0
KIONGOZI CCM KIBAHA AHUSISHWA NA VITENDO VYA USHOGA, AKANA ASEMA NI NJAMA ZA KUMCHAFUA KISIASA
Katibu wa uchumi, malezi na mazingira wa chama cha mapinduzi Kata ya Mailimoja BW. LAZARO KULIGWA amekanusha kuhusika kwake na ufanyaji wa mapenzi ya jinsia moja kama inavyosambazwa na mahasimu wake wa kisiasa ndani ya chama hicho kwa lengfo la kumharibia mafanikio ambayo ameyapata katika medani ya siasa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisi ya CCM wilaya ya KIBAHA, BW. KULIGWA amesema kuwa yeye binafsi kwa kipindi kirefu sasa amekuwa akisikia watu wakimsema chinichini na alikuwa anangoja mwenye kujitokeza amuulize kuhusiana na hilo lakini hakutokea mpaka alipokutana na mwandishi wa hizi.
BW.KULIGWA amebainisha kuwa kwa mara ya kwanza ilikuwa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu uliopita ambapo mmojka wa wagombea alikusanya vijana na kujenga maneno hayo kwa lengo la kumharibia kisiasa ingawa mpaka sasa anasubiri mtuwa kujitokeza kuthibitisha madai hayo ambayo yana lengo la kumchafua.
Akizungumzia kuibuka kwa maneno hayo ya kumhusisha na mapenzi ya jinsia moja,inatokana na yeye kamaKatibu wa uchumi, malezi namazingira wa kata ya Maili kluamua kuzitambua mali mbalimbali za Jumuiya ya wazazi kwa lengo la kuzihakiki na kuziendelezakwa faida ya chama kitu kinachuwauzi baadhi ya watu.
Hata BW.KULIGWA ameelezea kutotetereshwa na maneno hayo kwani ameshabaini mbinu ya wahasimu wake wa kisiasaa ya kutengeneza maneno ambayo hayajengi mshikamano katika chama na matokeo yake yanakibomoa chama, Na amelaumu uongozi wa CCM mjini Kibaha kwa kutotafuta ufumbuzi wa busara kuhusiana na tuhuma hizo zenye lengo la kumuaibisha mtu binafsi.
KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI OMBENI SEFUE ATEMBELEA MRADI WA JENGO JIPYA LA OFISI YA MKUU WA MKOA DODOMA
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue (wa
tatu kushoto) akitoa maelekezo alipotembelea mradi wa ujenzi jengo la ofisi ya
mkuu wa mkoa Dodoma. Kulia ni Katibu Tawala Mkoa Dodoma Ndg. Rehema Madenge.
Mafundi wa kampuni ya China Railway Jiachang
Engeneering Ltd (CRJE Co. Ltd) inayojenga Jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma wakiendelea na kazi kama walivyokutwa na Katibu Mkuu Kiongozi (hayupo
pichani) mwishoni mwa wiki alipotembelea mradi huo.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amewataka watumishi wa serikali kutambua kuwa wanawajibu mkubwa wa kujenga taswira nzuri ya utumishi wa umma hapa nchini kupitia utendaji uliotukuka.
Balozi Sefue alieleza hayo mwishoni mwa wiki alipokutana na watumishi wa sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma ambapo alisisitiza kuwa watendaji na viongozi wote wa umma kuanzia ngazi za chini za uongozi na utumishi wanatakiwa kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo na kuondoa taswira mbaya inayouandama utumishi wa umma.
Katika hatua nyingine baada ya katibu Mkuu Balozi Sefue kuona tatizo la ukosefu wa ofisi kwa watumishi wa sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma na kutembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma unaokwenda taratibu kutokana na upatikanaji wa fedha, balozi Sefue amesema serikali inawajibu wa kuhakikisha mradi huo unakamilika haraka iwezekanavyo.
Vilevile ameahidi katika mwaka wa fedha ujao 2013/14 serikali inaweza kutoa mara mbili ya fedha zilizoombwa na sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa mradi huo wa ofisi ambapo jumla ya shilingi bilioni tatu ziliombwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi katika bajeti ya mwaka 2013/14.
Kwa upande wake katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Ndg. Rehema Madenge alibainisha kuwa pamoja na tatizo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutokuwa na jrngo lake la ofisi, matatizo mengine yanayoikabili sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma ni pamoja na Ufinyu wa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo na fedha kidogo za kuendeshea ofisi wakati gharama za uendeshaji zinapanda.
