CCM, Chadema kufunga kampeni za ubunge kesho


Iringa. Kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga zinatarajiwa kufungwa kesho huku CCM ikitarajia kumaliza kampeni zake katika ngome ya Chadema iliyopo eneo la Kidamali.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana anatarajia kuongoza ufungaji huo huku Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitaraji kuongoza maandamano ya kufunga mkutano wa kampeni hizo.

Katibu wa CCM mkoani hapa, Hassan Mtenga alisema Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Dk Yahya Msigwa, viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Khamis Dadi (Katibu) na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo ni miongoni mwa watakashiriki kufunga kampeni hizo.

Timu ya kampeni ya CCM inaratibiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula ambaye ameweka kambi katika Kata ya Ifunda, inayoaminika kuwa ni moja ya ngome ya Chadema .

Wengine ni Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Shaibu Akwilombe makatibu wa CCM wa wilaya zaidi ya 10 ambao wameweka kambi kwenye kata 13 na vijiji vilivyopo jimboni humo.

Mkutano wa Chadema unatarajiwa kufanyika katika Kata ya Ifunda, Jimbo la Kalenga kwa mwenyekiti kuongoza maandamano pamoja na jopo la wabunge 40 wa chama hicho. Uchaguzi mdogo wa Kalenga unatarajiwa kufanyika Machi 16,baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Marehemu Dk William Mgimwa.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva amevitaka vyama vya ushirika kuwarudishia shahada zao wakazi wa Kalenga ili waweze kupiga kura.

Vita dhidi ya Al Shabaab vinaathiri raia-UN

Mwanajeshi wa serikali akishika doria mjini Mogadishu

Umoja wa mataifa umesema kuwa mashambulizi makubwa ya kijeshi yaliyofanywa nchini Somalia na Wanajeshi wa Umoja wa Afrika, AMISOM, dhidi ya makundi ya wapiganaji wa Kiislamu, yanaweza kuwaathiri watu milioni tatu katika maeneo ya katikati na Kusini mwa nchi hiyo.

Mashambulizi hayo yanayowahusisha maelfu ya wanajeshi wa AU, yaliyoanzishwa juma lililopita na sasa yamesambaa hadi katika maeneo ya jangwa na milima.

Umoja wa Mataifa umeongezeka kusema kuwa umo katika hali ngumu zaidi Nchini Somalia.

Kwa sasa inaisaidia Umoja wa Afrika kwa hali na mali pamoja na vifaa vinavyohitajika kupambana na wapiganaji wa Kiislamu, na pia misaada ya kibinadam.

Inaunga mkono Jeshi moja kwa moja katika kutekeleza mashambulio makali dhidi ya makundi ya wapiganaji wa kiislamu yaliyo katika vuguvugu la Al-Shaabab.

Lakini kitengo kingine cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu, sasa yanatahadharisha kuhusiana na makali yanayotekelezwa na wanajeshi hao dhidi ya wananchi.

Shambulio mjini Mogadishu

Mashirika hayo pia yanasema wapiganaji wa Kiislamu kwa upande wao wanawahamasisha wananchi dhidi ya operesheni hiyo ya kijeshi inayojumuisha wanajeshi kutoka mataifa wanachama pamoja na wanajeshi wa serikali ya Somalia.

Siku za kwanza kwanza za operesheni hiyo kali, hasa katika maeneo ya vijijini, haikuwa rahisi kwa wafanyi kazi wa Umoja wa Mataifa kujua kilichokuwa kikiendelea.

Lakini tayari maelfu ya watu wanaingia katika mji wa Baidoa ulioko katikati mwa Somalia unadhibitiwa kwa sasa na Wanajeshi wa umoja wa mataifa kukimbia mapigano au kujaribu kupanga mashambulizi.

Bensouda kukata rufaa kesi ya Katanga

Fatou Bensouda

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ICC, Fatou Bensouda amesema huenda akakata rufaa hukumu iliyotolewa kwa mbabe wa zamani wa kivita nchini Congo Germain Katanga.

Katanga alipatikana na hatia nne za uhalifu wa kivita na hatia moja ya uhalifu dhidi ya binadamu, lakini akaondolea makosa kuhusu ubakaji.

Wapiganaji wake walishutumiwa kuwabaka wanawake na kuwateka huku wakiwatumia kama watumwa wa ngono.

Makundi ya wanawake nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo yameelezea hasira na masikitiko yao kutokana na hatua ya mahakama hiyo ya ICC ya kumuondolea Bwana Gatanga makosa hayo.

Wakati wa ziara yake katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa, Bensouda alisema kuwa huenda akakata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.

''Majaji hawakumuhumu kuhusiana na mashtaka ya unyanyazaji wa kimapenzi, mashtaka ambayo tulikuwa tumemshtaki nayo, pamoja na ile ya kuwasajili watoto jeshini'' Alisema Bensouda.

Bensouda, amesema kuwa wanachunguza hukumu hiyo kwa undani na kuchunguza ikiwa kuna dosari kadhaa za kisheria ambazo wanaweza kutumia kukata rufaa.

''Majaji kwa hekima zao walihisi kuwa bwana Katanga hakuhusika moja kwa moja na mashtaka hayo. Nadhani waadhiriwa wanafurahia kuwa ofisi yake inafuatilia suala hili, ili kuhakikisha kuwa mashtaka mazito kama hayo yanachunguzwa.'' Aliongeza Bensouda.

