Polisi yazuia msafara wa Lowassa

Polisi wakiwa wamefunga barabara katika Kijiji
Polisi wakiwa wamefunga barabara katika Kijiji cha Maroro wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, walipokuwa wakizuia msafara wa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa aliyekuwa akielekea Usangi, Mwanga kuhudhuria mazishi ya mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo yaliyofanyika wilayani humo jana. Na mpiga picha maalumu. 

Jeshi la Polisi, jana liliuzuia msafara wa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa kwenda Usangi, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro kushiriki mazishi ya kada wa CCM, Peter Kisumo, likitaka kupunguzwa kwa idadi ya watu.

Mbali na kuzuia msafara huo, chombo hicho cha Dola kimepiga marufuku shughuli za kutafuta udhamini kwa wagombea urais wa vyama vya siasa kuambatana na misafara.

Lowassa, ambaye aliwasili Kilimanjaro jana asubuhi kabla ya kuanza safari ya kwenda Mwanga, alijikuta akikumbana na kizuizi cha polisi walioziba barabara kwa magari yao eneo la Kijiji cha Mroro, mita chache kutoka Mji wa Mwanga, wakati akielekea na msafara wake katika Tarafa  ya Usangi kuhudhuria mazishi ya mwanasiasa huyo mkongwe aliyefariki wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Lowassa hakukubaliana na agizo la polisi la kumruhusu aendelee na safari na kuwaacha wafuasi wake kwenye msafara huo, ambao awali walitakiwa wasibebe bendera, lakini baadaye wakazuiwa.

Kisumo alizikwa jana katika mazishi yaliyohudhuriwa na maelfu ya waombolezaji, wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.

“Kwa kuwa tumezuiwa na polisi, kitendo hiki kimeondoa mwafaka wa kitaifa kwamba mpinzani hawezi kumzika mtu wa CCM na wa CCM hawezi kumzika mpinzani.... mpasuko huu ni mkubwa. Wameyataka wao,” alisema Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia baada ya polisi kuwazuia.

“Kwa kuwa wametuzuia kwenda kumzika Mzee Kisumo, sisi tunarudi lakini Watanzania wapewe taarifa kuwa CCM inalipasua Taifa.”

Alipoulizwa sababu za polisi kuwazuia, Mbatia alisema: “Wanahofia Mheshimiwa Lowassa na msafara wake. Magari mangapi? Magari 10 tu ya Mheshimiwa Lowassa! Magari gani hayo?”

Ilivyokuwa

Msafara huo ulikuwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani ambao ni pamoja na Mbunge wa Moshi Mjini, Phillemon Ndesamburo, Joseph Selasini (Rombo), Mbatia na na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mremaambaye pia ni Mbunge wa Vunjo pamoja na viongozi wa Chadema ngazi ya mkoa na wilaya.

Msafara huo ulipofika Mroro, ulikutana na kizuizi cha polisi pamoja na askari wa kuzuia ghasia waliowataka watoe bendera na kuachana na msafara huo.

Kutokana na kauli hiyo, Mbatia, ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) aliwataka madereva wa bodaboda kutoa bendera zao na kutoongozana na msafara, agizo ambalo walilitii na kuondoka lakini polisi walikataa magari kuvuka kizuizi hicho.

Baadaye, Mbatia alizungumza kwa simu na Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu  kabla ya kumpelekea simu Lowassa ambaye naye alizungumza naye na kusema wameruhusiwa, lakini askari waliokuwa wameweka doria walikataa kuwaruhusu.

Kutokana na hali hiyo, Mbatia baadaye alizungumza kwa simu na kudai anawasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Mponji  lakini askari waliokuwapo walidai kuwa wamepewa maagizo kuzuia msafara huo.

Msafara huo ulikaa eneo hilo zaidi ya saa mbili na baadaye polisi waliruhusu  gari ya Lowassa, Mbatia na Ndesamburo kupita, lakini watu waliokuwa kwenye msafara wabaki kitendo ambacho viongozi hao walikipinga na kuamua kurudi Moshi.

“Tumeongea na IGP, RPC lakini tunaambiwa OCD amekataa, tunataka Watanzania wajue kuwa CCM wameanza kupasua amani ya Taifa hili,” alisema Mbatia.

Baada ya kukubaliana, Mbatia aliwataka wananchi waliokuwa wanakwenda kwenye msiba kwa msafara wao kuingia kwenye magari na kuanza safari ya kurejea Moshi  na baada ya kufika Njia Panda Himo, walikutana na wananchi wengi waliokuwa wakitaka kumuona Lowassa na kufunga barabara.

Polisi walilazimika kutumia bomu la machozi kuwatawanya, lakini wengi waligoma kuondoka na Lowassa alilazimika kusimama kwenye gari na kuwapungia ndipo walipokubali kusogea pembeni kupisha msafara uendelee na safari.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kamanda Mponji alikiri jeshi lake kuzuia msafara huo, akisema kazi yake ni kuhakikisha Rais anamaliza safari yake Kilimanjaro kwa amani.

