Dola 377,000 zatumika kununua iPad bungeni

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni. 


BUNGE nchini Uganda limetumia zaidi ya  dola 377,000 kununa kompyuta aina ya iPad kwa ajili ya wabunge wote .

Maofisa wa bunge hilo walisema kuwa mbali na kuwaweka wabunge hao karibu na  ulimwengu wa teknolojia, wanatarajia kuwasaidia kupunguza gharama za fedha zinazotokana na matumizi ya uchapishaji wa nyaraka mbalimbali.

Kamishna wa bunge hilo Elijah Okupa alisema kuwa kompyuta hizo ni bora na zinafaa kwa matumizi hivyo ni vyema zikatumiwa vizuri.

Alisema  iPad hizo zitakuwa ni mali ya wabunge lakini kama mtu atatumia kwa muda wa miaka mitano asitegemee itakuwa na ubora uleule wa kumwezesha mwingine atumie kwa miaka hiyo alisema Okupa

Kwa mujibu wa takwimu kutoka katika bunge hilo zilionyesha Serikali imekuwa ikitumia zaidi ya dola 12 katika miaka miwili sasa kwa ajili ya mahitaji ya kama kompyuta, uchapishaji wa nyaraka, mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha mawasiliano kuwa bora katika bunge.

Kwa mujibu wa mbunge kutoka mashariki, Medard Segona alisema kuwa kutokana na uwepo wa ipad hizo wanategemea kupunguza matumizi ya fedha zilizokuwa zikipotea hapo awali.

‘’Vifaa hivyo vitapunguza sana matumizi ya fedha kwa kuwa hapo awali wizara ya fedha ilikuwa ikichapisha zaidi ya nyaraka 400 kwa kila mbunge na maofisa wengine waliopo ndani ya bunge hilo’’alisema

Aliongeza kuwa komputa hizo ni muhimu kwa utendaji kazi hasa katika kipindi hicho cha kuendeleza matumizi ya teknolojia.

Hata hivyo taarifa zilisema kuwa wabunge hao bado hawana uelewa mzuri juu ya matumizi hayo licha ya kuwa kampuni imeahidi kutoa  mkataba wa mafunzo ambayo pia yatasaidia kupunguza gharama za matumizi.

FBI yaingia Zanzibar kusaka wauaji wa Padri Mushi

Waziri wa mambo ya Ndani,Dk Emmanuel Nchimbi. 


ASKARI wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), wamewasili Zanzibar kufanya uchunguzi wa kuwabaini waliomuua kwa kumpiga risasi, Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki.


Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema kwa simu jana kuwa wapelelezi wa kigeni wamewasili Zanzibar na tayari na wameanza kazi hiyo.
Wapelelezi hao wameingia kazini kushirikiana na wenzao wa Tanzania kuwasaka wauaji wa padri huyo aliyepigwa risasi Februari 17, mwaka huu.


Padri Mushi aliuawa asubuhi alipokuwa akienda kuongoza ibada katika Kanisa la Mtakatifu Teresia, Beit el Raas, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kuzikwa Kitope, Kaskazini Unguja Februari 20, mwaka huu.


“Wapelelezi kutoka nje wamefika na wapo kazini,” Kamishna Mussa alisema bila ya kutaja wanatoka nchi gani.


Pia Kamishna Mussa hakutaka kueleza ni lini wapelelezi hao walifika Zanzibar na idadi yao kwa maelezo kwamba hizo ni siri za Polisi na zikivuja, zitaingilia uchunguzi wanaoufanya.
Hata hivyo, vyanzo vya ndani ya Serikali, vililithibitishia gazeti hili kuwa FBI walikuwa wameanza kuwasaka wauaji wa Padri Mushi.


Kutua kwa wapelelezi hao wa Marekani kunafuatia kauli iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete katika salamu zake za rambirambi baada ya mauaji ya Padri Mushi kuwa ameliagiza Jeshi la Polisi kutumia nguvu zake zote pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya usalama vya ndani na mashirika ya upelelezi ya nchi rafiki katika kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.


Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alihusisha tukio hilo na vitendo vya ugaidi wakati akitoa tamko la Serikali na kueleza kuwa Rais Kikwete ameidhinisha Serikali kugharamia wapelelezi kutoka nje.


Pia ujio wa FBI unaweza kuhusishwa moja kwa moja na dhamira iliyoonyeshwa mapema na Serikali ya Marekani iliyokuwa tayari kusaidia upelelezi wa mauaji hayo na hiyo ilibainishwa katika salamu za rambirambi za kifo hicho na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt.
Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya Serikali vimeeleza kuwa kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo, maofisa wa FBI walifanya mazungumzo na Waziri Nchimbi na viongozi wengine wa Serikali kwa ajili ya kuangalia ni namna gani watafanya shughuli hiyo.


“Pia hawa jamaa wa FBI walifanya vikao na maofisa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ili kuweka sawa mazingira ya kufanya upelelezi huu,” kilisema chanzo kingine.


Habari zaidi zinaeleza kuwa uchunguzi wa wapelelezi hao wa FBI na wale wa Tanzania hautajikita katika kusaka wauaji wa Padri Mushi pekee, bali watakwenda mbali zaidi na kuchunguza wale wote wanaojihusisha na wimbi la vurugu za kidini nchini ambalo linatishia amani.


Hii itakuwa mara ya pili kwa FBI kuja nchini kufanya operesheni kubwa ya upelelezi. Mwaka 1998 walifika kuchunguza kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani na kugundua kuwa Kundi la Al-Qaeda lilihusika.


