Malleko: Tanzania inaweza kupata Rais Mwanamke 2015

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Wilaya ya Arumeru, Ester Malleko. 

 TANZANIA inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa Rais wa awamu ya tano mwaka 2015. Uchaguzi huo pia utahusisha nafasi za ubunge na udiwani ukitanguliwa na ule wa serikali za mitaa mwakani.

Mengi yanazungumzwa kuhusu chaguzi hizo, ikiwemo uwezekano kuwa na Rais, Makamu wake au Waziri Mkuu mwanamke kutokana na uwezo wa kiuongozi unaoonyeshwa na wanawake waliopata fursa za uongozi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), wilaya ya Arumeru, Ester Malleko anazungumzia nafasi na uwezekano huo  kama alivyozungumza na Mwandishi Wetu, Peter Saramba.

Swali: Nini kilikusukuma kuingia kwenye siasa na nini malengo yako ya baadaye?
Jibu: Nimeingia kwenye siasa kuwatumikia wananchi na kuthibitisha kuwa wanawake tunaweza. Nimekuwa mwenyekiti wa UVCCM wilaya na sasa ninaongoza wanawake.
Nafasi ya mwanamke kwenye jamii siyo kuzaa na kutunza familia pekee. Tunapaswa na hakika tuna haki ya kushiriki katika ujenzi wa taifa sawasawa na wanaume kwa kila mmoja kutekeleza na kutimiza wajibu wake pale alipo.

Swali: Wewe ni mwanachama na kiongozi wa CCM. Kuna madai kwamba chama chako kimepoteza haiba mbele ya umma kutokana na ninyi viongozi kuacha misingi iliyoasisi chama hicho. Nini maoni yako?
Jibu: CCM kama taasisi haina tatizo na haijapoteza haiba. Bado ipo na itaendelea kudumu katika misingi yake ile ile iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa hili ambayo ni amani, upendo, udugu na mshikamano bila kujali tofauti zetu za kikabila, kidini wala maeneo mtu anakotoka.

Chama hiki bado kinaaminiwa na umma. Hilo linathibitishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu ambapo CCM ilipewa ridhaa ya kuunda Serikali baada ya kushinda kiti cha urais na kupata wabunge na madiwani wengi.


Hata hivyo, ni kweli kuna kosoro ndogo ndogo zinajitokeza kutokana na makosa ya watu binafsi ambazo zinashughulikiwa  kupitia vikao, katiba, kanuni na taratibu za chama.

Swali: Mwaka 2015 tunaingia kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani,  kuna maneno kuwa wanawake waliopata fursa wameonyesha uwezo mkubwa kiuongozi. Unadhani muda umefika wa kuwa na Rais, Makamu au Waziri Mkuu mwanamke?

Jibu: Muda umefika, tena unapita. Ninaamini Taifa hili linaweza

kuongozwa na mwanamke kwa sababu viongozi wanawake waliopata fursa za kuongoza wameonyesha kuwa wanaweza.


Wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja na kutoa uamuzi wa haraka wenye faida na maslahi kwa umma.

Wanawake viongozi wamethibitisha kuwa hawapigi dili kama ambavyo mama nyumbani asivyoweza kuisaliti familia.

Swali: Unaweza kutaja kwa uchache majina ya wanawake unaodhani wana uwezo wa kuwa Rais wa taifa hili?

Jibu: Wapo wanawake wengi wanaonivutia katika uongozi wao. Baadhi wapo kwenye nafasi zao uongizi hadi sasa katika medani mbalimbali ikiwemo uongozi wa kisiasa, kijamii na harakati mbalimbali.

Ingawa wako wengi ambao siwezi kuwataja wote, lakini kwa uchache wapo Dk Asha Rose Migiro, Dk Hellen Kijo-Bisimba, Profesa Anna Tibaijuka, Ananilea Nkya, Mama Anna Abdalah, Mama Gertrude Mongella na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda.

Swali: Kuna msemo kwamba mwanamke anaweza akiwezeshwa. tupe maoni yako?


Jibu: Binafsi sikubaliani na msemo huo, kwani unafifisha uwezo wa

kijiamini kwa wanawake ambao hukaa kutegemea kuwezeshwa ndipo wafanye jambo.

Siyo kweli kwamba ili mwanamke afanikiwe au kuweza jambo lazima awezeshwe. Nadhani kauli hii iliyotumika huko nyuma kuwahamasisha na kuwatia moyo wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi sasa imepitwa na wakati.


Mimi naamini uwezo wa mwanamke upo dhahiri ndiyo maana nyuma ya kila mwanaume shupavu na mwenye mafanikio, yupo mwanamke shupavu na jasiri. Na huu unathibitishwa na usemi kuwa “Kila mwanaume aliyefanikiwa,nyuma yake kuna mwanamke”

Kifamilia, mshauri mkuu wa baba ni mama. Sasa tutakubali vipi kwamba ili mwanamke afanikiwe lazima awezeshwe? Awezeshwe na nani? Huyo huyo mwanaume ambaye yeye anamshauri?

Hata hivyo, pamoja na ukweli huo, lazima tukubali kwamba adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe. Wanawake hatujiamini. Lakini hata anapotokea mwenzetu kujiamini na kujitokeza, hatumuungi mkono, pengine kwa ile

ile dhana kuwa hatuwezi au wivu tu wa kike.

Swali: Jiji la Arusha ni miongoni mwa halmashauri zenye chaguzi ndogo za madiwani kujaza nafasi zilizo wazi. Unatarajia chama chako kitamudu kurejesha kata hizo nne zilizonyakuliwa na upinzani uchaguzi uliopita?

Jibu: Yeyote anayeingia kwenye mashindano, lengo lake ni kushinda. CCM tuna matumaini makubwa ya kushinda baada ya kugundua na kurekebisha makosa madogo madogo yaliyosababisha tupoteze kata hizo.

Tumesimamisha wagombea wanaokubalika na tumejiandaa kuwanadi kukamilifu kupitia sera za chama. Hatutatukana wala kuzungumzia watu binafsi kama wenzetu wanavyofanya. Tutanadi sera ili kutoa fursa kwa wananchi kuzilinganisha na za wenzetu.

Napenda kuchukua fursa hii kuwaasa watu wa  Arusha tusikubali

kutenganishwa wala kufarakanishwa kutokana na chaguzi hizi. Ni kweli kila mtu ana haki ya kufuata na kuamini itikadi aipendayo kisiasa, tufanye hivyo bila kubezana, kufarakana wala kusababisha ufa kwenye uhusiano wetu.

Baada ya uchaguzi huu na zingine zijazo, Arusha inapaswa kuendelea kuwa sehemu salama kwa maisha na mali zetu. Wananchi tunataka ufumbuzi wa matatizo yanayotukabili kwa pamoja bila kujali tofauti zetu kisiasa, kidini wala kibabila.

'Mafisadi wanamtisha Mkurugenzi Mkuu wa NHC'

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu

Serikali imeombwa kumwekea ulinzi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu, kutokana na vitisho ambavyo ameanza kupata kutoka kwa mtandao wa mafisadi waliojimilikisha nyumba za shirika hilo baada ya mirija yao ya wizi kukatwa na mkurugenzi huyo.

Ombi hilo lilitolewa jana bungeni mjini Dodoma na Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Magdalena Sakaya, wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Sakaya alisema Mchechu  amekuwa akifanya kazi nzuri tangu aingie NHC, lakini mafisadi wachache ambao walikuwa na mirija ya kufanya ufisadi ndani ya shirika hilo wamekuwa wakimwandama na wakati mwingine wakimtumia ujumbe wakumtisha ili kumkatisha tamaa asiendelee na jitihada zake za kupambana na ufisadi uliokuwapo.

