Kocha Stewart Hall kutua Azam leo

Aliyekuwa kuwa kocha wa Azam, Stewart Hall, atawasili nchini leo kuanza kuifundisha tena timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kutwaa nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mrithi wake wakati akiondoka nchini, Mserbia Boris Bunjak.

Afisa Habari wa Azam, Jaffer Idd, alisema jana kuwa maamuzi ya kumrejesha kocha wao wa zamani ambaye alikuwa akiifundisha Sofapaka inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya yametokana na ushauri wa kiufundi walioupata kutoka kwa wadau mbalimbali wa timu hiyo.

Idd alisema kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo ilifikia maamuzi hayo baada ya kuamua kuvunja mkataba wa Bunjak, ambaye alianza kuiongoza Azam tangu mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Aliongeza kwamba Hall ambaye mwaka huu aliifikisha Azam kwa mara ya kwanza katika fainali za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), ataanza kazi yake rasmi kesho wakati atakapoiongoza timu hiyo katika mechi yao dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Chamazi, Mbagala jijini Dar es Salaam.

BUNJAK ASHANGAA

Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Bunjak alisema kuwa amesikitishwa na uamuzi wa kutimuliwa kwake Azam kwani hadi kufikia jana alikuwa hajapata maelezo ya kina kuwa ni kwanini amefungashiwa virago.

“Kesho (leo) napanda ndege kurejea kwetu (Serbia). Uamuzi huu umenishtusha sana kwa sababu tumecheza mechi nane bila kufungwa kabla ya kupoteza mechi moja dhidi ya Simba,” alisema Bunjak aliyekuwa ameambatana na kocha wa makipa aliyetimuliwa pia baada ya siku 25 tangu watue Oktoba 5, Torlakovic Slobodan. 

“Niamini, sijui sababu za kutimuliwa kwangu, lakini naamini watu wanaozunguka klabu ya Azam ndiwo wameshauri hivyo.

“Nimesikitishwa sana na uamuzi huu wa Azam kwani nilikuwa na ndoto za kuipeleka mbali timu yao.”

Aidha, Bunjak aliyekuwa na mkataba wa miaka miwili ya kuinoa Azam, hakusita kusifia wachezaji na uongozi wa klabu kwa kumpa ushirikiano wa kutosha katika muda wote aliokaa nao.

“Baada ya kupewa taarifa hizo jana (juzi) nilienda klabuni kuagana na wachezaji. Naushukuru uongozi kwa kutimiza kila kitu kilichomo katika mkataba wetu. Meneja wa Azam (Patrick Kahemele) amenilipa kila kitu na kunipatia tiketi ya ndege ya kuirejea Serbia,” alisema Bunjak huku akikataa kutaja kiasi alicholipwa kwa kile alichodai kuwa ni siri.

Kwa upande wake, Kahemele alisema jana kuwa wakurugenzi wamefikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na kiwango cha timu yao tangu waikabidhi kwa kocha huyo.

Alisema wameamua kumrejesha Hall kwa kuwa wachezaji walikuwa wameshazoea mfumo wake wa ufundishaji na kwamba kocha huyo amewaahidi kujirekebisha kwa mambo mbalimbali aliyowakosea na kuamua kumtimua.

“Bunjak ni kocha mzuri, lakini mfumo wake unahitaji muda mrefu kuzoeleka kwa wachezaji wetu. Tumeamua kumrejesha Stewart na atatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kesho saa moja usiku,” alisema.

Simba,Yanga viwanjani leo


Timu ya Simba

Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambayo imefika kwenye raundi ya 11 ya mzunguko wa kwanza itaendelea leo kwenye viwanja vitano tofauti ambapo timu 10 zitashuka dimbani kuwania pointi tatu muhimu, zikiwamo za Simba na Yanga zilizo kileleni mwa ligi hiyo.

Mechi nyingine ya ligi iliyotarajiwa kufanyika leo kati ya Ruvu Shooting dhidi ya Prisons ya Mbeya imeahirishwa hadi itakapotangazwa baadaye kufuatia ajali ya gari waliyoipata wachezaji wa Prisons wiki iliyopita wakati walipokuwa njiani kuelekea jijini Tanga.

