Malaysia:Shughuli zaendelea kuisaka ndege

Picha za kinachodhaniwa kuwa mabaki ya ndege ya Malaysia nchini Australia
Ndege na meli kutoka nchi mbali mbali zinaendelea kuitafuta mabaki ambayo huenda yanatokana na ndege ya Malaysia iliyopotea takriban wiki mbili zilizopita ikiwa imebeba takriban watu 240.
Matumaini ya kutatua kitendawili hicho yaliongezeka baada ya Australia kutoa picha za Satelaiti za vitu viwili vilivyoonekana baharini vuikidhaniwa kuwa vifusi vya ndege hiyo.
Hata hivyo hadi kufikia sasa hakuna cha maana kilichopatikana.
Afisa mmoja mkuu wa New Zealand amesema operesheni hiyo ilitatizwa na kuchafuka kwa bahari na kutoona vizuri.
Meli ya mizigo ya Norway ilitumia taa kuyatafuta mabaki hayo pasina kufanikiwa.

Kizungumkuti cha amani Sudan Kusini


Makamu wa Rais wa zamani wa Sudan Kusini Riek Machar analaumiwa kwa kupanga njama ya mapinduzi

Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan Kusini na waasi wanaoongozwa na aliyekuwa naibu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar yanatarajiwa kuanza tena leo mjini Addis Ababa Ethiopia.

Mazungumzo hayo yaliahirishwa mapema mwezi huu baada ya mazungumzo ya hapo awali kukwama.

Aidha, pande zote mbili zimetuhumiwa kwa kukiuka mkataba wa kusitisha mapigano uliotiwa saini mwezi Januari.

Mnamo siku ya Jumatano, mataifa ya magharbi yanayohusika na mgogoro huu wa Sudan Kusini katika kuutafutia suluhu la kudumu, walitishia kuwawekea vikwazo wahusika wakuu kwenye mgogoro huo ikiwa hawatausuluhisha.

Mazungumzo ya kuzipatanisha pande hizo hayajapiga hatua kwa wiki mbili zilizopita huku wahusika wakilaumiana.

Serikali na waasi wanalaumiana kwa kuyumbisha mazungumzo ya amani

Nao mkataba wa amani uliotiwa saini kusitisha vita pia haujafanikiwa katika kumaliza mgogoro huo.

Baadhi ya wanadiplomasia kutoka nchi za magharibi, wamehoji ikiwa viongozi wamejitolea kikweli kutafuta muafaka huku kila mhusika akimlaumu mwenzake kwa kizungumkuti kilichoko.

Mazungumzo hayo yanaanza tena baada ya wiki mbili ya kusitishwa kwake, ingawa wajumbe wamesema haijulikani ikiwa pande hizo mbili zitakuwepo.

Maswala makuu yanayoyumbisha mazungumzo hayo, ni matakwa ya waasi wa Sudan Kusni kwamba wafungwa wanne wa kisiasa ambao bado wanazuiliwa, sharti waachiwe huru.

Wanne hao walilaumiwa kwa kupanga njama ya mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir wakiongozwa na aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar

Majibizano kati ya Marekani na Urusi UN


Mabalozi wa Marekani na Urusi wameshambuliana katika Umoja wa mataifa.
Majibizano makali yameshuhudiwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo mataifa mengi yameshutumu
uamuzi wa Urusi kunyakua eneo la Crimea,kilele hatahivyo ilikuwa majibizano makali baina ya mabalozi wa Marekani na

Urusi .

Balozi wa Urusi, Vitaly Churkin, alisema kuwa watu wa Crimea walikuwa wamefanya maamuzi yao juu ya siku zao za

usoni.

Naye Balozi wa Marekani, Samantha Power akajibu akisema kile kinachotajwa na Urusi kama kura ya maoni ni kura

bandia.

Akikasirishwa na matamshi ya Power, Bwana Churkin alisema kuwa Balozi Power alikuwa amejishushia hadi kufikia

kiwango cha magazeti ya udaku.

Balozi huyo wa Urusi pia alitisha kuwa huenda Urusi ikakataa kushirikiana na Marekani katika maswala mengine muhimu

ya kimataifa iwapo Marekani itaendelea na msimamo wake juu ya Ukraine.

Majibizano hayo makali yanaendelea wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon anapoelekea Urusi kufanya

mashauriano na Rais Putin kwa lengo la kutafuta suluhu ya kidiplomasia.

Mkuu wa Majeshi nchini Ukraine, Andriy Parubiy, amesema Serikali yake inafanya kila juhudi kuwarejesha nyumbani

wanajeshi wake na familia zao walio eneo la Crimea, kufuatia hatua ya Urusi ya kunyakua Crimea.