Aidha uchache wa watumishi hasa kwenye kada za afya ni tatizo linguine lenye kuhitaji utatuzi na kumuomba katibu mkuu kiongozi kutoa vibali kwa maombi yote ya kuajiri yatayomfikia mezani kwake na kuiomba serikali itenge bajeti ya kuajiori watumishi wa kada zenye upungufu ili sekretarieti za Mikoa ziweze kuajiri na kuziba nafasi wazi.
Akiwakilisha watumishi wengine, Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Hospitali ya Mkoa wa Dodoma Dr. Lucy Mkandawile alisema kuwa matatizo mengine yanayogusa watumishi moja kwa moja ni pamoja na uchelewaji kupanda vyeo, malimbikizo ya Mishahara baada ya kupanda vyeo, malipo ya nauli za likizo na matibabu, fedha kwa ajili ya sare za kazi, ufadhili wa masomo kwa watumishi kwa ajili ya kujiendeleza na mishahara midogo.
Akijibu hoja hizo katibu Mkuu alieleza kuwa serikali inazifahamu baadhi ya changamoto zilizoelezwa na inazichukua zote pamoja na zile mpya zinazoendelea kuibuliwa na kuahidi kuwa serikali itaongeza jitihada katika kuzishughulikia lengo likiwa kuzidi kuboresha mazingira ya utumishi wa umma na hali za maisha za watumishi.
AMUUA MAMA YAKE KWA KUMPIGA MTALIMBO KICHWANI
Habari zilizotufikia punde zinasema kuwa Kijana Fransis Chiza, mkazi wa Kiluvya A, Wilaya ya Kisarawe anashikiliwa na jeshi la polisi kwa kumuua mama yake mzazi kwa kumpiga kwa mchi au mtalimbo kichwani na kufa papo hapo.
Inadaiwa kuwa kijana huyo ambaye ni mototo wa pili wa mama huyo alifika jana usiku na kumgongea mlango mama yake lakini mama yake hakuweza kumfungulia kutokana na kuwa na mlemavu jambo hilo lilimkasirisha na hivyo ilipofika asubuhi ya leo aliamua kutuliza hasira yake kwa kumpiga mama yake.
Baada ya kufanya tukio hilo kijana huyo alikimbia na baadaye kukamatwa na wanakijiji. Jeshi la polisi wilaya ya kisarawe wameshafika eneo la tukio na kwa taarifa zaidi juu ya tukio hili zitakujia muda si mrefu….
Na John Banda, Dodoma
WANANCHI wa katongoji cha Njedengwa wamefurahishwa na hatua zilizochukuliwa na viongozi wa juu wa serekali ngazi ya Wilaya baada ya kuingilia kati malalmiko waliyoulalamikia uongozi wa kata kutoingilia kati Swala la kuitisha mkutano kitongojini hapo.
Wananchi hao waliokuwa wakidai kuitishwa kwa mkutano ili waweze kutoa kelo mbalimbali zinazowasumbua kitongojini hapo walisema wamefurahishwa na hatua yaserekali kusikia kilio chao na kuamuru mkutano uitishwe.
Mwenyekiti wa Uhamasishaji wa madai hayo Khatibu Mayuni alisema kutokana na barua walioandikiwa viongozi wa kata hiyo ya kutakiwa kuitisha mkutano mkuu wa kitongoji jumanne ijayo imewapa faraja na kuona kumbe serekali inaweza kusikiliza kilio cha wananchi.
Mayunini aliongeza kuwa kutokana na usumbufu waliokuwa wanaupata toka kwa viongozi hao wa kata walikuwa wameadhimia kuomba kibali na kufanya maandamano mpaka bungeni ili wakatetewe na wabunge waliowachagua kutokana na kukosa haki ya kuuliza wala kutoa maoni ya mapato na matumizi.
‘’Mwanangu unadhani tungeweza kutolea maoni yetu wapi
kama si katika mikutano ambayo viongozi wamegoma
kuiitisha kwa kipindi cha miaka mitatu sasa bora sasa
nadhani kitaeleweka kwa sababu hata mkurugenzi atakuwepo ili ajionee mwenyewe wananchi unavyotafunwa’’, alisema
Wakati huohuo Barua iliyoandikwa na afsa utumishi wa Manispaa Lawrence Malangwa Kwa niaba ya Mkurugenzi imemtaka afsa mtendaji wa kata hiyo Magreth Songolo kushiriki kuuandaa na kuhudhuria mkutano huo ambao mkurugenzi atasikiliza kelo za wananchi hao.