Vinara wa ligi hiyo, Simba, ambao waliwasili Morogoro jana saa 7:00 mchana, watakuwa wageni wa Polisi Morogoro katika mechi itakayofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati watani zao wa jadi, Yanga, wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi  watawakaribisha JKT Mgambo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic, aliliambia gazeti hili kwamba wachezaji wake wako tayari kwa mechi hiyo ya ligi na jana jioni walitarajiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Jamhuri ili kuuzoea kabla ya kushuka dimbani leo jioni.

Mserbia huyo alisema kwamba licha ya ushindani mkali wanaokabiliana nao katika mechi zao za mikoani, Simba inataka kuendeleza kasi yake ya kufanya vizuri na hatimaye kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo na kutowapa nafasi mahasimu wao, Yanga kuwashusha.

Alisema kwamba amewataka nyota wake kutoidharau Polisi Morogoro licha ya kuonekana kuwa hawakufanya vizuri katika mechi zao zilizopita kwani timu ya aina hiyo huwa ni hatari zaidi.

"Tunatarajia kushinda na nimewaeleza kuwa wasiidharau kwa sababu haijashinda mechi yoyote tangu ligi ilipoanza," alisema kocha huyo.

Kocha Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts, alisema kwamba kikosi hicho sasa kimeiva na kinataka kusonga mbele tu.

Brandts alisema kwamba kila siku amekuwa akiwakumbusha wachezaji wake kupambana katika dakika zote 90 za mechi na kutoruhusu wapinzani kukaribia lango lao.

Daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani, alisema kuwa wachezaji, Kevin Yondani, Said Bahanunzi na Didier Kavumbagu ambaye jana alirejea mazoezini kuungana na wenzake, wako vizuri na maamuzi ya kucheza au kutocheza yako kwa kocha Brandts.

Daktari huyo alimtaja beki Salum Telela ambaye aliteguka kifundo cha mguu ndiye anayeendelea na matibabu kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hana nafasi ya kucheza mechi ya leo na ya Jumapili dhidi ya Azam.

Mechi nyingine zitakazochezwa leo ni kati ya Toto Africans dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza huku JKT Ruvu wakiikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi, Mbagala na jijini Arusha, wenyeji JKT Oljoro nao wataikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Arusha, kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime, alisema kwamba timu yake haijapata matokeo mazuri hivi karibuni lakini hali hiyo ni ya kimchezo kwa sababu wachezaji wamekuwa wakipambana kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.

Maxime alisema kwamba wanaamini watazinduka na kurejesha kasi yao kuanzia leo na watatumia vyema uwanja wa nyumbani katika mechi zote zinazofuata.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwenye Uwanja wa Chamazi kwa kuzikutanisha Azam inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo dhidi ya Coastal Union iliyo kwenye nafasi ya pili.

Serikali ‘yaipiga stop’ Tanesco kupandisha bei ya umeme

Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)

Wizara ya Nishati na Madini imelizuia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) kupandisha bei ya umeme kama lilivyokuwa limepanga kufanya hivyo Januari, mwakani.

Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo, alisema hayo juzi wakati akihojiwa kwenye kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya ITV.

“Kumekuwa na madai kwamba, Tanesco watapandisha bei ya umeme ifikapo Januari 2013. Lakini nimewaelekeza Tanesco na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji) wasipandishe bei ya umeme,” alisema Profesa Muhongo.

Alisema ameielekeza Tanesco isipandishe bei kwa sababu katika deni la dola za Marekeni milioni 250 inazodaiwa, serikali imekuwa ikilisaidia kulipa.

Profesa Muhongo alisema hadi sasa serikali imekwishatoa dola za marekani milioni 50 kupunguza deni hilo, ambalo limebaki dola za Marekani milioni 200.

Alisema serikali imepunguza bei ya kuunganisha umeme wananchi ili ifikapo mwaka 2015 asilimia 30 ya Watanzania wawe wanapata nishati hiyo tofauti na sasa, ambapo wanaopata ni asilimia 18.4 tu.

Profesa Muhongo alisema wizara yake imejipanga kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme kifikie megawati 2,780 kutoka megawati 1,438 zinazozalishwa hivi sasa ifikapo mwaka 2015.

Alisema uzalishaji huo utaongezeka kutokana na mkakati uliopo wa kuongeza vyanzo vya uzalishaji umeme na kwamba, hivi sasa matumizi ya umeme kwa nchi nzima ni megawati 830.

“Mgawo wa umeme haupo na wala hautakuwapo, wengine wanaufurahia uwapo  kwa sababu zao binafsi za kibiashara na kisiasa. Lakini nawahakikishia wananchi hakutakuwa na mgawo wa umeme,” alisema Profesa Muhongo.

Akizungumzia suala la gesi, alisema wizara yake imewasilisha sera ya gesi katika Baraza la Mawaziri na rasimu ya sera hiyo imepelekwa kwa wakuu wa mikoa ili wananchi waweze kutoa maoni yao kabla ya kupelekwa bungeni Februari, mwakani.

Profesa Muhongo alisema rasimu ya sera hiyo imepelekwa katika mikoa, ambayo gesi na mafuta inapatikana na, ambayo inatumia gesi hiyo kwa wingi ni Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani, Rukwa (Sumbawanga), Katavi, Mbeya na Arus
ha.

Bomu laua watoto watano


  *Waliliokota na kuanza kulichezea
  *Ajali yaua watu wawili yajeruhi 20
Kamanda wa Oparesheni Maalum wa Jeshi la Polisi, Peter Mvulla, akiwa na bomu la kutoa machozi alilolichukua kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kimnyaki iliyopo wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha jana. Bomu hilo lilirushwa kwa wanafunzi hao na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) bila ya kulipuka na kuwaepusha na madhara ambayo yangeweza kutokea.
Watoto watano wamekufa baada ya kulipukiwa na bomu la kutupa kwa mkono walilookota wakati wakikusanya vyuma chakavu wilayani Karagwe Mkoa wa  Kagera.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Philip Kalangi, alithibitisha kutokea tukio hilo jana asubuhi katika Kijiji cha Rugarama Kata ya Iyande wilayani humo wakati wakichezea bomu hilo nyumbani ambalo liliokotwa juzi na Evadius Robert (17) akidhani kilikuwa chuma chakavu.

Aliwataja watoto  kuwa ni Fenias Frank (3);  Faraji Frank (1); Edgar Gidion (15); Faustin Alfonce (17) na Patric Kamali (12).

Alisema watalaam wa mabomu wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walifika eneo hilo kufanya uchunguzi  ili kubaini bomu hilo lilitoka wapi hadi kufika hapo.

Aliwataka wakazi wa eneo hilo kuacha kuokota kitu wasichokijua ambacho kinachofanana na chuma ili kuepuka majanga ya kulipukiwa na mabomu kama yamebakia sehemu hizo.

TAARIFA ZA AWALI

Taarifa za awali kabla Kamanda Kalangi kuzungumza na NIPASHE jana jioni, zilieleza kuwa watu saba wakiwamo wanne wa familia moja, wakazi wa kijiji hicho wamekufa kwa kulipukiwa na  bomu.

Taarifa hizo kutoka wilayani Karagwe zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea jana  saa nne asubuhi kijijini hapo na kusababisha vifo vya watu saba wakiwa watoto chini ya miaka 18.

 Waliotajwa kufa o ni  Eladius Robert (15), Fenius Frank (3), Faraja Frank (1), Scatus Kamali (15), Nelson Alphonce (14), Edger Gidion (14) na mmoja ambaye jina lake halikufahamkika, lakini alikadiriwa kuwa na umri wa miaka 17.

Imeelezwa kuwa watoto hao walikuwa katika shughuli ya kuokota vyuma chakavu katika kijiji hicho kwa ajili ya kuuza kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na ununuzi wa vyuma chakavu wilayani humo.

