Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Philip Mangula
Jeshi la Polisi
mkoani Simiyu, linamshikilia mkazi wa kijiji cha Ng’wang’wali, Wilaya ya
Itilima, aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 15 gerezani akiwa na
silaha ya kivita.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Salum Msangi, alimtaja mfungwa
huyo aliyekamatwa juzi na silaha hiyo kuwa ni Masanja Maguzu (42).
Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, Maguzu alikamatwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) ikiwa na risasi 31 nyumbani kwake.
Kamanda Msangi alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu jana kutoka wilayani Bariadi.
Alisema kwa mara ya kwanza Maguzu alikamatwa na bunduki aina ya SMG na
risasi 622 mwaka 2010 na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
mkoani Shinyanga na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 15 gerezani
baada ya kupatikana na hatia.
Hata hivyo, alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida, jeshi hilo tena limemkamata mfungwa huyo akiwa uraiani.
Kamanda Msangi alisema mbali na bunduki, pia alikamatwa na magazini tatu na risasi 31 za SMG kinyume cha sheria.
Alisema bunduki hiyo anatuhumiwa kuifanyia vitendo vya kihalifu na
ujangili katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la Akiba la Maswa.
Kamanda Msangi alisema jeshi lake linaendesha uchunguzi wa kina ili
kufahamu mazingira yaliyosababisha mfungwa huyo kuwa nje ya gereza baada
ya kuhukumiwa adhabu hiyo.
Alisema Novemba 6, mwaka huu, polisi walimkamata mke wa mfungwa huyo
aliyetambuliwa kwa jina la Holo Mabuga (30), akiwa na silaha nyingine ya
kivita aina ya G3.
Kamanda Msangi alisema silaha hiyo ilikamatwa ikiwa na risasi zake 36
pamoja na risasi nyingine zinazotumika katika bunduki aina ya SMG.
Siku 10 baada ya kukamatwa kwa mwanamke huyo, polisi walifanikiwa
kumnasa mumewe, ambaye ni mfungwa aliyeaminika yumo gerezani akitumikia
adhabu yake ya kifungo cha miaka 15 akiwa na silaha hiyo ya SMG na
risasi 31 na magazini tatu; moja hutumika katika bunduki aina ya Uzi gun
ya Kiisraeli.
“Jamani, tukio hili limetushitua na kutusikitisha sana. Maana wakati
tukipambana na kukabiliana na vitendo vya uhalifu na wahalifu, bado kuna
watu wengine wanakwamisha juhudi zetu sisi polisi. Mfungwa huyu kila
mmoja hapa mkoani anaelewa kuwa yuko gerezani anatumikia adhabu yake.
Ajabu leo amekutwa tena uraiani akiendelea na vitendo vyake vile vile.
Je, tutashindwa kulaumiwa kuwa tunakula na wahalifu?” Alihoji Kamanda
Msangi na kuongeza:
“Haiwezekani mfungwa aliyehukumiwa kutumikia jela miaka 15 kwa muda
mfupi hivi akawa nje hata kama ni kwa msamaha. Ni muda mfupi sana na
hasa ikilinganishwa na kosa lenyewe. Maana ni la kupatikana na silaha
tena ya kivita. Na iliyokuwa ikitumika kwa vitendo vya kijambazi na
ujangili ndani ya hifadhi, hii inaonyesha kuna namna imefanyika. Na sisi
tunaendelea kuchunguza kujua ukweli wa jambo hili.”
Alisema inawezekana mfungwa huyo alitoka gerezani katika mazingira ya
kutatanisha, lakini bado aliendelea kujihusisha na vitendo vya uhalifu
kwa kutumia silaha za kivita, kinyume cha sheria na mitego ya polisi
ilifanikiwa kumnasa baada ya kumkamata mkewe, ambaye pia alikutwa akiwa
na silaha nzito za kivita.
Alisema uchunguzi wa awali wa polisi ulibaini kuwa mke wa mfungwa huyo,
Holo Mabuga, pamoja na kupatikana akiwa na silaha hizo za kivita kinyume
cha sheria, hakuwa peke yake katika matumizi ya silaha hizo, bali nyuma
yake kulikuwa na kundi la watu aliokuwa akishirikiana nao.
Kamanda Msangi alisema kupatikana kwa magazini ya Uzi gun,
kunathibitisha kwamba, bunduki yake, ambayo matumizi yake ni sawa ya
SMG, bado iko mikononi mwa mtandao wa wahalifu na watu wabaya.
Alisema kama haitapatikana haraka itaendelea kusumbua wananchi na
kuhatarisha usalama wa maisha na mali zao na hata wanyama katika hifadhi
za wanyamapori.
NIPASHE iliwasiliana kwa njia ya simu jana na Msemaji wa Jeshi la
Magereza nchini, Omary Mtiga, kutaka aeleze mfungwa huyo aliondokaje
gerezani na kurudi uraiani lakini alisema hakuwa na taarifa hizo.
“Mimi sina taarifa. Niandikie meseji (ujumbe mfupi wa simu ya mkononi
(sms) ili nifuatilie huko Simiyu kujua ni gereza gani alilokuwa
akitumikia kifungo hicho,” alisema Mtiga.
Naye Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, aliomba apewe kufuatilia suala hilo.
“Nami nitafuatilia kesho (leo) kujua kulikoni,” alisema Nantanga.
No comments:
Post a Comment