Aidha hiyo ni mara ya tatu kwa wapelelezi wa Tanzania kushirikiana na wageni kuchunguza matukio ya uhalifu baada ya mwaka 1984, Idara ya Upelelezi ya Uingereza, Scotland Yard ya Uingereza kuchunguza kuungua kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

 Habari zaidi zinaeleza kuwa kabla ya ujio wa FBI, Serikali ya Tanzania ilizungumza na taasisi za upelelezi za nchi tano ili kuongeza nguvu. Taasisi nyingine zinazodaiwa kuombwa kufanya kazi hiyo ni pamoja na Scotland Yard na Shirika la Upelelezi la Israel, Mossad.


Akizungumzia upelelezi wa mauaji ya Padri Mushi, Kamishna Mussa alisema watu kadhaa wametiwa mbaroni kwa mauaji lakini asingeweza kutaja idadi.

Kuuawa kwa padri huyo ni miongoni mwa matukio ya  kushambuliwa kwa viongozi wa dini huko Zanzibar baada ya kumwagiwa tindikali Katibu wa Mufti, Fadhil Soraga, kupigwa risasi kwa Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki na kuuawa kwa Sheikh Ali Khamis shambani kwake huko Kidoti, Mkoa wa Kaskazini Unguja

Malipo Muhimbili sasa kupitia benki

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,Dk Marina Njelekela akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam juzi. Kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa hospitali hiyo,Agnes Kuhenga. 

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam,  imeanza  mkakati wa  kudhibiti mianya ya ufisadi chini ya  mpango utakaowawezesha wagonjwa, kulipia gharama za huduma kupitia benki.
Pamoja na mkakati huo, menejimenti  ya hospitali hiyo kubwa nchini, imesema  imebaini kuwa mrundikano wa wagonjwa, unachangiwa na udhaifu katika utoaji tiba kwenye hospitali za mikoa na wilaya.

Akizungumzia mkakati wa kudhibiti mianya ya ufisadi, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo,  Dk Marina Njelekela, alisema uchunguzi umebaini hatua ya kutumia benki katika kukusanya malipo ya gharama za huduma mbalimbali, itasaidia kuokoa  zaidi ya asilimia 20 ya fedha zinazopotea.

“Kufanikiwa kwa mkakati huu, kutaiwezesha hospitali kuvuka lengo la kugharamia bajeti ya matuminzi ya kawaida, kwa kutumia mapato ya ndani kwa asilimi 40 kama sera ya mabadiliko ya taasisi za umma inavyoeleza,” alisema Dk Njelekela.

Alisema mabadiliko ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia benki, yataongeza uwezo wa kifedha kwa matumizi ya kawaida ya mapato ya ndani kutoka asilimia 58 hadi kufikia zaidi ya asilimia 72 katika mwaka wa fedha wa 2013/14.

Mkurugenzi huyo  alisema tayari hospitali   imeingia makubaliano na Benki ya NMB, ili kutekeleza mkakati wa  kukusanya mapatio yake na kwamba hatua hiyo itaanza rasmi Machi 11 mwaka huu.

“Mfumo huo utamwezesha mgonjwa kupata hati ya gharama ya malipo ya huduma itakayokuwa inatolewa na  mfanyakazi  wa hospitali katika kituo cha karibu na huduma ,’”alisema

Kuhusu hospitali kuelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa, mkurugenzi alisema  udhaifu katika utoaji wa huduma za tiba na hasa hospitali za mikoa na wilaya, unachangia kwa kiasi kikubwa.
Alisema kama Seriklai itaboresha huduma katika hospitali hizo kwa kuzipatia madaktari wa kutosha na wataalam, tatizo hilo litapungua kama si kumalizika kabisa .

Alisema Shirika la Afya la Dunia (WHO,) litaka  daktari mmoja kuwahudumia  wagonjwa 10,000 lakini kwa Hospitali ya Muhimbili  madaktari wake wanatoa huduma kwa zaidi ya idadi hiyo.

Akizungumzia tatizo la wagonjwa kulala sakafuni,  mkurugenzi alisema  tatizo si  upungufu wa vitanda na kwamba tatizo ni nafasi ya kuweka viwanda vya wagonjwa.

Alisema majengo ya hospitali  yalijengwa kwa uwezo wa kuwekeza vitanda 35 tu.

Mauaji ya albino,ukataji viungo vyazidi kutikisa nchi (3)

Ofisa mmoja wa polisi alipendekeza nimwulize Kulwa kama mabaki ya Maganga bado yapo kaburini kwa kuwa halikujengewa kwa nondo na zege.

Nilimshauri awasilishe wazo lake kwa viongozi wake ili waiombe Mahakama ruhusa ya kulifukua kaburi la Maganga na kupata uhakika kama viungo vyake bado vipo au vimeondolewa.
Niliwaacha polisi wakiendelea na uchunguzi wao na mimi nikaanza safari ya kurejea Dar es Salaam.

Nilipokea taarifa za jaribio la kumdhuru mtoto wa miezi saba ambaye ana ulemavu wa ngozi, Makunga Baraka Februari 5, mwaka huu katika Kijiji cha Nyaruhande, Kitongoji cha Nyasubi, Kata ya Nyaruhande, Wilaya ya Busega, Mkoa wa Simiyu. Nilizungumza na mama mzazi wa mtoto huyo, Jane Daudi ambaye aliniambia kuwa alikuwa amehifadhiwa kwa muda katika kituo cha polisi kwa usalama wa mwanae.

“Nilipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni George wa eneo la Ndiko. Akaniambia, “Dada nakuhurumia sana kwa kuwa una mtoto mwenye ulemavu wa ngozi.  Niliwasikia watu hotelini wakipanga njama za kuja kumuua.”  Niliogopa sana na nikamweleza mama yangu. Tukaenda hadi kwa mwenyekiti wa mtaa hatukumkuta. Baadaye tukatoa taarifa kwa wanakijiji.