Ulevi wa Shisha washika kasi

Mtumiaji wa shisha akipata kilevi hicho


Dar es Salaam. Umeibuka ulevi mpya nchini ambao umethibitika kuwateka vijana hasa wa jiji la Dar es Salaam, huku kukiwa na taarifa za kitaalamu kwamba ulevi huo una athari za kiafya kwa watumiaji.

Ulevi huo ni kupitia starehe au anasa mpya ya uvutaji shisha; ulevi ambao watengenezaji hutumia chombo maalumu chenye bomba la kutolea moshi, ambacho huwekwa tumbaku, maji na moto.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa tumbaku huwekwa katika chombo hicho na kuunguzwa kwa moto, kisha moshi wa tumbaku hupita kwenye maji na huingia kwenye bomba, kisha watumiaji huanza kuvuta.

Sehemu maarufu ambako shisha inauzwa ni Ufukwe wa Coco, maeneo ya Kinondoni, Mwananyamala, Sinza Barabara ya Shekilango na maeneo kadhaa ya mitaa ya mjini.

Mmoja wa watumiaji wa shisha, Ismail Ndunguru alisema yeye na vijana wenzake hutumia siku za mwisho wa wiki kwenda kuburudika kwa uvutaji katika hoteli moja iliyopo mjini, Mtaa wa Garden jijini Dar es Salaam.

“Kuvuta shisha kwa siku nzima ni Shilingi 10,000, mkimaliza, mnarudisha bomba. Tukiwa vijana wengi inafurahisha sana kuvuta,” alisema Ndunguru.

Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kuwa, mkupuo mmoja wa shisha, una kemikali hai 4,800 na kwamba kemikali hizo husababisha saratani ya mapafu, maradhi ya moyo na maradhi ya mfumo wa upumuaji.

WHO inaeleza kuwa, kiasi cha uvutaji wa shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 100 au 200.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili na mfumo wa hewa, Meshack Shimwela alisema madhara ya shisha ni kama yale yanayosababishwa na uvutaji wa sigara pengine na zaidi kutokana na kilevi hicho kuwa na tumbaku nyingi.

Dk Shimwela alisema licha ya kuwa watengenezaji na wavutaji wa shisha hudai kuwa haina madhara kwa sababu huchanganywa na maji, lakini bado madhara yake ni makubwa.

“Maradhi yote yanayosababishwa na uvutaji wa sigara ndiyo yanayosababishwa na shisha, kwa mfano saratani ya mapafu na mdomo, kifua kikuu na mzio ambao unaweza kusababisha pumu,” alisema Dk. Shimwela.

Dk. Shimwela alisema ni vizuri watumiaji wakajua madhara ya shisha, badala ya kuchukulia kuwa ni mtindo wa maisha tu au starehe isiyo na madhara.

Hivi karibuni, Profesa Twalib Ngoma, Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, alisema asilimia 40 ya saratani zote nchini zinasababishwa na matumizi ya tumbaku.

Biashara inavyofanyika

Shisha inauzwa katika sehemu kadhaa za starehe za Jiji la Dar es Salaam kwa sasa na maeneo yanayouza bidhaa hiyo yanafahamika kama ‘shisha lounge au shisha point’.

Mwandishi wa Mwananchi akiambatana na Ndunguru walikwenda hadi Kinondoni katika hoteli moja ambako wavutaji wa shisha walikuwa wakiendelea ‘kuburudika’ huku wakipuliza moshi hewani.

Waliitozwa Sh15,000 kisha nao waliletewa chombo cha kuvutia. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa bei ya shisha hutegemea sehemu inapouzwa, hivyo huuzwa kati Sh10,000 na 70,000.

Ndunguru alisema shisha haina madhara kwake ingawa alipovuta kwa mara ya kwanza, alikohoa sana lakini sasa anaiona kuwa kiburudisho kinachompa faraja kama wavutaji wa sigara na kwamba hamu ya kuvuta kila mara imeingia mwilini mwake.

Ilibainika kuwa kwenye shisha huwekwa ladha kadhaa kama vile vanila, strawberry, mint, chocolate au kahawa ili kuwavutia wavutaji. Ladha hizo zinatajwa kuwa kivutio cha mabinti ambao wameingia kwa kasi kwenye uvutaji huo.

Kadhalika uchunguzi ulibaini kwamba wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu, kwa makundi hujikusanya na kuchanga fedha kwa ajili ya kuvuta shisha.

Habari zaidi zinadai kuwa wafanyabiashara wa shisha hivi sasa wanachanganya dawa za kulevya kama heroin na bangi katika shisha kama kivutio kwa watumiaji.