“Mheshimiwa Spika, wale mafisadi baada ya kuona mirija yao imekatwa wanamtumia ujumbe wa vitisho wakimwambia kuwa kijana  umekuja na utaondoka... naomba serikali imlinde, Mkurugenzi huyu ni  kijana mdogo, lakini mzalendo wa kweli na amefanyakazi kubwa sana,” alisema Sakaya.

Akizungumza na NIPASHE nje ya ukumbi wa Bunge, Sakaya alisema kuna watu ambao walikuwa wamehodhi nyumba nyingi za NHC na kuzikodisha kwa watu kwa bei kubwa huku wakilipa fedha ndogo kwa shirika hilo.

Sakaya alisema kuna watu ambao walikuwa wanaingiza hadi Sh. 7, 000, 000 kwa mwezi kwa kupangisha nyumba za NHC, hivyo ujio wa Mchechu umekuwa balaa kwao kwani mirija mingi imefungwa.

Alisema kuna watu walikuwa wanamiliki hadi nyumba nne za NHC na kuzikodisha kwa bei kubwa kwa watu mbalimbali, hivyo baada ya kuona mirija hiyo imekatwa wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ikiwamo kumtisha Mchechu.

“Mimi nimekuwa mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa zaidi ya miaka saba, ningekuwa na tamaa ya mali ningekuwa na hata ghorofa namiliki sasa, lakini siko hivyo, mimi nataka NHC iwe mali ya Watanzania na iwanaufaishe Watanzania, hakuna ndugu yangu hata mmoja anayeishi NHC ingawa ningetaka wangepata,” alisema Sakaya na kuongeza:

“Nimefuatwa mara nyingi na wafanyabiashara wakiniuliza ninataka Shilingi ngapi ili niwatetee bungeni wauziwe nyumba, lakini nimekataa kwa sababu mimi ni mzalendo na sitaki ufisadi kabisa, ningetaka utajiri ningeshaupata kupitia NHC.”

Mbunge huyo alisema baadhi ya wafanyabiashara hao wamekuwa wakiwatumia hadi baadhi ya wabunge kuwatetea bungeni wengine wakitaka Mchechu aondolewe kwenye nafasi hiyo ili waendelee kula.

Alisema kabla ya Mchechu kuingia NHC, kulikuwa na mtandao mkubwa wa wafanyabiashara wanaohodhi nyumba hizo za shirika hilo na ndio wanaohangaika hadi kuwatumia baadhi ya wabunge wakitaka serikali iwauzie zile nyumba na isiwaongezee kodi wapangaji na wengine wakiishauri serikali imwondoe Mchechu.

“Usione kila anayefoka kuhusu NHC ukadhani ana uchungu na Watanzania wanyonge, wengine wametumwa na wafanyabiashara hao hao ambao wana mtandao unaomiliki nyumba za NHC, hakuna mlalahoi wanayemtetea, wanataka wauziwe zile nyumba ili wazilangue kwa bei kubwa,” alisema Sakaya na kuongeza:

“Alichofanya Mchechu kimewaathiri mafisadi wengi sana waliokuwa wanalinyonya shirika, unakuta mfanyabiashara amempangisha mtu nyumba moja ya  NHC na analipwa Shilingi 1,000,000 kwa mwezi wakati NHC anakwenda kulipa 400,000, sasa kilichofanyika NHC imewafuata wale waliopangishwa na wafanyabiashara na kuwapa mikataba yenyewe ili wailipe NHC badala ya wale walanguzi hapo ndipo wanahangaika.”

Sakaya aliishauri pia serikali iondole Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwa vifaa vya ujenzi  kwa NHC ili wajenge nyumba bora na za bei nafuu ambazo Watanzania wa hali ya chini watamudu kuzinunua.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Kiwelu, alisema ni aibu kwa serikali kushindwa kulipa madeni inayodaiwa na NHC wakati kila mwaka bajeti imekuwa ikitengwa kwa ajili ya kulipia pango.

Alisema kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ambayo yeye ni mjumbe inamuunga mkono Mkurugenzi wa NHC, lakini amekuwa akikwamishwa na serikali ambayo inashindwa kulipa madeni ya muda mrefu, hivyo kushindwa kujenga nyumba mpya.

“Bajeti tunapitisha kila mwaka hapa, lakini hamlipi pango la NHC, Waziri tunaomba utueleze hizo fedha huwa mnazipeleka wapi?” alihojiu na kuongeza:  “Tunaomba katika bajeti hii Wizara inayodaiwa deni lake lipelekwe Hazina ikatwe huko huko wapewe NHC.”

Alishauri NHC ikipata fedha za kutosha ijenga nyumba za matabaka ya wenye nazo na nyumba ambazo watu wa tabaka la chini kabisa watamudu kuzinunua kwa kuwa za sasa hakuna mlalahoi atakayezimudu.

Kiwelu alisema inasikitisha kuona kuwa Tume nyingi zimeundwa kuchunguza mambo zikitumia fedha zinazotokana na kodi wanazolipa walalahoi, lakini ripoti hizo huwa haziwekwi hadharani.

Alitoa mfano wa Tume ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuchunguza majengo 100 jijini Dar es Salaam, lakini kwa mshangao mkubwa kamati yake imeitafuta kwa muda mrefu na haijulikani iliko.

“Tumeitafuta ripoti ya Tume ya Lowassa, lakini tumeikosa na hadi sasa ripoti hiyo haijulikani iliko, sasa naomba Waziri atueleze iliko ili isomwe na ifanyiwe kazi kwa kuwa kuna majengo zaidi ya 100 ambayo ilisemekana ni mabovu na yanapaswa kubomolewa,” alisema.

Herbert Mtango (Lushoto-CCM), alisema kuna wawekezaji ambao wamejilimbikizia mashamba makubwa miaka 40 iliyopita bila kuyaendeleza, lakini bado wanamiliki hatimiliki za mashamba hayo.

Alisema licha ya mashamba hayo kugeuka mapori kwa miaka yote hiyo huku wawekezaji hao wakiwa nje ya nchi, serikali imeshindwa kuzifuta hati hizo na kusababisha wananchi wengi wa Muheza kukosa sehemu za kuendesha shughuli za kilimo.

“Mheshimiwa Spika, hii ni aibu kubwa sana, mwekezaji anapewa hati ya kumiliki shamba kwa miaka 99 na sasa kwa zaidi yamiaka  40 iliyopita ameshindwa kuendeleza shamba, lakini anaendelea kumiliki ardhi wakati wazawa hawana ardhi,” alisema.

 
CHANZO: NIPASHE

Serikali inavyoulea mgogoro wa gesi Mtwara

Tangu mgogoro wa kupinga gesi itakayozalishwa mkoani Mtwara uliponza kufukuta Desemba 2012, Serikali imeshindwa kutatua kiini chake, badala yake nguvu kubwa za kijeshi zimetumika kiasi cha kusababisha mauaji, majeruhi na chuki kwa wananchi.

Kimsingi mgogoro huu unatokana na maoni ya wananchi kuhusu rasilimali ya gesi inayotarajiwa kuchimbwa mkoani humo wakitaka gesi hiyo isisafirishwe kwa bomba kwenda Dar es Salaam.

