ya kilomita nane yaani kwenda na kurudi, umekuwa ukilalamikiwa na baadhi ya wanafunzi kuwa unawasababishia wengi wao kuchoka, hivyo kusababisha kurudisha nyuma maendeleo yao kimasomo.

Usikose mfululizo wa makala hii kesho kujua kinachoendelea, pamoja na kauli za uongozi wa shule.

Dk Mvungi afariki dunia


Dk Sengondo Mvungi


Dar es Salaam.Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi (61) amefariki dunia katika Hospitali ya Millpark Netcare, Johanesburg, Afrika Kusini.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana kutoka Afrika Kusini na kuthibitishwa na Msemaji wa Hospitali ya Millpark, Tebogo Nyembezi zinasema Dk Mvungi alifariki dunia jana mchana. “Ni kweli tulimpokea mgonjwa huyo kutoka Tanzania na alifariki 6:00 mchana (saa 7:00 kwa saa za Afrika Mashariki),”alisema Nyembezi.

Nyembezi alisema kwamba walimpokea mgonjwa huyo akiwa na majeraha ya kichwa, lakini aliahidi kueleza sababu ya kifo chake leo baada ya kuzungumza na madaktari waliokuwa wakimtibu.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba pia alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kwamba walikuwa wakiendelea kuandaa taratibu za kuleta mwili wake nchini.

“Ni pigo kubwa kwetu, tunaangalia namna ya kuusafirisha kuja nchini na baadaye tutatoa taarifa rasmi,”alisema Jaji Warioba na kuongeza:

“Kwa kweli ni pigo kubwa siyo kwetu tu, lakini pigo kubwa kwa nchi yetu, tumepoteza mtu muhimu na kiungo muhimu sana. Dk Mvungi, wengine tulimfahamu tangu alipokuwa mwanafunzi, alikuwa mtu aliyesema kile alichokiamini, akikwambia kitu kilikuwa ni kile kilichopo moyoni mwake”.

Jaji Warioba alisema Dk Mvungi alikuwa msomi aliyebobea katika masuala ya sheria na kwamba alikuwa na mchango mkubwa katika tume. Pia alisema marehemu atakumbukwa kwa ushiriki wake wa dhati katika kupigania haki za binadamu, kazi aliyoifanya kwa moyo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani alisema: “Dk Mvungi alikuwa mfanyakazi hodari, alikuwa hachoki na hata ulipotokea ubishi mkubwa katika majadiliano kiasi cha watu wengine ku-loose temper (kupandwa na jazba), yeye alibaki vilevile na alizungumza vilevile bila kubadilika. Kweli tumempoteza mtu muhimu sana maana alikuwa akifahamu vizuri sana sheria, hatuna jinsi maana tumempoteza, kwahiyo itabidi tuendelee na kazi hii. Hatuna namna nyingine ya kufanya,”alisema Jaji Ramadhani.

Jaji Ramadhani alisema taratibu nyingine zitatangazwa baadaye kwani lazima washirikiane na chama chake, NCCR- Mageuzi alikokuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji, familia yake na Chuo Kikuu cha Bagamoyo ambako alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliliambia gazeti hili kwamba walipokea taarifa ya kifo cha Dk Mvungi saa 9.30 alasiri jana. “Tumepokea taarifa hizo alasiri kwamba amefariki. Ni kweli na sasa ninaelekea nyumbani kwake ili kuitaarifu familia,”alisema Mbatia.

Taarifa ya Tume

Jana jioni, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa rasmi kuhusu kifo cha Dk Mvungi ikisema: “Kwa masikitiko makubwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dk Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Millpark iliyopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini amefariki dunia.”

Taarifa iliyotolewa Katibu wa tume hiyo, Assaa Rashid ilisema Dk Mvungi alifariki dunia saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini.

Iliendelea kusema taarifa hiyo kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka Afrika Kusini kuja nchini kwa maziko zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa baadaye.

Dk Mvungi, alikuwa akitibiwa Afrika Kusini baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana walipovamiwa nyumbani kwake Kibamba, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu.

Alipelekwa nchini Afrika Kusini, Novemba 7, 2013 kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa siku tano kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi) jijini Dar es Salaam.

Dk Mvungi, ambaye aligombea urais mwaka 2010 kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi, alijeruhiwa vibaya kichwani na sehemu nyingine za mwili wake baada ya kukatwa mapanga na wavamizi hao.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Profesa Costa Mahalu alisema chuo hicho kimepoteza mtu muhimu sana, kwani ni mmoja wa waanzilishi waliokuwa wakifahamu vyema malengo na dira yake.

