Bandari
CCM wapinga serikali tatu
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
Dodoma. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepinga muundo wa Muungano wa Serikali tatu unaopendekezwa katika rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Chama hicho tawala kimesema bado kinaamini katika muundo wa Serikali mbili.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kwamba mapendekezo yaliyowasilishwa mbele ya Tume hiyo yanabaki kama yalivyo, hivyo msimamo wao ni kuwapo kwa muungano wenye muundo wa Serikali mbili.
“Mapendekezo ambayo ndiyo msimamo wa chama tulishayawasilisha kwenye Tume kuwa sisi tunapendekeza mfumo wa Serikali mbili na siyo tatu wala moja,” alisema Nape alipokuwa akitoa taarifa ya uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyokutana usiku wa kuamkia jana kujadili suala hilo.
Kauli ya Nape inafanana na matamshi ambayo yamewahi kutolewa na baadhi ya wanasiasa wakongwe ambao ni makada wa CCM wakiwamo, mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na John Malecela, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na baadhi ya wabunge ambao mara kadhaa wamekaririwa wakipinga pendekezo la Serikali tatu.
Hata hivyo, Nape alisema matamshi ya viongozi hao yalikuwa ni maoni yao binafsi na kauli yake ndiyo rasmi ya chama hicho... “Mimi ndiye msemaji wa chama hiki. Ndiye ninayeeleza msimamo wa chama chetu, yanayozungumzwa na watu wengine hata kama ni viongozi siyo msimamo wa chama ni maoni yao binafsi.”
Habari ambazo gazeti hili ilizipata zinasema katika kikao hicho cha CC kulijitokeza hofu ya suala la wananchi kuwa na mamlaka ya kuwang’oa wabunge ikiwa hawatatekeleza masilahi yao na kwamba pendekezo hilo lina upungufu kwani halitafsiri masilahi hayo ni yapi.
Waunda kamati
Nape alisema rasimu iliyotolewa na Tume siyo waraka wa mwisho kwani bado unatoa fursa kwa Watanzania kuijadili na kutoa maoni yao na kwamba CCM kitatumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni yake kuhusu jambo hilo.
Alisema chama hicho kitawasiliana na wanachama wake zaidi ya 6,000 nchini ili waendelee kutoa maoni yao kuhusu suala hilo.
“Wengi wanadhani rasimu hii ndiyo ya mwisho… hii ni ya mwanzo tu, itajadiliwa italetwa ya pili na ya tatu, kwa hiyo hatuwezi kusema kilichoelezwa kwenye tume ndiyo msimamo. Ndiyo maana tumeamua kurejesha suala hili kwa wanachama wetu liendelee kujadiliwa,” alisema na kuongeza:
“Kama wanachama wetu wakiamua kuwepo kwa Serikali tatu, hatutachakachua, tutayachukua na kuyapeleka kama msimamo wetu, lakini tutakubaliana ikiwa uamuzi utakuwa umewahusisha wanachama wetu katika ngazi zote.”
“Hatuangalii kipengele kimoja tu. Tutapitia vipengele vyote hadi kuzimaliza kurasa zote zaidi ya 70 zinazoainisha mapendekezo ya Tume ya Jaji (Joseph) Warioba.”
Alisema wanachama wake wanapaswa kuipitia na kuijadili rasimu hiyo kwa kuzingatia mapendekezo kilichoyatoa awali wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya.
“Tulitoa maoni yetu na sasa tunaijadili Rasimu ya Katiba Mpya kwa kuzingatia maoni yetu yale, CCM tunakwenda kwa mujibu wa sheria,” alisema. Habari kutoka ndani ya CC ya CCM zinasema chama hicho kimeipa kazi kamati ambayo ilitumika kuandaa mapendekezo yake awali, kupitia rasimu hiyo na kufanya ulinganisho wa yale ambayo chama hicho kilipendekeza dhidi ya yale yaliyozingatiwa katika Rasimu ya Katiba hiyo.
“Kamati itafanya ulinganisho na baada ya hapo tutakwenda kwa wanachama kuwaeleza ni yapi tulipendekeza kama chama na ni yapi ambayo Tume imeyazingatia na hapo tutapata mawazo yao ambayo tutayatumia katika ngazi ya mabaraza ya Katiba,” kilisema chanzo chetu.
Wasanii waelimishwe athari za ulevi
Mwishoni wa wiki iliyopita nilikutana na msanii wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ Msafiri Diouf kwenye Viwanja wa Leaders Club, Dar es Salaam.
Alinimbia: “Nimeacha kutumia dawa za kulevya, si unaniona hata afya imerudi? Mimi siyo tena mtumiaji wa unga kwa miezi tisa sasa. Naomba Mungu anisaidie nisirudi nilipotoka.”
“Kuna wasanii wengi wanatumia madawa ya kulevya, wasipokata shauri na kubadili tabia kama mimi watapukutika na kuisha kabisa. Binafsi niko tayari kumsaidia atakayehitaji msaada wangu.”
Kikubwa ambacho ningependa kukizungumzia hapa ni kiasi gani wasanii wetu, vijana wanapuputika ama kupoteza mwelekeo wa maisha kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Tatizo hili siyo tu kwa Tanzania, bali kaya yote ya dunia hasa vijana wa fani mbalimbali. Filamu, muziki, urembo, michezo wote ni waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya.
Msanii wa Uingereza Amy Winehouse, malkia wa muziki wa Pop, RnB na Soul wa Marekani, Whitney Elizabeth Houston na Brenda Fassie wa Afrika Kusini, ni miongoni mwa wasanii walipoteza maisha kwa kuhusishwa na dawa za kulevya.
