Uhuru kuapa kama Obama
Uhuru Kenyatta
Mke wake ndiye atamshikia Biblia na yeye atakuwa anaishika kwa kuweka mkono kama alivyofanya Rais Obama wa Marekani
Nairobi. Rais Mteule wa Kenya,
Uhuru Kenyatta amesema kwamba wakati wa kuapishwa hataapa kwa kuinua
Biblia bali atasaidiwa na mkewe kama alivyoapishwa Rais Obama wa
Marekani.
Mkuu wa Majeshi ya Kenya (KDF), Jenerali Julius Karangi
alisema jana kuwa Kenyatta aliomba mkewe Margaret Kenyatta amshikie
Biblia atakapokuwa akiapishwa.
“Hili ni ombi la rais mteule na itakuwa vyema tukubali ombi lake katika siku hii ya kihistoria,” alisema Jenerali Karangi.
“Mke wangu atanishikia biblia kisha nitaweka mkono kama alivyofanya Omaba,hakuna Rais wa Kenya aliefanya hivyo” alisema
Kenyatta ataweka tu mkono wake wa kushoto juu ya Biblia ikishikiliwa na mkewe, katika kile anachotaja hatua ya kuachana na mtindo wa awali wa kuapisha marais wa Kenya wakiinua Biblia.
Kenyatta ataiga mfano wa Rais Barack Obama wa Amerika, alipoapishwa hadharani mjini Washington DC mnamo Januari 21, 2013, ambapo aliomba mkewe Michelle Obama amshikie Biblia.
Siku hiyo Rais Mwai Kibaki atamkabidhi katiba mpya
Kenyatta, ambayo ilianza kutumika mnamo Agosti 2010. Mtindo huu utakuwa
wa kwanza tangu nchi hiyo kupata Uhuru. Sherehe hiyo itafanywa katika
Uwanja wa Michezo wa Moi Kasarani, ambapo pia Naibu wa Rais William Ruto
ataapishwa.
Shughuli hiyo inatarajiwa kumalizika saa 7.45. Kamati ya
Mamlaka ya Ofisi ya Rais tayari ina ratiba ya mpangilio wa shughuli
hiyo.
Ratiba hiyo ina picha ya rais anayeondoka katika ukurasa wa
pili na ya Kenyatta katika ukurasa wa tatu. Kamati hiyo imeteua Rais
Yoweri Museveni kuzungumza kwa niaba ya wageni wote waalikwa siku hiyo.
Hapo jana asubuhi, kamati hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Kimemia, ilisema kwamba shughuli itaanza rasmi 5:45 asubuhi Rais Kibaki atakapowasili uwanjani.
Kulingana na mpangilio uliopo, wageni watahitajika kusimama Rais Kibaki akiwasili, wakati wa sherehe ya kuapishwa, saluti ya mizinga 21 itakapopigwa nje ya uwanja na wimbo wa taifa utakapoimbwa kabla ya Rais Kibaki na rais mpya kuondoka uwanjani.
Siku hiyo, Kenyatta atapambwa kwa vifaa vya mamlaka ambavyo ni pamoja na Mkuu wa Nakshi (CGH), pia atapokea mkuki, ngao na katiba.
Zana hizo zinaashiria mamlaka; kwa mfano Katiba inasimamia Kenya na watu wake, mkuki unasimamia Amiri Jeshi Mkuu ilhali CGH ni heshima kubwa zaidi Kenya.
Wadau wa Mbeya wamelipongeza Jeshi la Polisi Mkoani hapa kutokana na juhudi za kupambana na uhalifu hususani kudhibiti mtandao wa majambazi sugu.
| Baadhi ya waandishi wa habari mkoa wa Mbeya wakimsikiliza Mwakisu |
JE VIONGOZI WA SERIKALI KATA YA ILEMBO MBEYA VIJIJINI MMEIONA BENDERA HII AU SIYO YA TAIFA LETU?
| HIVI NDIYO INAVYOONEKANA BENDERA HII SHULENI HAPO |
| MASKINI WANAFUNZI HAWA HAWAJAWAHIONA BENDERA MPYA WAMEZOEA KUONA BENDERA ILIYOCHANIKA TANGU WAANZA SHULE HIYO YA HAZINA |
Watuhumiwa 11 kizimbani
Mtuhumiwa namba moja wa mashtaka 24 ya kuua bila kukusudia, Raza Hussein
Ladha (kushoto) akipelekwa chini ya ulinzi wa polisi kuingia katika
chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara Radha Hussein Ladha wa jijini Dar es Salaam, Diwani katika Manispaa ya Kinondoni, Ibrahim Mohamed maarufu kama Kisoki (59) na wenzao 9, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 24 ya kuua bila ya kukusudia.