“Hii ni biashara kubwa sana sasa hivi, kwa siku moja, mimi naingiza zaidi ya Sh150,000 kwa kuuza bomba la shisha,” anasema mfanyabiashara mmoja wa Kinondoni.

Muuzaji wa shisha katika eneo la Coco Beach, Said Coco alisema biashara hiyo ni nzuri na kwamba wateja wamekuwa wakiongezeka kadiri kila siku.

Coco alisema wateja wake wakubwa ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 40 ambao huvuta shisha kila mwishoni mwa wiki.

Hata hivyo, alikanusha habari kwamba wafanyabiashara wanaweka dawa za kulevya na bangi kwenye shisha, ingawa anasema kama wapo wanaofanya hivyo basi wanaharibu starehe hiyo ambayo yeye anasema haina madhara.

Serikali inasemaje?

Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid alisema anafahamu kuwa shisha imepata umaarufu nchini hususan Dar es Salaam, lakini ni vigumu kuwakamata watumiaji.

Alisema wizara haiungi mkono matumizi ya shisha kwani inafahamu kuwa ni kilevi hatari pengine kuliko sigara za kawaida na pombe.

“Shisha ni hatari na sisi hatuungi mkono, lakini hatuwezi kuwakamata watumiaji kama ambavyo hatuwezi kuwakamata walevi wa sigara na pombe. Lakini tunawaasa watengenezaji wa shisha kuweka nembo ionyeshayo kuwa ni kilevi hatari,” anasema.

Dk. Rashid alisema matumizi ya tumbaku yanasababisha maradhi mengine hasa saratani ambayo inasababisha kiharusi, maradhi ya moyo na ngozi.

Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema hana taarifa za ongezeko la matumizi ya shisha nchini, ingawa aliwahi kuona kilevi hicho nchini Misri.

Nzowa alisema ikiwa itagundulika kuwa shisha ina wingi wa Nicotine, atachukua hatua kali dhidi ya wahusika, huku akitoa mfano wa kilevi cha kuber kilichowahi kupigwa marufuku.

Asili ya shisha

Shisha ni jina lenye asili ya Misri (sheesha) lenye maana ya bomba la maji lililounganishwa kwenye kontena.

Tumbaku iliyochanganywa na ladha ya matunda, hujazwa kwenye chombo mfano wa chetezo, moto huwekwa kati na sehemu moja huwekwa maji.

Moshi wenye harufu au ladha hutoka kupitia bomba hilo na kuvutwa.

Mvutaji huvuta kwa kutumia bomba (huweza kuwa la plastiki) na mabomba mengine yanaweza kutumiwa na kutupwa (disposable).

Athari zake kiafya

Kuharibu ogani; Shisha inatajwa kuwa na hewa ya carbon monoxide ambayo huingia kwenye mapafu na kuchukua nafasi ya hewa safi ya oxygen, hivyo ogani muhimu kuharibika.

Saratani; Shisha ina wingi wa nicotine, kiwango cha kemikali za tar, carbon monoxide, metali za kiwango cha juu kama cobalt na lead ambavyo ni visababishi vya saratani.

Utegemezi (adiction); Uvutaji wa shisha husababisha kutengenezwa kwa kiwango kikubwa cha nicotine kwenye damu, hivyo mtu akishazoea kuvuta hawezi kuacha kwani kilichomo kwenye shisha huvutwa kwenye neva za fahamu na kusababisha mishipa hiyo kwenye ubongo kuhisi kupata faraja na raha ya kipekee.

Maradhi ya kuambukiza; Uvutaji wa shisha hutumia bomba ambalo watu kadhaa hushirikiana. Hali hii husababisha maradhi ya kuambukiza kama Kifua Kikuu (TB) na hepatitis B (homa ya ini).

Mwanasheria Mkuu SMZ haujui waraka wa Kificho

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Amir Pandu Kificho akimkaribisha kwenye kiti, Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge hilo, Samuel Sitta baada ya kuapishwa kushika nafasi hiyo, bungeni Dodoma jana.  
Picha na Emmanuel Herman 


Zanzibar. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Masoud Othman Masoud amesema hajawahi kuuona waraka ulioandikwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) na kusainiwa na Spika Pandu Ameir Kificho unaopendekeza Tanganyika na Zanzibar kuwa na mamlaka huru za dola na kuwasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akizungumza na Mwananchi AG Masoud amesema waraka huo ulitayarishwa na kamati ya uongozi chini ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Spika Kificho, baada ya kufanyika vikao vilivyowahusisha wajumbe wa kamati ya uongozi ya Baraza hilo na kutoa mapendekezo yake.