Mmoja wa wazazi wa watoto hao, Frank Robert (35),  mkazi wa kijiji hicho, aliwaambia waandishi wa habari kuwa watoto hao walionekana asubuhi wakiokota vyuma chakavu kwa ajili ya kuuza na kuwa ghafla alisikia mlipuko wa kishindo ambao ulisababisha vifo vyao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Luteni Kanali  Benedict Kitenga, alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo  ambavyo vinadaiwa kusababishwa na bomu la kutupwa kwa mkono.

 

Kitenga  aliwataka wakazi wa wilaya za Karagwe na Kyerwa hususani zile zinazopakana na nchi jirani kuwa waangalifu.

WAWILI WAFA, 20 WAJERUHIWA

Watu wawili wamefariki papo hapo na wengine 20 kujeruhiwa vibaya katika ajali ya lori aina ya Canter walilokuwa wakisafiri  kutoka Muheza mjini kuelekea Tarafa ya Amani, mkoani Tanga.

Ajali hiyo ilitokea jana  jioni katika maeneo ya Daraja Mbili  kijiji cha Ubembe, Kata ya Nkumba wilayani Muheza na kuthibitishwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tanga, Jafari Mohamed.

Inadaiwa kuwa Canter hilo lenye namba za usajili T 497 ATU lilipata ajali hiyo wakati likiwa limebeba zaidi ya watu 30 na mizigo.

Waliokufa ni  Omari Salim, mkazi wa Kazita Amani na Renard Yusuph (7). Miili yao imehifadhiwa chumba cha maiti cha Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza.

Waliojeruhiwa ni Zena Kasimu; Zuena Husseni; Mele Yohana; Salimu Luka; Mariam Mchongoma; Moza Omari; Rehema Omari; Happy Mkai; Mathayo Kusaga; Sadiki Omari; Emanuel Bakari na Godfrey Pesambili.

Wengine ni Chedi Hassan; Omari Juma; Joseph Logasila; Ibarahimu Rashidi;  Ramadhani Ally; Ally Abdallah; Ramadhani Athumani na Ibarahim Makame.

Kundi la watu jana jioni walifurika katika hospitali hiyo kuwatafuta ndugu zao ambao walikuwa wakisafiri kwa lori hilo huku vilio vikitawala.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Ibrahim Matovu; Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Amiri Kiroboto; Mkuu wa Wilaya hiyo, Subira Mgalu na madiwani walifika hospitalini hapo kuwajulia hali majeruhi hao na kuwapa pole.

Purukushani migodini nchini A. Kusini

Wafanyakazi wa migodi wanaogoma

Makabiliano makali yamezuka kati ya Polisi na wachimba migodi katika mgodi wa madini ya Platinum wanaogoma Kaskazini Magharibi mwa Johannesburg.

Polisi waliwafyatulia risasi za mipira na kuwarushia waandamanaji gesi ya kutoa machozi katika makabiliano hayo ambapo wachimba madini hao wanataka nyongeza ya mishahara.

Kampuni ya Anglo-American Platinum imekubali kuwarudisha kazini wachimba madini elfu kumi na mbili waliofutwa kazi na kuwalipa malimbikizo ya mishahara, suala lililokataliwa mbali na wachimba madini hao.

Msururu wa migomo ya wachimba migodi na madini imeendelea kukumba Afrika Kusini katika miezi ya hivi karibuni na kuathiri pakubwa uchumi wa nchi hiyo.

Wakimbizi wa Burundi nchini TZ warejeshwa makwao



Ramani ya Burundi

Serikali ya Tanzania imeanza rasmi hatua za kuwarejesha makwao raia wa Burundi waliovuliwa hadhi ya ukimbizi.

Ni katika hatua za kuifunga rasmi kambi ya Mtabila ambayo ni kambi pekee iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi nchini humo wapatao elfu thelathini na saba.

Sanjari na uamuzi wa kuwarejesha makwao raia hao, shughuli hii inaambatana na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote ambao hawako tayari kurejea Burundi.