Hawakutuamini. Hawakutaka kuja kutulinda. Kabla ya saa tatu usiku watu watatu walikuja nyumbani kwetu na kuanza kuturushia mawe dirishani na mlangoni. Wanakijiji wakawaona na wakawafukuza lakini hawakuwakamata. Usiku ule wanakijiji walipeana zamu kutulinda.”

“Kesho yake asubuhi Mwenyekiti wa Mtaa akaniandikia barua kwenda polisi na wanakijiji wakatusindikiza. Polisi wanafuatilia taarifa nilizowapa. Naogopa sana. Nahofia maisha ya mwanangu Makunga. Sitaondoka polisi hadi hapo nitakapopata ulinzi mkali,” anasema Jane.

Maria Chambanenge (39)
Nilipokea taarifa nyingine za kushambuliwa kwa Maria Chamanenge (39) katika Kijiji cha Mkowe, Miangalua, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Mkoa wa Rukwa.

Nilikwenda kumwona Maria katika Hospitali ya Mkoa ya Sumbawanga. Kulikuwa na ulinzi mkali na tulielezwa kwamba tunapaswa kupata kibali cha polisi ili kumtembelea wodini.
Kamanda wa Mkoa wa Polisi alikuwa safarini kikazi.  Maofisa tuliowakuta walituelekeza kuwa kibali kinapatikana kwa Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO).

Tulirejea tena hospitali na baadaye tulionana na Kaimu Mganga Mkuu, alitupa idhini ya kuzungumza na Maria lakini chini ya usimamizi.

Maria alikuwa bado ana maumivu makali, baada ya kukatwa mkono wa kushoto. Madaktari walituhakikishia kwamba hali yake inaendelea vizuri kwa upande wa matibabu. Swali lilikuwa je, kwa upande wa kisaikolojia?

Maria ni albino na haoni vizuri. Sasa ameongezewa ulemavu wa viungo. Huyu ni mama wa watoto wanne: Shukuru (8), Edron (6), Rahab (3) na Emma (miezi mitano). Mama huyu ni mke wa tatu wa Gabriel Yohana. Atawaleaje watoto wake akiwa na mkono mmoja sasa? Atafanyaje kazi za nyumbani na za kilimo bila mkono wa pili?

Baada ya kumjulia hali, nilimwomba anielezee jinsi alivyoshambuliwa na kukatwa mkono wa kushoto usiku wa Februari 11, mwaka huu, chumbani akiwa amelala na wanae.
“Usiku wa manane, kati ya saa saba na saa nane hivi, Nilisikia vishindo vya nyayo vikitokea sebuleni ambako mwanangu Shukuru na Edron walikuwa wamelala. Ghafla nikamwona mume wangu ameshika upanga ananishambulia kichwani. Nikawa nashangaa na kuwaangalia usoni bila kujua kwa nini alikuwa ananishambulia. Akasema, “Nyamaza!” Mimi nikawa nalia. Akasema, Pole!  Nyamaza!”

Hospitalini hapo, Mama mdogo wa Maria, Everada Palachi (42) alikuwa amesimama kando ya kitanda cha Maria akiwa amembeba Emma.

Amekuwa akimlea mtoto huyo wa Maria na huku akimuuguza Maria. Baada ya kukatwa mkono anahitaji kusaidiwa kwa mambo mengi tu sasa.  

Everada akaingilia kati, “Wewe unajua unasema nini?”  akanigeukia, “Maria amechanganyikiwa!”
Maria akajibu kuwa hajachanganyikiwa bali mume wake, ndiye aliyempiga panga kichwani mara tatu na alishirikiana na wengine watatu (majina nayahifadhi kwa sababu wanachunguzwa na polisi – wapo rumande) na kumkata mkono wake wa kushoto na kukimbia nao.

Everada alisisitiza kuwa Maria amechanganyikiwa. Akaanza kuzungumza naye Kinyiha (kabila la watu wa eneo hilo).

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI FEB.28

.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.

Mwanafunzi Mbeya anaswa mtandao wizi wa Benki NMB

 

POLISI wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, limewanasa watu wanne akiwamo mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana, wilayani Bunda, mkoani Mara, baada ya kukutwa wakiiba fedha Benki ya NMB tawi la Tukuyu kupitia mashine za kutolea fedha (ATM).

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispin Meela alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku.
Meela aliwataja watuhumiwa  hao kuwa ni mkazi wa mjini Tukuyu,  Mfanyabishara wa Mbozi, mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana wilayani Bunda na mkazi wa Msasani Tukuyu.

Alisema akiwa nyumbani kwake usiku, alipigiwa simu na msamaria mwema na kuambiwa taarifa za kuwapo watu  wakiwa kwenye mashine hizo za kutolea fedha, huku wakiwa wanatoa fedha mfululizo na aliwatilia shaka.

“Jana  usiku saa 2:30 nilipigiwa simu na msamaria mwema na kuniambia kuwa,  kuna watu wapo Benki ya NMB wanatoa fedha ATM tena mfululilo huko wakiwa na kadi nyingi za ATM,” alisema Meela na kuongeza:“Baada ya kuambiwa hivyo nilimpigia simu OCD (Mkuu wa polisi wilaya), akatuma timu ya makachero eneo ta tukio na wakabahatika kuwakuta na kuwatia nguvuni.”

Meela alisema watuhumiwa  walikutwa wakiwa na kadi bandia za ATM 150 za watu tofautitofauti  na kwamba, hadi wanatiwa mbaroni tayari walikuwa na Sh20.5 milioni mkononi. Alisema kadi zote ni za NMB na kwamba, zilikuwa zinaonyesha  wateja wote ni walimu kutoka wilayani Mbozi.

Alisema baada ya watuhumiwa kuhojiwa  walidai ni wafanyabiashara wanajihusisha na kukopesha fedha walimu, hivyo  katika kuzirejea fedha hizo walimu waliwapatia kadi zao ili waende kutoa  benki.

