Jaji wa kesi ya Tanesco, Dowans sasa asifiwa
Mitambo ya Dowans
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Fredrick
Werema na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu, wamemmwagia sifa kedekede Jaji
Emilian Mushi kutokana na hukumu ya kesi kampuni ya kufua umeme wa
dharura ya Dowans, dhidi ya Shirika la Umeme (Tanesco).
Katika hotuba zao za kumuaga Jaji Mushi
aliyestaafu hivi karibuni, Jaji Werema na Jaji Jundu walirejea hukumu za
kesi kadhaa alizozitoa Jaji Mushi kama kielelezo cha umakini, ujasiri,
uadilifu na weledi wake, ikiwamo hukumu hiyo ya Dowans.
Msimamo huo wa Jaji Werema na Jundu umekuja wakati
Tanesco ikihaha kukata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyosajiri tuzo ya
Dowans, iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro
ya Kibiashara (ICC).
AG Werema
Katika hotuba yake ya kumuaga Jaji Mushi, Werema
alisema kuwa Jaji Mushi katika utendaji wa shughuli zake alikuwa
akitenda bila kufungamana na upande wowote, pasipo hofu wala upendeleo,
nia mbaya au kuathiriwa na hali yoyote. Akizungumzia kesi ya Dowans,
Werema alisema kuwa Jaji Mushi amethibitisha kuwa ni mtafiti, mtu wa
kutafakari na mchambuzi wa sheria, huku akiifananisha na chuo cha sheria
za usuluhishi wa migogoro ya kibiashara.
“Wale wanaotamani kuwa wataalamu katika
usuluhishi, anawashauri kusoma hukumu yake katika shauri la Madai namba
8/2011 linalohusiana na usuluhishi baina ya Dowans Holdings SA (Costa
Rica) na Dowans Tanzania Ltd ya Tanzania dhidi ya Tanesco.”, alisema
Jaji Werema.
Jaji Jundu
Kwa upande wake Jaji Kiongozi, Jundu, akizungumzia
hukumu ya Dowans alisema kuwa ni mfano wa jinsi Jaji Mushi alivyokuwa
akisisitiza hukumu zinazozingatia ushahidi na ukweli, na kwamba alikuwa
mwangalifu, mwadililifu, mweledi, mtenda haki bila upendeleo.
Alisema kuwa katika hukumu hiyo Jaji Mushi
alizingatia sana ukweli na ushahidi, pamoja na sheria zinazohusiana na
masuala ya usuluhisi..
Kwa upande wake Jaji Mushi pia aliitaja kesi ya
Dowans kuwa ni miongoni mwa kesi ambazo hatazisahau katika maisha yake
ya ujaji kutokana na changamoto mbalimbali alizokabiliwa.
Alisema miongoni mwa changamoto aliyoipata katika
kesi hiyo ni jinsi ya kuwianisha uamuzi wa ICC na kulinganisha na sheria
zinazotumika hapa nchini, pamoja na msukumo wa kisiasa katika shauri
hilo.
Novemba 15, 2010 ICC, chini ya Mwenyekiti Gerald
Aksen akisaidiwa na wasuluhishi Swithin Munyantwali na Jonathan Parker,
iliiamuru Tanesco iilipe Dowans fidia ya Sh94 bilioni kwa kuvunja
mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment