Ukumbi bunge la Katiba sasa wakamilika
Spika wa Bunge, Anne Makinda (aliyekaa) akiwa na Wajumbe wa Tume ya
Utumishi wa Bunge wakati wakikagua Ukumbi wa Bunge, ambao utatumika kwa
ajili ya Bunge la Katiba, mjini Dodoma jana. Picha na Ofisi ya Bunge
Dodoma. Matengenezo yaliyotarajiwa ndani ya ukumbi wa bunge la Muungano ambao ndio utakaotumika kwa bunge la Katiba, yamekamilika na sasa ukumbi huo uko tayari kwa kazi inayotarajia kuanza Februari 18 mwaka huu.
Kukamilika kwa ukumbi huo kunaondoa hofu iliyoanza kutanda kuwa huenda bunge hilo lingesogezwa mbele kwa siku tatu kwani kulikuwa na mashaka kwa kazi hiyo.
Jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alitembelea ukumbi huo kwa mara ya mwisho na kujiridhisha katika maeneo muhimu yaliyokuwa yakifanyiwa marekebisho .
Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ukumbi huo, Lukuvi alisema tayari viti 676 vimeshafungwa pamoja vipaza sauti vyake ambavyo Rais Jakaya Kikwete alionyesha mashaka kama vingekamilika kwa wakati.
Februari Mosi, Rais Kikwete alipita kukagua ukumbi huo wakati akielekea mkoani Mbeya ambapo alionyesha kutokuridhika hasa akatilia mashaka katika eneo la vipaza sauti ambako alisema kuwa bado kulikuwa na kazi kubwa ya kufanya.
Hata hivyo, jana Lukuvi licha ya kushuhudia kuwa vimefungwa katika viti vyote, lakini alipotakiwa na waandishi kuwasha kwa majaribio, wajenzi wa ukumbi walizuia na kusema kitaalamu hakutakiwa kuwasha jana kwani kazi ilikuwa bado inaendelea.
Alisema kuwa Ofisi ya Bunge imeshatafuta kumbi nyingine nje ya bunge kwa ajili ya kufanyika mikutano ambayo itahitaji wajumbe zaidi ya 60.
Mgomo kila kona kuzipinga EFDs
Mikoani. Sakata la matumizi ya Mashine za Elektroniki za Kutolea Risiti (EFD), limechukua sura mpya baada ya wafanyabiashara mikoa mbalimbali kuja juu wakisema matumizi yake yanalenga kuwaangamiza katika biashara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao wameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufikiria upya mfumo wa kuzitumia, vinginenyo watajikuta wanaingia kwenye mgogoro mkubwa baina yao.
Tayari, wafanyabiashara miji ya Iringa, Songea na Mara wametoa msimamo wa kugomea matumizi ya mashine hizo na kuazimia kufunga biashara zao kama njia ya kupinga matumizi yake.
Wafanyabiashara wa Manispaa ya Iringa, jana walitangaza mgomo usio na kikomo kwa sababu mashine hizo zinawasababishia hasara. Wanadai mashine hizo licha ya kununuliwa kwa bei kubwa, inawabidi kuajiri wafanyakazi wenye ujuzi na kodi nyingine wanajikuta wakitumia sehemu za mitaji yao.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma aliwataka wafanyabiashara kuacha migomo isiokuwa na tija wala sababu, badala yake wafikishe malalamiko yao kwa uongozi husika kupitia viongozi wao.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Mara, Baltazar Gibogo alisema mgomo huo ni halali yao, kwani Serikali inawanyanyasa wananchi wake.
Gibogo alikanusha kuwa Serikali imeshindwa kukusanya kodi hadi kubuni kutumia mashine, bali chanzo kikubwa ni kukithiri kwa rushwa baina ya wafanyabiashara wakubwa na wafanyakazi wa TRA.
Mjini Mbeya, wafanyabiashara walishauri Serikali kuzitoa bure mashine za EFD ili kuwasaidia wafanyabiashara kujijenga kibiashara badala ya kufilisika.
“Pamoja na kwamba Mamlaka ya Mapato tanzania (TRA) inasema mfanyabiashara akinunua anaweza kurudisha fedha zake kwa kupunguza zile za kodi, ukweli unabaki palepale kwamba wafanyabiashara hawana fedha taslimu kununua kitu ambacho siyo cha kuuza na kupata fedha kwa wakati huo,’’ alisema Anania Kasisi.
Imeandikwa na Florence Focas , Musoma; Geofrey Nyang’oro na Zainab Maeda, Iringa na Lauden Mwambona, Mbeya
Mwenyekiti wa CCM Dar kizimbani kwa tuhuma za kusambaza ARV feki
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI),
Ramadhani Madabida (kulia) na Ofisa Ubora wa Bidhaa wa Bohari Kuu ya
Dawa (MSD), Evance Mwemezi walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana kusomewa mashtaka ya kuuza na kusambaza
dawa feki za ARV. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Ltd cha Dar es Salaam (TPI), Ramadhani Madabida na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kusambaza dawa bandia na kusababisha hasara ya Sh148.3 milioni.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi aliwataja washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo kuwa ni Mkurugenzi wa Operesheni wa TPI, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon Msofe, Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango pamoja na wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD), Sadick Materu na Evans Mwemezi.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nyigulile Mwaseba, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro alisema katika shtaka la kwanza, Aprili 5, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango wakiwa na nyadhifa hizo kwenye kiwanda cha TPI walisambaza makopo 7,776 ya dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) aina ya Antirectroviral.
Kimaro alidai kuwa washtakiwa hao, walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 76 (1)(2) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003, wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halali na kwamba zimetengenezwa Machi, 2011 na muda wake wa kutumika unakwisha 2013 wakati wakijua kuwa si kweli.
Katika shtaka la pili, Wakili Kimaro alidai kuwa Aprili 11, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango walisambaza na kuuza makopo 4,476 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral walizokuwa wakijaribu kuonyesha kuwa zilikuwa na viambatanisho vya Starudine 30mg, Nevirapine 200mg, Lamivudine 150mg pamoja na fungu namba OC 01.85.
Alidai kuwa washtakiwa hao waliweka viambatanisho hivyo wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halisi na kwamba zilitengenezwa Machi 2011 na muda wake wa kutumika ulikwisha Februari 2013 huku wakijua kwamba ni uongo.