Shughuli ya kuwarejesha makwao kwa hiyari raia wa Burundi waliokuwa wakimbizi hadi mwezi Agosti mwaka huu kabla ya kuvuliwa hadhi ya ukimbizi na serikali ya Tanzania,ilimalizika rasmi Jumatatu ambapo kuanzia leo kinachofuata dhidi ya wakimbizi hao ni kuandikishwa kwa kufuatwa kwenye maeneo wanakoishi kambini na kisha kupakiwa kwenye magari na kurejeshwa Burundi.

Akizungumza na mwandishi wa BBC mjini Dar es Salam Eric David Nampesya, mkuu wa kambi hiyo ambaye ni mwakilishi wa wizara ya Mambo ya ndani nchini humo, Bwana Frederick Nisajile, alisema utaratibu huo utakavyokuwa baada ya kukamilika kwa shughuli ya kurejea kwa hiyari ya 'Kimombo Voluntary repatriarition.'

Bwana Nisajile alisema inatarajiwa kuwa raia wa Burundi wapatao elfu moja watarejeshwa makwao kila siku katika utaratibu huu ambao pia utawahusisha maafisa wa idara ya Uhamiaji ili kuwakamata wale wote watakaokaidi kurejea makwao.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi UNHCR Bi Chansa Kapaya anasema hakuna uwezekano kwa Raia hao wa Burundi kutafutiwa nchi ya tatu kwa sababu wao si wakimbizi tena kwa wakati huu.

Nafasi hiyo haipo tena,nafasi kama hiyo hutolewa kwa wakimbizi,hawa walipokuwa wakimbizi zamani na kwa sasa walishavuliwa hadhi ya kuwa wakimbizi,kwa maana hiyo hawawezi kupewa nafasi ya kutafutiwa hifadhi katika nchi ya tatu,kwa maana hiyo suluhisho pekee kwao ni kurejea Burundi.

Kuanza kufungwa kwa Kambi hiyo ya Mtabila kunahitimisha miaka 19 tangu ilipofunguliwa mnamo mwaka 1993,wakati huo ilipoanza kupokea raia wa Burundi waliokimbia machafuko ya kivita yaliyofuatia mauaji ya aliyekuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Burundi hayati Melchior Ndadaye.

Kiongozi wa upinzani Rwanda ahukumiwa jela


Victoire Ingabire

Kiongozi wa upinzani nchini Rwanda Victoire Ingabire amehukumiwa miaka minane gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kosa la uhaini

Viongozi wa mashtaka walitaka afungwe maisha jela kwa kutishia usalama wa nchi.

Mahakama imempata na hatia ya kupuuza mauaji ya Kimbari yaliyotokea mwaka 1994.

Ingabire hakuwa mahakamani wakati hukumu ilipotolewa dhidi yake kwani amekuwa akisusia kuhudhuria vikao vya kusikilizwa kwa kesi hiyo akisema imeshinikizwa ksiasa,.

Alikamatwa mwezi Aprili mwaka 2010 na kuzuiwa kushiriki uchaguzi uliofanyika mwaka huo.

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI OKTOBA 31

.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.

WATUHUMIWA UCHOMAJI WA MAKANISA MBAGALA, WAPANDISHWA TENA KIZIMBANI

Na Musa Mateja

WATUHUMIWA 47 wanaokabiliwa na kesi ya kuharibu na kuchoma moto makanisa wakati wa vurugu za baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu Mbagala, leo wamepandishwa tena kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka mbele ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Bw. Tumaini Kweka, yanayowahusisha na kesi ya  kula njama kwa nia ya kutenda makosa kinyume na sheria.

Askari magereza akiwafungulia pingu baadhi ya watuhumiwa  tayari kwa kusomewa mashitaka yao.