Katika kundi hilo pia wamo vigogo wa Manispaa
ya Ilala ambao ni Mhandisi Mkuu, Mhandisi Charles Salu (48), Mhandisi wa
Majengo Godluck Sylivester (35) Mbaga na Mkurugenzi Mkuu wa Mkaguzi wa
Majengo, Willibrod Wilbard (42).
Washtakiwa wengine ni Mhandisi Mohamed Swaburi
(61), Mhandisi Mshauri, Zonazea Oushoudada (60), Mkadiriaji Majenzi,
Vedasto Nziko (59), Msanifu Majengo, Michael Hema (59), Msajili Msaidizi
AQRB, Albert Mnuo na Ofisa Mkuu Mtekelezaji OQRB, Joseph Ringo.
Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu
Mkazi, Devotha Kisoka, Wakili wa Serikali, Tumain Kweka akisaidiana na
mawakili wenzake watano, alidai kuwa washtakiwa walifanya makosa kinyume
na kifungu cha 195 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16
iliyofanyiwa marekebisho 2002.
Kweka anasadiana na wenzake Benard Kongora, Ladslaus Komanya, Neema Haule, Joseph Maugo na Mutalemwa Kishenyi.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao
kwa pamoja Machi 29, mwaka huu katika Mtaa wa Indira Gandhi, Wilaya ya
Ilala waliwaua bila ya kukusudia Yusuph Mohamed, Kulwa Khalfan na Hamada
Mussa.
Mbali na watu hao, pia wanadaiwa kuwaua bila
ya kukusudia Kessy Manjapa, Khamis Mkomwa, Boniface Benard, Suhail Ally,
Salmani Akbar, Seleman Haji, Seleman Mtego, Sikudhani Mohamed, Ahmed
Milambo, Salum Mapunda, Suleiman Rashid na John Majewa.
Wengine ni Mussa Mnyamani, David Severin
Herman, William Joackim, Abdulrahman Mwiha, Emmanuel Christian, Mmanyi
Ngadula, Adivai Desiki, Emmanuel Greyson na Augustino Kasiri.
Washtakiwa
wote hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mashtaka yanayowakabili
Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza hadi Mahakama Kuu.
Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili wa
Kujitegemea, Jerome Msemwa waliiomba mahakama kutoa dhamana kwa wateja
wao kwa sababu mashtaka ya kuua bila ya kukusudia yanayowakabili
yanadhaminika.
Wakili wa Serikali, Kongora alipinga maombi
hayo, huku wakili mwenzake Komanya akisema kuwa wakati huu si wa kutoa
dhamana kwa kuzingatia mazingira ya tukio lililosababisha kuwepo kwa
kesi hiyo.
Kutokana na hoja hizo, Hakimu Kisoka
aliiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 16, mwaka huu atakapotoa uamuzi iwapo
washtakiwa wapate dhamana ama la.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ametangaza kiama dhidi ya
wamiliki wenye maghorofa yaliyojengwa kinyume cha utaratibu jijini Dar
es Salaam.
Akizungumza kwenye Ofisi ndogo ya Bunge, Profesa
Tibaijuka alisema kwa kuanzia angesaini hati ya kuamuru kubomolewa kwa
jengo lililokuwa karibu na lile lililoanguka wiki iliyopita na kuua
idadi kubwa ya watu.
Alimwonya mmiliki wa jengo hilo anatakiwa kufanya ubomoaji mara moja tena kwa gharama zake.
“Serikali ikibomoa jengo hilo ina maana
atatakiwa kulipia gharama za zoezi hilo,” alionya Profesa Tibaijuka,
ambaye aliapa kuanza leo ukaguzi wa maghorofa mbalimbali ya jijini Dar
es Salaam.
Mvutano kuhusu haki ya kuchinja wanyama wazua vurugu Tunduma
Tunduma. Vurugu kubwa zilizuka jana katika Mji wa Tunduma ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya, baada kutokea mvutano mkali kuhusu nani anayepaswa kuchinja mifugo baina ya waumini wa dini mbili; Waislamu na Wakristo.
