Waandishi wafa ajalini
Mwandishi wa gazeti la NIPASHE wilayani Handeni, Sonyo Mwankale.
Mwandishi wa gazeti la NIPASHE wilayani Handeni, Sonyo Mwankale, ni miongoni mwa watu watatu waliofariki dunia wakiwa kwenye msafara wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, baada ya gari walilokuwa wakisafiria la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuacha njia na kupinduka.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 3:30 katika kijiji cha Misima wakati wakielekea katika kijiji cha Nzundu kwenye zoezi la upandaji miti lililokuwa likifanyika kiwilaya kijijini hapo.
Aliwataja waliofariki papo hapo baada ya ajali kutokea kuwa ni Hamis Bwanga ambaye ni mwandishi wa gazeti la Uhuru na Mzalendo na Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Handeni, Mariamu Hassani.
Rweyemamu alisema mwandishi wa gazeti la NIPASHE, Sonyo Mwankale (Hussein Semdoe), alifariki dunia akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni akipatiwa matibabu.
Katika ajali hiyo, Mwankale ambaye alijeruhiwa vibaya sehemu za kichwani, baada ya kupelekwa hospitalini hapo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni alimuomba helkopita Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Said Mwema, kuwachukua majeruhi hao, lakini kabla haijafika mwandishi huyo akafariki dunia.
Wengine waliyojeruhiwa katika ajali hiyo na kulazwa kwenye hospitali hiyo ni Mshauri wa Mgambo Wilaya, Athanas Paulo, Ofisa Misitu Wilaya, Natorin Mloe na dereva wa gari hilo lenye namba za usajili STK 4673, Mlawa Makata.
Awali, taarifa ambazo NIPASHE ilizipata zilieleza kuwa tukio hilo limetokea wakati msafara huo ukitokea Mjini Handeni kuelekea Misima ambako Mkuu huyo wa Wilaya alikwenda kuhamasisha upandaji wa miti.
Habari zilieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni gari hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Handeni, kupasuka gurudumu la nyuma na kuacha njia kisha kupinduka. Hata hivyo Mkurugenzi huyo hakuwamo katika gari hiyo.
Wakizungumzia ajali hiyo, kwenye eneo la tukio, mashuhuda hao alisema watu hao walipoteza maisha muda mfupi mara baada ya tukio hilo na kwamba wananchi waliyojitokeza kutoa msaada walishuhudia hali za majeruhi hao zikiwa mbaya.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Rweyemamu akizungumzia tukio hilo alisema kifo cha Afisa Uhamiaji huyo ni pigo kwa wilayani kwani ni hivi karibuni alisaidia kukamatwa kwa wahamiaji haramu 74.
Ofisa misitu Wilaya ya Handeni, Mloe akizungumzia jinsi ajali hiyo ilivyotokea akiwa katika hospitali ya Wilaya Handeni alikolazwa, alisema wakiwa safarini mbele alijitokeza mwendesha pikipiki (bodaboda) akitaka kujaribu kuwapita.
Alisema dereva wa gari lililobeba alimkwepa dereva wa bodaboda na kusababisha gari kuyumba na kusababisha kupinduka upande wa pili wa barabara na hivyo kusababisha kifo cha Afisa Uhamiaji na mwandishi wa gazeti la Uhuru papo hapo.
Chadema yatishia kujitoa kwenye mchakato wa Katiba
Msemaji wa kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHadema), kimesema hakitashiriki katika mchakato wa Katiba Mpya endapo serikali haitapeleka bungeni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ili kufuta vifungu mbalimbali kikiwamo kinachowaruhusu wajumbe wa Bunge Maalum kutoka Zanzibar kushiriki katika mijadala ya mambo yasiyo ya muungano.
Chama hicho kinataka marekebisho hayo kupelekwa bungeni kabla ya mwisho wa Aprili na isipofanya hivyo kitajitoa katika ushiriki wake katika mchakato huo.
Hayo yalisemwa jana na Msemaji wa kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, alipokuwa akitoa maoni ya kambi hiyo kuhusiana na hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2013/2014.
Pia Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai, alisema chama chake kitajitoa katika ushiriki ikiwa serikali haitafuta uteuzi wa wajumbe wa mabaraza ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za kata.
Alisema wajumbe hao wafutwe na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC.
Pia alisema wanataka kufutwa kwa vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya Rais kuitisha tena Bunge Maalum la Katiba baada ya Bunge hilo kuwa limeshapitisha Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya marekebisho katika Rasimu kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni.