Tathmini za karibuni zinaonyesha kuwa, matumizi ya dawa za kulevya kwa wasanii inazidi kuongezeka na hivyo kutishia kizazi cha sasa kuharibika kwa kiasi kikubwa.
Kuna baadhi ya wasanii ambao matumizi ya dawa za kulevya yaliwaletea matatizo na kujikuta wakifikishwa katika hospitali ya wagonjwa wa akili, Mirembe iliyopo Dodoma kwa ajili ya matibabu zaidi, na wengi wao wamedai kujitumbukiza katika utumiaji huo wa dawa za kulevya kunatokana na baadhi ya watu waliochangia kuwarudisha chini kimuziki.
Nathubutu kusema wasanii wetu ambao wengi wao wamekuwa wakichukulia maisha ni leo na hawaangalia baadaye, sitaki kuwataja lakini tumeshuhudia wengi wakipata mafanikio makubwa katika kazi zao na kutumia pesa nyingi katika anasa.
Kama kila anayeshuka katika maisha akatumia dawa ya kulevya tukaona alistahili kufanya hivyo, kweli tutajenga taifa gani la kesho? Wangapi wana matatizo wanaangalia njia bora ya kuyatatua na hawatumii dawa za kulevya.
Nafahamu yapo mengi ambayo hupelekea kubomoa mwelekeo wa maisha ya binadamu hasa vijana, ambao ndiyo nguvu kazi ya maisha yao binafsi, familia zao na taifa kwa jumla.
Uvutaji wa bangi, kunywa pombe kupita kiasi, matumizi ya mirungi na dawa za kulevya ni baadhi ya starehe ambazo vijana wengi hasa wenye vipato vya wastani wamekuwa wakijihusisha navyo.
Kila kukicha ongezeko la utumiaji wa vilevi limekuwa likiongezeka na kuzidi kupunguza nguvu kazi, bila ya watumiaji kufahamu kwa bahati mbaya au makusudi kuhusu madhara ya utumiaji wa vilevi hivi.
Tumeiona mifano mingi na bado kasi inaongezeka kama vile watu hawaelewi athari za dawa za kulevya, mfano wa karibuni wa wazi ni msanii Ray C ambaye kama siyo msaada wa watu akiwamo Rais Jakaya Kikwete basi bila shaka angekuwa miongoni mwa waathirika wakubwa.
Nionavyo mimi, wasanii wajue dawa za kulevya siyo suluhisho la matatizo yao wakati wa shida na badala yake watumie muda wao kufikiria jinsi ya kudumu katika soko la ushindani.
Ni changamoto kubwa pia kwa Serikali yetu ambayo imeshindwa kuweka sera ya kueleweka ya kulinda masilahi ya wasanii kiasi cha kazi za wasanii kuibwa kirahisi na wajanja.
Warioba: Ikulu kugawanywa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
Dar es Salaam: Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema iwapo Mfumo wa Serikali Tatu utaridhiwa na wananchi ni lazima mambo yaliyo ndani ya Muungano yatagawanywa ikiwa ni pamoja na Ikulu ya Rais.
Amesema kuwa kutokana na taifa kufanya mabadiliko ya Katiba ni lazima kuwepo mpangilio wa kugawana mambo mbalimbali yaliyokuwa chini ya Muungano ikiwamo majengo, wafanyakazi, Ikulu, hata vitendea kazi na kwamba utaratibu huo ni kama ule uliotumika wakati Tanganyika na Zanzibar zilipoungana.
Kauli ya hiyo ya Jaji Warioba imekuja siku tatu tangu Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kueleza kuwa Tanzania Bara itaanza mchakato wa kutunga Katiba yake Aprili mwaka 2014 na kumalizika Desemba mwaka huohuo.
Jaji Warioba aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na waandishi waandamizi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumamosi, Mwananchi Jumapili, Mwanaspoti, The Citizen na The Citizen on Sunday, Tido Mhando ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MCL na Theophil Makunga, Meneja wa Uendeshaji na Biashara MCL.
Swali: Makao Makuu ya Serikali ya Muungano yatakuwa wapi?
Warioba: Ukibadili Katiba wakati wowote ni lazima kuwe na makubaliano fulani.
Unajua Serikali ya Muungano na Tanganyika ilikuwa pamoja, sasa ukianzisha Serikali ya Tanganyika, lazima kwenye mpangilio muanze kugawana hata wafanyakazi kwa kuwa wafanyakazi hao walikuwa ni wa Muungano. Hapo ndiyo mtaamua wafanyakazi gani watakwenda katika Serikali ya Tanganyika, watakaobaki katika Muungano na wale watakaokwenda Zanzibar.
Hata katika majengo hali inakuwa hivyo hivyo, lazima kutakuwa na majengo yaliyokuwa yakitumiwa na wizara mbalimbali na hata Ikulu. Hapo pia lazima myagawanye na kukubaliana viongozi wa Tanganyika watakuwa wapi na wale wa Muungano watakuwa wapi. Lakini, hata vifaa vya kutendea kazi navyo inatakiwa mgawane kulingana na makubaliano yenu.
Suala hili linategemea zaidi mazungumzo ya pande zote mbili, baada ya kukamilika kwa mchakato huu kwa sababu hii iliyopatikana sasa ni rasimu tu, ambayo itajadiliwa na wananchi kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba na baadaye kuwepo kwa kura ya maoni. Wapo watakaokuwa wakihoji kuhusu vyeo, katika hili itakuwa kama tulivyokuwa tukiungana Tanganyika na Zanzibar, wakati huo wapo ambao walikuwa wakuu wa mikoa na wakajikuta wameingia katika Muungano huku wakiwa na vyeo hivyo. Kilichofanyika ni kuendelea tu na nafasi hizo mpaka utakapofanyika utaratibu mwingine kwa njia ya mazungumzo.