“Tumepata pigo kubwa sana kwani tumempoteza mtu ambaye tulishirikiana naye katika kuanzisha chuo hiki na aliyafahamu vyema malengo na dira yake, alikuwa ni mwalimu mzuri aliyebobea katika constitutional laws (sheria za Katiba) na wanafunzi walimpenda sana,”alisema Profesa Mahalu.

Profesa Mahalu alisema Dk Mvungi ambaye alikuwa naibu wake kabla ya kujiunga na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walifahamiana naye siku nyingi na kwamba wakati marehemu alipokwenda kusoma Shahada ya Uzamivu nchini Ujerumani alifikia nyumbani kwake (kwa Mahalu).

“Wakati huo nilikuwa nikifundisha Ujerumani, alikuja kusoma PhD yake ya masuala ya sheria na alifikia nyumbani kwangu, tutamkumbuka kwa uhodari wake katika kuchapa kazi, kweli tumempoteza mtu mahiri sana,”alisema.

Chadema, CCM wamlilia

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema amesikitishwa na taarifa za kifo cha Dk Mvungi na kwamba taifa limempoteza mwanzilishi wa mageuzi ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kudai Katiba Mpya.

“Tumepokea taarifa za kifo hiki kwa mshtuko mkubwa, tunamwomba Mwenyezi Mungu aipe nguvu familia ya Dk Mvungi, tunatoa pole kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na uongozi wa NCCR-Mageuzi,” alisema Mbowe.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa (CCM), Mwigulu Nchemba alisema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na kutoa pole kwa Watanzania wote kwa sababu Dk Mvungi alikuwa anafanya kazi muhimu ya kuwezesha kupatikana kwa Katiba Mpya.

Alisema amekufa wakati mchango na mawazo yake yakiwa yanahitajika kwa kiasi kikubwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba CCM kinaendelea kuisisitizia Serikali iwasake wahalifu hao ili wafikishwe kwenye vyombo vya dola.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema ameshtushwa na taarifa za kifo hicho ambacho kimetokea wakati Dk Mvungi akifanya kazi muhimu ya kuitafuta Katiba Mpya. “Naomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, amina,” alisema.

Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila alisema taifa limepoteza mtu muhimu na kwamba hali ya ulinzi ni suala linalohitaji mjadala wa kitaifa.“Tunahitaji kuangalia kiini cha uhalifu hapa nchini, watu wanateswa na kujeruhiwa ovyo ni lazima tuchukue hatua,” alisema.

Mitandao ya kijamii

Muda mfupi baada ya taarifa za kifo chake, mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Jamii Forum ilikuwa ilitawaliwa na salamu za pole kutoka kwa watu mbalimbali.

Hussein Bashe kwenye ukurasa wake wa Facebook aliandika kuwa, “Dr Sengondo Mvungi Is No More (hatunaye tena), taarifa zilizonifikia kutoka Hospitali ya Millpark, ndugu yetu Mvungi amefariki, mnamo saa tisa na nusu.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Wahalifu wamekatisha uhai wake wakati akifanya jukumu zito kwa ajili ya taifa letu. Jambo hili linaumiza sana Mungu atalipia uhalifu huu, poleni Tume ya Katiba, Poleni Familia, poleni NCCR-Mageuzi.”

Mtu mwingine aliyechangia suala hilo kwenye mtandao wa Jamiiforum ni yule aliyejitambulisha kwa jina la Ta Muganyizi aliyeandika kuwa, RIP Dr. Mvungi... Mungu akulaze mahala pema peponi. Japo umeondoka kivuli chako kitaishi... Naipa pole familia yako, maisha yetu kwa sasa nchini ni kudra za Mwenyezi Mungu. Ni kwamba tupigwe... wengine wamepona lakini wewe umeondoka.”

NABII ABAKA

Nabii Elisha Muliri anayetuhumiwa kwa ubakaji

 
Mama Mzazi wa Mwanafunzi anaedaiwa kubakwa Mary Mkombola akisimulia juu ya tukio la ubakaji lililompata Mwanae na kusababisha ujauzito mbele ya waandishi wa habari Kulia ni Martha Danie 17  aliyefanyiwa kitendo hicho.

Mwanasheria Mfawidhi Mkazi wa kituo cha msaada wakisheria cha Tanzania Legal Aid Centre [TALAC]
Godwin Ngongi akifafanua jambo kuhusu kitendo
cha ubakaji alichofanyiwa Mwanafunzi wa kidato cha tatu Martha Daniel [17] mbele ya waandishi wa habari ofini kwake jana, kulia ni mzazi wa mwanafunzi huyo Mary Mkombola


Na John Banda, Dodoma

NABII Elisha Muliri wa kanisa la Ebeneza mjini hapa ameingia matatani baada ya kudaiwa kumbaka na kumtia mimba  mwanafunzi na kukatiza masomo yake huku kutishia kumuua.