Katika shtaka la tatu wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kinyume na Kifungu cha 302 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Wakili Kimaro alidai kuwa kati ya Aprili 12 na 29, 2011, washtakiwa hao wakiwa na nia ya kulaghai, walijipatia Dola za Marekani 98,506 sawa na Sh148,350,156.48 wakijaribu kuonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha ni malipo halali ya makopo 12,252 ya dawa aina ya Antirectrovial yaliyokuwa katika fungu (batch) namba OC 1.85.
Alidai pia kuwa washtakiwa hao walikuwa wakionyesha dawa hizo bandia zilikuwa zimetengenezwa Machi, 2011 na kwamba muda wake wa kumalizika kutumika ni Februari, 2013 na wakafanikiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka MSD.
Katika shtaka la nne, Materu na Mwemezi wakiwa ni Meneja wa Udhibiti Viwango na Ofisa Udhibiti Viwango wa MSD, kati ya Aprili 2 na 13, 2011 huku wakijua nia ya kutendeka kwa makosa hayo ya usambazwaji wa dawa bandia, walishindwa kuzuia kinyume na Kifungu cha Sheria namba 383 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Katika shtaka la tano, wakili huyo wa Serikali alidai kuwa kati ya Aprili 5 na 30, 2011, washtakiwa Madabida, Shamte, Msofe, Shango pamoja na Materu na Mwemezi, kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi, walishindwa kutekeleza majukumu yao wakiwa watendaji.
Alidai kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kusambaza makopo 12,252 ya dawa bandia wakijaribu kuonyesha kuwa zilitengenezwa Machi 2011 na kwamba zitakwisha muda wake wa kutumika Februari 2013 na kuisababishia mamlaka hiyo ya Serikali hasara ya Sh148,350,156.48.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili na upande wa mashtaka ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Mwaseba alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao wanafanya kazi kwenye taasisi zinazotambulika kisheria na kwamba kila mdhamini angesaini bondi ya Sh6,181, 256.
Pia alimtaka kila mshtakiwa kutoa kiasi cha Sh12, 362,513 milioni taslimu mahakamani hapo au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Madabida na Materu waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti hayo huku wenzao wakipelekwa mahabusu kusubiri kuyakamilisha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, mwaka huu itakapotajwa.
MBOWE: ACHENI KUINGILIA TUME YA WARIOBA
MWENYEKITI
wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Taifa Freeman Mbowe,
amesema Kitendo cha baadhi ya vyama vya siasa kuingilia tume ya jaji
Joseph Warioba iliyoteuliwa na rais ili kuleta katiba mpya yenye neema
kwa watanzania ni Uoga wa kuondolewa madarakani.
Amesema tume ya jaji
Warioba haikujitengenezea maoni yake ili kuwafurahisha wananchi bali
maoni yaliyomo kwenye rasmu ya katiba ni maoni ya wananchi ambayo
hayatakiwi kuingiliwa na chama chochote.
Mbowe amesema hayo jana
jumatatu kwenye uwanja wa Magereza mjini Geita ikiwa ni ziara yake ya
vuguvugu la mabadiliko''M4C''Pamoja Daima akitokea wilayani Biharamulo
mkoani Kagera.
Amesema kuingilia tume ya mabadiliko ya katiba kuhusu
maoni ya wananchi yaliyokusanya na tume unatokana na kubaini mapema
kwamba kufikia mwaka 2015 chama kilichoko madarakani ccm itang'oka
madarakani.
Mbowe amesema endapo serikali haitalifanyia
marekebisho daftari la wapiga kura Chadema kitwahamasisha wananchi nchi
nzima wasishiriki kupiga kura za maoni ya katiba.
Aidha ameitaka
serikali kurekebisha daftari hilo ili kutoa fursa kwa watanzania wengi
kushiriki kuipigia kura maoni ya katiba na chaguzi mbalimbali zijazo
ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa,na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Majalada kesi yasombwa na mafuriko Moro
Magole. Wakati Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Magole, Fredy Mbogela akisema kesi zote zilizokuwa zikisikilizwa katika mahakama hiyo ambayo imesombwa na maji pamoja na mafaili yote, zitaanza upya, Mkuu wa Wilaya na Mkoa wa Morogoro wanahaha kukusanya takwimu za waathirika wa mafuriko.
Mafuriko makubwa yalitokea katikati ya wiki iliyopita Kijiji cha Magole, huku yakisababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu. Pia, mafuriko hayo yalisomba majalada ya kesi mbalimbali mahakamani hapo.
Akizungumza jana, Hakimu Mbogela alisema hivi sasa kesi zote za jinai zilizokuwa zikisikilizwa mahakamani hapo zitafunguliwa na kusomwa na kusikilizwa upya.
“Polisi ndiyo watakaofungua na kuzipeleka kesi hizo katika mahakama hiyo, kwa sababu wao wanazo kumbukumbu za kesi hizo kupitia kwa waendesha mashtaka na wapelelezi,” alisema Hakimu Mbogela na kuongeza:
“Hakuna kesi itakayofutwa kutokana kuharibiwa majalada hayo, kama nilivyosema polisi watazileta kesi mahakamani, hata kama kulikuwa na kesi iliyokuwa imekaribia hukumu itaanza upya.” alisema.
Alisema: mahakama itaanza kufanya kazi baada ya kufanyiwa usafi na kuweka samani.
Alisema hatua ya awali ambayo inaendelea kufanywa, ni kusafisha jengo la mahakama hiyo ndani na nje kwa kutoa matope, magogo ya miti na taka nyingine ambazo zilikwama eneo hilo na kwamba, utaratibu wa utendaji unaendelea kufanywa.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Nestory Munjunangoma alisema Idara ya Mahakama kwa kushirikina na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wapo kwenye mchakato wa ukaguzi na tathmini ya uharibifu wa jengo la mahakama hiyo.
Munjunangoma alisema hivi sasa jitihada za kufanya ukaguzi na upembuzi yakinifu zinafanyika kabla ya TBA kutoa ushauri kulingana na uharibifu uliotokea kamajengo hilo linaweza kukarabatiwa ama kujengwa upya.
Alisema hivi sasa shughuli za mahakama hiyo zimesimama, kuruhusu usafi wa mazingira.
Mauaji yazidi kutikisa Tarime
Tarime. Hali ya usalama Tarime imezidi kutoweka baada ya jambazi lisilofahamika likiwa na bunduki ambayo haijafahamika aina yake kuendelea kuua watu kwa risasi hasa wa jinsi ya kiume, ambapo idadi ya waliouawa imefikia saba hadi sasa na inadaiwa huwaua watu na kupotea bila kutambuliwa.
Jambazi hilo lisilofahamika liliua watu hao usiku wa Januari 27, mwaka huu katika maeneo ya Nkende likianza na kumuua Mwendesha Bodaboda, Juma Marwa Mkazi wa Nkende mjini Tarime akiwa anaelekea nyumbani kwake ambaye alikufa akiwa hospitali akipatiwa matibabu.
Mganga wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Marco Nega alisema tangu Januari 27 hadi sasa hospitali imeendelea kupokea watu waliouawa na majeruhi ambao wamefanyiwa uchunguzi na kugundulika wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi katika sehemu mbalimbali za mwili na kwamba watu wapatao 7 wamekwisha kufa mpaka sasa.
“Tumepokea maiti za watu na majeruhi na tumewafanyia uchunguzi wakagundulika wana majeraha ya risasi sehemu mbalimbali za mwili, ambapo tayari watu saba wamekufa wengine wamekufa wakiwa njiani wakienda kwenye matibabu Musoma, marehemu hadi ni saba,” alisema Nega.
Waliojeruhiwa wakosa huduma ya X-ray
Watu waliojeruhiwa wameshindwa kupatiwa huduma ya X-Ray kutokana na Hospitali ya Wilaya kutokuwa na huduma hiyo kwa muda wa zaidi ya miezi 3 na kusababisha wagonjwa kusafirishwa kwenda Musoma na Mwanza kwa matibabu, ambapo Samweli Richard amekufa akiwa njiani kuelekea Musoma kwenye matibabu ikiwamo huduma hiyo ya X-ray.
Hospitali ya Wilaya yashindwa kutoa huduma
Huduma kwa wagonjwa mbalimbali katika Hospitali ya Wilaya imeshindwa kuendela vilivyo baada ya kupatwa na misiba miwili ya watumishi wawili, ni baada ya waume zao kuuawa na jambazi hilo lisilofahamika.
Awali Januari 26 jambazi hilo lilimuuwa Robert Kisiri (45) mkazi wa Mugabiri ambapo Mstaafu wa JWTZ Zacharia Mwita(58) na Erick Makanya (25)wote wakazi wa Kijiji cha Mogabiri Kata ya Kitare Wilayani Tarime walikutwa wakiwa wameuawa na miili yao ikiwa na majeraha ya risasi mbavuni kushoto na mgongoni.
Pia jambazi hilo liliwajeruhi watu watano kwa risasi ambao ni Mgosi Marwa Mkazi wa Mogabiri, Joseph Richard Mkazi wa Rebu, Gastor Richard Mkazi wa Rebu, Juma Mwita Mkazi wa Mogabiri na Mkandarasi Binafsi wa ujenzi, Mwasi Yomami ambao kati ya hao wawili wamefariki wakati wakipatiwa matibabu.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Justus Kamugisha amesema wamemkamata mtu mmoja anayeshukiwa kuwa mhusika wa mauaji ambaye yuko chini ya ulinzi kwa mahojiano na kwamba anazidi kuongeza vikosi vya doria kuimarisha ulinzi na usalama na kuwasaka wahalifu.
Wananchi wacharuka
Wananchi Mjini Tarime waliitaka polisi kuhakikisha jambazi hilo linapatikana vinginevyo walitaka polisi kuwakabidhi bunduki ili waweze kumsaka jambazi huyo.
‘Kamanda kashindwa kazi haiwezekani mtu mmoja aue watu 7 ndani ya siku mbili, huu ni uzembe wa polisi katika kuimarisha ulinzi, tunaomba tukabidhiwe bunduki tulisake jambazi,” alisema mwananchi mmoja.
Mwimbaji wa injili Msomali ndani ya tamasha la Xmas Dodoma
Mwimbaji wa nyimbo za injili Toka nchini SomaliaMARY SINKALA atakaeshiriki katika tamasha la kristmas litakalofanyika Dodoma Des 25 ndani ya uwanja wa jamhur
Na John Banda, Dodoma
Waimbaji wa nyimbo za injili watakaotumbuiza katika Tamasha la kusifu [Shangwe za Xmas] Dodoma kutoka Nje ya nchi waendelea kuongezeka. Ni Baada ya mwimbaji kutoka Nchini Kenya TUMSIFU RUFUTU mwimbaji wa wimbo wa Mwambie Farao kuwa rasmi kwenye tamasha la Kristmas litakalofanyika Dodoma Tar 25.12.2013 katika uwanja wa Jamhuri, Hatima mwingine aongezeka kutoka nchini Somaria Bi. MARY SINKALA mwenye wimbo wa "Mkumbuke Muumba wako". Tayali waimbaji hao wote wameshawataka wakazi wote wa mkoa huo na vitongoji vyake na watakaotoka nje kujiandaa kwani wao wamejiandaa vya kutosha na kwamba watawafundisha namna ya kumkumbuka muumba wao na
jinsi ya kuelekea kaanani. Shangwe hizo ambazo kwa sasa ni gumzo mkoani humo kutokana na kuandaliwa kwa umahili mkubwa na kampuni ya Liberty Promotion Company ya mjini humo tayali wakurugenzi wake wamewataka watu kuhudhuri kwa wingi kutokana na kiingilio kidogo kitakachomuwezesha kila mtu kukimudu cha 2000 kwa wakubwa na watoto 1000. Kampuni hiyo imesema Dodoma imekuwa nyuma kwa muda mrefu hasa nyakati
za Sikukuu za kidini na hivyo wamekusudia kukata kiu za wananchi
mkoani humo kwa shangwe za kumuimbia na kumtukuza mungu kupitia matamasha ya mara kwa mara kuanzia KRISTMAS ya mwaka huu, huku wakiahidi kuibua vipaji vya chipukizi wengi.
Tamasha hilo litawaunganisha waimbaji toka ndani na nje ya nchi hasa wa mikoa ya DSM na Dodoma itakayobebwa na waimbaji toka makanisa mbalimbali na wanachuo wa chuo kikuu cha Dodoma [UDOM]
JK: Acheni urafiki wa dhambi na wachimbaji wakubwa
Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuacha urafiki wa dhambi na baadhi ya wachimbaji wakubwa wanaohodhi maeneo makubwa na badala yake wazingatie sheria ili kutoa haki kwa wachimbaji wadogo.