Unajua jambo hili siyo jukumu la tume hii, tunaliacha kwa sasa na hatujui litakuwaje kwa sababu ni suala la mazungumzo.
Swali: Majukumu ya Rais yatakuwaje?
Warioba: Rasimu imeeleza majukumu (roles) ya Rais kama mkuu wa nchi, ambaye anakuwa kama taasisi na sisi tulichokifanya ni kujenga taasisi hizo, kwamba ijulikane akifanya chochote awe ameshauriwa, isiwe yeye peke yake.
Kama ni kuteua mawaziri kwanza atashauriwa, hata wakiteua basi apeleke majina aliyoyateua kwenye Bunge, kama ni mtumishi wa umma analazimishwa kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma na hawezi kuteua kutoka nje.
Katika vyombo vya usalama, tumeshauri kianzishwe chombo cha Baraza la Ulinzi na Usalama na hao ndiyo watakaomshauri rais.
Swali: Kwa mantiki hiyo huoni kama bado kutakuwa na mianya ya kupitisha watu kulingana na umaarufu wao au nguvu yao katika jamii?
Warioba: Kama angekuwa anawateua mwenyewe sawa, lakini wateule hao wamepitia katika hatua fulani na aliyeteuliwa atatazamwa sifa zake.
Mfano ni Tume ya Uchaguzi (NEC), tulipokea mapendekezo mengi juu ya nini kifanyike ili iwe huru, lakini tulizingatia suala la sifa za mwombaji kwanza, si jambo rahisi watu kukaa kikao na kupanga nani ashike nafasi hiyo.
Wanaotaka nafasi NEC wataomba na watachunjwa kulingana na sifa zao, baadaye majina yao yatapendekezwa, hivyo Rais hawezi kwenda nje ya jambo hilo. Katika jambo hilo viongozi wengi walipendekeza wanasiasa ndiyo waingie katika Tume ya Uchaguzi. Sisi tuliangalia jambo hili kwa umakini sana sambamba na kuangalia uzoefu wa nchi nyingine, tuliona kwamba mahali popote pale ambapo Tume ya Uchaguzi ina wawakilishi wa vyama vya siasa, kumekuwa na matatizo na siku zote wamekuwa hawakubaliani.
Ndiyo maana tukaweka sifa katika Katiba na kuwa na utaratibu ambapo Rais atateua na orodha atakayopelekewa ndiyo ataitumia kuteua nani awe mwenyekiti, makamu na wajumbe wa tume hiyo, katika hilo sidhani kama vyama vitahusika.
Hata Rais wa Marekani anateua watu wengi, hata kama Bunge lina wabunge wengi wa chama chake anajua wazi kuwa asipopeleka watu wenye sifa wabunge watamkatalia.
Ndiyo maana tunakazania maadili, tunasema Rais ndiyo kiongozi pekee wa nchi aliyechaguliwa na watu wote, lakini kwa sababu ya upungufu wa maadili, hatujawahi kuona ni mtu gani tunaweza kumchagua na tumwamini kuwa atasimamia maadili ya nchi.
AJALI MBAYA YATOKEA IFISI MBALIZI LEO MCHANA, YAJERUHI ZAIDI YA ABIRIA 15.
Daladala ambayo ilikuwa inatoka Mbalizi kwenda Songwe yenye namba za
usajili T 635 ALS ikiwa imeharibika vibaya Baada ya Ajali kutokea Eneo
la Ifisi Mbalizi Mbeya
Hapa
ndipo eneo ambalo Daladala iliingia wakati ilijaribu kulipita Gari
lengine akiwa mwendo kasi na kuukutana na Tela la Mafuta
Daladala upande wa nyuma
Lori aina ya Scania yenye namba ZA usajili T378 AGD likiwa limepaki Baada ya ajali hiyo kutokea
Mabaki ya daladala
Wananchi mbalimbali wakiwa wanashuhudia ajali hiyo iliyo tokea Ifisi Mbalizi Mbeya
Hivi ndivyo Daladala inavyo onekana upande wa Mbele baada ya Ajali kutokea
Dereva wa daladala ambaye ndiye aliye sababisha ajali hiyo Nikutusya Mwanja akiwa anapelekwa chumba cha matibabu ya Haraka.
Baadhi ya Majeruhi waliokuwemo katika ajali hiyo
Wakazi mbalimbali wakiwa katika Hospitali ya Ifisi Mbalizi Mbeya kutazama ndugu zao waliopata ajali.
Askari wa usalama barabarani wakiandikishana Dhamana na ndugu wa Dereva wa Daladala ili apate dhamana ya kutibiwa
*****************WATU 17 wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuharibika vibaya kufuatia ajali iliyohusisha Gari la abiria aina ya Toyota Hiace na Scania.
Ajali hiyo imetokea leo majira ya Saa Saba Mchana katika eneo la Ifisi nje ya Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Ifisi(ICC) Mbeya Vijijini.
Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema gari la abiria Toyota Hiace lenye namba za usajili T 635 ALS likiendeshwa na Nikutusya Mwanja likitokea Mbalizi kuelekea Songwe iliingia kwenye Trela la Scania lililokuwa likitokea Tunduma kuelekea Dar Es Salaam.
Wamesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari ndogo ambapo Dereva alikuwa akijaribu kulipita gari lingine lakini mbele akakutana na Lori ambalo alipojaribu kulikwepa akaingia kwenye Trela lake na kupinduka vibaya.