Masoud alisema licha yeye kuwa si mjumbe wa kamati hiyo lakini huingia kama mjumbe mualikwa, ambapo kikao cha kwanza alishiriki kujadili mambo ya msingi yanayotakiwa kuwasilishwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba kama maoni ya taasisi lakini hakumbuki kuhudhuria kikao cha mwisho ambacho kiliandaa mapendekezo hayo.

“Mpaka sasa waraka uliowasilishwa mbele ya Tume ya Jaji Warioba bado sijauona kwa macho yangu, siwezi kusema kama ulikuwa waraka halali au batili ila nasikia mivutano inayojitokeza miongoni mwa wajumbe wake,” alisema AG Masoud.

Alisema Baraza kama Taasisi lilitoa maoni kama walivyotoa maoni baadhi ya makatibu wakuu wa SMZ na taasisi nyingine ambazo zinaguswa au kufanya kazi zinazohusiana na mambo ya msingi yaliomo katika orodha ya mambo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, alisema kama kamati ya uongozi ya Baraza akidi ya wajumbe ikitimia ina uwezo wa kutoa mapendekezo kwa niaba ya taasisi na kusema si mwafaka kwa sasa kumjadili Spika peke yake, kama kuna ukiukwaji wa sheria au kanuni za Baraza kulikojitokeza.

Pia Mwanasheria Mkuu huyo wa SMZ alibeza kitendo cha Baraza la Wazee wa CCM kuondoa imani kwa Spika Kificho na kumtaka ajiuzulu, badala yake alisema kama kuna makosa yamefanyika, basi kamati nzima ya uongozi ya Baraza hilo inatakiwa ijiuzulu.

“Si haki na sahihi kumshinikiza Spika ajiuzulu, kama kuna kasoro zimefanyika, kamati nzima ya uongozi ya BLW nayo inapaswa kuwajibika. Suala hilo halikuwa la Spika ila ni la taasisi,” alisema Mwanashseria Mkuu huyo wa SMZ.

Alisema kimsingi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haina maoni wala mapendekezo yake kuhusu mabadiliko ya muundo wa Muungano uweje na hata Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, hajawahi kuweka bayana msimamo wake kama kiongozi Mkuu wa Zanzibar.

Hata hivyo AG Masoud alikiri kuwa msimamo pekee ambao Dk Shein amekuwa akiutetea ni ule wa chama chake wa kuendelea kuwapo muundo wa Muungano wa Serikali mbili ambao hautokani na msimamo wa SMZ.

Mwanasheria Mkuu huyo pia alisema ni mapema kwake kutoa tathmini na mwelekeo wa mjadala wa Bunge la Katiba kama Zanzibar itaweza kufikia malengo yake ya kupata katiba yenye masilahi na Zanzibar, kutokana na mgawanyiko uliopo wa wajumbe kutoka Zanzibar uliojitokeza unaoegemea sera za vyama na itikadi za kisiasa.

Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar tayari limetoa tamko la kupoteza imani na Spika Kificho kwa kitendo chake cha kuandika waraka unaopendekeza Zanzibar na Tanganyika zipate mamlaka huru za dola, bila ya kuwepo kwa mapatano na uamuzi wa pamoja wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Wazee hao wamesema hiyo ni aina ya hujuma na usaliti kinyume na utaratibu wa hadhi ya Spika aliyekabidhiwa dhamana hiyo nyeti katika mgawanyo wa madaraka chini ya mihimili mitatu.

Kwa upande wake Spika Kificho amekiri kuwa hakuna uamuzi wa pamoja uliofikiwa na Baraza lake katika kupendekeza aina ya muundo wa mfumo wa Muungano, kutokana na pande mbili za kisiasa za CCM na CUF kila moja kuwa na msimamo wake kisera.

Kificho ameendelea kusisitiza kuwa waraka aliousaini na kuuwasilisha mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, ulijadiliwa na kuridhiwa na kamati ya uongozi jambo ambalo limekanushwa na Mnadhimu wa Baraza hilo upande wa CCM, Salmin Awadh Salmin ambaye alisema waliotoa mapendekezo hayo ni kigenge cha watu watano kinyume na utaratibu wa pamoja wa kamati ya uongozi yenye wajumbe 15.

Malaysia:Juhudi za kuisaka ndege zashika kasi

Marekani pia imejiunga na juhudi za kuitafuta Ndege ya Malaysia

Wiki moja tangu ndege ya Malaysia iliyokuwa imewabeba abiria 239 kutoweka, juhudi za kimataifa kuisaka ndege hiyo bado zinaendelea.

Mataifa kumi na mbili sasa yamejiunga pamoja kuisaidia serikali ya Malaysia na msako huo, juhudi zenyewe zikijikita zaidi Magharibi mwa rasi ya Malaysia.