“Kinachotupa hofu  hapa ni kwamba, kadi zote hizi zinaonyesha wateja kutoka wilayani Mbozi, sasa swali kwa nini waje kutolea fedha hizo wilayani kwetu?” alihoji Meela.

Alisema watuhumiwa wote wapo Kituo cha Polisi Tukuyu kwa mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alikiri kupata taarifa hizo, lakini alikataa  kulitolea ufafanuzi kwa sababu  wanaendelea na uchunguzi.

Mtanzania apewa uwaziri Rwanda

RAIS Paul Kagame 

RAIS Paul Kagame wa Rwanda amemteua Mtanzania, Profesa Silas Rwakabamba kuwa Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.


Kabla ya uteuzi huo, Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda. Ni mmoja wa mawaziri wanaoingiza sura mpya katika Baraza la Rais Kagame ambalo amelifanyia mabadiliko kwa kuunda wizara nyingine mpya.


Sura nyingine mpya katika Baraza hilo ambalo liliapishwa juzi Ikulu ya Rwanda ni pamoja na Seraphine Mukantabana (Wakimbizi na Menejimenti ya Maafa) na Oda Gasinzigwa (Ofisi ya Waziri Mkuu- Familia na Jinsia).


Akizungumza kwa simu na mwandishi wetu jana, mdogo wa Profesa Rwakabamba, Timothy Rwamushaija anayeishi Dar es Salaam, alisema ndugu yake alizaliwa katika Kijiji cha Bushagara, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.


Alisema Profesa Rwakabamba alikuwa Mtanzania aliyeamua kuchukua uraia wa Rwanda na wote baba yao ni Mzee Titus Rwamushaija... “Huyu ni kaka yangu wa tumbo moja na kwa kweli tumefurahi sana kwa mafanikio yake sisi kama wanafamilia.”


Naibu Makamu Mkuu - Taaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa Makenya Maboko alisema Profesa Rwakabamba alifanya kazi katika chuo hicho na aliondoka akiwa Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi.


“Aliondoka wakati Kagame alipoingia madarakani na alikwenda kuongoza Taasisi ya Teknolojia ya Kigali (KIST) kabla ya kwenda katika Chuo Kikuu cha Kigali,” alisema Profesa Maboko.


Msomi huyo alikwenda Rwanda mwaka 1997, baada ya kuombwa na Rais Kagame ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu katika taifa lake baada ya kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.


Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa kwanza wa KIST na kukifanya kuwa miongoni mwa vyuo bora barani Afrika kwa masuala ya teknolojia jambo lililomfurahisha Rais Kagame.


Baada ya mafanikio hayo, Rais Kagame alimteua kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, Butare ambako pia alijizolea sifa baada ya kusimamia vyema ujenzi wa mabweni kwa wingi na kiongozi huyo alimtunukia uraia wa nchi hiyo kama zawadi.


Hata hivyo, Profesa Rwakabamba atakuwa amelazimika kuukana uraia wa Tanzania kwa kuwa katiba ya nchi hairuhusu uraia wa nchi mbili.
Profesa Rwakabamba alipata elimu ya msingi huko Muleba na akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo.


Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza na kupata Shahada ya Uhandisi mwaka 1971 na 1975 alipata Shahada ya Uzamivu katika fani hiyohiyo.

 Alirejea Tanzania na kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Kitivo cha Uhandisi ambacho kilikuwa kimeanza mwaka huo.
Alipata nafasi mbalimbali katika muda mfupi aliokuwa hapo hadi alipotunukiwa kuwa Profesa mwaka 1981.


Mwaka 1985, Profesa Rwakabamba aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mwanzilishi wa Mafunzo katika Kituo cha Afrika cha Uhandisi Ubunifu na Uzalishaji (ARCEDEM), kinachodhaminiwa na Umoja wa Mataifa (UN) kilichopo Nigeria. Baada ya kazi hiyo, ndipo alipokwenda Kigali.


Tangu 1975, Profesa Rwakabamba amekuwa mjumbe wa bodi mbalimbali kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kuwa Bodi ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) na pia Kiongozi Mwandamizi wa Muungano wa Vyuo vya Kimataifa (IAUP).

‘Wafuasi 54 wa Ponda wana kesi ya kujibu’

Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (Kushoto) na Katibu wake,Sheikh Mukadam Swalehe wakiwa katikati ya askari magereza kwenye majengo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imetathmini ushahidi wa upande wa mashtaka yanayowakabili watu 54, wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda na kubaini kuwa wana kesi ya kujibu.


Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kufanya maandamano yaliyozuiliwa na polisi, kukusanyika isivyo halali , uchochezi na kusababisha uvunjifu wa amani.


Hayo yalisemwa jana na Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo ambaye alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 10 wa upande wa mashtaka na vielelezo , mahakama imeona kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu na kwamba wanapaswa kutoa utetezi wao.


Mapema wakili wa washtakiwa hao, Mohammed Tibanyendera aliiomba mahakama iwaachie huru washtakiwa kwa madai kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, umeshindwa kuthibitisha makosa dhidi ya washtakiwa.


Wakili Tibanyendera alidai kuwa, mashahidi wa upande wa mashtaka wote walikiri kuwa hakuna hata mmoja aliyewahi kuona tangazo la kuzuia maandamano.
Pia alidai kuwa hakuna ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ukionyesha kuwa kulikuwa na maandamano na kwamba mashahidi wote waliithibitishia mahakama kuwa walishiriki katika kukamata washtakiwa kwa njia ya simu ya upepo ya polisi.


Wakili huyo pia alidai kuwa mikusanyiko haikuwa ya kuvunja amani na kwamba wala hakuna shahidi hata mmoja aliyeieleza mahakama kuwa alishuhudia uvunjifu wa amani ama malalamiko kutoka kwa majirani kuhusu hofu.


“Hii inadhihirisha kuwa mkusanyiko waliokuwa nao washtakiwa ulikuwa halali na hakukuwa na amri yoyote ile ya kuzuia watu kukusanyika katika Jamhuri ya Tanzania hapo Februari 15, mwaka huu,” alidai wakili huyo.


Pia wakili huyo wa kujitegemea alidai kuwa hakukuwahi kutolewa wakati wowote ule, amri ya kuzuia mkusanyiko na kwamba walizuia maandamano.
Wakili Tibanyendera alidai kuwa ukamataji wa wateja wake, ulifanyika baada ya Swala ya Ijumaa, na kwamba watu walikamatwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Mkunguni na Makunganya.
Alifafanua kuwa waliokamatwa katika maeneo ya Mkunganya walikamatwa umbali wa mita 100 kutoka msikitini, DIT walikuwa karibu na kituo cha daladala na waliokamatwa katika eneo la Mkunguni walikuwa karibu na misikiti takriban mita tatu.


“ Huu ni uwiano mkubwa wa kimazingira, tulitarajia tutapata ushahidi tofauti baina ya watu waliotenda kosa na waliokusanyika katika nyumba za ibada,” alidai wakili huyo wa utetezi.
Baada ya kumaliza kutoa hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Benard Kongola aliiomba mahakama iwaone washtakiwa kuwa wana kesi ya kujibu.


Hakimu Fimbo aliiahirisha kesi hiyo hadi leo washtakiwa watakapoanza kujitetea.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya upande wa mashtaka kupitia mawakili wa Serikali waandamizi, Benard Kongola, Nassor Katuga na Joseph Mahugo kufunga ushahidi wao.
Upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake baada ya kupeleka mashahidi 10 mahakamani kutoa ushahidi dhidi ya washtaka wakiambatanisha pia vielelezo 12.


Alidai kuwa Februari 11, mwaka huu alipokea barua kutoka katika Shura ya Maimamu, ikimwomba kibali cha kufanya maandamano ya kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).


Alidai kuwa barua hiyo ilisainiwa na Sheikh Juma Idd na kwamba ndani yake pia ilikuwa inahoji sababu za kutokumpatia dhamana Sheikh Ponda .

 Pia walikuwa wakitaka maandamano hayo, yafanyike Februari 15, mwaka huu baada ya Swala ya Ijumaa na waandamanaji watakuwa wakitokea katika misikiti mbalimbali.
ACP Msangi alidai kuwa yeye na maofisa wenzake, walitafakari barua hiyo ili kujua uzito wa maandamano hayo.


Alidai kuwa Jeshi la Polisi lilibaini kuwa halikuwa na askari wa kutosha kuwapeleka katika kila msikiti kwa ajili ya kuwalinda waandamanaji.

Mali za mfanyabiashara aliyekamatwa kwa tuhuma za ujambazi zakamatwa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman

Sakata la Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kunasa watuhumiwa wa mtandao wa majambazi jana lilisababisha kundi la wakazi wa Jiji la Mbeya kujikusanya eneo Mwanjelwa katika maeneo ya maduka ya nguo, ili kumwona mfanyabiashara maarufu wa eneo hilo, Ghati Mbilinyi (32), aliyekamatwa na Polisi akihusishwa na mtandao huo.

Umati huo ulijitokeza baada ya Polisi kuongozana na mfanyabiashara huyo kwenda dukani kwake kwa ajili ya kufanya upekuzi na kuchukua baadhi ya mali zinazodaiwa kuwa ni za wizi kama kielelezo wakati atakapofikishwa mahakamani.

Mbilinyi akiwa chini ya ulinzi mkali, aliamuliwa kukusanya bidhaa karibu zote zilizokuwa ndani ya duka lake na kuzipakia katika gari la Polisi kisha kuondoka nazo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alisema kuwa walilazimika kwenda dukani kwa mtuhumiwa huyo na kuchukua mali zake kutokana na maelezo yake baada ya kukiri kuwa anajihusisha na matukio ya kupora mali na kufanya mauaji.

“Ni kweli kwamba tumelazimika kwenda na mtuhumiwa mwenyewe hadi dukani kwake na kuchukua mali alizokuwa nazo, tumefanya hivyo kutokana na mazingira yanayoonekana kuwa alikuwa anajihusisha na matukio ya ujambazi ya uporaji, utekaji, na mauaji,” alisema Kamanda Diwani.

Hata hivyo alisema kuwa Jeshi la Polisi halisemi moja kwa moja kuwa mali zote alizokuwa nazo ndani ya duka zilitokana na uporaji, lakini mtuhumiwa mwenyewe alitaja baadhi ya mali alizozipata kwa kufanya uhalifu.

Akizungumzia hatma ya watuhumiwa 13 wanaoshikiliwa na Polisi kwa kujihusisha na mtandao huo, Diwani alisema tayari watuhumiwa saba wamesafirishwa kwenda mkoani Iringa ambako ndiko watashtakiwa kwa tuhuma za kuteka na hatimaye kuwaua wamiliki wa gari lililokuwa likisafirisha mali za wafanyabiashara wa Mbeya.

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kukamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wengine sita waliobakia mkoani hapa.

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya juzi lilitangaza kunasa mtandao watuhumiwa wa ujambazi uliokuwa ukifanya uhalifu katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, ambao uliwahusisha askari mmoja wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mmoja wa Kikosi Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Mbeya.

Wanawake wanaotumia njia za kisasa uzazi wa mpango waongezeka

PSI Tanzania

Idadi wanawake wanaotumia njia za kisasa za muda mrefu za uzazi wa mpango, zinazotolewa na Shirika la PSI imeongezeka mara mbili kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Akizungumza na  Wahariri na Waandishi waandamizi kutoka vyombo vya habari nchini, Mkurugenzi wa Programu ya Afya ya Uzazi ya PSI Tanzania,  Dk. Nguke Mwakatundu, alisema ongezeko hilo ni zaidi ya asilimia 100 katika kipindi cha mwaka mmoja.


Alisema kipindi cha mwaka jana, jumla  ya wanawake waliopatiwa huduma hiyo ilikuwa 102,778 wakati mwaka 2011 waliopatiwa huduma ya uzazi wa mpango walikuwa 48,518.

Dk. Mwakatundu alisema kwa upande wa programu yao ni mafanikio ya kujivunia ingawa wangependa kuona idadi hiyo inaongezeka zaidi mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Romanus Mtung’e, alisema wamejipanga kuhakikisha wanawake nchini wanapatiwa huduma bora na za kisasa za uzazi wa mpango.


Alisema ni kipindi mwafaka kwa wananchi kutambua umuhimu wa kupanga familia zao ili watoto wanaozaliwa wapate malezi mazuri na huduma bora toka kwa wazazi, jamii na serikali.

Mramba: Mkapa aliniruhusu kusamehe kodi

Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam imeambiwa na Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba (74), kwamba alitoa msamaha wa kodi kwa kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation kabla ya kuliwasilisha suala hilo katika Baraza la Mawaziri.

Kadhalika, Mramba alidai katika kesi hiyo inayomkabili kama mshitakiwa wa kwanza wa kuisababishia hasara serikali ya Sh. bilioni 11.7 kuwa alipokea maagizo kutoka kwa Rais (wakati huo Benjamin Mkapa) kwa njia ya mdomo ya kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo. 

Mramba alitoa madai hayo jana wakati akihojiwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Osward Tibabyekomya, mbele ya jopo la 

mahakimu watatu linalowajumuisha Mwenyekiti John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela wanaosikiliza kesi hiyo.

Mshtakiwa huyo na wenzake wawili wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka, kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Tibabyekomya na Mramba:

Wakili: Juni 12, mwaka 2003 ulipoagiza Gavana aainishe mkataba, uchunguzi wa kujua nchi jirani zinafanyaje kazi na kampuni za ukaguzi za madini ulikuwa umefanyika?

Mramba: Ndiyo.

Wakili: Uchunguzi ulifanyika lini na nchi gani waliangalia?

Mramba: Sikumbuki.

Wakili huyo aliomba mahakama kumruhusu mshtakiwa kusoma barua ambayo ni kilelezo katika kesi hiyo iliyoonyesha kwamba kulikuwa na majadiliano kati ya Wizara ya Fedha, Mwanasheria Mkuu (AG), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Wizara ya Nishati na Madini.

Wakili: Je, mlijadiliana nao kama barua ilivyosema?

Mramba: Sijawahi kufanya majadiliano yoyote.

Wakili: Kwa mujibu wa maandishi ya barua hiyo inaonyesha kuwapo kwa majadiliano kweli au siyo kweli?

Mramba: Ndiyo, kwa mujibu wa maandishi kunaonyesha kuwapo kwa majadiliano kati ya Wizara ya Fedha, Nishati na Madini, BoT na AG.

Wakili: Rais alitoa maelekezo ya kushughulikia kampuni hiyo?  

Mramba: Ndiyo.

Wakili: Wakati unatoa maelekezo kwa Gavana, ulijua uwapo wa barua ya Mei 13, mwaka 2003 kutoka kwa Katibu wa Rais na Waziri wa Nishati na Madini?

Mramba: Hapana.

Mramba alionyeshwa barua ya Mei 21, mwaka 2003 kutoka kwa Gavana (wakati huo marehemu Daudi Balali) kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha.

Wakili: Kwa mujibu wa barua hiyo, Wizara ya Fedha ilikuwa inaombwa kumteua mjumbe atakayeshiriki kwenye majadiliano ya mkataba wa uteuzi wa mkaguzi wa madini. Je, ni kweli?

Mramba: Ndiyo kama barua inavyosema.

Wakili: Taratibu za kutafuta malipo zilianza hata kabla ya majadiliano ya mkataba huo?

Mramba: Ndiyo taratibu zilishaanza.

Wakili: Je, ulipeleka lini nakala ya mkataba kwenye Baraza la Mawaziri?

Mramba: Februari mwaka 2004.

Wakili: Je, shahidi utakubaliana na upande wa Jamhuri katika kesi hii wakati unatoa msamaha wa kodi ulikuwa haujaliarifu baraza?

Mramba: Ndiyo

Wakili: Rais (Mkapa) alitoa kwa njia gani suala la kuilipa fedha kampuni hiyo ya ukaguzi?

Mramba: Kwa njia ya mdomo.

Kesi hiyo itaendelea kusikiliza mahojiano kati ya upande wa Jamhuri na Mramba Aprili 9 hadi 12, mwaka huu.  Katika kesi ya msingi, washitakiwa wanadaiwa kuwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kama mawaziri na katibu mkuu walitumia vibaya madaraka.

Ilidaiwa kuwa kwa kupitia kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa ukaguzi wa madini kwa kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart 

( ASSAYERS) Government Business Corporation waliingia mkataba kukagua kiwango cha uzalishaji wa madini ya dhahabu kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Washitakiwa wengine ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Hazina, Gray Mgonja.

Moto wawaachia wanafunzi 70 umasikini

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas

Zaidi ya wanafunzi 72 wa Shule ya Sekondari ya Edmund Rice, inayomilikiwa na Kanisa Katoliki la Jimbo Kuu la Arusha, wamenusurika kuteketea kwa moto huku wengine 70 vifaa vyao vyote vikiteketea baada ya mabweli yao kuungua juzi usiku.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo iliyopo maeneo ya Engusheratoni, Kata ya Sokoni 1, Francis Nkwabi, mabweni yaliyoshika moto ni ya wanafunzi wa kidato cha tano.

