Maombi ya Lwakatare yapangiwa jaji
Dar es Salaam. Maombi ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare kupinga utaratibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kumfutia mashtaka kisha kumkamata na kumfungulia tena mengine, tayari yamepangiwa jaji wa kuyasikiliza.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na mmoja wa mawakili wanaomtetea Lwakatare, zinadai maombi hayo yamepangwa kusikilizwa na Jaji Lawrence Kaduri. Hata hivyo, tarehe ya kusikilizwa kwa maombi hayo haijapangwa.
Lwakatare anayekabiliwa na kesi ya ugaidi na
mwenzake Ludovick Joseph, kupitia kwa jopo la mawakili wanaomtetea, wiki
iliyopita aliwasilisha maombi Mahakama Kuu Dar es Salaam akipinga
uamuzi wa DPP kuwafutia mashtaka kisha kuwakamata na kuwafungulia tena
mashtaka hayo.
Siku hiyohihyo alipowasilisha maombi hayo,
Mahakama Kuu ilitoa hati ya kuita majalada yanayohusiana na kesi yao,
ikiiamuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iwasilishe majalada hayo
mahakamani hapo.
Majalada hayo namba 37 na namba 6 yote ya
mwaka 2013, yalishawasilishwa Mahakama Kuu, kwa awamu mbili. Jalada la
kwanza, namba 37 liliwasilishwa Mahakama Kuu Jumatatu na jalada la pili
namba 6 liliwasilishwa Jumanne, wiki hii.
Katika maombi yake Mahakama Kuu
yaliyowasilishwa chini ya hati ya dharura, yakiambatanishwa na hati ya
kiapo cha Wakili Peter Kibatala, Lwakatare anaomba mahakama hiyo iitishe
majalada hayo na ifanye marejeo ya mwenendo wa kesi katika Mahakama ya
Kisutu.
Kwa mujibu wa maombi hayo ya marejeo namba 14
ya mwaka 2013, lengo la kuiomba mahakama hiyo iitishe majalada hayo ni
kufanya uchunguzi ili kujiridhisha yenyewe kuhusu usahihi na uhalali wa
mwenendo wake.
Pia, wanaomba Mahakama Kuu ifanye marejeo na/au
kutengua hati ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuwafutia mashtaka watoa maombi
(Nolle Prosequi), kabla ya kuwakamata na kuwafungulia tena mashtaka
hayohayo.
Sambamba na hayo, wanaomba Mahakama Kuu iamuru
Mahakama ya Kisutu itoe uamuzi wa maombi ya dhamana, uliokuwa umepanga
kutolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Emillius Mchauru, Machi 20, mwaka
huu katika kesi namba 37.
Maombi mengine ni kurejea, au kutengua
mwenendo wa kesi katika kesi namba 6 iliyofunguliwa baada ya hati ya
kuwafutia mashtaka watoa maombi hao, badala yake mwenendo wa kesi katika
kesi namba 37 uendelee.
Pia, wanaomba Mahakama Kuu iamue kwamba
utaratibu uliotumiwa na wajibu maombi (Jamhuri) kutoa hati ya kuwafutia
mashtaka watoa maombi katika kesi namba 37, ilikuwa kinyume cha sheria
na/au haukuwa sahihi.
Lwakatare na mwenzake, Joseph, wanakabiliwa na
kesi ya ugaidi katika Mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka
manne ya kula njama na kufanya mipango ya kumteka, kisha kumdhuru kwa
sumu Dennis Msacky.
Walikamatwa Machi 13, mwaka huu na kupandishwa
kizimbani kwa mara ya kwanza Jumatatu, Oktoba 18, ambako walisomewa
mashtaka hayo, ambayo waliyakana, baada ya kuulizwa kama wanayakubali au
la.
Wasichana wadogo waongoza kuambukizwa VVU nchini
Ripoti ya viashiria vya Ukimwi nchini katika mwaka 2011/12 imeonyesha kuwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 23 na 24 wameambukizwa virusi vya Ukimwi kwa asilimia 6.6, ikilinganishwa na wavulana wa umri huo ambao ni asilimia 2.8.
Akisoma ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania, (Tacaids), Dk Fatuma
Mrisho alisema kiwango cha wasichana wa umri huo wenye virusi ni mara
mbili zaidi ya wavulana.