Awali Serikali ndiyo iliyounda kamati ya Nishati na Madini ambayo ilipita kwa wanachi nchini kote kutaka maoni yao. Ilipofika Mtwara, wananchi wengi hawakukubaliana na wazo la kusafirishwa kwa gesi.

Desemba mwaka 2012, vyama tisa vilifanya mikutano na hatimaye maandamano ambayo hata hivyo yalisusiwa na Mkuu wa Mkoa huo, Joseph Simbakalia.

Mbali na maandamano hayo, mapema mwaka huu, kulijitokeza vurugu wilayani Masasi ambazo zilihusishwa na madai ya gesi japo chanzo chake hakikuwa hicho.

Hapo ndipo viongozi wa Serikali wakaanza kutembelea Mtwara ili kutuliza hali ya mambo. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifika Mtwara mapema mwaka huu na kuzungumza na makundi ya wananchi, yaani, vyama vya siasa, Maaskofu na Masheikh, wazee na vijana.

Baada ya hapo yakafanyika majumuisho yaliyohusisha makundi hayo ambayo hata hivyo hayakuwaridhisha wananchi.

Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anna Makinda alizuia mjadala wa suala hilo Bungeni,  akidai kuwa kuna kamati imeundwa kuchunguza.

Licha ya Waziri Mkuu Pinda kushindwa kuafikiana na Wanamtwara katika ziara yake, akarudi Bungeni na kutoa taarifa kuwa mambo yamekwisha, hivyo na ile kamati ya Bunge iliyotumwa kuchunguzwa ikayeyuka.

Kama wanavyosema Waswahili, ‘La kuvunda halina ubani’, ule uvundo aliouacha Pinda Mtwara, sasa umezua vurugu upya Mei 22 ambapo watu wamekufa, kujeruhiwa na wengine kubakwa.

Pinda amerudi tena Mtwara kufanya mazingaombwe yake. Bunge nalo baada ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, imeunda tena kamati ya Wabunge iende kufuatilia suala hilo.

Tujiulize, kwa nini ile kamati ya kwanza ya Bunge iliyosababisha suala hilo lisijadiliwe ilivunjwa kabla haijaanza kazi?

Hii yote ni kuonyesha kuwa Serikali ndiyo inayoulea mgogoro huu, kwa sababu haitaki kuwasikiliza wananchi ili kufikia mwafaka. Huo ndiyo mzizi wa tatizo.

Suluhisho siyo kuleta majeshi ya kutuliza ghasia, ni kuwasikiliza wananchi, kwani wao ndiyo msingi wa mamlaka ya Serikali  kwa mujibu wa Katiba ibara ya nane.

Prof Tibaijuka akiri kuvutana na NHC

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa  Anna Tibaijuka akijibu hoja za wabunge waliochangia Makadirio na Mapato ya wizara yake kwa  mwaka wa fedha 2013/14, bungeni, Dodoma jana.

Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema kuwa kitendo cha kuvutana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhusu kesi ya ardhi iliyomhusu raia wa Tanzania mwenye asili ya Kichina, Jingling Li  ilikuwa ni kuzingatia sheria na siyo kwamba alikuwa na urafiki naye.

Alisema  hayo akinukuu taarifa iliyoandikwa na gazeti hili toleo la wiki iliyopita, wakati  akijibu hoja za wabunge wake kuhusu bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2013/14.

Alinukuu taarifa ya gezeti hili akisema kuwa NHC walishindwa kwenye kesi hiyo hatua ya rufani kama alivyokuwa ametabiri hapo awali akionyesha umuhimu wa kufahamu sheria za ardhi na makazi.

“Gazeti la Mwananchi waliandika ninavutana na Shirika la Nyumba ikaonekana kana kwamba namtetea Mchina labda kutokana na kwamba kuna masilahi ninayopata,” alisema Profesa Tibaijuka na kuendelea:

“Huyu raia wa Tanzania mwenye asili ya China, alikuwa ni mkalimani wa Baba wa Taifa (Hayati) Mwalimu (Julius) Nyerere. Alishinda kwenye kesi hiyo na kurejeshwa kwenye nyumba hiyo,” alisema Profesa Tibaijuka.

Alisema kwa sasa NHC hawana namna nyingine ya kufanya kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa kwenye ngazi ya rufaa. Alizungumza hayo akionyesha umuhimu wa kuwepo na vyombo vya usuluhishi  wa kesi  zinazohusiana na ardhi.

Gazeti hili liliripoti kuwako kwa mvutano wa chini kwa chini baina ya Profesa Tibaijuka na uongozi wa NHC.

Mvutano huo ulitokana na uamuzi wa NHC kuukatia rufaa uamuzi wa Mahakama Kuu (Kitengo cha Ardhi), uliompa haki, Jingling Li katika kesi ya ardhi namba 129 ya 2006 dhidi ya shirika hilo na wadaiwa wengine wawili.

Katika kesi hiyo, Li  alikuwa akilalamikia hatua ya kuondolewa kwenye nyumba Nambari 103 iliyopo katika vitalu namba 3, 5, 7  na 8, Barabara ya Haile Selassie, Oysterbay, Dar es Salaam.

Kesi dhidi ya NHC ilifunguliwa mwaka 2006 wakati shirika hilo likiongozwa na Martin Madekwe na imedumu kwa miaka sita hadi Aprili mwaka jana ilipotolewa hukumu wakati shirika hilo likiwa chini ya Nehemia Mchechu aliyeteuliwa mwaka 2010.

Katika hukumu yake ya Aprili 27, 2012, Jaji Atuganile Ngwala aliamuru NHC pamoja na washtakiwa wa pili na wa tatu katika shauri hilo; Lars Eric Hulstrom na Kampuni ya Udalali ya Manyoni, wamlipe Li karibu Sh478 milioni ikiwa ni fidia ya hasara na usumbufu uliosababishwa na kuhamishwa kwake kinyume cha sheria katika nyumba hiyo.

Mchanganuo huo unahusisha Sh70 milioni na Dola za Marekani 177,450 (Sawa na Sh283, 920,000 - Dola moja ni sawa na Sh1,600),   gharama za kesi pamoja na riba ambazo pia zinapaswa kulipwa.

Pia Mahakama hiyo iliamuru Li arejeshwe katika makazi hayo, amri ambayo inamaanisha kuondolewa katika nyumba hiyo kwa mpangaji aliyeingizwa badala ya Li ambaye ni Hulstrom aliyekuwa mdaiwa wa pili katika kesi hiyo.

Baada ya kupokea nakala ya hukumu ya Jaji Ngwala, NHC waliazimia kukata rufaa kupinga uamuzi huo, lakini habari kutoka ndani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinadai kwamba Waziri Tibaijuka alitoa maelekezo ya mdomo kwamba hakukuwa na haja kwa shirika hilo kukata rufaa. Hata hivyo, NHC walishindwa rufaa hiyo.

Mbunge: Askari wanaoishi uraiani wanajiingiza katika uhalifu


Mbunge wa Viti Maalumu Mariam Msabaha (Chadema) amesema, kitendo ha baadhi ya askari kukaa uraiani kinasababisha askari hao kujiingiza katika masuala ya uhalifu.

Msabaha alitoa kauli hiyo alipouliza swali la nyongeza bungeni, ambapo alihoji kuwa hali hiyo ya askari kuishi uraiani ni kutokana na upungufu wa nyumba za askari unaosababishwa na Serikali kutotoa kipaumbele kwa kada hiyo.