Trela hilo lenye namba za usajili T 675 ACT likiwa linavutwa na Kichwa chenye namba za usajili T 378 AGD halikuweza kuumia sana kutokana na kwenda kwa mwendo mdogo ambapo majeruhi wote wamekimbizwa katika Hospitale teule ya Ifisi kwa matibabu zaidi.
Muuguzi Msaidizi wa Hospitali Teule ya Ifisi Elimath Sanga amethibitisha kupokelewa kwa majeruhi 17 na kwamba kati ya majeruhi hao 3 hali zao siyo nzuri sana ingawa majina yao hayakuweza kupatikana.
Ameongeza kuwa majeruhi wengi wameumia sehemu za kichwani na miguuni na kwamba baada ya kumaliza kupatiwa huduma ya kwanza wataangalia ni wangapi wanaweza kuruhusiwa na wengine kulazwa.
Hata hivyo habari kutoka eneo la tukio zimesema kuwa Kondakta wa gari dogo aliyefahamika kwa jina moja la Ayubu alitoweka mara baada ya kutokea kwa ajali ingawa haifahamiki kama ni kurukwa kwa akili au ni kukimbia kesi.
polisi yawaangukia viongozi wa dini
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma
David Misime akizungumza na viongozi wa madhehebu ya dini ofisini kwake
alipowaita ili kujenga mahusiano ya kimawasiriano.
(PICHA NA JOHN BANDA)Na John Banda,Dodoma.
JESHI la Polisi Mkoani Dodoma imewaomba viongozi wa madhehebu ya dini kushirikiana katika mawasiliano ili kubaini uhalifu na wahalifu.
Ombi hilo limetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoani hapa David Misime, alipokuwa akizungumza na viongozi wa madhehebu ya dini ya Kiislamu na Kikristo alipowaita ofisini kwake ili kujenga mahusiano kati yao.
Miseme alisema viongozi wa madhehebu ya dini wapo karibu na jamii,hivyo wanayo fursa kubwa ya kuweza kubaini uhalifu na wahalifu
Aidha kamanda huyo wa polisi amewasisitiza viongozi hao kuendelea kufanya doria za kiroho maana wakifanya hivyo uharifu utapungua nchini na waumini wao watapata baraka na thwawabu,maana kwa upande wao polisi wanafanya doria za kimwili.
Misime ameongeza kwa kuwataka viongozi hao kuendelea kuhubiri utii wa sheria bila shuruti kutokana na wao kuwa karibu na wananchi kwa kuwa maana wakiitii sheria hiyo hata ajali za barabarani ambazo zimekuwa zinasababishwa na uzembe zitapugua
“Mimi ninawaheshimu sana viongozi wa dini kwa sababu wao ndiyo wanachangia utulivu uliopo nchini,na hata mimi ikiwa wataniona na kosa lolote wasisite kuniita na kunionya kama walivyokuwa wakifanya zamani bila kuongopa cheo cha mtu”alisema Misime.
Hata hivyo Kamanda huyo wa Polisi ametoa onyo kwa baadhi ya askari ambao wamekuwa siyo waamni wanaovujisha siri za Polisi ambazo wananchi wamekuwa wakizitoa kuhusu uharifu na waharifu
Misime alisema, kuwa ili kudhibiti tabia hiyo askari watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo na kufukuzwa kazi.
Kwa upande wa viongozi wa madhehebu ya dini wakizungumza baada ya kikao chao kwisha walisema kuwa watahakikisha wanashirikiana na jeshi hilo,
Kaminyoge Andendekisye ambaye ni mchungaji wa kanisa la Moroviani Iringa road alisema mahusiano kati ya jeshi la polisi na upande wao yalikuwa mabovu kutokana na kutotambuliwa kama wana uwezo wa kuweka hali ya utulivu katika jamii.
Kwa upande wake Usitadhi Musa Jamaa alisema kuwa kitendo cha jeshi la polisi kukaa nao ni dalili za jeshi hilo kutambua umuhimu wao hali itakayochagiza kuuweka mjini wa Dodoma kuwa ni sehemu ya utulifu na amani kutokana na ushirikiano huo.
Mwisho.Matapeli waendelea kukamatwa
Na John Banda, Dodoma
WATU watatu wanashikiliwa na polisi mkoani Dodoma kwa makosa ya utapeli kwa njia tofauti ikiwemo ya kutumia Dolla Bandia
Kaimu Kamanda wa polisi mkoa hapa Suzan Kaganda alisema jeshi hilo liliweka mtego na kufanikiwa kumkamata Abuu Mohmed Omary maarufu kwa jina la Rass Mfanya biashara soko la Sabasaba maeneo ya Nyerere Squere.
Kaganda alisema Rass alikamatwa akijaribu kumrubuni Agostino Mpanda alipokuwa akitaka kumtapeli 7, 500,000 kwa kutumia Dolla Bandia, Dolla nyeusi [Black Dolla] ambapo huwaambia watapeliwa watoe fedha ili kununulia Dawa ya kuzioshea.
Kaimu Kamanda huyo aliongeza kuwa baada ya kumkamata na kumpekua mtuhumiwa huyo nyumbani kwake walimkuta akiwa na Shl 2,600,000 ambazo alishindwa kueleza namna alivyozipata.
Wakati huohuo
Jeshi hilo limewakamata Fransisika Gerard Mchaga mkazi wa Area E 27 na
Ibahimu Mkwawa Mhehe 40 mkazi wa ipagala wakiwa kwenye Gari aina ya NOAH
yenye namba za usajili T 311 BLM likitokea Morogoro kuja Dodoma.