Akizungumza katika siku yake ya mwisho kutembelea Mgodi wa Dhahabu wa Baraka uliopo wilayani Geita katika Kijiji cha Nyaruyeye juzi, Rais Kikwete alisema kilio cha wachimbaji wadogo hivi sasa ni maeneo lakini wanaweza kuchimba sawa na wachimbaji wakubwa hivyo kuitaka wizara hiyo kuzingatia sheria kwa kuwafutia umiliki wenye maeneo ambayo hawayafanyii kazi.
“Mkiyatwaa watapiga kelele, acheni wapige kelele lakini timizeni sheria. Masele (akimwangalia Naibu Waziri Nishati na Madini Stephen Masele) na wenzako lazima mzingatie sheria. Wanyang’anyeni maeneo haya wapeni wachimbaji wadogo wachimbe. Acheni kufanya urafiki wa dhambi na hawa,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ambaye alieleza kufurahishwa kwake na wachimbaji wadogo kuanza kuchimba kisasa alisema sheria ya umilikaji wa maeneo ya utafiti na uchimbaji wa madini inaelekeza kuwa iwapo mwombaji akija kuomba tena (renewal) leseni ya eneo alilopewa anapaswa kulipunguza kwa asilimia 50 ili wapewe wengine na vivyohivyo anapokuja kwa mara ya pili, pia anapaswa kupunguziwa eneo lake kwa asilimia 50.
“Pamoja na kwamba sheria ipo wazi, ukiwauliza wizara kwa nini hawafanyi hivyo, hawana maelezo wapo kimya, sijui wanaingia kigugumizi gani kutimiza sheria hii. Wanaposhindwa kufanya haya ni hasara kwa taifa maana haya madini hayachimbwi, wangezingatia sheria hii na kuchukua maeneo haya wangewapa wengine wakachimba leo tusingekuwa na kelele za wachimbaji wadogo,” alisema. Rais Kikwete alisema madini yakiwa chini hayana thamani yoyote mpaka yanapochimbwa na kubainisha kwamba iwapo watu waliopewa leseni watazishikilia bila ya kuendeleza maeneo yao, watakwamisha ajira na maendeleo kwa nchi.
Aidha, aliitaka wizara hiyo kuwa makini wakati wa kutimiza matakwa ya sheria hiyo ya umiliki wa maeneo ya uchimbaji, akitahadharisha kuwa wamiliki wengine wanaweza kubadili majina pindi watakaponyang’anywa maeneo yao.
“Wana tabia ya kubadili majina, mkimnyang’anya atakuja upya. Kama alikuwa anaitwa Kikwete & Sons sasa atakuja tena anajiita SK lakini ndiye huyohuyo, tazameni sana. Najua, mnayajua mengi maana na ninyi ni wabia wao lakini ninachotaka ni kuzingatia na kusimamia sheria,” alisema.
Akizungumzia Mgodi wa Mzawa alioutembelea, Rais Kikwete alisema amejionea jambo kubwa na la kushangaza kiasi cha kusema kwamba iwapo angeishia kusimuliwa mambo hayo na watu bila ya kufika, asingeamini kama Watanzania wanaweza kuendesha migodi kama huo.
Alisema Serikali inathamini mchango wao na kuwataka kujiandikisha Tume ya Uwekezaji ili nao waweze kuomba msamaha wa mafuta na zana mbalimbali kama ilivyo kwa wawekezaji wakubwa wa nje.
Awali, Masele alimwomba Rais kuangalia uwezekano wa kuwapatia wachimbaji wadogo msamaha wa kodi akisema vifaa wanavyotumia havina tofauti na vile vya wachimbaji wakubwa.
Kilichomuua Dk Mvungi
Dk Sengondo Mvungi
Hospitali ya Millpark ya Johannesburg, Afrika Kusini, imesema madaktari waliokuwa wakimtibu aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi walibaini kuharibika kwa ubongo wake kutokana na kumwagika kwa maji yanayoutunza ambayo kitaalamu yanaitwa ‘cerebrospinal fluids’ au CCF.
Msemaji wa Hospitali hiyo, Tebogo Nyembezi alisema Dk Mvungi alicheleweshewa tiba baada ya kupata tatizo la maji hayo yanayotunza ubongo kumwagika mara baada ya kujeruhiwa.
Dk Mvungi (61), alipata majeraha makubwa baada ya kujeruhiwa na watu waliovamia nyumbani kwake Kibamba, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu. Alifariki dunia jana mchana.
“Maji hayo ambayo ni miligramu 50 tu katika ubongo wa mwanadamu ambayo huufanya ubongo uelee yakimwagika nusu tu, basi mgonjwa yupo hatarini, lakini akiwahishwa na kupata tiba sahihi anaweza kupona,” alisema Nyembezi.
Alisema iwapo mgonjwa atapewa tiba sahihi ndani ya saa 48, ubongo wake unaweza kurudi katika hali ya kawaida, lakini saa hizo zikizidi hawezi kupona kabisa kwa sababu maji hayo yanapomwagika ubongo hujigonga kwenye mifupa ya sakafu yake na kuharibika kabisa.
Mtaalamu wa mishipa na neva za fahamu (neurosurgeon) katika Hospitali ya Regency, Dar es Salaam, Dk Hariff Najin alisema kazi kubwa ya maji hayo ni kuulinda ubongo pindi inapotokea ajali ili usidhurike lakini endapo maji hayo yatamwagika nao huharibika.
“Haya maji yanaufanya ubongo uelee na usielemee kichwa. Hivyo inapotokea maji haya yakaisha au kupungua, ubongo hujigonga na kukosa ukinzani na kuharibika,” alisema.
Alisema maji hayo ambayo hufika hadi kwenye uti wa mgongo yakikosekana katika ubongo, husababisha damu isitembee kwenye eneo hilo jambo ambalo pia linaweza kusababisha mishipa katika sehemu ya nyuma ya ubongo kuharibiwa.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu Muhimbili (Moi), Profesa Lawrence Museru alisema anachofahamu ni kuwa Dk Mvungi alipelekwa Afrika Kusini kwa kuwa alipata madhara makubwa kwenye ubongo na wala si kwa sababu ya kumwagika kwa maji kama ilivyoelezwa Afrika Kusini.
“Majeraha hayo yalisababisha damu kuvilia katika ubongo na kusababisha uvimbe ambao kwa kitaalamu unaitwa ‘traumatic brain injury’ na sisi tulithibitisha vipimo hivyo vya awali na kumsindikiza mpaka huko,” alisema Profesa Maseru.
Profesa Museru alisema Dk Mvungi alipata majeraha makubwa kichwani na sehemu nyingine mwilini ambayo yanaonekana yalisababishwa na kupigwa kwa vitu vyenye ncha kali au magongo na hivyo kuleta madhara katika ubongo.