Marekani imesema kuwa inatuma manowari zake za kivita, pamoja na ndege maalum ya uchunguzi katika maeneo ya Bengal, Bahari ya Andaman na sehemu za Bahari hindi.

Mnamo Ijumaa taarifa ziliibuka kuwa ndege hiyo ilituma mawasiliano katika kituo cha trafiki ya ndege kwa karibu saa tano baada ya taarifa ya kupotea kwake kutolewa.

Taarifa zinasema kuwa mawasiliano hayo yanaweza kusaidia katika kujua iliko ndege hiyo na ndio maana Marekani ikaamua kutuma meli zake za kivita katika Bahari Hindi.

West Brom yamtimua Nicolas Anelka


Nicolas Anelka

Mchezaji wa klabu ya soka ya West Brom, Nicolas Anelka amefutwa kazi kwa kosa la utovu wa nidhamu.

Klabu hiyo iliamua kuchukua hatua hiyo baada ya Anelka kutangaza kupitia mtandao wa kijamii kuwa anaacha kazi.

Anelka alisema kuwa anaondoka katika klabu hiyo baada ya kukosa kutatua tofauti zilizopo kati yake na Albion kuhusu ishara yake yenye utata ambayo inasemekana kuwa ya kibaguzi dhidi ya wayahudi.

Mshambuluaji huyo mwenye umri wa miaka 35, alipigwa marufuku kutocheza mechi tano na kutozwa faini ya pauni 80,000 na shirikisho la soka Uingereza ,kwa kufanya ishara hiyo, baada ya kuingiza bao dhidi ya klabu ya West Ham mwezi Disemba.

West Brom imechukua hatua ya kumfuta kazi Anelka kutokana na ishara hiyo na pia kwa sababu ya matamshi yake kwenye mtandao wa kijamii.

Ishara hii inapigiwa debe na msanii wa Ufaransa Diedonne M'bala M'bala

Awali aliachishwa kazi mwa muda na Albion, wakati klabu hiyo ilipokuwa inafanya uchunguzi wake binafsi.

Mapema siku ya Ijumaa, Anelka alitangaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa anaondoka katika klabu hiyo.

Aliandika: "kufuatia mazungumzo kati yangu na maafisa wa klabu, kuna masharti kadhaa ambayo wamenipa kabla ya kujiunga tena na klabu hiyo, Masharti ambayo siwezi kuyakubali.''

Hata hivyo klabu ilisema kuwa masharti yaliyotolewa kwa Anelka ni pamoja na kumtaka awaombe msahama mashabiki , wadhamini na jamii kwa ujumla kwa athari iliyotokana na ishara yake aliyoifanya Disemba tarehe 28 na pili akubali kutozwa faini.

Jasusi wa zamani Rwanda jela miaka 25

Simbikangwa alikuwa mkuu wa ujasusi wa Rwanda wakati wa mauaji ya Kimbari

Mahakama nchini Ufaransa, imemhukumu kifungo cha miaka 25 jela jasusi mkuu za zamani wa Rwanda Pascal Simbikangwa kwa kuhusika na mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Simbikangwa alipatikana na hatia ya kuhusika na mauaji hayo na kutenda uhalifu dhidi ya binadamu.

Alikabiliwa na makosa ya kuchochea , kupanga na kusaidia katika juhudi za mauaji ya watutsi hasa kwa kuwapa silaha wapiganaji wa kihutu waliokuwa wanalinda vizuizi vya barabarani na kuwaua wanaume wa kabila la Tutsi, wanawake na watoto.

Simbikangwa alikanusha madai hayo.

Haijuikani kama mawakili wa Simbikangwa watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Simbikangwa,mwenye umri wa miaka 54, anatumia viti vya magurudumu baada ya kuhusika na ajali mwaka 2008 alipokuwa anaishi katika kisiwa cha Mayotte.

Maelfu ya watutsi na wahutu waliuawa mwaka 1994

Ni mwanamume wa kwanza kuhukumiwa nchini Ufaransa kuhusiana na mauaji ya Kimbari Rwanda miaka 20 iliyopita.

Upande wa mashitaka uliitaka mahakama kumfunga jela maisha Simbikangwa, baada ya kumtaja kuwa mtu mkatili na ambaye anaweza kufanya mambo mabaya zaidi ya aliyofanya.

Mawakili wake hata hivyo walisema kuwa kesi hiyo ilishinikizwa zaidi kisiasa na kuwataja mashahidi kama wasioweza kuaminika na ambao walikuwa na chuki wakati wakitoa ushahidi wao.

Takriban watu 800,000 wengi wao wa kabila la Tutsi , waliuawa katika kipindi cha siku miamoja.