Watu hao waliokamatiwa Wilaya ya Chamwino walikutwa na Chupa kubwa ya Chuma yenye uzito wa kilo 15 ikiwa na lebo ya Red Mercury Industry na Nembo ya UN iliyokuwa imejazwa Goroli ndogondogo za Baiskel wanazodaiwa kutumia kwa Utapeli wakidai ni madini.
Jeshi hilo limewapongeza wananchi wanaolisaidia kufichua waharifu na kuwataka kuendele ili hatimae waweze kupunguza kama siyo kuondoa kabisa tatizo hilo la watu kujipatia Fedha kwa njia zisizo za halali, huku jeshi hilo likiwataka wanaojihusisha na Utapeli wa namna yoyote kuacha tabia hiyo kwani Sheria haitawafumbia macho.
Malleko: Tanzania inaweza kupata Rais Mwanamke 2015
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Wilaya ya Arumeru, Ester Malleko.
TANZANIA inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa Rais wa awamu ya tano mwaka 2015. Uchaguzi huo pia utahusisha nafasi za ubunge na udiwani ukitanguliwa na ule wa serikali za mitaa mwakani.
Mengi yanazungumzwa kuhusu chaguzi hizo, ikiwemo
uwezekano kuwa na Rais, Makamu wake au Waziri Mkuu mwanamke kutokana na
uwezo wa kiuongozi unaoonyeshwa na wanawake waliopata fursa za uongozi.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), wilaya ya Arumeru, Ester
Malleko anazungumzia nafasi na uwezekano huo kama alivyozungumza na
Mwandishi Wetu, Peter Saramba.
Swali: Nini kilikusukuma kuingia kwenye siasa na nini malengo yako ya baadaye?
Jibu:
Nimeingia kwenye siasa kuwatumikia wananchi na kuthibitisha kuwa
wanawake tunaweza. Nimekuwa mwenyekiti wa UVCCM wilaya na sasa
ninaongoza wanawake.
Nafasi ya mwanamke kwenye jamii siyo kuzaa na
kutunza familia pekee. Tunapaswa na hakika tuna haki ya kushiriki katika
ujenzi wa taifa sawasawa na wanaume kwa kila mmoja kutekeleza na
kutimiza wajibu wake pale alipo.
Swali: Wewe ni mwanachama na
kiongozi wa CCM. Kuna madai kwamba chama chako kimepoteza haiba mbele ya
umma kutokana na ninyi viongozi kuacha misingi iliyoasisi chama hicho.
Nini maoni yako?
Jibu: CCM kama taasisi haina tatizo
na haijapoteza haiba. Bado ipo na itaendelea kudumu katika misingi yake
ile ile iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa hili ambayo ni amani, upendo,
udugu na mshikamano bila kujali tofauti zetu za kikabila, kidini wala
maeneo mtu anakotoka.
Chama hiki bado kinaaminiwa na umma. Hilo linathibitishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu ambapo CCM ilipewa ridhaa ya kuunda Serikali baada ya kushinda kiti cha urais na kupata wabunge na madiwani wengi.
Hata hivyo, ni kweli kuna kosoro ndogo ndogo
zinajitokeza kutokana na makosa ya watu binafsi ambazo zinashughulikiwa
kupitia vikao, katiba, kanuni na taratibu za chama.
Swali: Mwaka 2015 tunaingia kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, kuna maneno kuwa wanawake waliopata fursa wameonyesha uwezo mkubwa kiuongozi. Unadhani muda umefika wa kuwa na Rais, Makamu au Waziri Mkuu mwanamke?
Jibu: Muda umefika, tena unapita. Ninaamini Taifa hili linaweza
kuongozwa na mwanamke kwa sababu viongozi wanawake waliopata fursa za kuongoza wameonyesha kuwa wanaweza.
Wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja na kutoa uamuzi wa haraka wenye faida na maslahi kwa umma.
Wanawake viongozi wamethibitisha kuwa hawapigi dili kama ambavyo mama nyumbani asivyoweza kuisaliti familia.
Swali: Unaweza kutaja kwa uchache majina ya wanawake unaodhani wana uwezo wa kuwa Rais wa taifa hili?
Jibu: Wapo wanawake wengi wanaonivutia katika uongozi wao. Baadhi wapo kwenye nafasi zao uongizi hadi sasa katika medani mbalimbali ikiwemo uongozi wa kisiasa, kijamii na harakati mbalimbali.
Ingawa wako wengi ambao siwezi kuwataja wote, lakini kwa uchache wapo Dk Asha Rose Migiro, Dk Hellen Kijo-Bisimba, Profesa Anna Tibaijuka, Ananilea Nkya, Mama Anna Abdalah, Mama Gertrude Mongella na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda.
Swali: Kuna msemo kwamba mwanamke anaweza akiwezeshwa. tupe maoni yako?
Jibu: Binafsi sikubaliani na msemo huo, kwani unafifisha uwezo wa
kijiamini kwa wanawake ambao hukaa kutegemea kuwezeshwa ndipo wafanye jambo.
Siyo kweli kwamba ili mwanamke afanikiwe au kuweza jambo lazima awezeshwe. Nadhani kauli hii iliyotumika huko nyuma kuwahamasisha na kuwatia moyo wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi sasa imepitwa na wakati.
Mimi
naamini uwezo wa mwanamke upo dhahiri ndiyo maana nyuma ya kila
mwanaume shupavu na mwenye mafanikio, yupo mwanamke shupavu na jasiri.
Na huu unathibitishwa na usemi kuwa “Kila mwanaume aliyefanikiwa,nyuma
yake kuna mwanamke”
Kifamilia, mshauri mkuu wa baba ni mama. Sasa tutakubali vipi kwamba ili mwanamke afanikiwe lazima awezeshwe? Awezeshwe na nani? Huyo huyo mwanaume ambaye yeye anamshauri?
