Arusha Kwa Waka Moto Wafanyabiashara Wavamia Maeneo Kwa Nguvu


Na: Mahmoud Ahmad, Arusha
 

Wafanyabiashara wadogo almaarufu Machinga, wakiwa wamevamia eneo lililopo pembezoni mwa soko la Kilombero na kuvunja uzio na kujigaiya maeneo hayo kwa ajili ya Biashara. kwani eneo hilo ambalo lipo kwenye mgogoro kati ya halmashauri ya jiji la Arusha na mfanyabiashara mmoja wa jijini hapa, kwenye mahakama ya biashara hajajulikana hatima ya kesi hiyo lakini wafanyabiashara hao teyari wameshavamia eneo hilo. 

 Pichani ni wafanyabiashara hao wakiwa kwenye shughuli mbali mbali za kuandaa eneo hilo kwa ajili ya biashara na wengine teyari wamshapanga katika eneo hilo kama walivyokutwa na kamera yetu jijini Arusha leo Asubuhi

Mugabe agusia uchaguzi wa mapema


Rais Robert Mugabe

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amewasilisha Mahakamani pendekezo la kuifanyia kura ya maamuzi Katiba mpya mwezi Novemba kabla ya Uchaguzi wa Urais na Ubunge kufuatia baadaye mwezi Machi mwaka ujao.

Licha ya Kielelezo cha Katiba kuidhinishwa, viongozi wenye misimamo mikali katika chama cha Mugabe cha ZANU-PF wanapinga baadhi ya vifungu ikiwemo kile kinachopunguza uwezo wa rais.

 

Msemaji wa chama kikuu cha upinzani MDC, Douglas Mwonzora, amesema tarehe zilizopendekezwa na Mugabe haziwezi kuafikiwa na kwamba ZANU-PF inahitaji kubadili misimamo yake ili kuepuka ghasia kama zilizokumba Uchaguzi mkuu wa mwaka 2008.

Pande hizo mbili zimekosa kuafikiana juu ya kielelezo cha katiba mpya ambacho kinapaswa kupitisha kabla ya uchaguzi mpya kufanyika.

Hadi kufikia sasa , Rais Mugabe, 88,mwenye umri wa miaka 88, amekuwa akisisitiza kuwa uchaguzi ufanyike mwishoni mwa mwaka huu.

Chama cha MDC, kikiongozwa na Waziri Mkuu, Morgan Tsvangirai,akiungwa mkono na wapatanishi wa Afrika Kusini, kinasisitiza kuwa katiba mpya iwe tayari kabla ya uchaguzi kuhakikisha unafanyika kwa mazingira huru na ya haki.

Rais Mubage ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka 1980, anakana madai kuwa uchaguzi uliopita ulikumbwa na wizi wa kura kwa manufaa yake.

Bwana Tsvangirai alijiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais mwaka 2008, akilalamika kuwepo mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya wafuasi wake na jeshi la serikali pamoja na wafuasi wa Mugabe.

DRC kuimarisha uhusiano na Rwanda

Rais Joseph Kabila wa DRC kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa

Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ameambia BBC, kwamba atajitahidi kuimarisha uhusiano kati ya nchi yake na Rwanda,

Lakini alisema kuwa hana uhakika ikiwa awe na matumaini kuhusu mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa utakaojadili hali katika Maziwa makuu baadaye leo.

Bwana Kabila ameituhumu Rwanda kwa kusaidia waasi wa M23 Mashariki mwa Congo ambao wamekuwa kwenye mapambano na jeshi la Congo.

Rais Kabila na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame wamepewa onyo kali na Marekani kuwa lazima watatue mgogoro uo.

Kauli hii inakuja baada ya uamuzi wa Marekani mwezi Julai kusitisha msaada wa dola laki mbili kwa jeshi la Rwanda.

Sudan mbili zasaini makubaliano


Mazungumzo kati ya nchi hizo mbili yalifanyika nchini Ethiopia

Sudan na Sudan Kusini zimetia saini makubaliano kuhusu biashara, mafuta na usalama ingawa hazijakubaliana kuhusu mipaka.