“ Je, Serikali inasema nini katika kuhakikisha nyumba za askari zinajengwa nchi nzima ili watumishi hao wakae kambini na kujiepusha na kujiingiza kwenye masuala ya uhalifu?” alihoji Msabaha.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alisema polisi wawapo chuoni wanafundishwa mambo yote isipokuwa yanayotokea wawapo kazini ni makosa ya kibinadamu ambayo wizara hiyo inayafanyia kazi.

Alisema Serikali kupitia polisi, haioni haja ya kuongeza muda au mitalaa ya mafunzo ya awali kwani muda unatosha.

kuwapatia ujuzi na weledi wa kutosha.

Kuhusu ujenzi wa nyumba za askari nchini, alisema tatizo hilo limekuwa kubwa kutokana na kutochukuliwa hatua mapema lakini hivi sasa linashughulikiwa.

Kiongozi huyo alisema Serikali ina mpango wa kuboresha makazi ya askari kwa kukarabati na kujenga nyumba mpya ili wote waishi kambini, lakini akabainisha kuwa ufinyu wa bajeti unachangia.

 

Bandari D’Salaam yapoteza Sh3 trilioni kwa mwaka


Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikilikosesha taifa Dola 1.8 bilioni za Marekani (Sh2.8 trilioni) kwa mwaka, kutokana na kukosa ubora wa biashara.

Kutokana na hali hiyo, wataalamu wameeleza kuwa bandari hiyo inahitaji kufanyiwa maboresho muhimu ya hali ya juu, ili fedha hizo zisaidie nchi kuacha kutegemea misaada ya maendeleo.

Kwa mujibu wa ripoti iliyopo kwenye kitabu cha Opening the Gates: How the port of Dar es Salaam can transform Tanzania, licha ya Bandari ya Dar es Salaam kuwa sehemu nzuri, imekosa uwezo hivyo usimamiaji sera bora za kuiboresha zinatekelezwa taratibu. Ripoti hiyo inaeleza kuwa, mwaka 2012 pekee bandari hiyo ilikosesha taifa kiasi hicho cha fedha, huku ikizikosesha nchi jirani Sh1.3 trilioni.

“Fedha hizo ni sawa na asilimia saba ya pato la taifa, kitu ambacho kinawaathiri wanunuzi, wafanyabiashara na wakala mbalimbali wa Serikali,” inaeleza.

Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia (WB), Jacques Morisset ameihimiza Tanzania kuifanya bandari hiyo kuwa moja ya vipaumbele vyake vya juu kwa ajili ya kukua kwa uchumi.

“Watumiaji Bandari ya Dar es Salaam wanalipa fedha nyingi kwa wasimamizi wa bandari na wakala mbalimbali, kwa ajili ya huduma zao kuliko Mombasa,” alisema Morisset.

Akizungumzia ripoti hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha bandari hiyo, lakini kazi ya ziada inahitajika kuifanya iweze kushindana na nyingine. “Tunahitaji nchi jirani ziendelee kuitumia bandari yetu, bado tuna kazi kubwa ya kufanya ndiyo maana niko hapa, tunahitaji kuimarisha Kitengo cha Operesheni na maeneo mengine,” alisema Dk Mwakyembe.

Picha za matukio hayo

Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii na Watoto Ummy Mwalimu akiselebuka Wakati wa kampeni Dhidi ya ugonjwa wa Fistula zilizofanyika jana katika viwanja vya Nyerere [Nyerere Squere] Dodoma  kulia ni Mjumbe Wa kamati ya Bunge ya Maendelea ya jamii Mhe.Ritta Kabati na Kushoto ni Balozi wa Vodacom Nchini na msaani wa Muziki wa kizazi Kipya Mwana F A


 Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma David Misime akiwaonyesha wandishi wa Habari Mabomba ya plastik Inayotumika kama Mitambo ya kutengenezea Pombe Haramu Aina ya Gongo Mara Baada ya kuikamata wilayani Kongwa jana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma David Misime Akifungua Moja ya Madumu yaliyokamatwa na  Pombe Haramu ya Gongo yaliyokamatwa Wilayani Kongwa huku watu wanne wakishikiliwa na jeshi hilo.
PICHA NA JOHN BANDA

Mh. Tundu Lissu amwaga sera ndivyo sivyo.

DSC01254
Mbunge wa jimbo la Singida mashariki Mh. Tundu Lissu akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya nafasi ya udiwani kata ya Iseke tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi uliofanyika katika kijiji cha Iseke.
DSC01259
DSC01240
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Iseke tarafa ya Ihanja waliohudhuria uzinduzi wa kampeni ya udiwani kata ya Iseke uliofanywa na chama cha CHADEMA.
DSC01255
Baadhi ya viongozi wa CHADEMA waliohudhuria uzinduzi wa kampeni ya udiwani wa kata ya Iseke tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi. 
(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.

Mgeni rasmi katika kampeni ya uzinduzi wa nafasi ya udiwani kata ya Iseke tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi Mh. Tundu Lissu, ameashindwa kuuza sera za CHADEMA na badala yake ametumia muda na nguvu nyingi kuhimiza sera yake ya ‘katazo’ la wananchi kuchangia maendeleo yao .

Mh. Tundu Lissu ambaye ni mbunge wa jimbo la Singida Mashariki kupitia tiketi ya CHADEMA, alipanda jukwaani huku akiwa mabeba makabrasha ya michanganuo ya bajeti ya serikali ya kuanzia mwaka wa fedha wa 2010/2011 hadi 2013/2014.

 Akisema na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji cha iseke, Mh Tundu Lissu aliweka wazi kuwa “Mimi sitaki kabisa kuzungumzia habari za Amosi Mghenyi ambaye ametusaliti kwa kuhama CHADEMA na kurejea CCM.  Amosi kisiasa ni mfu, kwa hiyo siwezi kupoteza muda wangu kuzungumiza mambo ya mfu”.

Amesema ufunguzi wake utajikita zaidi katika kuwaelimisha wananchi wa kata ya Iseke kwamba serikali inayo fedha nyingi na za kutosha kugharamia maendeleo ya wananchi.

Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, amesema kwa mfano katika mwaka wa fedha wa 2010/2011, mkoa wa Singida, ulipewa zaidi ya shilingi milioni 903 za undeshaji wa shule, lakini zilizotumika ni zaidi ya shilingi milioni 464 na kubaki zaidi ya shilingi 438.2.

 Amesema fedha hizo zaidi ya shilingi 438.2 zilizobaki,  hazijaainishwa zilipelekwa wapi.  “Kwa vyo vyote zitakuwa zimeishia kwenye matumbo ya mgambo na watendaji wa serikali ya CCM”.

Mh. Tundu ambaye pia ni mwanasheria kitaaluma, amewataka wakazi wa kata ya Iseke, kumchagua Emmnuel Jackson Jingu awe diwani wao, ili waondokane na manyanyaso ya michango kama walivyojikomboa wakazi wa jimbo la Singida Mashariki.

 Wagombea wengine wa nafasi ya udiwani kata ya Iseke ni Amosi Munghenyi wa CCM na Abdallah Kinyenje maarufu kwa jina la Petro wa CUF.

Hotuba ya upinzani yaahirisha Bunge


Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi. 

Dodoma. Mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo jana uliingia dosari na kulazimika kusitishwa kwa muda baada ya Bunge kukubaliana na hoja ya Mbunge wa Mbozi Magharibi (CCM), Godfrey Zambi kuwa Hotuba ya Kambi ya Upinzani, imejaa uchochezi.

Zambi alitoa hoja hiyo wakati Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi alipokuwa akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu makadirio hayo, baada ya kuomba mwongozo wa Spika.