Hata hivyo, pamoja na ukweli huo, lazima tukubali kwamba adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe. Wanawake hatujiamini. Lakini hata anapotokea mwenzetu kujiamini na kujitokeza, hatumuungi mkono, pengine kwa ile
ile dhana kuwa hatuwezi au wivu tu wa kike.
Swali: Jiji la Arusha ni miongoni mwa halmashauri zenye chaguzi ndogo za madiwani kujaza nafasi zilizo wazi. Unatarajia chama chako kitamudu kurejesha kata hizo nne zilizonyakuliwa na upinzani uchaguzi uliopita?
Jibu: Yeyote anayeingia kwenye mashindano, lengo lake ni kushinda. CCM tuna matumaini makubwa ya kushinda baada ya kugundua na kurekebisha makosa madogo madogo yaliyosababisha tupoteze kata hizo.
Tumesimamisha wagombea wanaokubalika na tumejiandaa kuwanadi kukamilifu kupitia sera za chama. Hatutatukana wala kuzungumzia watu binafsi kama wenzetu wanavyofanya. Tutanadi sera ili kutoa fursa kwa wananchi kuzilinganisha na za wenzetu.
Napenda kuchukua fursa hii kuwaasa watu wa Arusha tusikubali
kutenganishwa wala kufarakanishwa kutokana na chaguzi hizi. Ni kweli kila mtu ana haki ya kufuata na kuamini itikadi aipendayo kisiasa, tufanye hivyo bila kubezana, kufarakana wala kusababisha ufa kwenye uhusiano wetu.
Baada ya uchaguzi huu na zingine zijazo, Arusha inapaswa kuendelea kuwa sehemu salama kwa maisha na mali zetu. Wananchi tunataka ufumbuzi wa matatizo yanayotukabili kwa pamoja bila kujali tofauti zetu kisiasa, kidini wala kibabila.
'Mafisadi wanamtisha Mkurugenzi Mkuu wa NHC'
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu
Serikali imeombwa kumwekea ulinzi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu, kutokana na vitisho ambavyo ameanza kupata kutoka kwa mtandao wa mafisadi waliojimilikisha nyumba za shirika hilo baada ya mirija yao ya wizi kukatwa na mkurugenzi huyo.
Ombi hilo lilitolewa jana bungeni mjini Dodoma na Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Magdalena Sakaya, wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Sakaya alisema Mchechu amekuwa akifanya kazi nzuri tangu aingie NHC, lakini mafisadi wachache ambao walikuwa na mirija ya kufanya ufisadi ndani ya shirika hilo wamekuwa wakimwandama na wakati mwingine wakimtumia ujumbe wakumtisha ili kumkatisha tamaa asiendelee na jitihada zake za kupambana na ufisadi uliokuwapo.
“Mheshimiwa Spika, wale mafisadi baada ya kuona mirija yao imekatwa wanamtumia ujumbe wa vitisho wakimwambia kuwa kijana umekuja na utaondoka... naomba serikali imlinde, Mkurugenzi huyu ni kijana mdogo, lakini mzalendo wa kweli na amefanyakazi kubwa sana,” alisema Sakaya.
Akizungumza na NIPASHE nje ya ukumbi wa Bunge, Sakaya alisema kuna watu ambao walikuwa wamehodhi nyumba nyingi za NHC na kuzikodisha kwa watu kwa bei kubwa huku wakilipa fedha ndogo kwa shirika hilo.
Sakaya alisema kuna watu ambao walikuwa wanaingiza hadi Sh. 7, 000, 000 kwa mwezi kwa kupangisha nyumba za NHC, hivyo ujio wa Mchechu umekuwa balaa kwao kwani mirija mingi imefungwa.
Alisema kuna watu walikuwa wanamiliki hadi nyumba nne za NHC na kuzikodisha kwa bei kubwa kwa watu mbalimbali, hivyo baada ya kuona mirija hiyo imekatwa wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ikiwamo kumtisha Mchechu.
“Mimi nimekuwa mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa zaidi ya miaka saba, ningekuwa na tamaa ya mali ningekuwa na hata ghorofa namiliki sasa, lakini siko hivyo, mimi nataka NHC iwe mali ya Watanzania na iwanaufaishe Watanzania, hakuna ndugu yangu hata mmoja anayeishi NHC ingawa ningetaka wangepata,” alisema Sakaya na kuongeza:
“Nimefuatwa mara nyingi na wafanyabiashara wakiniuliza ninataka Shilingi ngapi ili niwatetee bungeni wauziwe nyumba, lakini nimekataa kwa sababu mimi ni mzalendo na sitaki ufisadi kabisa, ningetaka utajiri ningeshaupata kupitia NHC.”
Mbunge huyo alisema baadhi ya wafanyabiashara hao wamekuwa wakiwatumia hadi baadhi ya wabunge kuwatetea bungeni wengine wakitaka Mchechu aondolewe kwenye nafasi hiyo ili waendelee kula.
Alisema kabla ya Mchechu kuingia NHC, kulikuwa na mtandao mkubwa wa wafanyabiashara wanaohodhi nyumba hizo za shirika hilo na ndio wanaohangaika hadi kuwatumia baadhi ya wabunge wakitaka serikali iwauzie zile nyumba na isiwaongezee kodi wapangaji na wengine wakiishauri serikali imwondoe Mchechu.