Makosa mengine yanayowakabiri watuhumiwa hao ni pamoja na kosa la  kuvunja jengo kwa nia ya kufanya uharifu, uharibifu wa mali za kanisa, wizi wa vifaa vya kanisa, kuchoma kwa makusudi jengo linalotumika kwa shughuli za ibada na kuhatarisha maisha ya mlinzi.
Mashitaka yote hayo leo yamewakilishwa mbele ya Hakimu, Bw. Binge Mashabala, ambaye alisikiliza pande zote mbili na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 7 mwaka huu kwa ajili ya kukamilisha upelelezi wa kesi hizo.

Watuhumiwa wakipelekwa kizimbani.
…wakipanda ngazi tayari kwa kuelekea chumba cha mahakama.
Baadhi ya watuhumiwa 47 waliyofikishwa kizimbani wakiwa ndani ya mahakama.
Wakirejeshwa mahabusu.
Baadhi ya ndugu na jamaa wa watuhumiwa hao wakiwa nje ya mahakama.
(Habari/Picha: Musa Mateja/GPL)

Pembe za mabilioni zamakatwa jijini Dar


  *Zakutwa kwenye nyumba jijini Dar
  *Zilikuwa zikisafirishwa kwenye jeneza
Baadhi ya watuhumiwa wanaodaiwa kukutwa na meno ya tembo katika eneo la Kimara Stop Over Jijini Dar es Salaam wakiwa chini ya ulinzi wa polisi. Nyuma yao (kwenye gari) ni baadhi ya meno hayo yenye thamani ya Sh. Bilioni 2.2

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekamata shehena ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh. bilioni 2.15.

Aidha, watu wanne wanashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na shehena hiyo.


Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova, jana aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwamba, shehena hiyo ni vipande 214 vya meno ya tembo na mifupa mitano ya mnyama huyo yenye uzito wa kilo 450.6.


Alisema watuhumiwa hao walikamatwa eneo la Kimara Stop Over juzi baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kwamba kuna nyumba inashukiwa  kuwa na mali zilizoibiwa pamoja na nyara za serikali.


Kamanda Kova aliongeza kuwa, baada ya Jeshi hilo kupata taarifa lilijipanga na kuipekua nyumba hiyo aliyopanga Peter Kami ambaye anaishi pamoja  na Leonida Kabi na kukuta vipande 214 vilivyokuwa vimehifadhiwa kwenye chumba kimojawapo.


Alisema meno hayo yalikutwa yakiwa yamehifadhiwa kwenye magunia 12 huku yakiwa yamefunikwa kwa bendera ya Taifa.


“Pamoja na meno hayo, pia zilikutwa pembe za ng’ombe 10 zikizokuwa zimeshindiliwa pamoja na chokaa, pamoja na mifupa ya tembo mitano, yenye kilo 450.6,” alisema Kova.


Aidha, Kamanda Kova aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni pamoja na dereva wa daladala aliyekuwa akijifanya kuwa ni ofisa wa polisi aliyejulikana kama Polisi Simoni (42), Charles Wainaine (41), mkazi wa Rombo Tarakea, ambaye ni ndugu yake na Peter Kabi, ambao wote ni Wakikuyu kutoka nchini Kenya.


Kamanda Kova alifafanua kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa watuhumiwa hao ni wahalifu wazoefu katika matukio ya mtandao wa ujambazi, usafirishaji, pamoja na umiliki wa nyara za serikali.


“Mpango wa siri uliokuwepo ni kutumia gari aina ya Coaster, iliyokuwa iendeshwe na dereva Polisi Simon na kuweka jeneza lenye meno hayo na kulifunika na bendera ya Taifa ili ionekane wanasafirisha maiti ya mtu maarufu serikalini kwa lengo la kuvihadaa vyombo vya dola,” alisema Kamanda Kova.


Kwa mujibu wa Kova, mtuhumiwa Leonida Kabi, anashikiliwa kwa kosa jingine ambalo ni kumshawishi askari aliyezikamata nyara hizo kwa kutaka kumpa rushwa ya Sh. milioni  15, na kuahidi kuwaongezea kiasi kingine siku ya pili yake.