Aidha, alisema wanataka kufutwa kwa vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya kikatiba na ya kisheria yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendesha na kusimamia kura ya maoni.
Alisema Tume hiyo imeonekana kutoa taarifa kwa Rais Jakaya Kikwete na kutangaza wazi wazi kwamba haiwajibiki kwa Bunge kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.
“Zaidi ya kumtuma Naibu Katibu wa Tume, viongozi wa Tume kama vile Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume wamekataa kuhudhuria vikao vya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ili kuieleza Kamati juu ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Nchi,” alisema Mbowe.
Kwa upande wa wanafunzi waliofeli mitihani ya kidato cha nne mwaka jana, Mbowe alisema kambi hiyo inaitaka Serikali kueleza bungeni inampango gani wa kupunguza idadi hii ya watoto wanaobaki mitaani bila shughuli rasmi ya kufanya.
Uhuru: Nitatumia siku 100 kutimiza ahadi
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akiwa ameongozana na mlinzi wake dakika
chache baada ya kuapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo jana.
Ataanza kwa ahadi ya matibabu bure kwa wanawake wanaofuata huduma za uzazi
Nairobi. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema kwamba atatumia siku 100 tu kutekeleza ahadi zake zote ambazo ameziahidi kipindi cha kampeni.
Alisema kwanza atatumia miezi mitatu tu kuondoa
kabisa malipo ya Afya ya uzazi kwa kina mama katika zahanati zote na
hospitali za umma.
Alisema kwamba Serikali yake itatoa kiasi cha Sh6 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mfuko wa vijana na wanawake .
Pia alikumbushia ahadi ya kutoa ‘laptop’ kwa wanafunzi wote wa shule za msingi watakaojiunga na shule za serikali mwakani.
Uhuru alisema kwamba kutekeleza ahadi hizo ni katika suala la utekelezaji wa sera na misimamo wa Muungano wa Jubilee.
“Mimi nina fahari kubwa kuwajali wanyonge
waliokubali kunipa nafasi hii ya uongozi na nimekubali kulivaa vazi hili
la uongozi hivyo nitasimamia sera za Jubilee kama tulivyoahidi Wakenya
wakati wa kampeni,’’ alisema Uhuru.
Aliongeza kwamba yupo kwa ajili ya Wakenya wote waliompigia kura na hata wale waliowapigia wapinzani wake.
Uhuru alisema atawasaidia Wakenya pamoja na taifa zima kuelekea katika mizizi imara ya kiutajiri kwa njia ya amani, hali ambayo alisema inawezekana ikafanikiwa kwa kiasi kikubwa baadaye.
Naye mtaalamu wa Uhusiano wa Kimataifa, Profesa
Munene Macharia alipokuwa akifanya mahojiano na Kituo cha Habari cha
Xinhua ,alisema kwamba kuchaguliwa kwa Rais Uhuru Kenyatta, kuna
uwezekano mkubwa kubadilika kwa sera za kiuchumi.
Alisema kwamba Rais
huyo ambaye awali alikuwa katika Baraza la Mawaziri la awamu
iliyopita akiwa Waziri wa Fedha anatakiwa kujenga uhusiano wa karibu na
mataifa ya nje ili aweze kubadili sera za kiuchumi.
Pia alimtaka waziri huyo kuangalia suala la kuimarisha uhusiano wa kibiashara na nchi jirani za Afrika na Afrika Mashariki.
Profesa Macharia alisema baada ya kuitumikia Serikali ya Kibaki, Kenyatta ana uwezo mkubwa wa kudumisha sera hiyo ya kiuchumi.
“Lengo
la msingi kwa Serikali ya Kenyatta inatakiwa kuimarisha mahusiano yake
na Jumuiya ya Afrika Mashariki nchi wanachama (EAC) Kama majirani wa
karibu,” Macharia alibainisha.
Wakati huohuo Rais mstaafu Mwai
Kibaki aliwahakikishia raia wa Wakenya kuwa, wapo katika mikono salama
baada ya yeye kustaafu rasmi juzi.
Alisema kwamba yeye anaanza maisha yake ya kustaafu, hivyo raia wote wa nchi hiyo wanatakiwa kufahamu kwamba wanabaki katika mikono salama wasiwe hivyo wasiwe na hofu yoyote ile.
Sumatra yakamata daladala 75 kwa kupandisha nauli
Dar es Salaam.Wakati nauli mpya zikianza kutumika leo huku Serikali ikizibariki, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) imekamata magari ya kubeba abiria (daladala) 75 katika operesheni maalum iliyoanza mwanzoni mwa wiki hii mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Uamuzi wa kukamata magari hayo umekuja baada
ya kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya abiria ya madai ya kutozwa nauli
kubwa kuliko iliyotangazwa na Serikali kuwa zianze kutumika leo.
Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe alisema
jana mjini Dodoma kuwa ongezeko la viwango vipya vya nauli si tatizo,
la muhimu ni wahusika kufuata vigezo.
Akizungumza na gazeti hili Dar
es Salaam jana, Ofisa Mfawidhi Kanda ya Mashariki wa Sumatra, Conrad
Shio alisema kuwa,daladala zilizokamatwa zilikuwa na makosa mbalimbali
yakiwemo kukatisha ruti, kutoza nauli, kuiba ruti na kufanya biashara ya
kusafirisha abiria bila ya kuwa na kibali.
Alisema kutokana na hali hiyo wamiliki wa
daladala zilizokamatwa wametakiwa kwenda na mikataba ya madereva wapya,
ili wale wa zamani waweze kukaguliwa na Jeshi la Polisi Tanzania juu ya
uhalali wa leseni zao.
“Tumepata malalamiko ya daladala 105 ambazo
zimekuwa zikivunja sheria ya usafiri barabarani, ambapo daladala 75
tayari tumezikamata,” alisema Shio.
Aliongeza kati ya hizo, daladala
36 zilikatisha ruti, wakati 18 ziliiba ruti na 21 zilitoza nauli kubwa,
jambo ambalo limewafanya wazichukulie hatua.
Alisema kuna nyingine zimebeba abiria bila ya kuwa na kibali, ambapo wamiliki wake wamechukuliwa hatua za kisheria.
Alisema kutokana na hali hiyo, wamiliki wa
daladala hizo wametakiwa kulipa faini na kwenda na mikataba ya madereva
wapya ili madereva waliofanya makosa wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa
ni pamoja na kuwafikisha mahakamani. Alisema daladala ambazo zilikuwa
zinafanya kazi bila ya kibali hasa nyakati za usiku katika baadhi ya
maeneo zimepelekwa kwenye yadi ya Serikali ili wamiliki wake waweze
kuchukuliwa hatua za kisheria kwa sababu ni kosa kubeba abiria wakati
huna kibali cha usafirishaji.
Alisema kuwa, ili kupunguza ukubwa wa tatizo, wamelifanya zoezi hilo kuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kuwataka madereva wa vyombo vya usafiri kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ili kupunguza malalamiko. Alisema kutokana na hali hiyo Sumatra itaendelea kukamata magari ambayo yataonekana yanaendelea kuvunja sheria kwa makusudi.
CAG abaini ubadhirifu mkubwa
dhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh
(katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu
ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha ulioishia 30 Juni, 2012
zilizowasilishwa bungeni jana mjini Dodoma. Kushoto ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na kulia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Rajab
Mbarouk Mohammed.
Dodoma. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilitolewa jana ikiweka bayana madudu mbalimbali ya ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma, udhaifu katika usimamizi wa mikataba na Serikali kushindwa kutoa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Moja ya matatizo yaliyojitokeza ni Wizara ya
Nishati na Madini kushindwa kukusanya nyongeza ya mrabaha wa madini
baada ya kuongezwa kutoka asilimia tatu hadi nne.
Akizungumza na
waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha ripoti hiyo ya mwaka wa
fedha unaoishia Juni 30, 2012, CAG Ludovick Utouh alisema pamoja na
kuwapo mafanikio ya kimahesabu ukilinganisha na miaka iliyopita, bado
kuna mambo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.
Alilishauri Bunge kuangalia upya suala la
kuivunja Kamati ya Hesabu ya Mashirika ya Umma (POAC) na kuunganisha
shughuli zake na Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na mkakati wa
ofisi kufanya ukaguzi wa misamaha ya kodi ambayo imeongezeka kuangalia
uhalali wake.
Hata hivyo, Utouh alikataa katakata kuzungumzia deni la taifa ambalo pia limeongezeka akisema “amefanya hivyo makusudi”.
Bajeti na miradi ya maendeleo
Kwa mujibu wa
CAG, imebainika kuwa kuna tatizo kubwa la Serikali kushindwa kutoa kwa
halmashauri mbalimbali fedha za maendeleo kama zilivyopitishwa na Bunge.
Alisema
Bunge lilipitisha vifungu vya fedha za maendeleo vyenye jumla ya
Sh595,064,422,505 katika halmashauri 113, lakini fedha zilizopokewa ni
Sh345,568,067,477 sawa na asilimia 42 tu, hivyo kufanya upungufu wa
Sh249,496,355,027.