Kesi ya kukutwa na sare za polisi yaahirishwa


Dar es Salaam. Kesi inayomkabili James Hassani (45),anayekabiliwa na mashtaka ya kujifanya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani na kukutwa na sare za jeshi hilo imeahirishwa hadi Machi 26 mwaka huu.

Kesi hiyo imeahirishwa baada ya mshtakiwa kuugua ugonjwa wa mafindofindo na kudai kuwa hataweza kufika mahakamani. Hii ni mara ya tatu kwa kesi hiyo kuahirishwa baada ya Februari 26 mwaka huu Mahakama kuiahirisha kesi hiyo baada ya shahidi wa pili katika kesi hiyo kuwa mgonjwa.

Hakimu Janeth Kinyage aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 26, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa na mshtakiwa alirudishwa rumande. Kesi hiyo ipo katika hatua ya kutoa ushahidi na tayari shahidi wa kwanza ameshatoa ushahidi wake.

Hata hivyo, Mahakama ya Wilaya ya Ilala ilimfungia dhamana Hassani, baada ya kubaini kuwa mshtakiwa huyo alikuwa na kesi nyingine iliyosababisha kutoroka katika Gereza la Msanga lililopo mkoani Dodoma alipokuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela.

CCM, Chadema kufunga kampeni za ubunge kesho


Iringa. Kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga zinatarajiwa kufungwa kesho huku CCM ikitarajia kumaliza kampeni zake katika ngome ya Chadema iliyopo eneo la Kidamali.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana anatarajia kuongoza ufungaji huo huku Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitaraji kuongoza maandamano ya kufunga mkutano wa kampeni hizo.

Katibu wa CCM mkoani hapa, Hassan Mtenga alisema Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Dk Yahya Msigwa, viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Khamis Dadi (Katibu) na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo ni miongoni mwa watakashiriki kufunga kampeni hizo.

Timu ya kampeni ya CCM inaratibiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula ambaye ameweka kambi katika Kata ya Ifunda, inayoaminika kuwa ni moja ya ngome ya Chadema .

Wengine ni Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Shaibu Akwilombe makatibu wa CCM wa wilaya zaidi ya 10 ambao wameweka kambi kwenye kata 13 na vijiji vilivyopo jimboni humo.

Mkutano wa Chadema unatarajiwa kufanyika katika Kata ya Ifunda, Jimbo la Kalenga kwa mwenyekiti kuongoza maandamano pamoja na jopo la wabunge 40 wa chama hicho. Uchaguzi mdogo wa Kalenga unatarajiwa kufanyika Machi 16,baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Marehemu Dk William Mgimwa.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva amevitaka vyama vya ushirika kuwarudishia shahada zao wakazi wa Kalenga ili waweze kupiga kura.

Vita dhidi ya Al Shabaab vinaathiri raia-UN

Mwanajeshi wa serikali akishika doria mjini Mogadishu

Umoja wa mataifa umesema kuwa mashambulizi makubwa ya kijeshi yaliyofanywa nchini Somalia na Wanajeshi wa Umoja wa Afrika, AMISOM, dhidi ya makundi ya wapiganaji wa Kiislamu, yanaweza kuwaathiri watu milioni tatu katika maeneo ya katikati na Kusini mwa nchi hiyo.

Mashambulizi hayo yanayowahusisha maelfu ya wanajeshi wa AU, yaliyoanzishwa juma lililopita na sasa yamesambaa hadi katika maeneo ya jangwa na milima.

Umoja wa Mataifa umeongezeka kusema kuwa umo katika hali ngumu zaidi Nchini Somalia.

Kwa sasa inaisaidia Umoja wa Afrika kwa hali na mali pamoja na vifaa vinavyohitajika kupambana na wapiganaji wa Kiislamu, na pia misaada ya kibinadam.

Inaunga mkono Jeshi moja kwa moja katika kutekeleza mashambulio makali dhidi ya makundi ya wapiganaji wa kiislamu yaliyo katika vuguvugu la Al-Shaabab.

Lakini kitengo kingine cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu, sasa yanatahadharisha kuhusiana na makali yanayotekelezwa na wanajeshi hao dhidi ya wananchi.

Shambulio mjini Mogadishu

Mashirika hayo pia yanasema wapiganaji wa Kiislamu kwa upande wao wanawahamasisha wananchi dhidi ya operesheni hiyo ya kijeshi inayojumuisha wanajeshi kutoka mataifa wanachama pamoja na wanajeshi wa serikali ya Somalia.

Siku za kwanza kwanza za operesheni hiyo kali, hasa katika maeneo ya vijijini, haikuwa rahisi kwa wafanyi kazi wa Umoja wa Mataifa kujua kilichokuwa kikiendelea.