Alisema hawezi kuthibitisha chanzo hasa cha kifo hicho kwani kinaweza kuwa ni kuharibika kwa ubongo au sababu nyingine zilizotokana na tatizo hilo (secondary causes).
Sekondari ya William Lukuvi wanafunzi walala darasani
Mmoja wa wanafunzi akiwa juu ya godoro hivi karibuni. Picha na Said Ng’amilo
Wiki iliyopita nilikwenda Morogoro ambako pamoja na mambo mengine nilikuwa na kipindi kwenye televisheni moja mkoani humo, kilicholenga kutoa ushauri kwa jamii kuhusu namna ya kupambana na changamoto za maisha. Baadaye nilikutana na watu waliokuja kwenye hoteli niliyokuwepo kwa lengo la kubadilishana mawazo zaidi kuhusiana na yale ambayo niliyaeleza kwenye televisheni. Mmoja wa watu alikuwa ni Erick Mtengele, kijana wa Kimasai ambaye amekuwa akihangaika huku na kule kutafuta namna ya kuwasaidia wafugaji nchini.
“Mimi ni kati ya Wamasai wachache nchini walio na elimu ya chuo kikuu, nimehitimu elimu ya maendeleo ya jamii katika Chuo Kikuu cha Tumaini mwaka 2010, kwa bahati mbaya hadi leo sina ajira,” anasema Mtengele ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Luganga, Kata ya Ilala Mpya, mkoani Iringa.
Tulizungumza mengi, yakiwemo matatizo ya sekta ya elimu nchini na harakati zake za kuwasaidia wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya William Lukuvi wapate angalau bweni, akisema kuwa ameandika barua maeneo kadhaa kuomba shule hiyo ijengewe bweni bila mafanikio.
“Shule haina mabweni, wanafunzi wanalala kwenye madarasa,” anasema Mtengele.
Baada ya mazungumzo hayo nililazimika kufuatilia ili kujua ukweli, nilibaini kuwa ni ukweli thabiti kwamba wapo wanafunzi wanalala kwenye madarasa katika shule hiyo, sababu kubwa ni kwamba shule haina uwezo wa kifedha wa kujenga mabweni.
“Huogopi kufuatilia shule hii?” anaonya mwandishi mmoja wa habari anayefanyia kazi mkoani Iringa kwa maelezo kuwa kufuatilia shule hiyo kunaweza kuzusha kutokuelewana na baadhi ya watu ambao kwa namna moja ama nyingine wanahusika na shule hiyo.
Mwandishi huyo anaonya kuwa hofu ya kufanyiwa mabaya ndiyo sababu waandishi walio wengi wanaogopa kuandika ukweli kuhusiana na shule hiyo kwamba baadhi ya wanafunzi wanalala katika madarasa tofauti katika shule hiyo.
“Kuna waandishi waliwahi kufuatilia suala hili na kuhoji kwa nini mabweni hayajengwi, matokeo yake siyo tu kwamba hawakupewa ushirikiano na wale ambao wanahusika kutolea maelezo jambo hilo, bali walionekana kama wanaingilia mambo yasiyowahusu, wengine hata wakajikuta katika hofu kuhusu maisha yao,” alionya mwandishi huyo.
Hata hivyo niliendelea kufuatilia kutokana na ukweli kwamba lengo la makala hii siyo kudhalilisha yeyote, bali kueleza ukweli ili kuangalia namna gani wanafunzi wanaweza kusaidiwa kwa kujengewa mabweni.
Kama yupo mwenye nguvu za kusumbua wale ambao wanaeleza ukweli kuhusiana na hali mbaya ya maisha ya wanafunzi kwa kukosa mabweni, nguvu hizo azielekeze kuhakikisha mabweni yanajengwa, tena ikiwezekana haraka.
Nguvu zake zitakuwa za maana zaidi ikiwa atafikiria namna ya kusaidia kupatikana kwa mabweni kuliko kukasirika kwa sababu ya kuandikwa ukweli kwamba Shule ya Sekondari William Lukuvi haina mabweni kiasi kwamba wanafunzi wanalazimika kulala darasani.
Katika kufuatilia ilibainika kuwa ni kweli kuna ugumu wa kupata ushirikiano, na pia hata baadhi ya waandishi wa habari wana hofu, kwa mfano kuna mwandishi alifanikiwa kupiga picha miezi kadhaa iliyopita wanafunzi wakiwa darasani wamelala, hakuweza kuzitumia, huku ulinzi ukiwekwa kuhakikisha hakuna mwandishi anayefanikiwa kufahamu hali hiyo ya watoto kulala darasani.
Changamoto
Japokuwa kuna changamoto kadhaa, lakini kutokuwa na mabweni inaonekana ni changamoto kubwa katika Shule ya Sekondari ya William Lukuvi iliyopo Jimbo la Isimani, wilaya ya Iringa.Shule hiyo ipo takribani kilomita 50 kutoka Manispaa ya Iringa.
Shule hiyo imepewa jina hilo kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Isimani, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, anayepongezwa kwa harakati mbalimbali za kuleta maendeleo katika jimbo hilo.
Shule hiyo imejengwa na wananchi wa Kata ya Ilolompya ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa shule ya sekondari katika kila kata ili kuhakikisha watoto wanaomaliza elimu ya msingi wanapata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari.
Sekondari ya William Lukuvi imejengwa na wananchi wa Kata ya Ilolompya kwa lengo la kuwahudumia wananchi wa vijiji vinne vya Magozi, Ilolo, Luganga na Mkombilenga; shule iko mbali na baadhi ya vijiji kiasi kwamba inalazimika baadhi ya wanafunzi kubaki shuleni kutokana na kushindwa kurudi nyumbani kwao kutokana na umbali na pia usalama kwani baadhi ya maeneo wanayopita ni mapori yanaonekana kutokuwa salama hasa nyakati za usiku.
Shule ina zaidi ya wanafunzi 251 wakiwemo wavulana 145 na wasichana 106 ambapo kidato cha kwanza kuna wanafunzi 100 wavulana 52 na wasichana 49, kidato cha pili 74 wavulana 49 na wasichana 25.
Kidato cha tatu 39 wanafunzi wakiwemo wavulana 26 na wasichana 13, kidato cha nne ni 36 ambapo wavulana 22 na wasichana 14. Tatizo la bweni ni kubwa hali inayosababisha wanafunzi wavulana kutumia chumba cha darasa kwa ajili ya matumizi ya kulala wakati wasichana wakitumia jengo ambalo linatumika kwa muda mfupi wakisubiri kukamilika kwa bweni lao.