Licha ya fedha hizo kutokutolewa zote, kiwango
kilichotolewa hakikutumika chote kutokana na kucheleweshwa. “Hadi
mwishoni mwa mwaka, kulikuwa na baki ya fedha za miradi ya maendeleo
kiasi cha Sh188,405,740,589 ambayo ni sawa na asilimia 55 ya fedha
zilizotolewa na Serikali,” alisema Otouh na kuongeza: “Tunashauri bajeti
iendane na shughuli zilizopangwa, kwa sasa utaratibu wa bajeti haujawa
mzuri.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hata fedha za Mfuko
wa Maendeleo ya Jimbo zinazotolewa kwa wabunge hazikutumika zote.
Sh2,561,882,820 zilizotengwa kwa ajili ya sampuli ya majimbo 69
zilibaki.
“Sababu ya kutokutumika ni ama halmashauri
hazina utaratibu maalumu wa kutumia fedha hizo au Serikali kutoa fedha
hizo mwishoni mwa mwaka,” alisema.
Udhaifu katika usimamizi wa mikataba ya madini
Katika
ripoti hiyo, CAG alisema Wizara ya Nishati na Madini ilishindwa
kukusanya Dola za Marekani 12,634,354 (sawa na Sh19,709,593,191)
zilizotokana na ongezeko la mirabaha ya madini, baada ya mabadiliko ya
Sheria ya Madini.
Katika iliyokuwa Wizara ya Miundombinu,
ukaguzi huo umebaini kuwa madeni yake ya mwaka 2010/11 yanayofikia Sh253
bilioni yamelipwa kwa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya
ujenzi wa barabara mwaka uliofuata wa 2011/12.
Katika kipindi hicho, CAG alisema dhamana za
Serikali za jumla ya Sh578.4 bilioni zilikuwa zimeisha muda wake na
hivyo kuifanya Serikali ikiwa mdhamini kuwajibika kulipa deni hilo.
Vilevile, CAG ameona kuna kodi inayopotea
kutoka sekta isiyo rasmi, hivyo kuishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kuwatumia vizuri makatibu kata kuwatambua walipakodi kama vile
wamiliki wa kumbi za harusi na mikutano.
Alishauri kuwa TRA ianze kukusanya kodi kwenye huduma za
kuhamisha fedha kwa njia ya simu za kiganjani maarufu kama M-Pesa, Tigo
Pesa, Airtel Money na nyinginezo.
Alisema kampuni hizo zinatakiwa
kulipa kodi ya zuio ya malipo ya kamisheni inayolipwa kwa wanaofanya
biashara hiyo na kodi hiyo ipunguzwe kutoka katika kodi ya mwisho
itakayotakiwa kulipwa na kampuni za simu.
Misamaha ya kodi
Ripoti hiyo ya CAG
ilishauri mikataba ya madini ijadiliwe na Kamati ya Bunge inayohusika na
kutoa mapendekezo kabla haijasainiwa na hati za misamaha ya kodi
ziwekwe bayana kuwa ni msamaha wa muda gani, inaanza na kumalizika lini.
Alishauri
pia vipengele vyote vya misamaha ya kodi vipitiwe na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kwa ajili ya kushauri kabla ya kusainiwa na upande husika.
Katika mwaka 2013/14, CAG ameamua kuanza
kuikagua misamaha yote ya kodi kwa madhumuni ya kuangalia manufaa yake
kwa uchumi wa taifa, kwa kuwa misamaha hiyo pia ni fedha za Serikali.
Hesabu za TRA zimeonyesha makusanyo ya kiasi cha Sh6,703,229,704,887
ikilinganishwa na makadirio ya Sh6,456,832,630,000 na kusababisha
makusanyo ya ziada ya Sh 246,397,074,887 sawa na asilimia nne ya
makadirio.
Taarifa ya CAG inaonyesha mwelekeo wa misamaha
ya kodi unaonyesha ongezeko kwa kiasi cha Sh789,883,259,827 sawa na
asilimia 78 kutoka kiasi cha Sh1,016,320,300,000 kilichoripotiwa mwaka
2010/2011 hadi Sh1,806,203,559,827 kwa mwaka 2011/2012.
Kuvunjwa kwa POAC
Utouh alisema kitendo cha
kuvunjwa kwa POAC na kuunganisha majukumu yake na PAC ni bahati mbaya
kwa kuwa sababu za kuanzishwa kwake bado zipo hai kama ilivyokuwa wakati
inaanzishwa na kwamba uamuzi huo hautakidhi matarajio ya wadau.