Lakini tayari maelfu ya watu wanaingia katika mji wa Baidoa ulioko katikati mwa Somalia unadhibitiwa kwa sasa na Wanajeshi wa umoja wa mataifa kukimbia mapigano au kujaribu kupanga mashambulizi.

Bensouda kukata rufaa kesi ya Katanga

Fatou Bensouda

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ICC, Fatou Bensouda amesema huenda akakata rufaa hukumu iliyotolewa kwa mbabe wa zamani wa kivita nchini Congo Germain Katanga.

Katanga alipatikana na hatia nne za uhalifu wa kivita na hatia moja ya uhalifu dhidi ya binadamu, lakini akaondolea makosa kuhusu ubakaji.

Wapiganaji wake walishutumiwa kuwabaka wanawake na kuwateka huku wakiwatumia kama watumwa wa ngono.

Makundi ya wanawake nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo yameelezea hasira na masikitiko yao kutokana na hatua ya mahakama hiyo ya ICC ya kumuondolea Bwana Gatanga makosa hayo.

Wakati wa ziara yake katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa, Bensouda alisema kuwa huenda akakata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.

''Majaji hawakumuhumu kuhusiana na mashtaka ya unyanyazaji wa kimapenzi, mashtaka ambayo tulikuwa tumemshtaki nayo, pamoja na ile ya kuwasajili watoto jeshini'' Alisema Bensouda.

Bensouda, amesema kuwa wanachunguza hukumu hiyo kwa undani na kuchunguza ikiwa kuna dosari kadhaa za kisheria ambazo wanaweza kutumia kukata rufaa.

''Majaji kwa hekima zao walihisi kuwa bwana Katanga hakuhusika moja kwa moja na mashtaka hayo. Nadhani waadhiriwa wanafurahia kuwa ofisi yake inafuatilia suala hili, ili kuhakikisha kuwa mashtaka mazito kama hayo yanachunguzwa.'' Aliongeza Bensouda.

Kuhusiana na kesi inayomkabili rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, makamu wake William Ruto na mwandishi wa habari Joshua arap Sang, Bensouda alisema kuwa ''Nimeonyesha wazi kuambatana na ombi niliowasilisha mbele ya mahakama, kuhusiana na changa moto tunazopata, baada ya mashahidi wakuu kujiondoa kwa sababu kadhaa''.

Bensouda amesema kuwa itakuwa vigumu sana kwa ofisi yake kuendelea na kesi hizo kama ilvyopangwa baada ya mashahidi wakuu kujiondoa.

''Nimewafahamisha majaji kuwa tulikuwa na mashahidi kadhaa wakuu ambao walikuwa tayari kutoa ushahidi kuhusiana na matukio muhimu nchini Kenya, lakini wameomba kujiondoa kutoka kwa kesi hiyo.

Na kama unavyofahamu mashtaka haya pia ni mazito, na kabla ya kwenda mahakamani mtu anapaswa kuwa na uhakika wa kuwa na ushahidi ambao utakidhi mahitaji muhimu ili kuhakisha kuwa washukiwa wanahumiwa.'' Alisema Bensouda.

Zeidan akanusha kufutwa kazi


Aliyekuwa Waziri mkuu wa Libya Akihutubia Wanahabari

Aliyekuwa waziri mkuu wa Libya, Ali Zeidan, amepuuzilia mbali kura ya kutokuwa na imani naye iliyotangazwa na Bunge la taifa hilo mapema juma hili iliyopeleekea kufutwa kwake.

Ameiambia shirika la habari la Channel France 24 kuwa kura hiyo ya kutokuwa na imani naye illikuwa imejengwa kwa misingi ya uwongo huku pia akikanusha madai ya ufisadi dhidi ya serikali yake.

Ali Zeidan aliondolewa Ofisini mnamo siku ya Jumanne baada ya meli ya mafuta kutoka bandari inayodhibitiwa na waasi kufaulu kuvunja nanga ya wanajeshi wa wanamaji wa Libya kuingia bahari kuu na kutoroka.

Bwana Zeidan alifaullu kuondoka nchi hiyo licha ya kupingwa marufuku ya kutosafiri nje ya taifa.

T.B Jushua adai ndege ya Malaysia iliyopotea kimaajabu imezama kwenye tope baharini

T.B Jushua

Wakati ambapo dunia ikiweka jitihada zote kuisaka ndege ya shirika la Malaysia aina ya Boing 777 iliyopotea ikiwa na watu 239 wakati ikielekea Beijing, mhubiri maarufu wa Nigeria T.B Joshua ametoa utabiri kuwa ndege hiyo imezama baharini!