“Usione kila anayefoka kuhusu NHC ukadhani ana uchungu na Watanzania wanyonge, wengine wametumwa na wafanyabiashara hao hao ambao wana mtandao unaomiliki nyumba za NHC, hakuna mlalahoi wanayemtetea, wanataka wauziwe zile nyumba ili wazilangue kwa bei kubwa,” alisema Sakaya na kuongeza:
“Alichofanya Mchechu kimewaathiri mafisadi wengi sana waliokuwa wanalinyonya shirika, unakuta mfanyabiashara amempangisha mtu nyumba moja ya NHC na analipwa Shilingi 1,000,000 kwa mwezi wakati NHC anakwenda kulipa 400,000, sasa kilichofanyika NHC imewafuata wale waliopangishwa na wafanyabiashara na kuwapa mikataba yenyewe ili wailipe NHC badala ya wale walanguzi hapo ndipo wanahangaika.”
Sakaya aliishauri pia serikali iondole Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwa vifaa vya ujenzi kwa NHC ili wajenge nyumba bora na za bei nafuu ambazo Watanzania wa hali ya chini watamudu kuzinunua.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Kiwelu, alisema ni aibu kwa serikali kushindwa kulipa madeni inayodaiwa na NHC wakati kila mwaka bajeti imekuwa ikitengwa kwa ajili ya kulipia pango.
Alisema kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ambayo yeye ni mjumbe inamuunga mkono Mkurugenzi wa NHC, lakini amekuwa akikwamishwa na serikali ambayo inashindwa kulipa madeni ya muda mrefu, hivyo kushindwa kujenga nyumba mpya.
“Bajeti tunapitisha kila mwaka hapa, lakini hamlipi pango la NHC, Waziri tunaomba utueleze hizo fedha huwa mnazipeleka wapi?” alihojiu na kuongeza: “Tunaomba katika bajeti hii Wizara inayodaiwa deni lake lipelekwe Hazina ikatwe huko huko wapewe NHC.”
Alishauri NHC ikipata fedha za kutosha ijenga nyumba za matabaka ya wenye nazo na nyumba ambazo watu wa tabaka la chini kabisa watamudu kuzinunua kwa kuwa za sasa hakuna mlalahoi atakayezimudu.
Kiwelu alisema inasikitisha kuona kuwa Tume nyingi zimeundwa kuchunguza mambo zikitumia fedha zinazotokana na kodi wanazolipa walalahoi, lakini ripoti hizo huwa haziwekwi hadharani.
Alitoa mfano wa Tume ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuchunguza majengo 100 jijini Dar es Salaam, lakini kwa mshangao mkubwa kamati yake imeitafuta kwa muda mrefu na haijulikani iliko.
“Tumeitafuta ripoti ya Tume ya Lowassa, lakini tumeikosa na hadi sasa ripoti hiyo haijulikani iliko, sasa naomba Waziri atueleze iliko ili isomwe na ifanyiwe kazi kwa kuwa kuna majengo zaidi ya 100 ambayo ilisemekana ni mabovu na yanapaswa kubomolewa,” alisema.
Herbert Mtango (Lushoto-CCM), alisema kuna wawekezaji ambao wamejilimbikizia mashamba makubwa miaka 40 iliyopita bila kuyaendeleza, lakini bado wanamiliki hatimiliki za mashamba hayo.
Alisema licha ya mashamba hayo kugeuka mapori kwa miaka yote hiyo huku wawekezaji hao wakiwa nje ya nchi, serikali imeshindwa kuzifuta hati hizo na kusababisha wananchi wengi wa Muheza kukosa sehemu za kuendesha shughuli za kilimo.
“Mheshimiwa Spika, hii ni aibu kubwa sana, mwekezaji anapewa hati ya kumiliki shamba kwa miaka 99 na sasa kwa zaidi yamiaka 40 iliyopita ameshindwa kuendeleza shamba, lakini anaendelea kumiliki ardhi wakati wazawa hawana ardhi,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
Serikali inavyoulea mgogoro wa gesi Mtwara
Tangu mgogoro wa kupinga gesi itakayozalishwa mkoani Mtwara uliponza kufukuta Desemba 2012, Serikali imeshindwa kutatua kiini chake, badala yake nguvu kubwa za kijeshi zimetumika kiasi cha kusababisha mauaji, majeruhi na chuki kwa wananchi.
Kimsingi mgogoro huu unatokana na maoni ya wananchi kuhusu rasilimali ya gesi inayotarajiwa kuchimbwa mkoani humo wakitaka gesi hiyo isisafirishwe kwa bomba kwenda Dar es Salaam.
Awali Serikali ndiyo iliyounda kamati ya Nishati na Madini ambayo ilipita kwa wanachi nchini kote kutaka maoni yao. Ilipofika Mtwara, wananchi wengi hawakukubaliana na wazo la kusafirishwa kwa gesi.
Desemba mwaka 2012, vyama tisa vilifanya mikutano na hatimaye maandamano ambayo hata hivyo yalisusiwa na Mkuu wa Mkoa huo, Joseph Simbakalia.
Mbali na maandamano hayo, mapema mwaka huu, kulijitokeza vurugu wilayani Masasi ambazo zilihusishwa na madai ya gesi japo chanzo chake hakikuwa hicho.
Hapo ndipo viongozi wa Serikali wakaanza kutembelea Mtwara ili kutuliza hali ya mambo. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifika Mtwara mapema mwaka huu na kuzungumza na makundi ya wananchi, yaani, vyama vya siasa, Maaskofu na Masheikh, wazee na vijana.
Baada ya hapo yakafanyika majumuisho yaliyohusisha makundi hayo ambayo hata hivyo hayakuwaridhisha wananchi.
Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anna Makinda alizuia mjadala wa suala hilo Bungeni, akidai kuwa kuna kamati imeundwa kuchunguza.