“Kamati ya PAC itazidiwa na ukubwa wa
majukumu, hivyo ofisi bado inashauri kuona uwezekano wa kurudisha kamati
hii hata kama itakuwa na haja ya kubadilisha jina lake,” alisema.
Spika Anne Makinda aliamua kuvunja kamati zote za Bunge kwa kuunda mpya na kuvunja nyingine.
POAC
iliyokuwa chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
iliunganishwa na ile ya PAC, ambayo pia inaongozwa na mbunge huyo.
“Kamati
ya PAC itazidiwa na ukubwa wa majukumu, hivyo ofisi bado inashauri
kuona uwezekano wa kurudisha kamati hii hata kama itakuwa na haja ya
kubadilisha jina lake,”
Wasomi nchini wasema rasilimali zinaporwa
Waziri wa Madini na Nishati, Profesa Muhongo
Dar es Salaam. Wasomi kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani wameilaumu Serikali ya Tanzania kwa kushindwa kulinda rasilimali zake kwa manufaa ya Watanzania na badala yake imekalia sera za kikoloni zinazochochea uporaji wa rasilimali hizo.
Wakizungumza katika tamasha la tano
lililoandaliwa na Kigoda cha kitaaluma cha Mwalimu Nyerere katika Ukumbi
wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana, wasomi hao walisema
Serikali imekumbatia sera mbovu zinazoruhusu uporaji huo.
Akichambua ripoti za ‘A golden Opportunity;
How Tanzania is failing to benefit from gold mining ya mwaka 2008 na The
One Billion Dollar Question; How can Tanzania stop losing so much tax
revenue’ ya mwaka 2012, Profesa John Saul kutoka Chuo Kikuu cha York cha
Toronto, Canada ameitaja Kampuni ya African Barrick Gold kuipunja
Tanzania katika mgawo wa madini.
“Kampuni ya African Barrick Gold ni adui wa
Tanzania, ripoti hizi ukizisoma zinaonyesha uporaji wa rasilimali ya
madini. Hata viongozi wa dini walishatembelea migodi hiyo wakajionea,”
alisema Profesa Saul akiwa na nyaraka za ripoti hizo.
Profesa Saul aliyewahi kufundisha UDSM kati ya
mwaka 1965 hadi mwaka 1972, aliilaumu Serikali ya Tanzania kwa
kushirikiana na wawekezaji wanaopora rasilimali za Tanzania.
“Tuliwahi kumtuma mtu wetu kuchunguza uporaji
wa rasilimali, Serikali ikamfutia kibali cha kuishi nchini,” alidai
Profesa Saul na kuongeza: “Kushindwa kukusanya kodi maana yake fedha
kidogo ndiyo inakwenda kwenye shughuli za maendeleo. Inakadiriwa kuwa
Tanzania hupoteza mapato yatokanayo na kodi kati ya Sh1.35 hadi 2.05
trilioni kwa mwaka.”
Akijibu tuhuma hizo, Waziri wa Madini na
Nishati, Profesa Muhongo alisema Tanzania haiwezi kubakia kuwa taifa la
kulaumiana bali watu wanatakiwa kufanya vitendo. “Profesa wa fani ipi?
Sidhani kama analo jipya lolote kwani huo ndiyo wimbo wake. Sijui kama
hapo ndiyo tamati yake?”
Mkurugenzi wa African Barrick Gold, Deo Mwanyika alizipinga ripoti hizo... “Huo siyo ukweli.
Ni upotoshaji mkubwa. Huyo Profesa anatumia ripoti ya kiharakati ambayo siyo sahihi. Mbaya zaidi hiyo ripoti kwenye mambo ya kodi iliegemea zaidi kwenye kazi ya Alex Stewart Asseyar Report (ASA).”
Alisema kampuni hiyo (ASA), haikuaminika na
Serikali kutokana na kutokuwa wazi kiasi cha kufikishwa mahakamani huku
Bunge likikataa mkataba wake usirudiwe.
“Kama mtu anasema tumeipunja
Serikali, kuna mamlaka moja tu ya kuyasema hayo, nayo ni TRA (Mamlaka ya
Mapato Tanzania) yenye mamlaka kisheria,” alisema Mwanyika.
Malalamiko haya yamekuja siku chache baada ya
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kudai kuwa Serikali inakosa
Dola 885 milioni (Sh1.5 trilioni) kutokana na kampuni za madini kukwepa
kodi. Akihutubia mkutano wa hadhara huko Shelui mkoani Singida, Zitto
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu ya Bunge, alizituhumu
kampuni hizo kuwa zinatumia mwanya wa kutoa mchanganuo wa ununuzi,
ambayo siyo wa kweli ili kukwepa kodi.