Barua hiyo Iliyoandikwa Tar 11 APR 213 yenye kichwa habari kuitisha Mkutano Mkuu wa Kitongoji cha njedengwa na nakala zake kupelekwa kwa Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Manispaa, Mkuu wa Polisi Wilaya [OCD], Diwani wa kata hiyo na Mwenyekiti wa kitongoji cha njedengwa ilisisitiza mkutano huo kufanyika Saa 9:30 alasili.
Kero za wananchi hao ni pamoja na Kutoitishwa kwa mikutano kwa kipindi cha miaka mitatu, Kutoshirikishwa Ugawaji wa viwanja 99 vilivyopimwa na CDA katika ugawaji, kubinfsishwa kisima cha maji na zaidi ya nyumba 119 zilizobomolewa tangu 2010 ili kupisha muwekezaji huku wakiahidiwa kupewa eneo jingine la makazi.
Mamia wamzika Semdoe Handeni
Mjane wa marehemu Hussein Semdoe akiwa amempakata mtoto wake wamiezi mitatu
Kilindi. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda ameongoza mamia ya watu katika kumzika mwandishi wa habari wa gazeti hili, Hussein Semdoe aliyefariki dunia Alhamisi iliyopita kutokana na ajali ya gari iliyotokea wilayani Handeni na kusababisha vifo vya watu watatu.
Dk Kigoda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Handeni alisema alilazimika kuacha kikao cha baraza la mawaziri na kuruhusiwa na Rais Jakaya Kikwete kuhudhuria mazishi hayo.
Alisema Rais Kikwete amestushwa na vifo hivyo vilivyosababisha vya waandishi wa habari wawili na Ofisa Uhamiaji.
Semdoe alizikwa katika shamba la baba yake Kijiji cha Mafureta wilayani hapa katika mazishi yaliyohudhuriwa na umati wa watu kutoka mikoa mbalimbali wakiwamo wawakilishi wa klabu za waandishi wa habari za mikoa ya Pwani na Morogoro na Tanga.
Mwakilishi wa Kampuni ya Mwananchi Mkoa wa Tanga, Burhani Yakub aliwasilisha kwenye mazishi hayo salamu za Mkurugenzi na wafanyakazi wa MCL.
Alisema: “Mkurugenzi, wahariri, waandishi wa habari pamoja na wafanyakazi wa Mwananchi Communications Ltd kwa ujumla wamestushwa na kifo cha Semdoe na kwamba ameacha pengo kubwa ambalo halitaweza kuzibika kirahisi.”
Alisema wakati wa uhai wake alikuwa tegemeo la kampuni katika kuandika habari za wilaya za Kilindi na Handeni.
Burhan aliwasilisha kwa familia ya marehemu ubani wa Sh 621,000.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa alifika kwenye mazishi hayo akiwa ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kuwafariji wafiwa.
Akizungumza katika msiba huo, Gallawa alisema, Semdoe na wenzake wamekufa wakati wakilitumikia taifa kwa sababu walikuwa wakienda kupanda miti.
Hata hivyo, Gallawa alilazimika kwenda pia kwenye mazishi ya mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru na Mzalendo, Hamis Bwanga aliyezikwa Muheza. Baadaye pia alienda kuhudhuria mazishi ya Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Handeni, mjini Handeni. Wote walikumbwa na mauti katika ajali hiyo.
Marehemu Semdoe ameacha mjane, Mariam Semdoe pamoja na watoto watano; Najma, Hussein, Saadam, Saada na Shakira ambaye ana umri wa miezi mitatu.
Maajabu Geita:Aliyefariki miaka mitano iliyopita afufuka
mwanamke anayedaiwa kufariki miaka mitano iliyopita
Geita: Mji wa Geita na maeneo ya jirani juzi ulikumbwa na taharuki ya aina yake, pale mwanamke ambaye anadaiwa kwamba alifariki miaka mitano iliyopita alipoonekana akiwa hai katika eneo la Kasamwa.
Inadaiwa kwamba Flora Onesmo (45) alifariki Februari 28, 2008 katika Hospitali ya Wilaya ya Geita na kuzikwa katika Kijiji cha Nakasenya, Kata ya Butundwe, lakini juzi alfajiri alikutwa ameketi nje ya nyumba ya dada yake aitwaye Monica James, anayeishi Kasamwa.
Aliyekuwa wa kwanza kumwona Flora ni mdogo wake aitwaye Monica Onesmo ambaye baada ya kuamka saa 11:00 alfajiri nyumbani kwa dada yake, alimwona mwanamke aliyekuwa ameketi nje ya nyumba hiyo, lakini alimfananisha mwanamama huyo na marehemu dada yake.