Aidha alisema kuwa uchunguzi wa kina utafanyika ili kubaini mtandao mzima wa wizi wa nyaraka za serikali hapa nchini pamoja na nchi za Kenya na Mashariki ya mbali na popote duniani ili kukomesha uhalifu huo.


Watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.


Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, kiasi hicho cha meno ya tembo ni sawa na tembo 91 waliouawa.


Aidha, kukamatwa kwa meno hayo kunakuja siku moja tu baada ya Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, kueleza kwamba mwendelezo wa matukio ya kuuawa kwa tembo ni matokeo ya kuwalinda majangili badala ya kuwachukulia hatua.


Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam Mchungaji Msigwa alimshauri Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati na kuvunja mtandao wa ujangili ili kunusuru wanyamapori na maliasili nyingine za Taifa.


Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), alisema mpaka sasa ni miezi mitatu tangu alipowasilisha taarifa za ujangili bungeni na kumtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, achukue hatua dhidi ya majangili hao na matokeo yake amewaajibisha watu watatu wa Idara ya Wanyamapori huku watuhumiwa wakubwa wakiachwa jambo ambalo alidai ni hatari na kusababisha idadi ya wanyama kupungua kila wakati.


Alisema wiki iliyopita pembe za ndovu zenye uzito wa tani nne kutoka Tanzania na Kenya zenye thamani ya Sh. bilioni 2.5 zimezipotiwa kukamatwa na vyombo vya usalama vya mamlaka ya Jiji la Hong Kong.


Katika Mkutano wa Bunge uliopita, Kambi ya Upinzani bungeni pamoja na maoni ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliwataja vinara wa ujangili akiwemo Bryson Baloshingwa ambaye ni kiongozi wa mtandao wa ujangili kwa kufadhili uwindaji wa faru na biashara haramu ya meno ya tembo; uharamia unaofanyika katika hifadhi za Serengeti, Katavi, Tarangire, Ziwa Manyara na Ngorongoro.


Alisema Baloshingwa anafadhili pia majangili wanaoua wanyama katika mapori ya akiba ya Ugalla, Rungwe, Moyowosi na Maswa.


Alisema inashangaza kwamba wafadhili na majangili wanafahamika kwa majina lakini hawachukuliwi hatua na pindi wanapokamatwa hufunguliwa kesi rahisi zenye dhamana hivyo huachiwa kwa dhamana.


“Usalama wa tembo uko hatarini kutokana na serikali kutochukua hatua dhidi ya ujangili wa tembo pamoja na taarifa hizi kuwepo serikalini na viongozi wa CCM kushiriki katika ujangili," alisema.


WATUHUMIWA MAUAJI YA BARLOW


Wakati huo huo, Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeeleza kwamba watu waliomuua aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow, walikimbilia jijini humu na kufanya uhalifu kabla ya kukamatwa.


Kamanda Kova alisema watu hao ni watuhumiwa wakubwa wa ujambazi wa kutumia silaha nchini na hususani katika majiji ya Dar es Salaam na Mwanza.


WATUHUMIWA SUGU MBARONI


Katika tukio jingine, Kamanda Kova alisema polisi wamekamata watuhumiwa sita sugu wa ujambazi, silaha mbili na risasi 25 za SMG pamoja na jambazi sugu akiwa na sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

CHANZO: NIPASHE

Ghasia kufuatia mauaji ya mwanasiasa Kenya

Ghasia zilizuka baada ya kifo cha Kwega mjini Kisumu

Mwanasiasa wa Kenya Shem Kwega ameuawa huku mke wake akijeruhiwa mjini Kisumu Magharibi mwa Kenya.

Bwana Kwega alikuwa mshirika wa karibu wa waziri mkuu, Raila Odinga, anayegombea urais.

Polisi waliwarushia gesi ya kutoa machozi waandamanaji waliokuwa wanaelezea kero lao kuhusu mauaji hayo wakidai kuwa yalikuwa mauaji ya kupangwa.

Hali ya taharuki inatanda nchini Kenya kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika mwezi Machi.