Awali, akitoa mada ya Miaka 50 ya Uhuru wa
Afrika, Profesa wa Maendeleo ya Afrika katika Shule ya Uchumi ya
Uingereza, Thandika Mkandawire alisema Afrika bado haijajikomboa katika
miaka yote hiyo.
Alitaja changamoto nne zilizoikabili Afrika
baada ya kupata uhuru kuwa ni ubinafsi uliosababisha vita vya wenyewe
kwa wenyewe, ukoloni mamboleo, umaskini na mgawanyiko wa matabaka ya
walionacho na wasionacho.
Serikali yarudisha viboko shuleni
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
Mpoki Bukuku, Mwananchi
Serikali imesema itarudisha adhabu ya viboko kwa wanafunzi shuleni ili kujenga nidhamu na kujituma.Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akizindua tovuti ya www.shledirect.co.tz inayowezesha wanafunzi kujisomea kwa njia ya mtandao, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo ilisema kuondolewa kwa adhabu ya viboko shuleni kumewafanya wanafunzi wengi kukosa nidhamu na wakati mwingine kujifanyia mambo kienyeji.
“Wasipotandikwa mambo hayaendi, nilipokuwa
mwalimu mkuu nilikuwa nawatandika kweli ndiyo maana shule yangu ilikuwa
ikiongoza Mkoa wa Mbeya hivihivi hawaendi...” alisema huku akishangiliwa
na wageni waalikwa.
Alisema watoto wa siku hizi wamekuwa wakitumia
vibaya teknolojia ambayo ingeweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika
masomo yao... “Tovuti kama hiyo ingewasaidia kwa masomo, lakini wao
wanakimbilia kwenye facebook na mambo mengine yasiyofaa.”
Aliyalaumu mashirika yasiyo ya kiserikali na
haki za binadamu ambayo yamekuwa yakipigania kuondolewa kwa adhabu hiyo
shuleni na kusababisha kushuka kwa nidhamu kwa kiasi kikubwa.
Kadhalika alisema Serikali imepiga marufuku
matumizi ya simu za mikononi kwa sababu baadhi ya wanafunzi wamekuwa
wakizitumia vibaya jambo ambalo linawarudisha nyuma kimasomo.
“Simu tunazipiga marufuku, mwalimu akimkuta mwanafunzi na simu amnyang’anye ndizo zinatuharibia taifa letu.”
Aliwapongeza wabunifu wa mtandao huo akisema ni wazalendo kwani wamekuwa msaada katika jitihada za Serikali kukuza elimu nchini.
“Watu wanapiga kelele Mulugo na Kawambwa
wajiuzulu, hata tukijiuzulu haitasaidia, bali kila Mtanzania atoe
mchango wake katika elimu ili kuweza kuiendeleza.”
Mwanzilishi wa
tovuti hiyo, Faraja Nyalandu alisema itakuwa na manufaa kwa wanafunzi wa
Tanzania kwani masomo yanayotolewa yanaandaliwa na walimu wazoefu wenye
shahada hivyo wanafunzi watakapoitumia watapata manufaa makubwa.
Maoni ya wadau
Akizungumzia
hatua hiyo ya Serikali, Waziri Kivuli wa Elimu Mafunzo ya Ufundi, Suzan
Lyimo aliitaka iache kuangalia mambo madogo ambayo yanachangia kwa
kiasi kidogo tu kudorora kwa elimu na kuacha mambo makubwa.
“Kuna mambo makubwa zaidi yaliyotufikisha hapa
tulipo, hii ni sawa na kushughulika na matawi na kuacha mizizi. Lazima
tuangalie suala hili kwa upana zaidi, kuna ripoti nyingi na nzito
hazijafanyiwa kazi mpaka sasa badala yake Serikali inaibuka na kuanza
kutangaza vitu vidogo kama hivyo, wafanyie kazi kwanza ripoti ambazo
zilitumia pesa nyingi za walipakodi kwani nyingi zina mapendekezo
mazuri.”
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mpwapwa, Rukonge Mwero alisema uzuri wa adhabu ya viboko ni kwamba haipotezi muda”
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo Bisimba alisema adhabu ya viboko haina
maana katika kipindi hiki akisema wanafunzi wanapaswa kupewa adhabu
ambazo zinawafundisha kama zile za kufanya usafi na kazi mbalimbali.