“Baada ya kumwona nilimwita mtoto wake tunayekaa naye na nikampigia simu dada (Monica) ambaye alikuwa amelala chumba kingine nikamwambia kwamba nimeamka na kumkuta mwanamke amekaa hapa nje, lakini kila nikimwangalia anafanana na marehemu dada yetu,”alisema Jubili na kuongeza kwamba alipowaita wote walitoka nje.
Alisema mtoto wa Flora (marehemu anayedaiwa kufufuka) anaitwa Rebeka Elisha (16) na kwamba walimchukua tangu 2008 wakati mama yake huyo alipofariki dunia katika Hospitali ya Geita ambako alikuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa ini.
Rebeka ambaye ni mtoto wa nne wa Flora alisema: “Mama mdogo alituita sisi tulikuwa tumelala akasema kwamba nje kuna mwanamke ambaye anafanana na marehemu mama yetu, ndipo na sisi tukatoka na kweli kumwangalia alikuwa ni yeye kabisa.”
Alisema walipomuhoji mama yake huyo kwamba ametokea wapi, aliwaeleza kuwa ametoka eneo la Katoro kwa mganga na aliletwa na watu ambao hakuwatambua Alhamisi saa 1:30 usiku ndani ya gari na watu hao walimshusha kwa mtu aitwaye Juma Luchunga ambaye ni jirani na dada zake hao.
Kauli ya Flora
Akizungumza na waandishi wa habari, Flora alisema yeye ni mkazi wa Katoro na kwamba alitokea Katoro nyumbani kwa mganga wa jadi ambaye hata hivyo hakumtaja kwa maelezo kwamba wataalamu wake (majini) wamemkataza.
“Nilikuwa naishi kwa mganga wa kienyeji ila alikuja mwanaume wakati nikiwa pale akaninywesha dawa kisha tukapakizwa kwenye gari na watu wawili ambao sikuwatambua, mmoja mwanamke na mwingine mwanaume mpaka hapa Kasamwa tukashushwa saa 1:00 jioni,”alisema Flora.
Alisema alipofika Kasamwa alikwenda kunywa uji kwa mama mmoja ambaye pia hakumtaja na kwamba baadaye alipelekwa nyumbani kwa mtu mwingine saa nne usiku, lakini watu wa nyumba hiyo walipomwona walimwambia: “Hapa si kwako twende tukupeleke kwa ndugu yako” na ndipo wakampeleka kwa dada yake ambako aliketi nje hadi alfajiri.
Flora alisema kabla ya kuishi kwa mganga alikuwa akiishi porini ambako alitupwa na watu asiowafahamu na baadaye aliokotwa na wasamaria wema ambao ndiyo walimpeleka kwa mganga ambako alikuwa akiishi muda wote.
Kuhusu ndugu, Flora alisema ana ndugu zake Sengerema na Geita kwamba Sengerema ndiko alikokuwa akiishi kabla ya kwenda porini.
Kadhalika mwanamke huyo anayedaiwa kufufuka alisema ana watoto watano, (idadi ambayo ni sawa na ile aliyoacha marehemu Flora), lakini alipoambiwa awataje alikuwa akichanganya majina.
Ndugu wapishana
Baba mzazi wa mwanamke huyo, James Tunge ambaye aliitwa baada ya kutokea tukio hilo alisema kuwa mwanaye alifariki, lakini anashangaa kuona leo anaonekana tena.
Hata hivyo, Tunge alisema alipomwona mwanamke huyo juzi asubuhi alikuwa akifanana kabisa na mwanaye Flora, lakini alipoondoka kwenda kufuata picha yake na kurejea alikuta amebadilika, kwani kovu alilokuwa nalo kabla ya kifo halikuwa likionekana.
“Kwa sasa naweza kusema huyu siyo ila asubuhi wakati namwona ni kweli alikuwa mwanangu marehemu, najua mwanangu alikuwa na kovu kubwa puani na shavu la kushoto, lakini sasa hivi anaonekana ana kovu moja la shavuni ila sehemu zingine za mwili wanafanana kabisa,”alisema Tunge.
Kwa upande wake Jubili alisema kuna kila dalili kwamba mwanamke huyo ni mdogo wake, kwani anavyojieleza maelezo yake yanafanana. Alisema anawatambua watoto wake na ndugu japo wakati mwingine ni kama anapoteza kumbukumbu na kubadilika badilika sura.
“Wakati tunamwona asubuhi alikuwa akifanana na dada yangu marehemu, kwani dada alikuwa na kovu kubwa puani na shavuni na kweli alikuwa nalo na baadaye tulipoendelea kumuhoji alianza kubadilika sura na mara kovu likawa halionekani tena, “alisema Jubili.