Baada ya mazungumzo ya siku ya nne, nchi hizo mbili zimeafikiana kuruhusu usafirishaji wa mafuta kutoka kusini kupitia mabomba ya Kaskazini na kuondoa wanajeshi mpakani.

Viongozi wa nchi hizo mbili hatimaye wamekubaliana baada ya mazungumzo ya siku nne mjini Addis Ababa Ethiopia.

Lakin maswala kadhaa muhimu yangali kutatuliwa ikiwemo kuafikia makubaliano kuhusu mipaka inayozozaniwa ikiwa ni mojawpao ya kilichosababisha mgogoro ambao nusura utumbukize nchi hizo kwenye vita mapema mwaka huu.

Baada ya mapigano kuzuka kuhusu mzozo wa mafuta na mipaka, Umoja wa mataifa ulitishia kuziwekea pande zote mbili vikwazo ikiwa hazitaafikia makubaliano ya kina.

Wapatanishi wa Muungano wa Afrika wangali kuthibitisha kuwa makubaliano yameafikiwa lakini rais wa Sudan Omar al-Bashir na mwenzake wa Kusini Salva Kiir, wanatarajiwa kutia saini makubaliano hayo hii leo.

Maelezo yametolewa tu kwa mukhtasari lakini wapatanishi wa pande zote mbili, walisema kuwa wamekubaliana kuhusu eneo la nchi hizo mbili ambalo halina ulinzi wa kijeshi.

Pia makubaliano ya kiuchumi yaliafikiwa kuruhusu Sudan Kusini kuanza tena shughuli zake za kuzalisha mafuta.

Lakini mwafaka haukupatikana kuhusu eneo linalozozaniwa la Abyei wala mipaka mingine mingi ambayo nchi hizo zinazozania.

Kwa hivyo makubalino hayo hayajaweza kutimiza masharti ya Umoja wa Mataifa kwa nchi hizo kuafikia mkataba unaotatua mzozo huo kwa kina.

Msako dhidi ya Boko haram, 35 wauawa


Waathiriwa wa mashambulizi ya Boko Haram

Takriban wapiganaji 35 wa kundi la kiisilamu la Boko Haram, wameuawa katika msako mkali dhidi ya kundi hilo Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa jeshi la Nigeria, wapiganaji wengine sitini walikamatwa wakati wa msako huo kwenye majimbo ya Adamawa na Yobe.

Kundi hilo la kiisilamu, linapinga mifumo ya kimagharibi na athari zake nchini Nigeria na wamekuwa wakifanya mashambulizi yanayolenga maslahi ya nchi za Magharibi pamoja na makanisa.

Mnamo siku ya Jumapili, kulitokea shambulizi dhidi ya kanisa moja katoliki na ambalo lilisababisha mauaji ya watu wawili. Boko Haram ndilo limelaumiwa kwa kufanya shambulizi hilo.

Msemaji wa jeshi nchini humo, alifahamisha shirika la habari la AFP kuwa msako huo ulifanyika usiku kucha kati ya siku ya Jumapili na Jumatatu.

Wanajeshi walifanya msako wa nyumba hadi nyumba, katika mitaa mitatu na wakati mwingine kufyatuliana risasi na wapiganaji hao, usiku kucha.

Wanajeshi wawili walijeruhiwa katika makabiliano hayo.

Bunduki na mabomu vilipatikana katika maficho ya wanamgambo hao pamoja na silaha zengine ikiwemo mishale 32 na panga.

Mji huo umekuwa mojawapo ya miji iliyoathirika sana kutokana na harakati za Boko Harama ambalo linataka kutumika kwa sheria za kiisilamu kote nchini humo.

Mali mwenyeji wa kikosi cha pamoja

Waasi wa Tuareg Kaskazini mwa Mali

Serikali ya Mali imekubali kuwa mwenyeji wa jeshi la pamoja la nchi za kanda ya Afrika Magharibi ambalo litasiadia katika juhudi za kupambana na wapiganaji wa kiisilamu ambao wanadhibiti eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo.

Nchi hiyo itatafuta uungwaji mkono wa umoja wa mataifa baadaye wiki hii kwa ushirikiano na muungano wa nchi za magharibi (Ecowas.)

Wanamgambo wa kiisilamu walitwaa eneo hilo mwezi Aprili na kusababisha hofu ya kuwepo vurugu katika kanda hiyo.