Alisema chanzo cha moto huo ulioanza saa 1:15 usiku na kufanikiwa kuzimwa saa 4, bado hakijafahamika.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema kuwa polisi  kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kikosi cha Zimamoto, wameanza uchunguzi ili kubaini chanzo.

Aidha, Nkwabi alisema wanafunzi 20 walipatwa na mshtuko na kuzimia na walikimbizwa hadi hospitali ya Mtakatifu Elizabeth, maarufu kama kwa Father Babu kwa matibabu na wengine waliwekewa hewa ya oksijeni.

Wanafunzi watatu kati yao bado wanaendelea kupatiwa matibabu.

Walisema mali na vifaa vyote vya watoto hao vimetetekea kwa moto na watoto 70 hawana kitu kabisa.

Alisema baada ya kuzuka kwa moto huo waliwasiliana na Kikosi cha Zimamoto ambao walifika eneo la tukio baada ya dakika 10, na kwa pamoja na wananchi wa jirani walisaidiana kuuzima moto huo.

Nkwabi alisema jana alipokea mamia ya wazazi waliofika shuleni hapo baada ya  kusikia kuwapo kwa moto huo na taarifa kwamba wanafunzi 20 walikuwa wamekufa wakati haikuwa kweli.

Mizengo Pinda aponda wanaoibeza tume yake kuchunguza matokeo

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda 

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewaponda watu wanaoipinga tume aliyoiunda kuchunguza sababu za idadi kubwa ya wanafunzi wa kidato cha nne kuvurunda katika mtihani huo akieleza kuwa huenda watu hao hawaelewi ukubwa wa tatizo na jinsi linavyotakiwa lishughulikiwe. Katika matokeo hayo ambayo yanatajwa kuwa mabovu kuliko yoyote yaliyowahi kutokea katika historia ya Tanzania, asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walipata sifuri.

Pinda alisema hayo jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa siku moja kuhusu mafanikio ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi.


Alisema ni lazima waelewe kuwa mambo yatakayoangaliwa ndani ya uchunguzi huo ni mengi na si kama wanavyofikiri baadhi ya wanaopinga hivyo ni muhimu wakatulia na kusubiri matokeo.


“Wengine wanasema tume zipo nyingi, si kweli kwamba zipo nyingi na hazifanyi kazi, kila mtu ana mawazo yake, jambo hili ni kubwa na lazima lishughulikiwe kwa ukubwa wake,”alisema Pinda.


Pinda alisema hivi sasa wako katika hatua za mwisho za kukamilisha tume hiyo na itaanza kazi kati ya leo au kesho.


“Tuko katika hatua za mwisho kwa kuwa tulihitaji kuhusisha wadau wote ikiwa ni pamoja na Zanzibar, dini mbalimbali, sekta binafsi pamoja na wabunge kadhaa ili tuunganishe nguvu na leo au kesho itaanza kazi rasmi,”alisema Pinda.


Wiki iliyopita Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo alisema kuwa tume hiyo inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote wiki hii, ambapo itajumuisha Chama cha Wamiliki wa Shule ya Sekondari na Vyuo Binafsi.


Lyimo aliwataja wadau wengine watakaohusika katika uchunguzi huo kuwa ni kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa)

“Tume hiyo itahusisha asasi zisizo za kiserikali (NGOs), zinazojishughulisha na masuala ya elimu. Wazazi, walezi na wananchi wote kwa jumla watoe ushirikiano kwa tume, ili ifanye kazi kwa ufanisi,” alisema Lyimo.

‘Wanafunzi 62 waliofaulu la saba hawajaripoti shuleni’


WANAFUNZI 62 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana na kutakiwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa wilayani Simanjiro, Manyara hawajaripoti shuleni.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Maendeleo cha Kata ya Endiamtu, katika Mji Mdogo wa Mirerani, Mkuu wa shule hiyo,Emmanuel Kallo alisema wanafunzi hao ni kati ya 157 waliochaguliwa kujiunga na shule yake.

Kallo alisema baadhi ya wanafunzi hao wamehamishiwa katika shule binafsi za sekondari.

Alisema wanafunzi wengine 12 wamehamishiwa katika shule nyingine za sekondari za Serikali .

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule, wengine hawajaripoti katika shule yoyote na kwamba wanahesabika kuwa ni watoro.

Kwa upande wake,Diwani wa Kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia, alisema jitihada lazima zifanyike ili kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanaripoti shule na kuungana na wenzao katika masomo.

“Hii tabia ya utoro siyo ya kuiachia, maana hata mwaka jana kwenye wilaya yetu kuna baadhi ya wanafunzi hawakupelekwa shule na zaidi ya wazazi sita walipelekwa mahakamani,” alisema Zacharia.

Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Edmund Tibiita ,alimweleza Kallo kuwa afikishe ofisini kwake majina ya wanafunzi wote ambao walifaulu kwenda kwenye shule yake na hadi sasa hawajaripoti.

“Naomba unipatie majina ya watoto wote ambao hawajafika shuleni ili nipambane na wazazi na walezi wao,kwa sababu katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia bila elimu watoto watapata athari kubwa,” alisema Tibiita.

Albino auawa, wawili wakatwa viungo


Vicky Ntetema

HALI ya wasiwasi imetanda miongoni mwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini, baada ya watu watatu kukatwa viungo na mmoja wao kuuawa mwezi huu.


Katika miaka ya hivi karibuni, jumla ya albino 72 wameuawa, 34 wamenusurika, wengi wao kwa kukatwa viungo au kuumizwa. Makaburi 15 yamefukuliwa na viungo kuchukuliwa na kumekuwa na majaribio manne ya kufukua makaburi.

