Polisi wazima maandamano vyuo vikuu Iringa kuhusu gesi

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Wakati Rais Jakaya Kikwete, akiwa ametoa msimamo kuhusu gesi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, limepiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani humo kupinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Wanafunzi hao kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi ambao wanasoma katika  vyuo vikuu vya Ruaha (RUCo) , Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE)  na Chuo Kikuu cha Tumaini (IUCo) vilivyopo mkoani Iringa, walipanga kuandamana jana.

Walitaka kufanya maandamano hayo ili kushinikiza serikali kuwapa muda wakazi wa mikoa ya Mtwara na Lindi kujadili mustakabali wa madai yao kuhusu rasilimali hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, akizungumza na NIPASHE kwa simu akiwa mjini Songea, alisema jana kuwa Jeshi la Polisi limelazimika kuzuia maandamano hayo kwa sababu wanafunzi hao katika barua yao ya kuomba kuandamana hawakueleza nani atayapokea maandamano yao.

Alisema wanafunzi hao hawakueleza madhumuni ya maandamano hayo, yangeanzia wapi na kuishia wapi na pia barua hiyo haikuonyesha imetoka kwa nani zaidi ya kuweka vivuli vya saini kwenye barua hiyo.

Kamanda Kamuhanda alisema hata hivyo, kama wanafunzi hao watatimiza masharti yote, Jeshi la Polisi litawaruhusu kufanya maandamano hayo kama ambavyo limekuwa likifanya kwa watu wanaotimiza masharti yanayotakiwa.

Wanafunzi hao wakizungumza na waandishi wa habari katika bustani za Manispaa ya Iringa, walilalamika kuwa Jeshi la Polisi kwa kukataa kuwapatia kibali kwa ajili ya kufanya maandamano yao ya kupinga usafirishaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Akisoma tamko la wanafunzi hao, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Namangaya Mhaji, alisema wameamua kufanya maandamano ili kuungana na wenzao wakazi wa mikoa hiyo kutetea gesi.

“Tunamkumbusha Rais  Kikwete, ahadi yake ya mwaka 2009-2010 aliyoitoa na kuahidi katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) itakuwa ukanda wa viwanda,” alisema.

Katika madai yao, wanafunzi hao waliikumbusha serikali juu ya ahadi walizoahidi kuwafanyia wakazi wa mikoa ya Kusini za kujenga tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mkoani Mtwara pamoja na Hospitali ya Rufaa katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

“Tunamuomba Rais Kikwete na wananchi wote kwa ujumla, watuelewe kuwa hatuna maana kwamba gesi yote ya Lindi na Mtwara itumike kwa wananchi wa mikoa hiyo tu, bali kiwanda au mitambo ya kufua umeme wa gesi ijengwe Mtwara na Lindi na siyo Dar es Salaam,” alisema Mhaji.

Mhaji alisema katika hali ya kawaida rasilimali yoyote inayopatikana katika eneo fulani ni lazima iwanufaishe wananchi waishio eneo husika, hivyo rasilimali iliyopo mikoa ya Lindi na Mtwara ni lazima wananchi wanufaike nayo.

Mwishoni mwa Desemba mwaka jana, mamia ya wakazi wa mkoa wa Mtwara waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Maandamano hayo ambayo yaliratibiwa na vyama vya siasa na kuwashirikisha wananchi wa wilaya za mkoa wa

No comments:

Post a Comment