“Viboko havifundishi zaidi ya kumpatia
mwanafunzi maumivu na kusababisha aichukie shule. Waelimishwe kwa
kuelekezwa lakini wakiendelea kukiuka, wapewe adhabu za kufanya kazi
mbalimbali.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT),
Gratian Mukoba alisema walimu hawapati faida yoyote kuwachapa au
kutowachapa viboko wanafunzi.
“Hawa viongozi kila kukicha wanazungumza mambo yasiyo na maana, badala ya kuzungumzia masilahi ya walimu wanazungumza kuhusu viboko, hatuelewi wakiamka kesho watasema nini,” alisema Mukoba.
Chadema kuwasha moto bungeni, ni kuhusu wanachodai 'utendaji usiofaa' wa Bunge
Dar es Salaam. Wakati Bunge la 11 la Bajeti kwa mwaka huu likianza kesho, Kamati Kuu ya Chadema imesema itatumia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kulibana Bunge kuhusu utendaji usiofuata Kanuni za Bunge unaofanywa na Spika na wasaidizi wake.
Pia wabunge hao wameitaka Serikali kuweka wazi mikataba iliyoingia hivi karibuni na Serikali ya China ili wananchi waweze kufahamu kilichomo vinginevyo watatumia kambi hiyo kuwabana wahusika.
Katika kikao cha 10 kilichomalizika Februari 8, mwaka huu mjini Dodoma, Mnadhimu wa kambi hiyo, Tundu Lissu alisema kuwa wanaandaa hoja za kumng’oa Spika na Naibu wake, Job Ndugai kwa kile walichodai kukiuka kanuni mbalimbali za Bunge.
Kambi ya upinzani ilikuwa ikilalamika kuondolewa kwa hoja binafsi za baadhi ya wabunge wao ikiwemo ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Maji), James Mbatia (Mitalaa ya Elimu) na Joshua Nassari, ambaye hoja yake ilihusu utendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda wakati akiahirisha kikao cha 10, alisema kuwa hoja binafsi zitakuja tena katika kikao cha 11 na wenye hoja watazifufua.
Jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema Kamati Kuu ilibaini kwamba matukio yaliyotokea katika kikao 10 yalitokana na meza ya spika kutofuata kanuni.
“Tumeamua kwamba Kambi ya Upinzani Bungeni itashughulikia tatizo hili la upindishwaji wa kanuni za Bunge ili wahusika wabanwe kwa vitendo wanavyovifanya,” alisema.
Alisema kambi hiyo itafanya hivyo kwa kufuata sheria na miongozo ambayo inawabana watendaji hao wa Bunge ili waweze kuwajibishwa kwa vitendo vyao.
Akizungumzia mikataba, Mnyika alisema kamati hiyo ina wasiwasi kuhusu mikataba 17 iliyoingiwa na Serikali za Tanzania na China na kutaka iwekwe hadharani.
Baadhi ya mikataba iliyotiwa saini ni katika kilimo, sekta ya afya, miundombinu ikiwamo mkataba wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani, ujenzi wa Reli ya Kati na ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), kwenda maeneo mbalimbali nchini hali itakayorahisisha usafirishaji wa mizigo.
Mikataba mingine ni uboreshaji wa sekta ya viwanda, kilimo hasa cha tumbaku na kulipatia Shirika la Utangazaji Tanzania zana za kufanyia kazi.
“Kamati Kuu inaitaka Serikali kuweka wazi mikataba hiyo vinginevyo watataka ufafanuzi katika kikao cha Bunge la Bajeti kinachotarajia kuanza rasmi kesho.
Kuporomoka kwa maghorofa
Mnyika alisema jopo la wanasheria wa chama hicho, wanafanya uchunguzi wa kuangalia maghorofa yaliyowahi kuanguka na hatua zilizowahi kuchukuliwa.
Alisema ingawa kuna watu ambao wamekuwa wakifikishwa mahakamani, lakini vigogo wengi wamekuwa hawawajibishwi kwa matukio yanayotokea.
“Tukikamilisha uchunguzi huo, tutalitumia Bunge kuwabana wahusika ili wawajibishwe kwa vitendo vyao vya kushindwa kusimamia sheria za ujenzi na kusababisha maafa,” alisema.
Kuteswa kwa Kibanda
Kamati hiyo imesikitishwa na kutekwa na kujeruhiwa kwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari, Absalom Kibanda na huku polisi wakiwa hawachukui hatua zinazotakiwa.
Alisema tukio hilo linafanana na lile la kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari, Dk Steven Ulimboka na mauaji ya Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi.