Katika matukio ya hivi karibuni, walemavu hao wakazi wa Tabora na Sumbawanga wamekatwa mikono ya kushoto. Ukatili huo safari hii umekwenda kinyume na ilivyokuwa mwaka 2010-2011 wakati mikono ya kuume ndiyo iliyokuwa inakisiwa.
Aliyeuawa ni
Lugolola Bunzari (7) na waliojeruhiwa ni Mwigulu Matonange (10) na Maria Chambanenge (39).


Katika matukio hayo, mtoto mwenye umri wa miezi saba alinusurika kuuawa baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumba ya mama yake usiku katika eneo la Lamadi, Wilaya ya Busega, Mwanza siku moja baada ya kupokea ujumbe mfupi wa simu kwamba mtoto wake anawindwa.


Marehemu Lugolola
Kijiji cha Kanoge kina umbali wa takriban kilomita 75 kutoka Tabora Mjini, barabara iendayo Ulyankulu kwenye machimbo ya dhahabu.
Imenichukua saa mbili na nusu kufika huko. Saa moja na nusu kati ya hizo, nilizitumia katika safari ya kilomita 15 tu kutoka Kanoge makao makuu ya kijiji hadi Kitongoji cha Kinondoni alikouawa mtoto Lugolola.


Nyumbani kwa Bunzari niliwakuta ndugu na jamaa kutoka vijiji vya jirani vya Wilaya hiyo ya Kaliua, Tabora. Bibi mzaa baba wa Lugolola, Gama Zengabuyanda (60), ndiyo kwanza alikuwa amerejea kutoka Hospitali ya Mkoa ya Kitete alikokuwa akitibiwa baada ya kushambuliwa na majambazi alipotaka kumwokoa mjukuu wake.


Huku akilia kwa huzuni, Zengabuyanda alinisimulia jinsi mjukuu wake na baba yake mzazi, Zengabuyanda Meli (95) walivyouawa kikatili.


Katika muda wa kati ya saa 10 na 11 alfajiri ya kuamkia Februari Mosi mwaka huu, Lugolola aliuawa kikatili baada ya kukatwa mkono kwa panga, kukwanguliwa nywele, kujeruhiwa mkono wa kulia na sikioni na kuondolewa ngozi kwenye sehemu ya paji la uso.


Katika mashambulizi hayo, babu yake Meli pia aliuawa alipojaribu kumwokoa mjukuu wake. Vilevile baba yake mzazi, Bunzari Shinga alijeruhiwa wakati alipojaribu kumlinda mwanaye.
Nilimkuta mama mzazi wa Lugolola aitwaye Kulwa akisaidiana na ndugu zake kumenya maharage mabichi waliyoyatoa shambani mwao muda mfupi tu uliopita.


Yeye ni mke mkubwa wa Bunzari Shinga (35). Walibahatika kupata watoto sita, wawili kati yao ni albino. Lugolola na marehemu mdogo wake aitwaye Maganga aliyefariki kwa malaria mwaka 2011.


Usiku wa mashambulizi hayo, Kulwa anasema alikuwa amelala na watoto wake wadogo wa kike (mmoja, Shija mkubwa) na Lugolola kwenye nyumba yake inayotazamana na ile ya mke mwenzake Pili, umbali wa takriban mita 20. Bunzari alikuwa amelala kwa mke huyo mdogo na binti yao mwenye umri wa mwaka mmoja hivi.


Mzee Meli alikuwa amelala na watoto wa kiume upande wa kulia wa nyumba ya Kulwa.
“Aliamshwa usingizini na kelele za watoto waliokuwa wakilalamika kwamba wanapigwa na fimbo. Alipotaka kwenda chumbani kwa watoto alishambuliwa kwa mapanga kichwani, usoni, mgongoni, mikononi na miguuni,” Gama anaelezea huku akilia.“Pamoja na hayo yote, Baba alijikongoja kuelekea kwenye nyumba alimolala mjukuu wangu, Lugolola huku akipiga mayowe, Tumevamiwa! Nani anataka kuwadhuru watoto wangu.”
Majangili hayo yakamshambulia zaidi kwa mapanga na marungu na huo ndiyo ulikuwa mwisho wake. Jamani Baba yangu!”
Gama anasema alikuwa amelala kwenye banda lake lililopo kati ya nyumba ya pili na ile ya babu.


Banda hilo la nyasi na kuta za udongo na miti lilikuwa limepambwa kwa vibuyu vya aina mbalimbali, tunguri, vyungu vilivyohifadhi mizizi, magamba ya miti, kauri (nyumba za konokono), hirizi, nywele za binadamu, taya za wanyama, vipande vya mifupa mbalimbali, fuvu la mnyama na gamba la kobe. Katika mazungumzo yetu niligundua kwamba Mzee Meli alikuwa mganga wa kienyeji.


Gama aliposikia vilio vya watoto alitoka nyumbani mwake na kukimbilia kwenye nyumba ya babu ili kujua kilichowatokea wajukuu wake na sababu iliyomfanya baba yake apige mayowe.


Akiwa nje alimwona baba yake akishambuliwa na watu watatu. Watu wengine wanne walikuwa wamesimama nje ya nyumba ya Kulwa wakiwa wameshika silaha mbalimbali ikiwa ni pamoja na magobole, mapanga na marungu. Gama alipiga kelele, ‘Tumevamiwa!’ na mmoja kati ya watu hao alimshambulia kwa panga kichwani, miguuni na mikononi.

Alianguka na akapata mwanya wa kutambaa chini kwa chini kama nyoka hadi akafika kwenye shamba la mahindi na kupotelea kwenye vichaka.
Hata hivyo, alizimia na alipozinduka alijikuta akiwa Wodi ya Wanawake ya Hospitali ya Kitete.

Gama alikuwa amefiwa na mjukuu wake na baba yake mzazi. Kinachomsikitisha zaidi ni kwamba waliuawa bila ya hatia na hakupata hata fursa ya kuwaaga na kuwazika.

Itaendelea kesho...

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI FEB.27



0
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.