Kwa ujumla ndugu wa mwanamke huyo wanahusisha tukio hilo na ushirikina kwa kusema kwamba huenda ndugu yao alichukuliwa kwa njia za giza, lakini Mungu amemwezesha kurejea katika maisha ya kawaida.
Jubili alisema kifo cha Flora miaka mitano iliyopita kilikuwa cha mazingira ya kutatanisha, kwani aliugua ghafla baada ya kula viazi vitamu kwenye mji wa jirani na hapo kuanza kuvimba tumbo.
Kwa kuzingatia mazingira hayo, juzi Flora alipelekwa wilayani Sengerema kwa mganga wa jadi aliyejitambulisha kwa jina la Dk. Mkonogi Masendena .
Kabla ya kupelekwa Sengerema, suala hilo lilifikishwa polisi ambao baadaye waliruhusu Flora kuondoka na wanaodai kwamba ni ndugu yao na hata walipofika Sengerema walilazimika kwenda polisi kwanza.
Polisi mkoani Geita walithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba ndugu zake waliondoka naye.
Aspirin inaweza kusababisha damu kuvuja tumboni
Dawa.
Wiki iliyopita nilizungumzia kuhusu Paracetamol, ambayo ni maarufu kwa jina la Panadol, tuliona kwamba dawa hiyo inapotumiwa kiholela, inaweza kusababisha madhara kwa viungo vya mwili kama vile ini, figo na ubongo.
Leo katika mfululizo huu wa kuzungumzia madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya dawa za maumivu, nitazungumzia Asprin.
Siyo watu wengi wanapendelea kutumia Aspirin kwa ajili ya kutuliza maumivu kama ilivyo kwa Panadol na Diclopar au diclofenac.
Pamoja na mazingira hayo, kuna wanaoitumia bila kujua, kupitia dawa nyingine zilizochanganywa na paracetamol pamoja na caffeine.
Dawa hizo ni kama vile Headex, Mifupen, Action ama dakika tatu. Zote hizo ni mchanganyiko wa dawa kadhaa, asprini ikiwa ni miongoni.
Dawa hizi kwa sasa zinapatikana hadi kwenye maduka ya vyakula na hazina udhibiti wowote kwani hata machinga anaweza kuzijumuisha kwenye bidhaa anazouza.
Kama nilivyoeleza awali, matumizi holela ya dawa hizi za kutuliza maumivu yamekithiri, hivyo baadhi hutembea nazo mifukoni au kwenye pochi.
Watu wa namna hii huwa hawatibu chanzo cha matatizo yao, bali wanatumia dawa hizo ili kujipa ahueni ya maumivu ambayo ni dalili tu ya yale yanayowasumbua.
Leo katika kuzungumzia Aspirin nimezungumza na Mtaalamu wa Dawa nchini, Mfamasia Mildred Kinyawa.
Kinyawa ambaye ni Msajili wa Baraza la Wafamasia Tanzania anaanza kwa kueleza:
“Kwa jumla, kitu chochote kikishaitwa dawa ni muhimu kutumiwa kwa uangalifu. Hakuna dawa isiyo na kiwango fulani cha madhara kwa mtumiaji. Pia hiyo ni mbaya zaidi kwa wale wanaotumia kiholela.”
Anasema kuwa kitaalamu Aspirin ni dawa nzuri kuliko dawa nyingine za kutuliza maumivu kwa sababu huweza kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.
Anabainisha kuwa kama ilivyo paracetamol, Aspirin inaweza kutuliza maumivu madogomadogo kama vile kuumwa kichwa, mafua na kushusha homa.
Kinyawa anafafanua kwamba, tofauti na Paracetamol, Aspirin inaweza kutuliza maumivu makali kama vile ya mifupa, meno na hata kutibu uvimbe.
Faida nyingine za Aspirin ni kwamba huweza kumsaidia mtu asipate matatizo ya moyo au kiharusi kutokana na damu kuganda na kuziba mishipa ya damu.
Anaeleza kuwa Aspirin huweza kuyeyusha vipande vidogovidogo vya damu iliyoganda na kujikuta ikiendelea kusafirishwa kwenye mfumo wa damu.
Kinyawa anaielezea damu iliyoiganda kuwa inaweza kuziba mirija kwenye moyo au ubongo na kusababisha madhara makubwa ikiwamo kifo cha ghafla.