Wengi wa wanafunzi wanatoka umbali wa kati ya kilomita moja hadi nne kufika shule na kuwa kwa wale wanaotoka umbali wa kilomita nne, maana yake ni kuwa wanatembea kilomita nane kwenda shule na kurudi nyumbani.
Umbali huo wa zaidi ya kilomita nane yaani kwenda na kurudi, umekuwa ukilalamikiwa na baadhi ya wanafunzi kuwa unawasababishia wengi wao kuchoka, hivyo kusababisha kurudisha nyuma maendeleo yao kimasomo.
Usikose mfululizo wa makala hii kesho kujua kinachoendelea, pamoja na kauli za uongozi wa shule.
Dk Mvungi afariki dunia
Dk Sengondo Mvungi
Dar es Salaam.Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi (61) amefariki dunia katika Hospitali ya Millpark Netcare, Johanesburg, Afrika Kusini.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana kutoka Afrika Kusini na kuthibitishwa na Msemaji wa Hospitali ya Millpark, Tebogo Nyembezi zinasema Dk Mvungi alifariki dunia jana mchana. “Ni kweli tulimpokea mgonjwa huyo kutoka Tanzania na alifariki 6:00 mchana (saa 7:00 kwa saa za Afrika Mashariki),”alisema Nyembezi.
Nyembezi alisema kwamba walimpokea mgonjwa huyo akiwa na majeraha ya kichwa, lakini aliahidi kueleza sababu ya kifo chake leo baada ya kuzungumza na madaktari waliokuwa wakimtibu.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba pia alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kwamba walikuwa wakiendelea kuandaa taratibu za kuleta mwili wake nchini.
“Ni pigo kubwa kwetu, tunaangalia namna ya kuusafirisha kuja nchini na baadaye tutatoa taarifa rasmi,”alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Kwa kweli ni pigo kubwa siyo kwetu tu, lakini pigo kubwa kwa nchi yetu, tumepoteza mtu muhimu na kiungo muhimu sana. Dk Mvungi, wengine tulimfahamu tangu alipokuwa mwanafunzi, alikuwa mtu aliyesema kile alichokiamini, akikwambia kitu kilikuwa ni kile kilichopo moyoni mwake”.
Jaji Warioba alisema Dk Mvungi alikuwa msomi aliyebobea katika masuala ya sheria na kwamba alikuwa na mchango mkubwa katika tume. Pia alisema marehemu atakumbukwa kwa ushiriki wake wa dhati katika kupigania haki za binadamu, kazi aliyoifanya kwa moyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani alisema: “Dk Mvungi alikuwa mfanyakazi hodari, alikuwa hachoki na hata ulipotokea ubishi mkubwa katika majadiliano kiasi cha watu wengine ku-loose temper (kupandwa na jazba), yeye alibaki vilevile na alizungumza vilevile bila kubadilika. Kweli tumempoteza mtu muhimu sana maana alikuwa akifahamu vizuri sana sheria, hatuna jinsi maana tumempoteza, kwahiyo itabidi tuendelee na kazi hii. Hatuna namna nyingine ya kufanya,”alisema Jaji Ramadhani.
Jaji Ramadhani alisema taratibu nyingine zitatangazwa baadaye kwani lazima washirikiane na chama chake, NCCR- Mageuzi alikokuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji, familia yake na Chuo Kikuu cha Bagamoyo ambako alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliliambia gazeti hili kwamba walipokea taarifa ya kifo cha Dk Mvungi saa 9.30 alasiri jana. “Tumepokea taarifa hizo alasiri kwamba amefariki. Ni kweli na sasa ninaelekea nyumbani kwake ili kuitaarifu familia,”alisema Mbatia.
Taarifa ya Tume
Jana jioni, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa rasmi kuhusu kifo cha Dk Mvungi ikisema: “Kwa masikitiko makubwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dk Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Millpark iliyopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini amefariki dunia.”
Taarifa iliyotolewa Katibu wa tume hiyo, Assaa Rashid ilisema Dk Mvungi alifariki dunia saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini.
Iliendelea kusema taarifa hiyo kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka Afrika Kusini kuja nchini kwa maziko zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
Dk Mvungi, alikuwa akitibiwa Afrika Kusini baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana walipovamiwa nyumbani kwake Kibamba, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu.
Alipelekwa nchini Afrika Kusini, Novemba 7, 2013 kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa siku tano kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi) jijini Dar es Salaam.
Dk Mvungi, ambaye aligombea urais mwaka 2010 kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi, alijeruhiwa vibaya kichwani na sehemu nyingine za mwili wake baada ya kukatwa mapanga na wavamizi hao.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Profesa Costa Mahalu alisema chuo hicho kimepoteza mtu muhimu sana, kwani ni mmoja wa waanzilishi waliokuwa wakifahamu vyema malengo na dira yake.
“Tumepata pigo kubwa sana kwani tumempoteza mtu ambaye tulishirikiana naye katika kuanzisha chuo hiki na aliyafahamu vyema malengo na dira yake, alikuwa ni mwalimu mzuri aliyebobea katika constitutional laws (sheria za Katiba) na wanafunzi walimpenda sana,”alisema Profesa Mahalu.
Profesa Mahalu alisema Dk Mvungi ambaye alikuwa naibu wake kabla ya kujiunga na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walifahamiana naye siku nyingi na kwamba wakati marehemu alipokwenda kusoma Shahada ya Uzamivu nchini Ujerumani alifikia nyumbani kwake (kwa Mahalu).
“Wakati huo nilikuwa nikifundisha Ujerumani, alikuja kusoma PhD yake ya masuala ya sheria na alifikia nyumbani kwangu, tutamkumbuka kwa uhodari wake katika kuchapa kazi, kweli tumempoteza mtu mahiri sana,”alisema.
Chadema, CCM wamlilia
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema amesikitishwa na taarifa za kifo cha Dk Mvungi na kwamba taifa limempoteza mwanzilishi wa mageuzi ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kudai Katiba Mpya.