Mamia ya polisi kutoka wilaya zinazouzunguka
Mji wa Tunduma walimwagwa na walilazimika kutumia mabomu ya machozi na
maji ya kuwasha ili kuwatawanya waandamanaji pia, kutuliza vurugu
zilizodumu kwa zaidi ya saa nne.
Vurugu hizo ambazo zinahatarisha amani, zimetokea siku tatu tu tangu Rais Jakaya Kikwete aonye kwamba kwamba vurugu zenye sura ya kidini ni hatari na zinaweza kuvuruga amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi nchini.
Mijadala kuhusu vurugu hizo ilitawala katika
mitandao ya kijamii ikiwamo facebook, Mabadiliko Forum na Jamii Forums
ambako watu mbalimbali walionyesha kukerwa nazo, huku wakiitaka Serikali
ichukue hatua za kudhibiti.
Kutokana na vurugu hizo zilizoanza saa 4:30
asubuhi, wakazi wa mji huo walijifungia ndani kwa kuhofia usalama wa
maisha yao, huku maduka na shughuli za biashara nazo zikifungwa.
Mwandishi
wa Mwananchi aliyekuwa katika eneo la tukio anaripoti kwamba katika
vurugu hizo, watu zaidi ya 35 wamekamatwa wakiwamo Diwani wa Kata ya
Tunduma Frank Mwakajoka na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Gidion Mwamafupa.
Habari zaidi zinasema barabara za mji huo
zilifungwa, umeme ulizimika baada ya moto kulipuka kwenye moja ya nguzo
za umeme. Pia mpaka wa Tanzania na Zambia ulifungwa kwa muda.
Magari ya abiria na yale ya usafirishaji
yaliyokuwa yakitoka na kuelekea Zambia, Dar es Salaam, Sumbawanga na
Mbeya Mjini pia yalikwama na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria.
Msikiti ulivunjwa na watu wawili akiwamo askari polisi walijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani
Athuman alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kwamba tukio hilo
limetokea wakati Serikali ikiwa kwenye mazungumzo na baadhi ya wahusika
katika mgogoro wakiwamo viongozi wa dini na wachinjaji wa nyama.
“Mgogoro wa kuchinja umedumu kwa siku tatu,
jana kamati ya ulinzi na usalama chini ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas
Kandoro ilikutana na baadhi ya viongozi wa dini na wadau wa kuchinja
nyama na kuna mambo matatu ambayo yalitolewa katika mkutano huo,”
alisema Diwani.
Alisema katika mkutano huo Kandoro aliagiza
kuwa wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki, ambacho
Serikali ngazi ya kitaifa inalishughulikia na kuwataka kuendelea na hali
uchinjaji kama ilivyokuwa awali na kila mmoja afanye kile anachoamini
katika dini yake wakati wa kula.
Hata hivyo, baadhi ya Wakristo waliafikia
lakini wengine hawakuafiki. Hivyo jana asubuhi walihamasisha maandamano
katika mji huo ambayo yalisababisha vurugu hizo.
“Pamoja na hayo yote uchunguzi wa kitaalamu
tumebaini kuwa vurugu hizo siyo za kidini, bali zimehusishwa siasa kwani
hata viongozi wa dini waliohusika ni baadhi siyo wote ambao
wanajishughulisha na suala hili,” alisema Diwani.
Alisema kwa upande mwingine vurugu hizo zinafanywa na baadhi ya vijana wenye nia ya kuzitumia kwa lengo la kufanya uporaji.
Maafa juu ya maafa, Dar 36 Arusha 20
Kile kilichodhaniwa kuwa kilele cha sikukuu ya pasaka, kimegeuka msiba baada ya wachimba kokoto 20 kufukiwa katika kifusi Jijini Arusha.
Hiyo ilikuwa ni kama ndimu katika kidonda kibichi, kwani ni ijumaa iliyopita tu wakati watu wakijiandaa kwa sikukuu ya Pasaka jengo la ghorofa 16 lilidondoka Jijini Dar es Salaam na kuua watu 36.
Vifo hivi vilivyotokea katika msimu wa sikukuu vimeweka idadi ya watu waliopoteza maisha kufikia 56 hivi, ndani ya siku nne tu.