Akisimulia tukio hilo mbele ya waandishi wa habari mwanafunzi huyo Martha Daniel [17] kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya City ilyopo manispaa ya Dodoma alisema kabla ya kufanyiwa kitendo hicho alikuwa anaangushwa na mapepo.

Martha alisema baada ya kuhangaika kwa muda mrefu bila mafanikio walipata taarifa za ujio wa nabii huyo mjini humo na wapofika ili kupata msaada wa kuombewa mapepo hayo yalilipuka na binti akaponywa hata leo na kuahidiwa mbele ya kanisa kusaidiwa ada na Nabii huyo.

Binti huyo alisema baada ya kuponywa akaendelea kwenda kusali kanisani hapo ambapo kutokana na kila mtu anayefika na kufanyiwa maombi huacha mawasiliono kwenye vikaratasi, na Juni 8 mwaka huu akapigiwa simu na Nabii huyo akipewa maelekezo ya kufika nyuma ya ukumbi wa Paradise ambapo walikuwa wakifanyia ibada.

Anatanabaisha kuwa baada ya kuonana na Nabii alimwambia aingie kwenye Gari akaingia akifikili kuna heri akapewa soda aina ya Fanta orange alipokunywa akapoteza fahamu na alipokuja kuzinduka alijikuta akiwa nyumba za kulala wageni makole na Nabii akiwa amemlalia kama alivyozaliwa huku akiangalia mkanda wa Ngono.

‘’Wakati nataka kupiga kelele alinitishia kwamba ataniua kama nitathubutu kumwambia mtu yoyote jambo hilo, akanipiga kofi na kuniambia yeye hawezi kunilipia ada bure kwa sababu mimi siyo ndugu yake lazima lazima alale na mimi mara 5 kwa hiyo bado mara 4 na kunisisitiza asisikie popote kuwa alinifanyia hivyo’’, alisema Mwanafunzi huyo

Kwa upande wake Mama mzazi wa mwanafunzi huyo Mary Mkombora alisema alimpeleka kuombewa kutokana na kusubuliwa na mapepo tangu akiwa Darasa la sita na wakakubaliana na Nabii huyo kumlipia ada kwa awamu hivyo akachukue 50,000 kila mwezi ili kukamilisha 400,000 inayotakiwa shule.

Nilimgundua yupo tofauti kuanzia mwezi wa saba nilipomuuliza alisema yeye haelewi siku moja asubuhi nikamshuhudia akitapika  ndipo nilipomchapa na kumfukuza. Nikapigiwa simu na waliompokea mtoto kua aliyempa mimba ni  Nabii huyo ndipo nikachoka, na  alipopimwa alikuwa na mimba.

Nabii huyo ambaye alikuwa Mume wa mwimbaji Marufu wa Nyimbo za Injili marehemu Anjela Chibalonza kwa sasa hajulikani alipo japo mara kadha wasaidizi wa kanisa hilo ambalo limebadilishwa jina kutoka Shakinah Pentecostal Church na kuitwa Ebeneza .

 ‘’sasa hivi mimi na mtoto wangu tumekuwa tukiishi mashakani baada ya Msaidizi wake Nabii Monica  nimpe Martha akamtoe mimba kwa wataalamu anaowajua wao, siku ambayo alichukua kadi yenye namba za simu na kufuta meseji zote mwanangu alizokuwa akiandikiwa na Nabii,’’

Nabii huyo kwa sasa hajulikani alipo na hata alipotafutwa kwa simu yake ka mkono 0756 409118 ilikuwa amezimwa na msaidizi wake Nabii Monica Nyambura raia wa nchini Kenya anakotokea Elisha Muliri alisema yeye hawezi kuongelea jambo hilo kwakua yeye ni mgeni ameachiwa kanisa hilo baada ya mwenyeji wake kuwa safarini hivyo asubiliwe hatachelewa.

Tukio hilo limefikishwa katika kituo cha sharia cha Tanzania Legal Centre [TALAC] na mwanasheria mfawidhi mkazi Dodoma Godwin Ngongi tayali ameshamuandikia mkuu wa kituo cha polisi kati barua ya kuwataka kumkamata mtuhumiwa huyo ili afikishwe kwenye vyombo vya sharia na pia kuepusha  mwanfunzi huyo na hatari nyingine.

Jeshi hilo limekiri kuwa na taarifa ya tukio hilo na kwamba wanaendelea na  uchunguzi