Jumapili iliyopita, T.B Joshua ameeleza kanisani kwake (SCOAN) kuwa ndege hiyo ilianguka na imezama ndani kabisa kwenye tope za bahari na kwamba hivi karibuni vipande vya ndege hiyo vitaanza kuonekana vikielea.

“Ndege hiyo iko ndani kabisa ya bahari. Baadhi ya vipande vitaanza kuonekana vikielea baharini muda wowote kuanzia sasa." Alisema T.B Joshua.

“Roho zao zipumzike kwa Amani. Tunaomba bwana azipe familia zao na wapendwa wao nguvu/uimara kushinda upotevu huu. Maombi yetu na upendo viko nao, nchi ya Malaysia na nchi nyingine ambazo zilikuwa na abiria katika ndege hiyo.” Alisema T.B Joshua kwa mujibu wa mtandao wa Nigeria wa Informationnng.

Hayo ni mambo ya imani!

Wakati dunia ikiwa bado haijafahamu ilipo ndege hiyo, wizara ya mambo ya nje ya China imeitaka Malaysia kuharakisha juhudi zake za kuitafuta ndege hiyo iliyokuwa na abiria 154 raia wa China kati ya abiria 239 waliokuwa katika ndege hiyo.

Ndege hiyo ilipotea mwishoni mwa juma na kumekuwa na mashaka kwamba huenda ni bomu au utekaji nyara unaweza kuwa uliiangusha ndege hiyo.

Waziri mkuu wa Libya azuiwa kusafiri

ali zeidan

Kiongozi wa mashtaka Nchini Libya Abdel-al-Qader Radwan amemzuia Waziri mkuu wa taifa hilo aliyevuliwa madaraka, Ali Zeidan, kusafiri nje ya taifa hilo hadi pale uchunguzi dhidi yake utakapokamilika.

Anatuhumiwa kwa madai ya ubathirifu wa pesa za umma.

Bwana Zeidan amesimamishwa kazi mapema siku ya Jumanne na Bunge la taifa hilo, baada ya Wabunge kudai kuwa meli ya mzigo ya Korea Kaskazini iliyokuwa imezuiliwa baada ya kunaswa ikibeba mafuta ghafi toka bandari moja linalokaliwa na waasi huko Libya, ilivunja nanga na kusafiri baharini.

Kura ya kutokuwa na imani na Bwana Zeidan iliitishwa baada ya meli hiyo iliyokuwa na bendera ya Korea Kaskazini kuabiri na kufikia maji makuu ya mipaka ya kimataifa baharini.

Mafuta hayo yalikuwa yamenunuliwa kutoka kwa waasi wanaodhibiti bandari ya Al- Sidra.

Wabunge hawana imani na Waziri Mkuu

Bunge la Libya limemuachisha kazi Waziri huyo mkuu, baada ya kupitisha agizo la kutokuwa na imani naye.

Hilo limeafikiwa baada ya meli ya Korea Kaskazini kuingia katika bandari ya taifa hilo na kuondoka na mafuta ghafi bila idhini ya serikali.

Makundi ya wapiganaji yamekuwa yakidhibiti baadhi ya bandari ya taifa hilo mashariki mwa taifa, tangu Julai mwaka jana na kuuza mafuta nje ya taifa.

Mwaandishi wa BBC Rana Jawad anatuarifu kutoka Tripoli.

Meli ya Mafuta iliyonaswa na wanajeshi ikisafirisha mafuta ghafi kisiri

Bunge la Libya limekuwa likijadiliana namna ya kumtimua Waziri mkuu Ali Zeidan kwa miezi kadhaa sasa.

Wabunge 200 wa taifa hilo walipiga kura na kupata maoni 124 iliyotosha kumuondoa madarakani.

Serikali ya mpito

Kiwanda cha mafuta nchini Libya

Waziri wa sasa wa ulinzi Abdullah Al-Thani amechukua mahala pake kama kama kaimu waziri mkuu.

Anatarajiwa kuhudumu kwa kipindi cha majuma mawili, kuruhusu bunge kukubaliana kumteuwa mridhi wa wadhifa huo.

Chama cha Libya National Congress, tume ya kwanza ya uchaguzi ndio yenye majukumu ya kumteuwa waziri mkuu mpya.

Lakini shinikizo kali limekuwepo Nchini humo la kutaka Bunge livunjwe.

Bwana Zeidan amekuwa akilaumu baadhi ya wanasiasa katika tume hiyo, hasa kutoka ndani ya vyama vya kiislamu ya kutaka kumtimua toka uongozini.

Hatua hiyo ya hivi punde inatazamiwa kuibua maswala mbalimbali ya udhibiti wa uongozi Nchini Libya, inapojikakamua kutafuta uungwaji mkono kutoka pembe zote za Nchi.