Watu waliofukiwa na kifusi mkoani Arusha, walikuwa wakichimba kokoto katika eneo la Moshono.
Imeelezwa kuwa ni maiti 14 tu ndizo zilizoopolewa na watu wengine bado wanahofiwa kuwa ndani ya kifusi hicho.
Ilikuwa ni saa tano asubuhi, juzi, gema la kokoto liliporomoka kisha kuwafunika wote waliokuwamo ndani, sababu kubwa ikielezwa kuwa ni mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha mjini Arusha.
Vilevile magari mawili yaliyokuwa yamepaki pembeni kwa ajili ya kubeba mzigo huo yalizama ndani ya shimo hilo kubwa la kokoto.
Watu saba walikufa 1997
Inaelezwa kuwa hii ni mara ya pili kwa mgodi huu kuua watu kwani mwaka 1997 wachimbaji wa kokoto walifukiwa na saba kati yao walipoteza maisha.
Tukio la Dar
Mlinzi wa msikiti wa Shia, aliyeshuhudia kudondoka kwa ghorofa hilo amesema alianza kuona mashine ya zege ikianguka kutoka ghorofa ya 17 ambapo ujenzi wa sakafu ya ghorofa hiyo ulikuwa ukiendelea.
Mlinzi huyo, Athuman Salum Mnere anasema alisikia sauti ya kukatika kwa kitu, ghafla sauti kubwa ya maporomoko, kisha mashine ya zege na baada ya sekunde kadhaa, jengo lote likawa chini.
Anasema walionusurika walianza kuwaokoa watoto
waliokuwa wakicheza mpira katika uwanja wa ndani ya msikiti uliokaribu
na jengo hilo.
Aliwakanya watoto waliopoteza maisha
Anasema aliwaambia watoto waliokuwa wakicheza mpira katika uwanja huo waende nyumbani lakini hawakusikia.
Hata kabla ya dakika tano kwisha, jengo hilo liliporomoka na wale wanne waliokuwa wamekaa katika benchi walifunikwa na jengo.
“Wengine waliumia vibaya, ndiyo hao walioko hospitali. Wale waliokuwa kwenye benchi walikufa palepale”anasema.
Shughuli za uokoaji zilimalizika juzi na eneo lilipokuwepo ghorofa hilo kubaki mithili ya shimo.
Ajifungua mtoto kwa mshtuko
Sumbawanga. Katika hali isiyokuwa ya kawaida mwanamke, mkazi wa kitongoji cha Chemka ,Kata ya Chanji Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa amejikuta akipata uchungu wa ghafla na kujifungua mtoto wa kiume chooni, nyumbani kwake kutokana na mshtuko alioupata baada ya kutolewa kwa nguvu katika nyumba hiyo na dalali wa mahakama.
Katika tukio hilo ambalo mwanamke huyo (jina linahifadhiwa) alipata mshtuko mkubwa baada ya dalali wa mahakama kufika nyumbani kwake na kuanza kutoa nje vyombo vyake vyote kwa madai kuwa nyumba hiyo ilikuwa na mgogoro.
Kwa mujibu wa mwanamke huyo baada ya dalali kuwatoa kwa nguvu katika nyumba hiyo kwa kutoa nyombo vyao vyote nje na kufunga nyumba hiyo kwa makufuli baada ya kuhaha na kukosa sehemu ya kuhifadhi vyombo hivyo yeye na familia yake walilazimika kulala nje ya nyumba hiyo na kunyeshewa na mvua usiku kucha.
Alisema baada ya kutaabika usiku kucha kwa kunyeshewa na mvua ilipofika saa tano asubuhi alibanwa na uchungu mkali alipolazimika kukimbilia chooni na kujifungua mtoto wa kiume akiwa hai.
Nauli ni Kiama: Sumatra yapandisha nauli za daladala, mabasi ya mikoani, treni na meli
Abiria wakigombania kuingia katika daladala.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imepandisha nauli za daladala, mabasi ya kwenda mikoani, usafiri wa reli na tozo za majini kuanzia Aprili 12, mwaka huu.Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Ahmad Kilima alisema jana kuwa nauli za daladala zimeongezeka kwa asilimia 24.46 kwa kuzingatia maoni ya wadau na gharama za uendeshaji.