“Kuhusu utaratibu,” alisema Zambi. Baada ya kurudia kauli hiyo mara kadhaa, Spika wa Bunge, Anne Makinda alimsitisha Mbilinyi kuendelea na hotuba yake na kumpa Zambi nafasi.

“Mheshimiwa Spika, hotuba hii ya upinzani ni ya uchochezi. Sisi kama Bunge hatuwezi kuruhusu ikaendelea kusomwa hapa na Watanzania wakasikiliza uongo. Kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa 14, imejaa uongo tu,” alisema Zambi na kuongeza:

“Kusema kwamba Tanzania inawatesa waandishi wa habari kwa kuwang’oa meno na kucha, siyo kweli. Huu ni uchochezi na ningependa kutoa hoja hotuba hiyo iondolewe bungeni, ni ya kichochezi.”

Baada ya kutoa hoja hiyo, karibu wabunge wote wa CCM walisimama kumuunga mkono na baadaye, Spika wa Bunge Anne Makinda alisimama na kusema: “Naomba wote mkae chini... kwanza kaeni,” kisha aliendelea: “Humu humu bungeni, sisi wenyewe, tulipitisha kanuni kwamba tusiingize neno uchochezi kwenye mijadala yetu. Haya, sasa naahirisha kikao mpaka jioni na naagiza Kamati ya Kanuni iende ikapitie hotuba hiyo kwanza kabla haijaletwa tena bungeni.”

Nje ya Bunge

Wakiwa wanatoka bungeni, mvutano ulioanzia ndani ya ukumbi, uliibuka nje ya lango kuu la Bunge ambako wabunge kadhaa wa CCM na Chadema waliendeleza mjadala huo na kuzozana hadharani.

Wabunge waliozozana kuhusu hotuba hiyo nje ya ukumbi ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anna Kilango, Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage na Lucy Kihwelu (Viti Maalumu Chadema).

“Hamuwezi mkaharibu kanuni za Bunge letu kwa hotuba zenu za uchochezi,” alisema Kilango akimwambia Lissu.

“Hiyo kanuni ni ipi ambayo tumeiharibu? Huo ni ukorofi wenu tu, tunafahamu siku nyingi,” alijibu Lissu.

Baadaye akadakia Rage; “Hawa dawa yao ni .....” Kauli hiyo ya Rage ilijibiwa na Kihwelu aliyemwambia “Makofi yako ni Yanga tu. Umesahau umepigwa mabao 2-0.”

Mbilinyi atetea hotuba yake

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Bunge, Mbilinyi alitetea hotuba yake akisema kuwa haina tatizo lolote na imefuata kanuni zote za kusomwa bungeni.

“Hili kwetu (Chadema) ni changamoto, ila niseme tu kwamba hotuba yangu haikuwa na tatizo lolote na ilipitia hatua zote halali kabla ya kusomwa bungeni,” alisema.

Utaratibu uliowekwa na Bunge unataka hotuba za hoja za bajeti kuwasilishwa kwa Spika siku mbili kabla ya kusomwa.

Alisema hotuba hiyo haina chembe ya uongo, akisema ni ukweli kwamba waandishi nchini hawana uhuru wa kufanya kazi na baadhi wanateswa na kunyanyaswa.

 

Baadaye jioni

Katika kikao cha jioni, Spika Makinda alitoa mwongozo wake na kueleza sababu za kuahirisha hotuba ya Mbilinyi na kusema anakubaliana na hoja iliyokuwa imetolewa asubuhi na Zambi kwamba maneno yaliyopo katika hotuba ya Mbilinyi kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa 14 yaondolewe kwa kuwa yanaingilia Mahakama.

“Kwa kutumia Kanuni ya 72 ni mamlaka ya Spika kusimamia Bunge hivyo kwa kutumia Kanuni ya 64, naagiza maneno yote yanayozungumzia mauaji ya Daudi Mwangosi yaondolewe,” alisema Spika Makinda.

Alisema amefikia uamuzi huo baada ya Kamati ya Kanuni kupitia hotuba hiyo na kuona kwamba maneno yaliyopo katika kurasa hizo yanaingilia mhimili wa mahakama.

Baada ya Spika kueleza hayo, Mbilinyi aliruhusiwa kuendelea na hotuba yake na kuomba kuanzia jana jina la Sugu lisitumike tena bungeni.

Washirika sita wa ‘polisi wa bangi’ wakamatwa wakiwa na magunia 30

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha Leberatus Sabas akionyesha bangi iliyokamatwa jana 

Arusha. Polisi mkoani Arusha, imekamata magunia mengine 30 ya dawa za kulevya aina ya bangi kwa watu sita ambao inadaiwa ni washirika wa polisi wawili, waliokamatwa na magunia 18 ya bangi katika maeneo ya Himo mkoani Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema watuhumiwa hao, walikamatwa Mei 19 saa 10 jioni katika Kijiji cha Kisimiri juu, Kata ya Ngaramtoni wilayani Arumeru.

“Wakati askari hao, waliokamatwa mkoani Kilimanjaro, polisi mkoani Arusha pia tulikuwa katika msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaoshirikiana na polisi hao, katika biashara ya kusafirisha bangi kutoka Arumeru kupeleka nchini Kenya,” alisema Sabas.

“Siku za karibuni tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kuna mtandao wa wahalifu wanaoshirikiana na baadhi ya polisi wasiyo waaminifu,” alisema Kamanda Sabas.

“Watuhumiwa hawa walifanikiwa kukimbia kabla ya kukamatwa na kutelekeza bangi hiyo kwenye nyumba zao”alisema Sabas.

Kamanda Sabas alisema uchunguzi wa tukio hilo, ukikamilika watuhumiwa hao, watafikishwa mahakamani.

Habari zilizopatikana baadaye jana kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz kuwa askari wawili waliokamatwa juzi na magunia 18 ya bangi, watashtakiwa katika mahakama za kiraia kama wakosefu wengine.

Wakati huo huo, Kamanda Sabas jana alikiri kuwapo taarifa ya kuuawa Watanzania watatu nchini Kenya kwa tuhuma za ujambazi na kupatikana na bunduki ya polisi aina ya Sub Mashine Gun (SMG).

Watanzania hao,Tigiki Pasto,Steven Webo na mmoja ametambulika kwa jina moja la Kadogoo, waliuawa Mei2, mwaka huu baada ya kuvamia wafanyabiasha na kuwapora na kuwaua wawili.

Hata hivyo, baadaye walizingirwa na wananchi hao na kuuawa na ndipo waliipata bunduki hiyo mali ya polisi.

“Ni kweli tukio hilo lipo, ila sasa kwa kuwa linahusisha nchi mbili, linashughulikiwa kwa taratibu nyingine za nchi na nchi”alisema Kamanda Sabas.

Hata hivyo, alikiri pia kushikiliwa kwa polisi wawili kwa uchunguzi kutokana na kupotea kwa silaha hiyo, kwenye ghala la polisi Wilaya ya Ngorongoro.Matukio ya polisi kujihusisha kwenye vitendo viovu yalikuwa yakilalamikiwa kwa siku nyingi bila kuchukua hatua. Lakini tangu mwaka huu uanze Polisi makao makuu wametangaza kuwasafisha polisi wote wanaojihusisha katika matukio maovu.

Serikali yaahidi kugawa mbegu bora kwa wakulima nchini

biashara: popote Wakazi wa eneo la Makambako Chimbadwa, mkoani Njombe, wakisubiri wateja barabara ya Dar es Salaam- Mbeya ili wawauzie bidhaa hizo kama walivyokutwa juzi. Picha na Godfrey Kahango.   


Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imeweka mkakati madhubuti wa kuwapatia wakulima mbegu na mbolea kwa utaratibu ulio bora na wenye maslahi mapana, Bunge lilielezwa jana.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima ambaye alisema kuwa mkakati huo utatokana na ushauri wa kitaalamu wa kutoka kwa watalaamu wa ngazi zote wakiwamo wakulima, watafiti, wagani na mawakala wa mbolea.

Alikuwa akijibu swali la Athuman Mfutakamba (Igalula-CCM) aliyehoji juu ya Serikali kuwapatia wakulima wa maeneo ya Uyui mbegu bora na kuwabadilishia kutoka mbegu za zamani na kuwapatia mbegu za mahindi aina ya DKC 8053.

Malima alisema kuwa utaratibu uliopo ni kwa wakulima wa halmashauri husika kuwasilisha wizarani mahitaji halisi ya aina ya mbegu za mahindi wanazopendelea.

Kuhusu utaratibu wa utoaji wa ruzuku ya pembejeo kwa utaratibu wa vocha, alisema wakulima hunufaika kwa kupatiwa seti ya vocha tatu za mbolea ya kupandia.

Mbali na mbegu za mahindi lakini alisema wakulima kwa baadhi ya maeneo hupewa mbegu bora za mpunga ambapo wakulima wa eneo husika huchagua mbegu wanayoihitaji baada ya kushauriwa na maofisa ugani.

Vurugu kubwa Iringa, Mchungaji Msigwa mbaroni

Iringa. Mji wa Iringa uligeuka kuwa uwanja wa vita kati ya polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wafanyabiashara jana asubuhi. Watu 50 walikamatwa kutokana na tukio hilo akiwamo Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Katika vurugu hizo, gari la zimamoto lilivunjwa kioo na gari lingine dogo liliharibiwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda alisema Mchungaji Msigwa alikamatwa saa saba mchana kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo na kwamba watu wapatao 50 walikuwa wamekamatwa katika fujo hizo zilizochukua karibu saa tatu.

“Mchungaji Msigwa amekamatwa kwa makosa ya uchochezi, kufanya maandamano bila kibali na kuhamasisha watu kufanya biashara kwenye eneo ambalo limekatazwa kisheria.

Tumemkamata na hatutamwachia hadi uchunguzi wa suala hili utakapokamilika. Pia na hao watu wengine,” alisema Kamanda Kamhanda.

Alisema waliamua kufanya doria katika eneo hilo baada ya kupata taarifa za kiitelijensia kuwa wafanyabiashara walikuwa na mpango wa kuwashambulia mgambo wa Iringa kama wangekwenda kuwazuia.

Vurugu hizo zilichangiwa na mvutano uliokuwa unafukuta kwa muda mrefu kati ya Uongozi wa Manispaa na Mbunge huyo kuhusu amri ya kuzuia watu kufanya biashara kwenye Barabara ya Mashine Tatu, Iringa.

Uongozi wa Manispaa ya Iringa ulitoa tangazo Aprili 28, mwaka huu ukipiga marufuku kufanya biashara katika eneo hilo jambo ambalo lilipingwa na Mchungaji Msigwa na wafanyabiashara hao.

Alfajiri

FFU walianza kuimarisha ulinzi katika Barabara ya Mashine Tatu tangu alfajiri jana na wafanyabiashara hao walipofika kwenye eneo hilo walikuta limezingirwa na polisi.

Kusambaa kwa taarifa hizo kulimfikia Mchungaji Msigwa ambaye alifika hapo saa mbili asubuhi na kuanza kuzungumza na wafanyabiashara hao.

Watu walipomwona ndipo wakamzunguka na kuanza kuimba nyimbo za kumsifu na kumshangilia: “Rais wetu... Rais wetu... Rais wetu.”

Maofisa wa Polisi walimfuata Mchungaji Msigwa na kumwomba aondoke lakini aligoma akidai ni mwakilishi halali wa wananchi kwa hiyo hawezi kuondoka.

Badala yake alipanda kwenye gari lake na kuanza kuzunguka eneo hilo huku akifuatwa na umati wa watu. Polisi nao walikuwa wakimfuatilia kwa magari yao.

HATARI:MSICHANA WA MIAKA 16 APIGWA RISASI BAADA YA KUKUTWA ANASHIRIKI TENDO LA NDOA NDANI YA GARI NA MWANAUME JIJINI DAR ES SAALAM


JESHI la polisi limekumbwa na

 kashfa nyingine baada ya askari wake

 kudaiwa kumpiga risasi msichana wa

 miaka 16 baada ya kumkuta akivunja amri ya sita ndani ya gari.

Msichana huyo..

(Jina tunalihifadhi) alikumbana na mkasa huo

 Jumatano usiku eneo la Mbagala Zakhem

 jijini Dar es Salaam, ambapo alipigwa

 risasi sehemu ya makalio wakati

 akijaribu kuwakimbia polisi kwa 

kutumia gari la mpenzi wake.

Mpenzi huyo (jina linahifadhiwa), 

alikamatwa na kuwekwa mahabusu na

 kufunguliwa kesi ya ubakaji.

Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana katika wodi

 ya Hospitali ya Temeke alikolazwa, msichana

 huyo alisema siku ya tukio alikutana na

 kijana huyo majira ya saa 8:00 usiku

 katika baa moja inayoitwa Kindau na

 kukubaliana kwenda kushiriki 

tendo la ndoa kwa malipo ya Sh 20,000.
Alisema kutokana na muda huo kuwa

 usiku sana hawakuweza kwenda katika

 nyumba ya kulala wageni na badala yake

 walikwenda eneo la Zakhem na kisha

 walipaki gari kwenye uchochoro na

 baadae walianza kubanjua amri ya sita.
Wakiwa kwenye kilele cha mapenzi yao

, ghafla walishtukia gari la polisi likiwajia 

kwa kasi kwa nia ya kuwakamata.

“Tuliagana anilipe elfu ishirini wala

 hakunibaka kama anavyodai, wao 

polisi walitukuta tayari tunamaliza

 lakini kutokana na woga 

tulikimbia ili tusikamatwe,” alisema msichana huyo.

Alisema wakati wanakimbia 

kwa kutumia gari la mpenzi wake

 askari mmoja alifyatua risasi

 iliyopenya kwenye taa ya gari na

 kwenda kumjeruhi sehemu ya makalio yake.

“Nilisikia mlio mkubwa wa bunduki,

 ghafla nilihisi kitu kimeingia mwilini

 mwangu na kuishiwa nguvu,” alisema kwa uchungu.

Alisema kwa kuona hali hiyo, 

mpenzi wake alisimamisha gari kwa 

kujisalimisha na polisi walipowafikia

 walimtaka mpenzi wake huyo atoe pesa

 kama malipo ya kitendo chao cha 

kukutwa wakifanya mapenzi

 ama sivyo watampeleka kituoni.

Alieleza kuwa mpenzi wake hakuweza

 kutoa pesa hizo ndipo walipoamua

 kumpiga na kumpeleka kituo cha

 polisi cha Mbagala na yeye alifikishwa 

hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo, ndugu na jamaa wa mpenzi

 wake wanapinga hatua ya polisi hao

 kutumia nguvu kubwa kama watu hao

 walikuwa watuhumiwa wa ujambazi.