Licha ya Waziri Mkuu Pinda kushindwa kuafikiana na Wanamtwara katika ziara yake, akarudi Bungeni na kutoa taarifa kuwa mambo yamekwisha, hivyo na ile kamati ya Bunge iliyotumwa kuchunguzwa ikayeyuka.
Kama wanavyosema Waswahili, ‘La kuvunda halina ubani’, ule uvundo aliouacha Pinda Mtwara, sasa umezua vurugu upya Mei 22 ambapo watu wamekufa, kujeruhiwa na wengine kubakwa.
Pinda amerudi tena Mtwara kufanya mazingaombwe yake. Bunge nalo baada ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, imeunda tena kamati ya Wabunge iende kufuatilia suala hilo.
Tujiulize, kwa nini ile kamati ya kwanza ya Bunge iliyosababisha suala hilo lisijadiliwe ilivunjwa kabla haijaanza kazi?
Hii yote ni kuonyesha kuwa Serikali ndiyo inayoulea mgogoro huu, kwa sababu haitaki kuwasikiliza wananchi ili kufikia mwafaka. Huo ndiyo mzizi wa tatizo.
Suluhisho siyo kuleta majeshi ya kutuliza ghasia, ni kuwasikiliza wananchi, kwani wao ndiyo msingi wa mamlaka ya Serikali kwa mujibu wa Katiba ibara ya nane.
Prof Tibaijuka akiri kuvutana na NHC
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
akijibu hoja za wabunge waliochangia Makadirio na Mapato ya wizara yake
kwa mwaka wa fedha 2013/14, bungeni, Dodoma jana.
Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema kuwa kitendo cha kuvutana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhusu kesi ya ardhi iliyomhusu raia wa Tanzania mwenye asili ya Kichina, Jingling Li ilikuwa ni kuzingatia sheria na siyo kwamba alikuwa na urafiki naye.
Alisema hayo akinukuu taarifa iliyoandikwa na gazeti hili toleo la wiki iliyopita, wakati akijibu hoja za wabunge wake kuhusu bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2013/14.
Alinukuu taarifa ya gezeti hili akisema kuwa NHC walishindwa kwenye kesi hiyo hatua ya rufani kama alivyokuwa ametabiri hapo awali akionyesha umuhimu wa kufahamu sheria za ardhi na makazi.
“Gazeti la Mwananchi waliandika ninavutana na Shirika la Nyumba ikaonekana kana kwamba namtetea Mchina labda kutokana na kwamba kuna masilahi ninayopata,” alisema Profesa Tibaijuka na kuendelea:
“Huyu raia wa Tanzania mwenye asili ya China, alikuwa ni mkalimani wa Baba wa Taifa (Hayati) Mwalimu (Julius) Nyerere. Alishinda kwenye kesi hiyo na kurejeshwa kwenye nyumba hiyo,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema kwa sasa NHC hawana namna nyingine ya kufanya kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa kwenye ngazi ya rufaa. Alizungumza hayo akionyesha umuhimu wa kuwepo na vyombo vya usuluhishi wa kesi zinazohusiana na ardhi.
Gazeti hili liliripoti kuwako kwa mvutano wa chini kwa chini baina ya Profesa Tibaijuka na uongozi wa NHC.
Mvutano huo ulitokana na uamuzi wa NHC kuukatia rufaa uamuzi wa Mahakama Kuu (Kitengo cha Ardhi), uliompa haki, Jingling Li katika kesi ya ardhi namba 129 ya 2006 dhidi ya shirika hilo na wadaiwa wengine wawili.
Katika kesi hiyo, Li alikuwa akilalamikia hatua ya kuondolewa kwenye nyumba Nambari 103 iliyopo katika vitalu namba 3, 5, 7 na 8, Barabara ya Haile Selassie, Oysterbay, Dar es Salaam.
Kesi dhidi ya NHC ilifunguliwa mwaka 2006 wakati shirika hilo likiongozwa na Martin Madekwe na imedumu kwa miaka sita hadi Aprili mwaka jana ilipotolewa hukumu wakati shirika hilo likiwa chini ya Nehemia Mchechu aliyeteuliwa mwaka 2010.
Katika hukumu yake ya Aprili 27, 2012, Jaji Atuganile Ngwala aliamuru NHC pamoja na washtakiwa wa pili na wa tatu katika shauri hilo; Lars Eric Hulstrom na Kampuni ya Udalali ya Manyoni, wamlipe Li karibu Sh478 milioni ikiwa ni fidia ya hasara na usumbufu uliosababishwa na kuhamishwa kwake kinyume cha sheria katika nyumba hiyo.
Mchanganuo huo unahusisha Sh70 milioni na Dola za Marekani 177,450 (Sawa na Sh283, 920,000 - Dola moja ni sawa na Sh1,600), gharama za kesi pamoja na riba ambazo pia zinapaswa kulipwa.
Pia Mahakama hiyo iliamuru Li arejeshwe katika makazi hayo, amri ambayo inamaanisha kuondolewa katika nyumba hiyo kwa mpangaji aliyeingizwa badala ya Li ambaye ni Hulstrom aliyekuwa mdaiwa wa pili katika kesi hiyo.
Baada ya kupokea nakala ya hukumu ya Jaji Ngwala, NHC waliazimia kukata rufaa kupinga uamuzi huo, lakini habari kutoka ndani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinadai kwamba Waziri Tibaijuka alitoa maelekezo ya mdomo kwamba hakukuwa na haja kwa shirika hilo kukata rufaa. Hata hivyo, NHC walishindwa rufaa hiyo.
Subscribe to:
Posts (Atom)