Athari za Aspirin
Mfamasia huyo anasema kwamba kwa namna ilivyotengenezwa, Asprin ina asili ya aside, hivyo inapotumiwa wakati tumbo likiwa wazi hukwangua tumbo na kumsababishia vidonda tumboni.
Kwa watu wenye matatizo ya vidonda vya tumbo, hushauriwa kutokutumia kabisa asprini kwa sababu huchangia kuongeza tatizo.
Tafiti nyingine ambazo zimewahi kufanywa na kuandikwa kwenye majarida mbalimbali ya afya duniani zinaonyesha kuwa mtu akitumia aspirin na pombe anaweza kusababisha damu kuvuja tumboni kiasi cha kuhatarisha maisha yake.
Utafiti uliofanywa mwaka 2009, ulibaini kwamba matumizi mabaya ya Aspirin kutibu mafua makali kwenye kipindi cha mwaka 1918-19 ilisababisha athari mbalimbali zikiwamo za mapafu kujaa maji, vifo na udhaifu wa mwili kushambuliwa na bakteria pamoja na virusi.
Utafiti huo ulisababisha matumizi ya Aspirin kupungua na hata kupendekezwa isitumike kwa watoto chini ya miaka 16.
Inafanyaje kazi?
Aspirin inafanya kazi kwa
kupunguza uzalishaji wa kemikali inayojulikana kama prostaglandin ambayo
kwa kawaida husababisha maumivu.
Mara nyingi Aspirin inapendekezwa kutumiwa na watu wazima na mtumiaji awe ameshakula au kutumia wakati anakula.
Wiki ijayo nitamalizia mada hii kwa kuelezea juu ya Diclopar na Diclofenac.
Polisi wawahoji waandishi sakata la gesi Mtwara
Mwanza. Sakata la vurugu za gesi Mtwara limeingia sura mpya baada ya waandishi wa habari kuanza kuhojiwa na polisi wakidaiwa kuhusika na uchochezi uliosababisha vurugu hizo.
Vurugu hizo zilitokea Januari 26, mwaka huu na kuendelea kwa nyakati tofauti hata kusababisha nyumba za baadhi ya wabunge, viongozi wa CCM, Mahakama na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi pamoja na magari 18 na pikipiki saba kuteketezwa kwa moto na wananchi ambao walidaiwa kupinga mpango wa Serikali kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mtwara (MPC), Hassan Simba alithibitisha kuhojiwa kwa waandishi wa habari kuhusiana na sakata hilo.
Waandishi waliohojiwa hadi jana jioni ni Andrew Mtuli (Redio Pride FM), anayedaiwa kuendesha kipindi cha Amka na Pride kinachorushwa na redio hiyo kila alfajiri wakati Emmanuel Msigwa ambaye ni mtangazaji wa vipindi mbalimbali, Hassad Mdimu mtangazaji wa Kipindi cha Joto la Wiki ambaye anatuhumiwa kuweka hotuba ya kiongozi mmoja iliyoitwa ya uchochezi, wote wakiwa ni watangazaji wa kituo hicho cha redio.
Ilielezwa kuwa mahojiano hayo yanafanywa na makachero wa polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam na kwamba mbali na waandishi wa habari pia imeelezwa watu wa kawaida wamehojiwa na wengine wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na vurugu hizo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki hakuweza kupatikana jana katika simu yake kutokana na kudaiwa kuwa katika pilikapilika za uhamisho kutokana na Inspekta Jejenrali wa Polisi (IGP) Said Mwema kufanya mabadiliko kwa baadhi ya Makamanda wa Polisi kwa Mikoa ya Singida na Mtwara.
Wakati huohuo, mwandishi wa habari wa vyombo mbalimbali Majid Mjengwa ataendelea kuhojiwa na polisi Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam leo asubuhi.
CAG ataka kigogo Tanesco, mkewe washitakiwe
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amemuweka kitanzini aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, baada ya kushauri ashtakiwe pamoja na mkewe, Clara, kutokana ukiukwaji wa sheria katika kutoa zabuni.
Mbali na Mhando, wengine ambao CAG amependekeza wachukuliwe hatua za kisheria ni Mkurugenzi wa Kampuni ya McDonald Live Line Technology, watu wote walioingia katika biashara na Tanesco kinyume cha sheria pamoja na wafanyakazi waliohusika kutoa zabuni hizo.
Mapendekezo hayo ya CAG, Utouh yamo katika ripoti yake ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ya 2011/12, aliyoiwasilisha bungeni wiki iliyopita ikirejea ukaguzi maalumu uliofanyika katika shirika hilo kutokana na maombi ya bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo.