Wakizungumza wakiwa kwenye kituo 

cha Polisi cha Mbagala kufuatilia

 hatma ya ndugu yao, ndugu hao

 ambao hawakutaka majina yao 

yatajwe gazetini walisema hatua ya

 polisi kupiga risasi huku wakitambua

 watu hao sio majambazi ni kitendo cha kinyama.

“Tunachoshangaa ni kwa nini polisi

 wapige risasi wakati wakijua hawakuwa

 majambazi ila walikuwa wakifanya 

mapenzi, hata hilo jalada la kesi 

walilofungua wanataka kuficha maovu

 yao na sio vinginevyo,” alisema ndugu

 mmoja ambaye alijitambulisha kuwa shemeji yake.

Alisema kimsingi tukio hilo lilikwenda 

katika makubaliano yao na sio ubakaji

 kama wanavyodai, ila kinachofanyika

 kwa sasa ni kutaka kumlinda askari

 mwenzao aliyejeruhi kwa risasi.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke,

 David Misime, alipopigiwa simu kuelezea 

tukio hilo, alisema kwa sasa hawezi

 kulizungumza kwa kuwa yupo nje ya Mkoa kikazi.

Waziri Nchimbi awapasha wapinzani

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi 


Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi juzi aliwaondolea uvivu wapinzani na kuwaeleza kuwa hawezi kujiuzulu wala kufanya kazi kwa shinikizo la wanasiasa.

Mbali na hilo, aliwataka wapinzani kugombea na kupata nafasi za urais ili waweze kuweka utaratibu wa kuwafukuza mawaziri wao watakaoona hawafanyi kazi ipasavyo.

Nchimbi alitoa kauli hiyo wakati akijibu hoja kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka 2013/14.

“Nataka kumwambia ndugu yangu Lissu kuwa, kazi ya wagombea wote ni kuomba ridhaa ya kuchaguliwa ili waweze kuweka taratibu za kuajiri na kufukuza,hivyo ili kumwondoa waziri, nawashauri nanyi mgombee urais na mpate ili mjiweke katika nafasi ya kufukuzana,” alisema Nchimbi.

Alimsifia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda kuwa anafanya kazi nzuri licha ya malalamiko yanayotolea na wanasiasa na baadhi ya wanaharakati na kusema hatakiwa kuacha kazi hiyo kwa shinikizo hizo.

Hata hivyo alikubaliana na hoja iliyotolewa na msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Vicent Nyerere kuwa kuna silaha nyingi ambazo zimezagaa nchini.

“Hilo nakubaliana nalo, kuna ongezeko la silaha nyingi nchini jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa raia wetu,mbali na hilo pia nachukizwa na vitendo vya rushwa ndani ya jeshi la polisi”.

Alisema Serikali imejipanga vizuri kwa ajili ya kukabiliana na vitendo hivyo na kuwawajibisha askari wake ambao si waaminifu ndani ya jeshi.

Malecela: Nchi imepasuka, aonya Watanzania mpasuko wa kidini

Kwa siku za karibuni viongozi mbalimbali wa kitaifa na wastaafu wamekuwa wakitoa matamko ya kusisitiza amani nchini.

Dodoma/Pwani.Wakati Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela ameonya Watanzania kuhusu mpasuko wa kidini akibainisha kuwa utaigawa nchi vipande vipande, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi ametoa wito maalumu akiwataka waumini wa dini tofauti kuvumiliana.

Malecela na Mwinyi walitoa kauli hizo mjini Dodoma na Kibaha, Pwani jana kwa nyakati tofauti, wote wakiwa na nia ya kusisitiza ulinzi wa amani ya nchi inayoanza kutetereka.

Kauli ya Malecela

Malecela alisema kwa namna ilivyo sasa, Tanzania imekuwa ni tofauti na ile aliyoanza kuiona yeye katika kipindi cha uhuru kwenye miaka ya 1960 wakati huo nchi ikiwa moja na watu wake wakiwa ni wamoja.

“Msipokuwa makini na amani yenu, nchi hii mtaigawa vipande vipande na kamwe amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa mambo ya kusingiziana, badala yake tusaidiane sisi kwa sisi, na sisi na viongozi,” alisema.

Onyo la Malecela limekuja kutokana na mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa amani na mpasuko wa kidini unaoanza kujitokeza nchini.

Malecela alieleza wasiwasi wake juu ya tofauti za kidini katika ibada maalumu ya kuombea amani iliyofanyika katika Kanisa Anglikana Chiwondo lililoko kijiji cha Hombolo katika Manispaa ya Dodoma.

Anafuata nyayo za viongozi wa kitaifa walioonya masuala ya udini kama Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Marais wastaafu, Mwinyi na Benjamin Mkapa pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Alisema waliovamia na kupiga bomu kanisani Arusha ambapo Balozi wa Vatican nchini, Francisco Montecillo Padilla alinusurika kuuawa, si wajinga na wanaweza kufanya mambo kama hayo eneo lolote nchini.

 “Kujenga nchi ni kazi ngumu sana lakini kuibomoa ni kitendo cha muda mfupi ambacho kinaweza kufanyika kwa kutumia sekunde chache ni lazima kuisaidia serikali katika kuitafuta amani,” aliongeza Malecela.

  Malecela ameonya baadhi ya watu kutochukua sheria mikononi kuhusu yale yanayowapata na badala yake waiachie Serikali yao kufanya uamuzi wa nini kifanyike ili amani ibaki.

 

Nasaha za Mwinyi

Kwa upande wake Rais Mstaafu Mwinyi alisisitiza amani idumishwe na kuwataka Waislamu na Wakristo kupendana na kuvumiliana ili jamii iweze kuishi bila hofu.

“Haiwezekani dini moja kuitaka dini nyingine isiwepo,” alisisitiza Mwinyi. Mwinyi alitoa msisitizo huo jana mjini Kibaha wakati akitoa mawaidha yaliyolenga kusisitiza amani nchini kufuatia matukio kadhaa yaliyoripotiwa kutokea  nchini na kudaiwa yanahusiana na masuala ya kidini.

Alisema si ajabu kukuta hata sasa baadhi ya watu wameingiwa na hofu na waumini wakisikia kitu hata kama ni paka wanakimbia na kuacha maubiri.

 “Hakuna sababu ya kutufikisha hapo jamani, mbona dini hazijaanza leo? Tangu enzi watu wanaabudu kila mtu kwa imani yake, watu wanaoana, wanakula pamoja, wapo ofisi moja, magari wanapanda pamoja sasa iweje hii itokee leo hii?” alihoji Mwinyi.

Mapya bomu la Arusha:Majeruhi aeleza bomu lilivyokuwa

Majeruhi wa mlipuko wa bomu Arusha, Mwalimu Fatuma Tarimo akionyesha kipande cha chuma  baada ya kuondolewa kwenye mguu wake, katika Hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam jana.


Dar es Salaam/Arusha. Bomu lililorushwa na kuua watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 60 kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi huko Arusha, inadaiwa lilitengenezwa kienyeji.

Wakati kukiwa na madai hayo, mazishi ya marehemu hao Regina Kurusei, (45), James Gabriel (16) na Patricia Joachim (9) yanatazamiwa kufanyika leo Olasiti, Arusha na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anatarajiwa kuhudhuria.

Ofisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alimdokeza mwandishi wetu jana kuwa kwa ujuzi na uzoefu wake wa masuala hayo, bomu hilo si la kiwandani akisema msingi wa imani yake ni jinsi vyuma vilivyotawanyika na kuumiza watu zaidi ya 20.

Watu saba wamefikishwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuondolewa vyuma na kupata matibabu zaidi.