Kwa upande wa usafiri wa daladala nauli
zimepanda kwa umbali tofauti kutoka Sh300 hadi 400, Sh350 hadi 450,
Sh500 hadi 600, Sh650 – 750 na kwa wanafunzi kutoka Sh150 hadi 200
katika sehemu yoyote watakayokwenda.
Nauli za usafiri wa mabasi makubwa ya masafa
marefu nauli hizo zimeongezeka kwa viwango tofauti. Mathalan kwa basi la
kawaida kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya ni Sh30,700, njia ya vumbi
kutoka Kigoma hadi Sumbawanga Sh25,400 na basi la hadhi ya kati (Semi
Luxury) kati ya Dar na Mwanza ni Sh61,400, wakati basi la hadhi ya juu
(Luxury) kati ya Dar na Arusha ni Sh 36,000.
Kilima alisema: “Kuanzia Aprili 12 mwaka huu,
kati ya kilometa 0 hadi 10, nauli ya daladala itakuwa Sh400 badala ya
Sh300 zinazolipwa hivi sasa.
“Pia nauli za mabasi ya kwenda mikoani
zimeongezeka kwa asilimia 20.3 kwa mabasi ya kawaida, mabasi ya kati kwa
asilimia 16.9 na mabasi ya daraja la juu kwa asilimia 13.2,” alisema.
Kilima alisema nauli za mabasi ya mikoani
zimepanda kutoka Sh30.67 hadi Sh36.89 kwa kilometa kwa mabasi ya daraja
la kawaida katika njia za lami.
Kwa upande wa mabasi ya kawaida kwa
njia ya vumbi imepanda kutoka Sh37.72 hadi Sh 46.11 kwa kilometa na
kwamba mabasi ya hadhi ya kati, nauli zimepanda kutoka Sh45.53 hadi Sh
53.22 kwa kilometa.
Alisema mabasi ya hadhi ya juu nauli zimepanda kutoka Sh51.64 hadi Sh58.47 kwa kilometa.
“Kupanda
kwa nauli kunatakiwa kwenda sambamba na huduma bora na kwamba Sumatra
imepiga marufuku kutumia wapigadebe kuuza tiketi za safari”alisema.
Usafiri wa Reli
Katika
uamuzi huo, usafiri wa reli pia umepanda ambapo daraja la kwanza Dar es
Salaam hadi Morogoro, nauli mpya na ya zamani katika mabano ni
Sh21,100, (Sh16,852), Dar hadi Dodoma Sh34,700, (Sh27,788), Dar es
Salaam-Tabora Sh54,800, (Sh43,859).
Dar es Salaam-Isaka Sh62,100,
(Sh49,662), Dar- Shinyanga Sh65,300 (Sh52,229) Dar –Mwanza Sh74,800 (Sh
59,818), Dar- Kigoma Sh75,700, (Sh60,599)
Daraja la pili, Dar es Salaam-Morogoro
Sh16,600, (Sh13,280), Dar es Salaam-Dodoma Sh26,400 (Sh 21,092), Dar es
Salaam-Tabora Sh40,500 (Sh 32,364), Dar es Salaam-Isaka Sh45,800,
(Sh36,605), Dar es Salaam-Shinyanga Sh48,000 (Sh38,390), Dar es Salaam-
Mwanza Sh54,700 (Sh43,747), Dar es Salaam-Kigoma Sh55,400 (Sh44,305).
Daraja la tatu, dar es Salaam-Morogoro Sh8,800
(Sh6,138), Dar es Salaam-Dodoma Sh13,500 (Sh9,374), Dar es
Salaam-Tabora 20,400 (Sh14,173), Dar es Salaam-Isaka Sh22,800
(Sh15,847), Dar es Salaam –Shinyanga Sh24,000 (Sh16,628), Dar es
Salaam-Mwanza Sh27,200 (Sh18,860), Dar es Salaam- Kigoma Sh27,500
(Sh19,084).
Akizungumzia tozo za majini, Kaimu Mkurugenzi
huyo alisema mamlaka hiyo imeridhia ongezeko la tozo la asilimia 34.3
kwa vyombo vinavyotumia bandari za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TPA).
Alisema awali TPA walipendekeza tozo hizo
kuongezeka kati ya asilimia saba hadi 400 kulingana na aina ya huduma
zinazotolewa kwa meli zinazotumia bandari za mamlaka hiyo.
Subscribe to:
Posts (Atom)