Mazishi ya mwanasiasa huyo mkongwe yalitarajiwa kumkutanisha Lowassa na Rais Kikwete, marafiki wawili wa muda mrefu ambao katika siku za karibuni wanaonekana kutofautiana baada ya jina la waziri huyo mkuu wa zamani kuenguliwa kwenye mchakato wa urais kwa tiketi ya CCM mapema Julai.

Lowassa, ambaye amepitishwa na Chadema kugombea urais na ambaye ataungwa mkono na vyama vinne vya NCCR-Mageuzi, NLD, Chadema na CUF, anatarajiwa kuanza kusaka wadhamini leo mkoani Mbeya na baadaye ataelekea Mwanza.

Maandamano yazuiwa Mbeya

Lakini wakati akianza ziara hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi amesema katika taarifa yake kwamba wamekubaliana na viongozi wa Chadema kwamba hakutakuwa na maandamano, bali utakuwapo msafara wa kawaida bila kuathiri shughuli za wakazi.

Msangi alisema sababu kubwa ya kuafikiana hivyo ni za kiusalama kutokana na ukweli kwamba barabara inayotumika ni moja.

Misafara kwenda NEC marufuku

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano ya aina yoyote ya vyama vya siasa wakati wa kwenda kuchukua fomu, kuzirudisha na kutafuta wadhamini mikoani.

Hatua hiyo ya polisi imekuja ikiwa ni siku kadhaa baada ya wafuasi wa vyama viwili vikubwa; CCM na Chadema kujitokeza kwa wingi kuwasindikiza wagombea wao kwenda kuchukua NEC na kusababisha msongamano katikati ya jiji.

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki alisema kutokana na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi walioshindwa kufika kwa wakati katika shughuli nyingine za kijamii, wameamua kusitisha utaratibu huo.

Alisema misafara hiyo ilisababisha usumbufu na malalamiko mengi kutokana na wananchi kutopata huduma kwa wakati, wagonjwa kushindwa kufika hospitalini kwa wakati, kuchelewa ofisini na watu kushindwa kupata huduma za kijamii kutokana na maduka kufungwa.

Alieleza kuwa hali hiyo ilijitokeza siku walipochukua fomu wagombea urais wa CCM na Chadema, hivyo kwa sababu za kiusalama, polisi imesitisha maandamano ya aina yoyote.

Kaniki alisema unaandaliwa utaratibu maalumu wa kuwakutanisha wadau wote wa siasa ili kuona namna bora ya kuhakikisha mchakato mzima wa uchaguzi unafanyika katika hali ya amani na utulivu.

Viongozi wa vyama walonga

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya viongozi wa vyama ambavyo wagombea wake wameshachukua fomu, walipinga hatua hiyo ya polisi, wakisema ni sawa na  kuwanyima wananchi haki ya msingi inayokubalika kikatiba.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena  Nyambabe alisema polisi ilipaswa kuchukua hatua mara baada ya CCM kufanya maandamano yao, lakini si kutoa tamko hilo baada ya Chadema.

Alikanusha kuwapo kwa sababu za kiusalama, akieleza kuwa kazi ya polisi ni kulinda usalama na hivyo wanaweza kupanga maandamano yaanzie wapi na kuishia wapi ili kupunguza vurugu.

Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi  Dovutwa alisema jeshi hilo lilijichanganya kwa kutoa taarifa awali kuwa linaruhusu maandamano hayo, lakini akasema kama limejiridhisha kuwa kwa kufanya hivyo linalinda usalama wa raia, haoni kama kuna tatizo.

“Wapo sahihi kabisa kuzuia, kwani kuna madai kuwa baadhi ya vijana walifanya vurugu, walilewa. Kuna dalili za kuhatarisha usalama kwa mwenendo huo, ” alisema.

Mgombea wa urais kupitia TLP, Maxmillian Lyimo alisema polisi wanapotoa kauli wawe makini wasije kuonekana wanapendelea upande fulani kwani wakati wa CCM walikaa kimya, lakini baada ya Chadema ndipo wametoa tamko. Alisema wao ndiyo wenye jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao, hivyo wanapaswa kuhakikisha mikusanyiko hiyo inalindwa.

Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi alisema watu wanatumia vibaya uhuru waliopewa, lakini akataka ieleze sababu ya kuzuia na kama ni usalama, ni wajibu wa polisi.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chaumma, Hashim Rungwe alisema hakuna haja ya kuwepo kwa maandamano wakati kuna kampeni ambazo wafuasi na wanachama watahudhuria hadi wachoke.

Kauli ya Kova

Mapema jana, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilisema haitatumia mabomu na nguvu wakati wa uchaguzi na badala yake itashirikiana na viongozi wa vyama vya siasa ili kudumisha amani na utulivu.

Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema polisi imejipanga kikamilifu kudhibiti vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.

No comments:

Post a Comment