Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI),
Ramadhani Madabida (kulia) na Ofisa Ubora wa Bidhaa wa Bohari Kuu ya
Dawa (MSD), Evance Mwemezi walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana kusomewa mashtaka ya kuuza na kusambaza
dawa feki za ARV. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa
CCM, Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda
cha Tanzania Pharmaceutical Ltd cha Dar es Salaam (TPI), Ramadhani
Madabida na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kusambaza dawa bandia
na kusababisha hasara ya Sh148.3 milioni.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi aliwataja
washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo kuwa ni Mkurugenzi wa
Operesheni wa TPI, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon Msofe, Mhasibu
Msaidizi, Fatma Shango pamoja na wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD),
Sadick Materu na Evans Mwemezi.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa
Mahakama hiyo, Nyigulile Mwaseba, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro
alisema katika shtaka la kwanza, Aprili 5, 2011, Madabida, Shamte, Msofe
na Shango wakiwa na nyadhifa hizo kwenye kiwanda cha TPI walisambaza
makopo 7,776 ya dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) aina ya
Antirectroviral.
Kimaro alidai kuwa washtakiwa hao, walifanya kosa
hilo kinyume na kifungu cha 76 (1)(2) cha Sheria ya Chakula, Dawa na
Vipodozi ya mwaka 2003, wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa
halali na kwamba zimetengenezwa Machi, 2011 na muda wake wa kutumika
unakwisha 2013 wakati wakijua kuwa si kweli.
Katika shtaka la pili, Wakili Kimaro alidai kuwa
Aprili 11, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango walisambaza na kuuza
makopo 4,476 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral walizokuwa wakijaribu
kuonyesha kuwa zilikuwa na viambatanisho vya Starudine 30mg, Nevirapine
200mg, Lamivudine 150mg pamoja na fungu namba OC 01.85.
Alidai kuwa washtakiwa hao waliweka viambatanisho
hivyo wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halisi na kwamba
zilitengenezwa Machi 2011 na muda wake wa kutumika ulikwisha Februari
2013 huku wakijua kwamba ni uongo.
Katika shtaka la tatu wanadaiwa kujipatia fedha
kwa njia ya udanganyifu, kinyume na Kifungu cha 302 cha Sheria ya Kanuni
ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Wakili Kimaro alidai kuwa kati ya Aprili 12 na 29,
2011, washtakiwa hao wakiwa na nia ya kulaghai, walijipatia Dola za
Marekani 98,506 sawa na Sh148,350,156.48 wakijaribu kuonyesha kuwa kiasi
hicho cha fedha ni malipo halali ya makopo 12,252 ya dawa aina ya
Antirectrovial yaliyokuwa katika fungu (batch) namba OC 1.85.
Alidai pia kuwa washtakiwa hao walikuwa
wakionyesha dawa hizo bandia zilikuwa zimetengenezwa Machi, 2011 na
kwamba muda wake wa kumalizika kutumika ni Februari, 2013 na
wakafanikiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka MSD.
Katika shtaka la nne, Materu na Mwemezi wakiwa ni
Meneja wa Udhibiti Viwango na Ofisa Udhibiti Viwango wa MSD, kati ya
Aprili 2 na 13, 2011 huku wakijua nia ya kutendeka kwa makosa hayo ya
usambazwaji wa dawa bandia, walishindwa kuzuia kinyume na Kifungu cha
Sheria namba 383 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Katika shtaka la tano, wakili huyo wa Serikali
alidai kuwa kati ya Aprili 5 na 30, 2011, washtakiwa Madabida, Shamte,
Msofe, Shango pamoja na Materu na Mwemezi, kinyume na Sheria ya Uhujumu
Uchumi, walishindwa kutekeleza majukumu yao wakiwa watendaji.
Alidai kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao
kwa pamoja walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kusambaza
makopo 12,252 ya dawa bandia wakijaribu kuonyesha kuwa zilitengenezwa
Machi 2011 na kwamba zitakwisha muda wake wa kutumika Februari 2013 na
kuisababishia mamlaka hiyo ya Serikali hasara ya Sh148,350,156.48.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili na upande wa
mashtaka ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Akitoa
masharti ya dhamana, Hakimu Mwaseba alimtaka kila mshtakiwa kuwa na
wadhamini wawili wanaoaminika ambao wanafanya kazi kwenye taasisi
zinazotambulika kisheria na kwamba kila mdhamini angesaini bondi ya
Sh6,181, 256.
Pia alimtaka kila mshtakiwa kutoa kiasi cha Sh12,
362,513 milioni taslimu mahakamani hapo au hati ya mali isiyohamishika
yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Madabida na Materu waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti hayo huku wenzao wakipelekwa mahabusu kusubiri kuyakamilisha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, mwaka huu itakapotajwa.