Akizindua ripoti hiyo, Rais Jakaya Kikwete
alisisitiza Watanzania na sekta zote zinazojihusisha na mapambano dhidi
ya Ukimwi, zitilie mkazo umuhimu wa kukomesha unyanyapaa na kuhamasisha
upimaji wa hiari.
“Watanzania zaidi ya milioni mbili wamefariki
tangu Ukimwi ugundulike miaka 30 iliyopita, tunatakiwa tupambane kwa
dhati kabisa,” alisema Rais Kikwete.
Alipongeza ongezeko la idadi ya watu waliopima kwa hiari na kuwataka wanaume kupima badala ya kuwaachia jukumu hilo wanawake.
Rais pia alizitaka taasisi za Ukimwi,
kudhibiti kasi ya maambukizi katika miji mikubwa na katika barabara kuu
zikiwemo za Chalinze na Njombe.
“Maeneo hayo yanahitaji nguvu zaidi,
hata maeneo yenye kiwango kidogo cha maambukizi nayo yasibweteke
yanahitaji tahadhari,” alisema.
Kuhusu tohara kwa wanaume, Rais Kikwete
alisisitiza zaidi tohara kwa wanaume na kwamba wasiotahiriwa wanaongeza
kasi ya maambukizi kwa asilimia 60 na wanaotahiriwa wanapunguza kwa
asilimia 60 pia.
Kwa upande wake, Dk Kikwete alisema maambukizi
kwa vijana wenye umri mdogo yanatokea wakati vijana hao wana umri wa
kati ya miaka 15 na 19 na matokeo yake kuwa wazi katika umri wa miaka 23
na 24. Alisisitiza kuwa matokeo haya ni kama ya sensa na kwamba si kila
Mtanzania mwenye umri wa miaka 14 hadi 49 amepimwa.
“Kwa jumla asilimia 2.0 ya wasichana na
wavulana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wana maambukizi ya virusu,”
alisema. Hata hivyo ripoti hiyo ilionyesha kuwa kasi ya maambukizi kwa
Tanzania nzima, imepungua kutoka asilimia 5.8 mwaka 2008 hadi kufikia
asilimia 5.1 mwaka 2011/2012.
Utafiti wa kwanza wa aina hii ulifanywa mwaka 2003 -2004 ambapo maambukizi yalikuwa asilimia 7.06.
Utafiti mwingine ulifanyika mwaka 2009-2010 ambapo maambukizi yalishuka toka asilimia 7 hadi asilimia 5.8
Pia, ripoti hiyo ilionyesha kuwa asilimia tisa
ya wasichana na 10 ya wavulana wenye umri wa miaka 15 na 24 walianza
kujamiiana kwa mara ya kwanza kabla ya kutimiza miaka 15.
Ripoti hiyo
ilionyesha kuwa Mkoa wa Njombe una maambukizi ya juu zaidi ya asilimia
14.8 ya maambukizo kuliko mikoa yote Tanzania.
Maeneo ya visiwani yana asilimia ndogo zaidi ya maambukizi ambapo Unguja ilikuwa na asilimia 1.2 na Pemba asilimia 0.5 tu
“Matokeo
ya ripoti hii yatatupa mwanya zaidi wa kujua nini kifanyike na wapi
nguvu iongezwe katika kupambana na maradhi haya hatari,” alisema
Kikwete.
Takwimu za sasa zinaonyesha kuwa maeneo ya
mijini yana maambukizi mengi zaidi ambapo kwa wanawake ni asilimia 6.2
na wanaume ni asilimia 3.8
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa zaidi ya robo ya Watanzania walioko kwenye ndoa wana maambukizi ya Ukimwi.
Ripoti hiyo ya kwanza na ya aina yake ilichambua pia idadi ya
wenza kati ya wanaume na wanawake ambapo kwa Tanzania nzima, asilimia 21
ya wanaume walikuwa na mwenza zaidi ya mmoja wakati ni asilimia nne tu
ya wanawake walikuwa na mwenza zaidi ya mmoja.
“Uwiano wa wanaume
wenye miaka 15 hadi 49 ambao walikuwa wamejamiiana na wenza wawili au
zaidi miezi miwili iliyopita ni zaidi ya mara tano ya uwiano wa
wanawake,” ilisema ripoti hiyo.