Mnyika alisema uchunguzi wa matukio hayo unatia mashaka na kwamba kumekuwa na usiri katika uchunguzi unaofanywa na polisi na hivyo Kamati Kuu inataka kuingilia kati ili kubaini ukweli.
Ufisadi bandari
Mnyika alisema katika Bunge lijalo watawasilisha vielelezo bungeni vinavyoonyesha namna Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alivyotoa zabuni ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa Kampuni ya Jitegemee Trading Company Ltd inayodaiwa kuwa ya CCM, kinyume na taratibu.
Madiwani wa Chadema
Mnyika alisema kumekuwa na madiwani wengi ambao wanakamatwa na polisi kwa makosa ambayo hayaeleweki.
Mkapa atema cheche; ataka viongozi wafuate misingi ya Nyerere
Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.
Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa amesifia utawala wake kwa kuongoza taifa bila ya kubaguana na amesikitishwa na matukio ya udini, ambayo yanaashiria kuvuruga amani na utulivu wa Tanzania katika siku za karibuni.
Akitoa salamu zake baada ya kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Desdelius Rwoma, Mkapa alisema anachojivunia ni kuheshimiwa na waumini wa madhehebu yote.
“Katika kipindi cha uongozi wangu, viongozi wa madhehebu yote walikuwa wakinisisitizia kuwa sisi sote ni ndugu pamoja na tofauti zetu za kiimani. Wakati wa utawala wangu nilijitahidi kwa uwezo wangu wote kuwahudumia wananchi bila kuwepo kwa malalamiko ya kubaguana katika jamii,” alisema Mkapa, ambaye aliiongoza Tanzania kuanzia mwaka 1995-2005.
Mkapa alionya kuwa taifa limeacha misingi aliyoiacha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mara zote alisimamia umoja wa taifa.
“Wakati wa utawala wangu nilijitahidi kwa uwezo wangu wote kuwahudumia wananchi bila kuwepo kwa malalamiko ya kubaguana katika jamii,” alisema.
Mkapa ambaye hakupanga kuongea lolote katika tukio hilo, alitaka taifa lijenge utamaduni wa kupendana, huku akilaumu kuwa kizazi kipya cha uongozi kimeanzisha mambo ya ajabu ya kukosa upendo na kudhalilishana.
Pia alitahadharisha kuwa zama hizi kumeibuka mitafaruku mbalimbali na kuwakumbusha Watanzania kuwa ni wakati wa kumwabudu Mwenyezi Mungu.
Mkapa alisema mara nyingi alishauriana na viongozi wa dini katika masuala ya kijamii na kiroho na kumtaja askofu mpya wa Bukoba, Rwoma na Mtangulizi wake aliyestaafu Nestory Timanywa kuwa alishirikiana nao katika masuala ya wananchi. Onyo la Mkapa limekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kukemea mambo ya kidini na kutetea Serikali yake haiongozi kwa misingi ya ubaguzi.
Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alikwenda mbali zaidi na kudai amekuwa akilalamikiwa na viongozi wa madhehebu ya Kikristo na yale ya Kiislamu.
Maneno ya Mkapa na Kikwete yamekuwa katika kipindi hiki taifa likiwa limetikiswa na matukio yenye mwelekeo wa chuki za kidini. Matukio makubwa yakiwa yale ya kuuawa wa Padri Evarist Mushi huko Zanzibar na Mchungaji Mathayo Kachila wa Geita.
Pia kupigwa risasi kwa Padre Ambrose Mkenda na kumwagiwa tindikali kwa Sheikh Fadhil Soraga na vurugu za mambo ya kuchinja huko Geita na Tunduma.
Askofu Mpya wa Bukoba Rwoma alimshukuru Mkapa kwa kuzungumzia umuhimu wa amani ya nchi, huku akisisitiza suala la upendo miongoni mwa wananchi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye jana alitaja vyanzo vya vurugu zinazoendelea nchini kuwa unatokana na tofauti kubwa kati ya walionacho na wasionacho.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua santuri ya nyimbo za dini kwa Kwaya ya Mt Joseph, Mfanyakazi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Sumaye alionya kuwa kama hali ya utajiri kwa baadhi ya watu itaachwa na kuendelea hivyo, ni wazi kuwa nchi haitatawalika kwa amani.
“Binadamu mwenye njaa na aliyekata tamaa kamwe hawezi kutawalika kwani kila wakati anahisi kutengwa na kundi jingine,” alisisitiza Sumaye.
Subscribe to:
Posts (Atom)