CAG pia ameweka wazi kuwa Tanesco iligubikwa na ukiukwaji uliokithiri wa Sheria ya Ununuzi ya 2004 na kanuni zake za mwaka 2005, uliosababishwa na viongozi wake wa juu.
“Mkurugenzi Mkuu wa Shirika akiwa ndiye mwenye uamuzi wa kuhusu ununuzi, alishindwa kuzuia ukiukwaji huu wa sheria ya ununuzi na mara nyingi aliidhinisha ununuzi wa chanzo kimoja au usiozidi ushindani,” inasema ripoti hiyo na kuongeza:
“Bodi inatakiwa kuripoti kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) yale yote yaliyogunduliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kubaini kuwapo kwa rushwa na ubadhirifu.”
Katika ripoti hiyo, CAG amebainisha ukiukwaji mkubwa wa sheria uliofanywa na Mhando, huku akibainisha kuwa mkewe, ambaye ni Mtendaji wa Mkuu wa Kampuni za Santa Clara Supplies Company Limited, alipewa zabuni katika shirika hilo kwa kutumia taarifa za kughushi.
Pia CAG amebainisha kuwa kampuni hiyo haikuwasilisha katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), rejesho la kodi kiasi cha Sh4.854 milioni ilizolipwa na Tanesco.
Santa Clara
CAG amebainisha kuwa kampuni hiyo iliyosajiliwa Aprili 18, 2011, ilipewa Leseni ya Biashara, Mei 2011 na kwamba wakurugenzi na wanahisa wa kampuni ni mke na watoto wawili wa Mhando.
Mke wa Mhando aliwahi kuwa mfanyakazi wa Tanesco, lakini aliacha kazi baada ya mumewe kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
CAG amebainisha kampuni hiyo iliingia mkataba na Tanesco na kupewa zabuni Namba PA/001/11/HQ/G/011 ya ugavi wa vifaa vya ofisi, vifaa vya matumizi ya kompyuta na mashine za kudurusu, kwa mwaka 2011 hadi 2012, mkataba ulianza Desemba 20, 2011.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa mkataba huo ulisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, ukishuhudiwa na Mwanasheria wa Shirika la hilo na Mkurugenzi wa Santa Clara aliyeshuhudiwa na shuhuda mmoja.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, moja ya masharti ya zabuni hiyo yalikuwa ni wazabuni kuwasilisha taarifa za hesabu za karibuni zilizokaguliwa. “Kampuni ya Santa Clara iliwasilisha hesabu zilizokaguliwa kwa mwaka 2010 katika kujaribu kutimiza matakwa ya kupewa zabuni, “ inasema ripoti hiyo.
Pia CAG katika ripoti hiyo, amefafanua kuwa hesabu hizo zilisainiwa na Kampuni ya Ukaguzi ya Fix Capital Certified Public Accountants ambayo usajili wake kwenye Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) ulikuwa umesitishwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Januari 24, 2012 Santa Clara ilipewa oda namba 2000009446-1 ya kuuza rimu 2,500 za karatasi kwa bei ya Sh7,000 kila moja. “Jumla ya gharama ya oda nzima ilikuwa ni Sh20.65 milioni ikijumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT),” inaeleza ripoti hiyo ya CAG.
Hata hivyo, Santa Clara iliwasilisha rimu 500 tu za karatasi zenye thamani ya Sh4.13 milioni na baadaye ikashindwa na hatimaye zabuni hiyo kutekelezwa na kampuni nyingine.
“Kwa maana hiyo Santa Clara haikustahili kupewa zabuni hiyo na hali hiyo ingejulikana mapema wakati wa tathmini ya zabuni, kwani mali zake zilikuwa ni Sh107.7 milioni,” inaeleza ripoti hiyo.
Mkataba wa McDonald
Mkataba mwingine ambao CAG ameubaini kusainiwa na Mhando, kinyume cha sheria ni ule na Kampuni ya McDonald Live Line Technology Limited, wa zabuni ya kukarabati na kutengezeza njia za umeme (live line), mwaka 2008, 2009, 2010 na 2011.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa mmiliki wa McDonald Live Technology Ltd alikuwa mfanyakazi wa Tanesco, lakini aliachishwa kazi Julai19, 1999 kwa sababu za utoro kazini, kutowajibika na upotevu wa pesa, Sh1.280 milioni na kuharibu gari la Tanesco.
Hata hivyo, ripoti hiyo imebainisha kuwa Julai 17, 2008 McDonald aliingia kwenye makubaliano ya ubia na Mhando, ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco katika ubia ambao Mhando alikuwa na jukumu la kutafuta miradi na kazi kutoka kwa wateja na McDonald itawajibika na utekelezaji.