“Tumepokea taarifa za kifo hiki kwa mshtuko mkubwa, tunamwomba Mwenyezi Mungu aipe nguvu familia ya Dk Mvungi, tunatoa pole kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na uongozi wa NCCR-Mageuzi,” alisema Mbowe.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa (CCM), Mwigulu Nchemba alisema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na kutoa pole kwa Watanzania wote kwa sababu Dk Mvungi alikuwa anafanya kazi muhimu ya kuwezesha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Alisema amekufa wakati mchango na mawazo yake yakiwa yanahitajika kwa kiasi kikubwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba CCM kinaendelea kuisisitizia Serikali iwasake wahalifu hao ili wafikishwe kwenye vyombo vya dola.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema ameshtushwa na taarifa za kifo hicho ambacho kimetokea wakati Dk Mvungi akifanya kazi muhimu ya kuitafuta Katiba Mpya. “Naomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, amina,” alisema.
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila alisema taifa limepoteza mtu muhimu na kwamba hali ya ulinzi ni suala linalohitaji mjadala wa kitaifa.“Tunahitaji kuangalia kiini cha uhalifu hapa nchini, watu wanateswa na kujeruhiwa ovyo ni lazima tuchukue hatua,” alisema.
Mitandao ya kijamii
Muda mfupi baada ya taarifa za kifo chake, mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Jamii Forum ilikuwa ilitawaliwa na salamu za pole kutoka kwa watu mbalimbali.
Hussein Bashe kwenye ukurasa wake wa Facebook aliandika kuwa, “Dr Sengondo Mvungi Is No More (hatunaye tena), taarifa zilizonifikia kutoka Hospitali ya Millpark, ndugu yetu Mvungi amefariki, mnamo saa tisa na nusu.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Wahalifu wamekatisha uhai wake wakati akifanya jukumu zito kwa ajili ya taifa letu. Jambo hili linaumiza sana Mungu atalipia uhalifu huu, poleni Tume ya Katiba, Poleni Familia, poleni NCCR-Mageuzi.”
Mtu mwingine aliyechangia suala hilo kwenye mtandao wa Jamiiforum ni yule aliyejitambulisha kwa jina la Ta Muganyizi aliyeandika kuwa, RIP Dr. Mvungi... Mungu akulaze mahala pema peponi. Japo umeondoka kivuli chako kitaishi... Naipa pole familia yako, maisha yetu kwa sasa nchini ni kudra za Mwenyezi Mungu. Ni kwamba tupigwe... wengine wamepona lakini wewe umeondoka.”
NABII ABAKA
Mama Mzazi wa Mwanafunzi anaedaiwa kubakwa Mary Mkombola akisimulia juu ya tukio la ubakaji lililompata Mwanae na kusababisha ujauzito mbele ya waandishi wa habari Kulia ni Martha Danie 17 aliyefanyiwa kitendo hicho.
Mwanasheria Mfawidhi Mkazi wa kituo cha msaada wakisheria cha Tanzania Legal Aid Centre [TALAC]
Godwin Ngongi akifafanua jambo kuhusu kitendo
cha ubakaji alichofanyiwa Mwanafunzi wa kidato cha tatu Martha Daniel [17] mbele ya waandishi wa habari ofini kwake jana, kulia ni mzazi wa mwanafunzi huyo Mary Mkombola
cha ubakaji alichofanyiwa Mwanafunzi wa kidato cha tatu Martha Daniel [17] mbele ya waandishi wa habari ofini kwake jana, kulia ni mzazi wa mwanafunzi huyo Mary Mkombola
Na John Banda,
Dodoma
NABII Elisha Muliri wa kanisa la Ebeneza mjini hapa ameingia matatani baada ya kudaiwa kumbaka na kumtia mimba mwanafunzi na kukatiza masomo yake huku kutishia kumuua.
Akisimulia tukio hilo mbele ya waandishi wa habari mwanafunzi huyo Martha Daniel [17] kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya City ilyopo manispaa ya Dodoma alisema kabla ya kufanyiwa kitendo hicho alikuwa anaangushwa na mapepo.
Martha alisema baada ya kuhangaika kwa muda mrefu bila mafanikio walipata taarifa za ujio wa nabii huyo mjini humo na wapofika ili kupata msaada wa kuombewa mapepo hayo yalilipuka na binti akaponywa hata leo na kuahidiwa mbele ya kanisa kusaidiwa ada na Nabii huyo.
Binti huyo alisema baada ya kuponywa akaendelea kwenda kusali kanisani hapo ambapo kutokana na kila mtu anayefika na kufanyiwa maombi huacha mawasiliono kwenye vikaratasi, na Juni 8 mwaka huu akapigiwa simu na Nabii huyo akipewa maelekezo ya kufika nyuma ya ukumbi wa Paradise ambapo walikuwa wakifanyia ibada.
Anatanabaisha kuwa baada ya kuonana na Nabii alimwambia aingie kwenye Gari akaingia akifikili kuna heri akapewa soda aina ya Fanta orange alipokunywa akapoteza fahamu na alipokuja kuzinduka alijikuta akiwa nyumba za kulala wageni makole na Nabii akiwa amemlalia kama alivyozaliwa huku akiangalia mkanda wa Ngono.
‘’Wakati nataka kupiga kelele alinitishia kwamba ataniua kama nitathubutu kumwambia mtu yoyote jambo hilo, akanipiga kofi na kuniambia yeye hawezi kunilipia ada bure kwa sababu mimi siyo ndugu yake lazima lazima alale na mimi mara 5 kwa hiyo bado mara 4 na kunisisitiza asisikie popote kuwa alinifanyia hivyo’’, alisema Mwanafunzi huyo
Kwa upande wake Mama mzazi wa mwanafunzi huyo Mary Mkombora alisema alimpeleka kuombewa kutokana na kusubuliwa na mapepo tangu akiwa Darasa la sita na wakakubaliana na Nabii huyo kumlipia ada kwa awamu hivyo akachukue 50,000 kila mwezi ili kukamilisha 400,000 inayotakiwa shule.
Nilimgundua yupo tofauti kuanzia mwezi wa saba nilipomuuliza alisema yeye haelewi siku moja asubuhi nikamshuhudia akitapika ndipo nilipomchapa na kumfukuza. Nikapigiwa simu na waliompokea mtoto kua aliyempa mimba ni Nabii huyo ndipo nikachoka, na alipopimwa alikuwa na mimba.
Nabii huyo ambaye alikuwa Mume wa mwimbaji Marufu wa Nyimbo za Injili marehemu Anjela Chibalonza kwa sasa hajulikani alipo japo mara kadha wasaidizi wa kanisa hilo ambalo limebadilishwa jina kutoka Shakinah Pentecostal Church na kuitwa Ebeneza .