Mstaafu huyo alieleza kuwa mabomu mengi zaidi ya kienyeji hutengenezwa kwa kutumia bakuli za chuma, zikiwekewa baruti ndani na kufungwa kwa waya.

“Hawa jamaa huweka vipande kama 36 vya baruti na hufungiwa ndani ya bakuli kwa kubanwa sana ili kuvipa joto na bomu likitua, husababisha madhara makubwa,” alisema ofisa huyo ambaye alishiriki Vita ya Uganda mwaka 1978 hadi 1979.

Mstaafu huyo alisema mabomu ya aina hiyo yametumika kwenye mashambulizi ya kigaidi katika nchi mbalimbali duniani kama Lebanon, Vietnam, Libya, Ireland Kaskazini, Syria, Afghanistan, Iraq, Chechnya na India.

Mmoja wa majeruhi, Mwalimu Fatuma Tarimo amesimulia alivyoshuhudia bomu likitua mbele yake na kulipuka.

Tarimo, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema jana kuwa aliliona bomu hilo likiwa na rangi ya shaba. Pia alisema lilikuwa na waya kwa juu.

“Baada ya kutua, nilisikia kishindo kikubwa nikashtuka ikabidi niangalie. Baada ya kuona ni kitu kama chuma nilipata hofu nikafikiria kuondoka,” alisema mwalimu huyo wa Shule ya Msingi ya Burka Estate, nje kidogo ya Jiji la Arusha. Hata hivyo, alisema kabla ya kuondoka, alishtukia amenyanyuliwa juu na hakujua kilichoendelea kwani aliposhtuka alijikuta akiwa katika Hospitali ya Mount Meru.

Tarimo ametolewa kipande cha chuma katika mguu wake wa kulia.
“Nina maumivu bado lakini nina matumaini nimechukuliwa kipimo cha ‘T-Scan’ kwa matibabu zaidi,” alisema Mwalimu Tarimo ambaye anaaminika kuwa na kipande kingine kwenye mapafu.

Majeruhi mwingine, Jenipher Joackim ambaye amefiwa na mwanaye Patricia Joackim (9) hana taarifa za kifo hicho kilichotokea katika Hospitali ya KCMC.
“Nimeambiwa kwamba yupo ICU sijui anaendeleaje,” alisema.

 Jeshi la Polisi mkoani Arusha limetangaza donge nono la Sh50 milioni kwa watu watakaosaidia upelelezi wa ulipuaji bomu huku likiwashikilia na kuwahoji watuhumiwa 12 hadi sasa.

Bomu Arusha: Pengo afichua siri

 Kadinali Pengo 

Dar es Salaam/Arusha. Kadinali Pengo alisema amepata taarifa kutoka kwa watu ambao hana na shaka nao.

“Jana (juzi), niliongelea kwamba suala zima la tukio la Arusha halihusiani na imani yoyote ya kidini. Tamko hilo nilitamka kutokana na taarifa nilizofikishiwa na watu ambao sikuweza kuwa na shaka kwamba wanaoniambia ni kweli na sidhani kama ningekuwa na sababu ya kusema wamefika kwa kunidanganya kwa hiyo tamko litakuwa limesimama juu ya msimamo huo,” alisema Kadinali Pengo na kuongeza:

“Lengo la msingi kabisa, langu na la kanisa ni kwamba tukio lolote lile liwe kwa nia mbaya au nzuri kwa upande wetu isiwe ni sababu ya kuanza mapambano na kuwa chimbuko la ukosefu wa amani katika nchi yetu,” alisema Pengo.

Alisema kuwa kila anayehusika ajue amani ya kweli ya taifa lolote haiwezi ikapatikana isipokuwa ikijengwa juu ya ukweli na ukweli kabisa bila kufuta au kujaribu kupotosha ukweli kwa namna yoyote ile.

“Tusipojua kusema ukweli ulivyo hatuwezi kufaulu kuleta amani katika taifa letu. Kwa hiyo pamoja na kuendelea kuwaomba waumini wa Katoliki pamoja na watu wenye mapenzi mema kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu arehemu taifa letu na mapambano ya aina yoyote ile. Tuendeleze nia yetu njema ya kusema ukweli, haidhuru ukweli huu unamgusa nani,” alisema Pengo.

Alisema kujaribu kuficha ukweli na kupotosha ni njia sahihi kwa ibilisi kuleta vurugu katika jumuiya ya watu na ieleweke hivyo.

“Naomba kila mtu akubaliane na tamko langu haidhuru pana kosa, amani ya taifa letu ni jambo la msingi na amani itajengwa tu iwapo kila mtu anayehusika atakuwa tayari kusema ukweli kama ulivyo,” alisema.

Mwingine afariki, 20 wakutwa na vipande vya chuma miilini
Katika hatua nyingine, majeruhi mmoja katika shambulio hilo lililotokea Jumapili iliyopita, amefariki dunia juzi jioni na kufikisha idadi ya waliopoteza maisha kufikia watatu.

Aliyefariki ni mtoto wa miaka tisa, Patricia Joachim ambaye alikuwa amehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi. Wengine waliofariki katika tukio hilo ni Regina Losyoki (45) na James Gabriel (16).

Mazishi ya watu hao watatu yamepangwa kufanyika katika eneo la kanisa hilo Ijumaa.
Katika hatua nyingine, majeruhi 20 wamebainika kuwa na chembechembe za vyuma walivyopata katika shambulio hilo. Hao ni miongoni mwa majeruhi 42 waliolazwa hadi sasa kwenye hospitali mbalimbali za Arusha.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Dk Thomas Kway alisema majeruhi hao 20 wamedhuriwa na chembechembe za vyuma vya mabomu na baada ya miili yao kubainika kuwa na vyuma vyenye urefu hadi wa sentimita tisa.

Dk Kway alisema hayo wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipofika katika hospitali hiyo kuwafariji majeruhi hao.

 

Kutokana na hali hiyo, Pinda aliwataka madaktari waliowafanyia upasuaji majeruhi waliolipuliwa na bomu kuhifadhi vipande hivyo ili vitumike katika uchunguzi.
Aliwaambia wabunge kuwa vyuma hivyo vitasaidia upelelezi ili kufahamu aina ya bomu lililotumika.

“Tumeamua kuwa vipande vya vyuma vinavyotolewa baada ya upasuaji visitupwe, vitumike kwa uchunguzi,” alisema Pinda na kuongeza kuwa baadhi ya majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Waliokamatwa
Akitoa taarifa kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye alifika Arusha jana, Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema watu tisa wamekamatwa hadi sasa.
Aliwataja baadhi yao kuwa ni Victor Ambrose na wengine aliowataja kwa jina mojamoja ni Joseph na David.

Alisema wengine ni raia watatu wa Saudi Arabia, ambao walikuwa na wenyeji wao wawili na Watanzania wengine watatu.

Kauli ya Kikwete
Akizungumza Arusha jana, Rais Kikwete amewataka waumini wa dini zote waendelee kusali akiahidi kwamba Serikali itaimarisha ulinzi. Alisema amekerwa na kukasirishwa na tukio hilo.

Rais Kikwete alitanguliwa kufika Arusha na Makamu Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd ambao pia walitembelea Kanisa lililolipuliwa na baadaye kwenda kuwatembelea wafiwa na kuwafariji majeruhi hospitali.

Viongozi wote hao walitoa wito kwa Watanzania kulinda amani iliyopo na kuacha malumbano ambayo hayana tija kwa maslahi ya taifa.