CAG anasema kati ya 2009 na 2011, Mhando baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, aliipa kampuni hiyo mikataba mitano ya zabuni za kukarabati na kutengeneza njia mbalimbali za umeme ambayo iliiwezesha McDonald kulipwa zaidi ya Sh1.12 bilioni.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa mikataba hiyo ilitolewa mingine bila kuwasilisha nyaraka kwa ajili ya ukaguzi kama inavyotakiwa, wala kuwa na dhamana ya Benki Kuu.
CAG amebainisha kuwa katika mkataba Na.PA/001/09/HW/W014 wa kukarabati njia ya Kiyungi – Arusha 66kV wa Machi 11, 2010, wenye thamani ya zaidi ya Sh1.417 bilioni haukutekelezwa na McDonald.
Utekelezaji wake ulianza Julai 28, 2010 na ilitakiwa kuwa imemalizika Machi 9, 2011, lakini haukukamilika na hata baada ya kuongezewa muda mara mbili na kutokana na hali hiyo, Juni 19, 2012, Tanesco ilivunja mkataba huo wakati McDonald walikwishalipewa malipo ya awali ya Sh475.6 milioni, sawa na asilimia 33 ya mkataba mzima.
CAG katika ripoti yake anabainisha kuwa malipo hayo yalifanywa kinyume cha masharti ya zabuni ambayo inaelekeza kwamba malipo ya awali yalitakiwa kuwa asilimia 15.
Amebainisha kuwa licha ya Tanesco kufanya tathmini na kubaini kuwa McDonald ilitakiwa kuirejeshea Sh 504.7 milioni ikiwa ni faini, fidia na kiasi cha dhamana ya benki kilichokadiriwa, lakini hadi wakati wa ukaguzi huo pesa hizo zilikuwa hazijarudishwa.
Shule yateketea kwa moto Dar
Dar es Salaam. Mabweni ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wazo Hill nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, yameteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.
Moto huo uliozuka mapema asubuhi, inadaiwa ulisababishwa na hitilafu ya umeme.
Akizungumza jana shuleni hapo, mmiliki wa shule hiyo, Valence Msaki alisema moto huo ulianza saa 11 asubuhi wakati wanafunzi wakiwa kwenye mazoezi ya viungo.
Alisema ulianzia kwenye chumba cha viongozi wa mabweni na licha ya kuwa haukuleta madhara kwa binadamu, lakini umesababisha hasara ya mali mbalimbali za wanafunzi vikiwemo nguo, madaftari, vitanda na magodoro.
Msaki alisema mlinzi aligundua moto huo alipokuwa anakagua mabweni hayo kwani aliona ukitokea kwenye chumba cha viongozi.
Alisema ni asilimia 40 tu ya wanafunzi hao waliokoa baadhi ya vitu vyao na asilimia 60 hawakufanikiwa, hivyo vimeteketea.
“Moto huu ulianzia kwenye chumba wanacholala viongozi wa bweni inawezekana ikawa chanzo ni hitilafu ya umeme kwa kuwa chumba hicho muda wote taa huwa hazizimwi,” alisema Msaki.
Msaki alisema magari ya Kikosi cha Zimamoto yalifika saa 2.30 asubuhi, huku juhudi kubwa za kuuzima moto huo zikifanywa na wananchi, walimu na wanafunzi ambao walitumia maji, mchanga na baadhi ya vifaa vya kuzimia moto vya shule hiyo.
“Sasa hivi tunajipanga ili watoto waweze kulala na kesho tutafanya tathmini ya vitu vilivyoungua ili tujue vitu vingapi vimeungua,” alisema Msaki.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema: “Kizuri ni kwamba hakuna vifo wala mtu aliyejeruhiwa.”
Aliwataka wakuu wa shule mbalimbali katika mkoa huo kufanyia ukaguzi vifaa vya moto na kuziweka shule zao katika hali ya tahadhari ili kusitokee maafa pindi inapotokea ajali za moto.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Samueli Nainda alisema kwamba wanaiomba Serikali iwasaidie kutokana na hasara iliyosababishwa na moto huo.
“Kama hivi vitu vyangu vyote vimeungua kilichobakia ni nguo nilizovaa mwilini sielewi nitafanya nini, huku wazazi wangu wote wameshafariki na wanaonisomesha ni wafadhili ambao wapo Mkoa wa Kigoma,” alisema Nainda
Subscribe to:
Posts (Atom)