‘’sasa hivi mimi na mtoto wangu tumekuwa tukiishi mashakani baada ya Msaidizi wake Nabii Monica nimpe Martha akamtoe mimba kwa wataalamu anaowajua wao, siku ambayo alichukua kadi yenye namba za simu na kufuta meseji zote mwanangu alizokuwa akiandikiwa na Nabii,’’
Nabii huyo kwa sasa hajulikani alipo na hata alipotafutwa kwa simu yake ka mkono 0756 409118 ilikuwa amezimwa na msaidizi wake Nabii Monica Nyambura raia wa nchini Kenya anakotokea Elisha Muliri alisema yeye hawezi kuongelea jambo hilo kwakua yeye ni mgeni ameachiwa kanisa hilo baada ya mwenyeji wake kuwa safarini hivyo asubiliwe hatachelewa.
Tukio hilo limefikishwa katika kituo cha sharia cha Tanzania Legal Centre [TALAC] na mwanasheria mfawidhi mkazi Dodoma Godwin Ngongi tayali ameshamuandikia mkuu wa kituo cha polisi kati barua ya kuwataka kumkamata mtuhumiwa huyo ili afikishwe kwenye vyombo vya sharia na pia kuepusha mwanfunzi huyo na hatari nyingine.
Jeshi hilo limekiri kuwa na taarifa ya tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi
Atupa kichanga
Na John Banda, Dodoma
JESHI la polisi mkaoani Dodoma linamshikilia Mwanamke mmoja kwa kosa la kumtumbukiza mtoto chooni akiwa hospitali ya mkoa alikopelekwa kujifungua.
Tukio la kukamatwa kwa mwanamke huyo aliyekuwa amepelekwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoani hapa baada ya kushikwa na uchungu wa kujifungua lilitokea majira ya saa tisa usiku.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Damas Nyanda Alimtaja mwanamke huyo kuwa anaitwa Sinsia Laurent 28 msandawe mkazi wa uhindini mjini hapa.
Nyanda alisema baada ya kufikishwa hospitalini aliomba kwenda chooni kujisaidia na baadae manesi walibaini kulikuwa na mwili wa kichanga muda mfupi baada ya mtuhumiwa huyo kutoka chooni.
‘’tulipokea taarifa muda huo na tulipofika tulikuta mwili wa kichanga cha jinsia ya kiume ukiwa nje wakati kichwa kikiwa tayali kimesukumwa ndani ya choo hicho tulipomtoa alikuwa tayali ameshafariki’’, alisema Nyanda.
Aidha nyanda alisema wanaendelea kumshikilia mwanamke huyo na uchunguzi utakakamilika atafikishwa mahakamani.
Kwa upande wake Leah aliyempeleka hospilini hapo ambae ni mfanyakazi mwenzie katika baa ya CDA Clab iliyopo Uhindini alisema mtuhumiwa huyo siyo mkweli kwa kutoweka wazi kuwa mimba yake ilikuwa na miezi mingapi maana wao waliambiwa ilikwa na miezi 5.
Aliongeza kuwa kitendo hicho alichokifanya Mwenzao ni cha kinyama na hakikustahili kufanywa katika nyakati tulizonazo maana kuna njia nyingi za kuzuia mimba kama anakuwa hayuko tayali kupata mtoto.
Unyama Kenya : Waliouawa na magaidi wafikia 69
Baadhi ya raia, waliokuwa ndani ya jengo hilo wakitoka nje kwa hofu kubwa jana,
Bado jengo hilo limezingirwa na wanajeshi, kuhakikisha magaidi hao hawatoki nje kuhatarisha usalama wa wananchi.
Nairobi. Magaidi wanaokadiriwa kuwa kati ya 10 na 15 wamelitikisa Jiji la Nairobi kwa siku mbili mfululizo baada ya kuteka jengo kubwa la biashara la Westgate lililopo Westlands na kuua watu wapatao 69 hadi leo asubuhi.
Magaidi hao walivamia jengo hilo juzi saa tano asubuhi na hadi jana, jitihada za kuwadhibiti zilikuwa hazijafanikiwa. Zaidi ya watu 1,000 wameokolewa na wengine zaidi ya 170 wamejeruhiwa.
Tukio hilo limesababisha shughuli mbalimbali katika Jiji la Nairobi kusimama na hata maduka mengine makubwa ya Nakumatt kufungwa, hivyo kusababisha upatikanaji wa bidhaa mbalimbali kuwa shida kwa wakazi wengi wa Nairobi.
Wakazi wengi wa eneo la Westlands jana walikwama kufika katika maeneo yao na watu wengi waliokuwa kwenye jengo hilo waliacha magari yao na kukimbia huku na huko ili kujiokoa huku vyombo vya usalama vikiwataka wananchi kukaa mbali na eneo hilo.
Magaidi hao wanaodaiwa kuvalia vitambaa vyeusi vinavyofunika nyuso zao, wameteka eneo hilo kwa siku mbili, huku wakiwa wamezima taa zote za ili kujilinda na askari wa Kenya ambao waliingia kupambana nao.
Risasi zimekuwa zikisikika usiku kucha na watu zaidi wameendelea kuuawa huku Serikali ikisema mateka wanaodaiwa kuwepo ndani ya jengo hilo wakiwa chini ya magaidi hao ni 30.
Jengo hilo limezingirwa na vyombo vya usalama vya ndani na nje ya Kenya vikiongozwa Mkuu wa Majeshi ya Kenya pamoja Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), David Kimaiyo, ambaye amekuwa akitoa taarifa mbalimbali za tukio hilo kupitia account yake ya Tweeter ili kuhakikisha vyombo vya habari na jamii vinajua kinachoendelea.
Pia Wizara ya Mambo ya Ndani imekuwa ikitoa taarifa kupitia mitandao yake, huku televisheni zote za Kenya zikirusha tukio hilo moja kwa moja tangu lilipotokea juzi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku akizungumza na vyombo vya habari alisema watu 69 waliouawa ni pamoja na raia wa kigeni kutoka nchi mbalimbali. Hata hivyo, alisema haijajulikana ni wangapi na wanatoka nchi gani haswa.
Canada imethibitisha kuwa raia wake wawili wameuawa kwenye tuko hilo, pia raia wawili wa Ufaransa nao wameuawa.
Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limedai kuhusika na tukio hilo ambalo ni kubwa kutokea Kenya tangu ubalozi wa Marekani ulipolipuliwa mwaka 1998 jijini Nairobi.
Subscribe to:
Posts (Atom)





