Chama
cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rufiji kimepongeza hatua ya Chama cha
Chadema kumchukua aliyekuwa kada wake Seleman Ndumbugani na kueleza
kuhama kwake sawa na kuutua mzigo ulioshindikana.
Akizungumza na NIPASHE Jumamosi, Katibu wa Uenezi na Uhamasishaji wa
Wilaya hiyo, Hemed Mnyeresa alisema CCM kamwe haisikitiki kuondoka kwa
mwanachama wake huyo wa siku nyingi kutokana na kuwepo kwake kulikuwa na
migogoro isiyokwisha na kusababisha chama hicho kuyumba.
Alisema kauli ya Ndubugai ambaye alikuwa Katibu wa Uenezi na
Uhamasishaji wa Wilaya hiyo, kwamba ameondoka ndani ya Chama hicho kwa
sababu kinaendeshwa kiukoo, hazina msingi na badala yake alimtaka aseme
ukweli kilichomfanya aondoke.
Ndubugai alikihama chama hicho na kuhamia Chadema Desemba 13, mwaka huu,
ambapo alinukuliwa na vyombo vya habari akisema aliondoka CCM kutokana
na chama hicho Wilaya ya Rufiji kutawaliwa kiukoo.
Mnyeresa alisema chama hicho kinaendelea kuwabaini na kuwaondoa
wanachama wote wanaodhani uongozi ni mali yao na kuwepo kwao humo ni
moja ya maisha yao.
"Hatutaki watu wanaodhani wao hawawezi kushindwa kwenye uongozi na kuona
ni mali yao milele, tunaendelea kuwasaka watu wa aina hiyo na kuwapa
mkono wa kwaheri wakishindwa kufuata kanuni na maadili ya chama,"
aliongeza kusema katibu huyo.
Alisema Ndubugai aliingia nyongo na kuchukua hatua hiyo baada ya
kushindwa nafasi hiyo katika uchaguzi uliopita, ambapo alianza kufanya
mambo mbalimbali yanayokwenda kinyume na chama hicho na alipoona kuna
dalili ya kumuondoa aliamua kujiondoa mwenyewe.
Hata hivyo, katibu huyo alieleza kwa sasa CCM imejikita katika
kuhakikisha kinaondoa kero zinazowakabili wananchi wa chama hicho
ikiwemo kuishinikiza serikali kutafuta soko la korosho pamoja na
kusimamia usambazaji wa zana za kilimo katika msimu huu wa kilimo.
CHANZO:
NIPASHE