Zaidi ya watu 1,000 waliuawa kwenye ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 zilizofuatia uchaguzi uliozua utata mkubwa kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya tangu uhuru.

Wiki jana kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya ICC, Fatou Bansouda alielezea wasiwasi kuhusu tatizo la vurugu nchini humo.

Mahakama ya ICC itawafungulia mashtaka washukiwa wanne wa ghasia hizo za baada ya uchaguzi akiwemo naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta ambaye pia anawania urais kwa kuhusika na ghasia hizo.

Bwana Kwaga na mkewe walipigwa risasi na washukiwa waliokuwa wanaendesha pikipiki.

Aidha marehemu Kwega alikuwa mfanyabiashara maarufu ambaye alikuwa anagombea kiti cha ubunge kwa chama cha waziri mkuu.

Ingawa polisi wangali wanashuku kuwa huenda kilikuwa kitendo cha wizi, lakini wafuasi wake wanaamini kuwa yalikuwa mauaji ya kupangwa.

13 wafariki kutokana na kimbunga Sandy

Athari za kimbunga Sandy mjini New York

Mojawapo ya vimbunga vikubwa zaidi kuwahi kupiga Mashariki mwa Pwani ya Marekani kimesababisha mafuriko makubwa katika baadhi ya sehemu za mji wa New York.

Maeneo mengi mjini yamewachwa katika giza baada ya huduma za umeme kukatizwa.

Kimbunga hicho kilipiga ardhi kwenye Pwani ya New Jersey karibu na mji wa Atalanta muda mfupi jana usiku/

Dhoruba kali kutoka mjini Florida hadi nchini Canada imepiga Mashariki mwa Marekani na kusababisha mawimbi makali mjini New York.

Maji yamefurika kwenye barabara na katika njia za reli pamoja, maeneo ya kuegesha magari na katika eneo la Ground Zero, eneo ambalo mashambulizi ya Septemba kumi na moja yalitokea.

Sehemu kubwa za mji wa New York ziko kwenye giza baada ya milingoti ya umeme kuharibiwa.

Wagonjwa waliondolewa kwenye hospitali moja baada ya umeme kukatika.

Zaidi ya watu milioni tano walisemekana kukosa umeme katika eneo la Pwani baada dhoruba kali huku takriban wengine milioni moja wakishauriwa kuhama nyumba zao. Athari za kimbunga hicho labda huenda zikajulikana baadaye leo.

Jeshi la wanamaji la Iran lawasili Sudan


Meli za Iran ilitia nanga katika badnari ya Sudan.

Msururu mdogo wa meli za jeshi la wanamaji la Iran umetia nanga katika bandari ya Sudan kuwasilisha kile ambacho shirika la kitaifa la habari Iran ISNA linasema ni ujumbe wa amani na usalama.

Ziara hiyo katika bandari ya Sudan inajiri siku sita baada ya shambulio la angani dhidi ya kiwanda cha silaha mjini Khartoum ambalo serikali nchini humo imeilaumu Israeli kulitekeleza.

Sudan imelalamikia Umoja wa Mataifa kuwa Israel ilishambulia kiwanda chake ambacho kinaaminiwa kuendeshwa na Iran.

Hata hivyo, Israel haijathibitisha au kukana ikiwa ndiyo ilihusika na shambulio hilo.

Kulingana na shirika la habari la serikali, meli hizo zilizowasili nchini Sudan Jumatatu asubuhi, inajumuisha meli inayoweza kubeba helikopta tatu.

Ziara ya meli ya kivita za Iran nchini Sudan, ni ishara kuwa uhusiano wa kiusalama kati ya nchi hizo mbili.

Kiwanda cha silaha ambacho kililengwa kwa mashambulizi hayo, inaaminiwa na wadadisi kuwa kiwanda cha Iran kinachotengeza silaha na zana zengine za kivita baadhi ambazo huingizwa kimagendo nchini Misri kuwaendea wapiganaji wa Hamas katika ukanda wa Gaza.

Israel imekataa kutoa tamko lolote kuhusu shambulizi hilo

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI OKTOBA 30

.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.