Awali Mali ilipinga kuwa mwenyeji wa kikosi hicho cha wanajeshi 3,000 mjini Bamako ingawa sasa imebadili msimamo wake.

Baada ya juhuzi kubwa za kidiplomasia zikijumuisha viongozi wa kanda hiyo, maafisa wakuu sasa wametoa idhini ya kuweza kuwa na kambi za jeshi hilo katika vitongoji vya mji mkuu.

Rais wa muda wa Mali, Dioncounda Traore alisemekana kutoridhia wanajeshi hao wageni kuwa nchini humo.

Wapiganaji hao wa kiisilamu walichukua udhibiti wa eneo la Kaskazini mwa nchi, baada ya nchi hiyo kukumbwa na vurugu kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwezi Machi mapema mwaka huu.

Wapiganaji hao wameanza kutumia sheria za kiisilamu katika miji ya Timbuktu, Kidal na Gao huku madhabahu ya kale ambayo yanaonekana kama ambayo yanatumiwa kwa ushirikina yakiharibiwa.

Jeshi la Kenya lakiri mauaji ya wasomali 6

Wanajeshi wa Kenya nchini Somalia

Jeshi la Kenya limekiri kuwa mwanajeshi wake mmoja alifyatua risasi na kuwaua raia sita wa somalia mnamo siku ya Jumapili.

Jeshi la Kenya lenyewe limesema kuwa linafanya uchunguzi na kwamba litachukua hatua zinazostahili.

Uftyauaji risasi ulitokea katika kijiji cha Jana Abdalla, ambacho kiko umbali wa kilomita sita kutoka mji wa Kismayo ambao umekuwa ngome kubwa ya wapiganaji wa Al Shabaab.

Msemaji wa jeshi la Kenya Kanali Cyrus Oguna alikana madai kuwa mauaji hayo yalifanywa kwa maksudi na kuelezea kuwa wanajeshi wake walivamiwa na wanamgambo hao ambao waliwaua wanajeshi wawili wa Kenya.

Hapo awali Ujumbe wa Umoja wa Afrika wa kudumisha amani nchini Somalia AMISOM, ulisema utachunguza mauaji hayo.

Msemaji wa kikosi cha Somalia, Mohemmed Hirsi, ameiambia BBC kuwa mauaji hayo yalitokea wakati jeshi la Kenya lilipovamiwa na wapiganaji wa Al Shabaab takriban kilomita sitini kutoka kwa ngome kubwa ya kundi hilo.

Msemaji wa AMISOM kanali Adi Aden amesema wakati ukweli wa kesi hiyo utakapojulikana watachukua hatua.

Msemaji huyo aliambia BBC kuwa wanajeshi wa Kenya waliwafyatulia risasi wanaume hao waliokuwa wameketi nje ya duka moja katika kijiji cha Janaay Cabdalla.

Wanajeshi wa Kenya na wale wa Somalia awali walivamiwa na wapiganaji wa Al Shebaab huku ripoti zikisema kuwa pande hizo mbili, zilipata majeruhi.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, wanakijiji waliouawa ambao ni wanaume saba hawakuwa wanamgambo bali raia wa kawaida.

Duru zinasema kuwa wanaume hao walikuwa wamepiga foleni kununua sukari.Aidha msemaji wa jeshi la Muungano wa Afrika nchini Somalia, (AMISOM) alisema kuwa hawezi kuthibitisha tukio hilo, lakini madai hayo yatachunguzwa.

Wanajeshi wa Somalia wakiungwa mkono na wale wa Uganda na Kenya pamoja na vikosi vingine kutoka nchi tofauti za Afrika, wanakaribia kuuzingira mji wa Kismayo,na ili waweze kufanikiwa katika kuuteka mjihuo, wanachi wa pale watahitaji kushirikiana nao.

Wanajeshi wa Kenya wamewahi kutuhumiwa kwa kuwaua raia wakati wakifanya mashambulizi katika maeneo ya Al Shabaab .

Shirika la kuwahudumia wakimbizi UNHCR linakadiria takriban wakimbizi 10,000 wameutoroka mji wa Kismayo katika kipindi cha wiki moja iliyopita.