Uzinduzi wa ripoti hiyo ulihudhuriwa pia na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri Wa Fedha Dk William Mgimwa, waziri wa
afya, Dk Hussein Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Sedicy Mecky na
wadau mbalimbali wa Ukimwi nchini na nje ya nchi.
Hatima ya vigogo waliosimamishwa Tanesco kitendawili
Dar es Salaam. Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) imeendelea kusuasua kutoa majibu sahihi kuhusu hatima ya
vigogo watatu, waliosimamishwa kazi mwaka jana kwa tuhuma za ubadhirifu
na matumizi mabaya ya ofisi.
Tayari bodi hiyo imeunda jopo la watu sita
kuwahoji maofisa hao kabla ya kutoa uamuzi, lakini zaidi ya mara tatu
Mwenyekiti wake, Jenerali mstaafu Robert Mboma anapotafutwa kuelezea
kilichobainika baada ya kuhojiwa kwa vigogo hao, amekuwa akieleza kuwa
kazi hiyo itaanza baada ya wiki moja.
Uamuzi wa kuwahoji maofisa hao ulikuja baada
ya bodi hiyo kukabidhiwa ripoti na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), kuonyesha upungufu kadhaa wa utendaji kwa
watumishi hao.
Katika maelezo yake ya jana, Mboma alisema:
“Tumeshapata jopo la watu sita ambao watakuwa katika makundi mawili
yenye watu watatu, tumechelewa kuanza kuwahoji kwa sababu tulikuwa
tukichambua mafaili ya watu wanaounda jopo hili.”
“Pia, tulikuwa
tukipitia ushauri wa watu mbalimbali, ili kutokuwa na watu ambao wana
mgongano wa kimasilahi na maofisa hawa wa Tanesco.”
Tangu Januari mwaka huu, Jenerali Mboma
ameshazungumza na gazeti hili zaidi ya mara tatu, kila alipokuwa
akiulizwa juu ya suala hilo, alisema kazi ya kuwahoji maofisa hao
ingeanza baada ya wiki moja.
Maofisa hao ambao wanasubiri kuhojiwa ni Naibu
Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa
Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi Ununuzi, Harun Mattambo.
Katika maelezo yake, Jenerali Mboma alisema
ripoti ya CAG inaonyesha kuna kasoro hasa ununuzi usiofuata taratibu na
ubadilishaji fedha za kigeni (dola).
“Kikubwa alichogundua CAG ni ununuzi usiofuata
taratibu na suala la kubadilishwa kwa Dola za Marekani benki, ambazo
Shirika halina akaunti,” alisema Mboma na kuongeza:
“Benki ambayo shirika halina akaunti na ambayo
wangeweza kubadilishia fedha hizo ni Benki Kuu (BoT) pekee, lakini
haikufanyika hivyo jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.”
Alisema baada ya jopo kumaliza kuwahoji watuhumiwa hao, litawasilisha mapendekezo kwa bodi ambayo itatoa uamuzi wake.
Maofisa hao walisimamishwa kazi Julai 14,
mwaka jana, sambamba na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco,
William Mhando ambaye baadaye alifukuzwa kazi.
Kima cha chini kutangazwa mwezi ujao
Dar es Salaam. Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka amesema mwezi ujao wanatarajia kutangaza kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta zote.
Akizungumza jana wakati wa mkutano kuhusu sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa Baraza Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), alisema kwa muda mrefu kiwango cha kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta zote kilikuwa hakijabadilishwa.
“Kwa muda mrefu tulikuwa hatujatangaza kima cha chini cha mshahara, lakini nafurahi kuwajulisha tu kwamba mwezi ujao tutatangaza rasmi,”alisema Kabaka.
Pia alitahadharisha kuhusu utitiri wa vyama katika sehemu moja ya kazi kushauri waajiri wasiruhusu wafanyakazi waanzishe kwa sababu vitakosa nguvu ya kujadiliana na mwajiri katika kufunga mikataba ya hiyari .
Waziri huyo alisema sekta ya hifadhi ya jamii ina idadi ndogo ya wanachama waliojiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ukilinganisha na idadi ya nguvu kazi iliyopo ambayo ni milioni 22.
Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Irene Isaka alisema hadi sasa michango katika mifuko hiyo imefikia Sh 1.4 trilioni na kwamba mafao yanayolipwa yamepanda kutoka Sh500 bilioni hadi kufikia Sh 724 bilioni.
Subscribe to:
Posts (Atom)