Kuhusiana na kesi inayomkabili rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, makamu wake William Ruto na mwandishi wa habari Joshua arap Sang, Bensouda alisema kuwa ''Nimeonyesha wazi kuambatana na ombi niliowasilisha mbele ya mahakama, kuhusiana na changa moto tunazopata, baada ya mashahidi wakuu kujiondoa kwa sababu kadhaa''.

Bensouda amesema kuwa itakuwa vigumu sana kwa ofisi yake kuendelea na kesi hizo kama ilvyopangwa baada ya mashahidi wakuu kujiondoa.

''Nimewafahamisha majaji kuwa tulikuwa na mashahidi kadhaa wakuu ambao walikuwa tayari kutoa ushahidi kuhusiana na matukio muhimu nchini Kenya, lakini wameomba kujiondoa kutoka kwa kesi hiyo.

Na kama unavyofahamu mashtaka haya pia ni mazito, na kabla ya kwenda mahakamani mtu anapaswa kuwa na uhakika wa kuwa na ushahidi ambao utakidhi mahitaji muhimu ili kuhakisha kuwa washukiwa wanahumiwa.'' Alisema Bensouda.

Zeidan akanusha kufutwa kazi


Aliyekuwa Waziri mkuu wa Libya Akihutubia Wanahabari

Aliyekuwa waziri mkuu wa Libya, Ali Zeidan, amepuuzilia mbali kura ya kutokuwa na imani naye iliyotangazwa na Bunge la taifa hilo mapema juma hili iliyopeleekea kufutwa kwake.

Ameiambia shirika la habari la Channel France 24 kuwa kura hiyo ya kutokuwa na imani naye illikuwa imejengwa kwa misingi ya uwongo huku pia akikanusha madai ya ufisadi dhidi ya serikali yake.

Ali Zeidan aliondolewa Ofisini mnamo siku ya Jumanne baada ya meli ya mafuta kutoka bandari inayodhibitiwa na waasi kufaulu kuvunja nanga ya wanajeshi wa wanamaji wa Libya kuingia bahari kuu na kutoroka.

Bwana Zeidan alifaullu kuondoka nchi hiyo licha ya kupingwa marufuku ya kutosafiri nje ya taifa.

T.B Jushua adai ndege ya Malaysia iliyopotea kimaajabu imezama kwenye tope baharini

T.B Jushua

Wakati ambapo dunia ikiweka jitihada zote kuisaka ndege ya shirika la Malaysia aina ya Boing 777 iliyopotea ikiwa na watu 239 wakati ikielekea Beijing, mhubiri maarufu wa Nigeria T.B Joshua ametoa utabiri kuwa ndege hiyo imezama baharini!

Jumapili iliyopita, T.B Joshua ameeleza kanisani kwake (SCOAN) kuwa ndege hiyo ilianguka na imezama ndani kabisa kwenye tope za bahari na kwamba hivi karibuni vipande vya ndege hiyo vitaanza kuonekana vikielea.

“Ndege hiyo iko ndani kabisa ya bahari. Baadhi ya vipande vitaanza kuonekana vikielea baharini muda wowote kuanzia sasa." Alisema T.B Joshua.

“Roho zao zipumzike kwa Amani. Tunaomba bwana azipe familia zao na wapendwa wao nguvu/uimara kushinda upotevu huu. Maombi yetu na upendo viko nao, nchi ya Malaysia na nchi nyingine ambazo zilikuwa na abiria katika ndege hiyo.” Alisema T.B Joshua kwa mujibu wa mtandao wa Nigeria wa Informationnng.

Hayo ni mambo ya imani!

Wakati dunia ikiwa bado haijafahamu ilipo ndege hiyo, wizara ya mambo ya nje ya China imeitaka Malaysia kuharakisha juhudi zake za kuitafuta ndege hiyo iliyokuwa na abiria 154 raia wa China kati ya abiria 239 waliokuwa katika ndege hiyo.

Ndege hiyo ilipotea mwishoni mwa juma na kumekuwa na mashaka kwamba huenda ni bomu au utekaji nyara unaweza kuwa uliiangusha ndege hiyo.

Waziri mkuu wa Libya azuiwa kusafiri

ali zeidan

Kiongozi wa mashtaka Nchini Libya Abdel-al-Qader Radwan amemzuia Waziri mkuu wa taifa hilo aliyevuliwa madaraka, Ali Zeidan, kusafiri nje ya taifa hilo hadi pale uchunguzi dhidi yake utakapokamilika.

Anatuhumiwa kwa madai ya ubathirifu wa pesa za umma.

Bwana Zeidan amesimamishwa kazi mapema siku ya Jumanne na Bunge la taifa hilo, baada ya Wabunge kudai kuwa meli ya mzigo ya Korea Kaskazini iliyokuwa imezuiliwa baada ya kunaswa ikibeba mafuta ghafi toka bandari moja linalokaliwa na waasi huko Libya, ilivunja nanga na kusafiri baharini.

Kura ya kutokuwa na imani na Bwana Zeidan iliitishwa baada ya meli hiyo iliyokuwa na bendera ya Korea Kaskazini kuabiri na kufikia maji makuu ya mipaka ya kimataifa baharini.

Mafuta hayo yalikuwa yamenunuliwa kutoka kwa waasi wanaodhibiti bandari ya Al- Sidra.

Wabunge hawana imani na Waziri Mkuu

Bunge la Libya limemuachisha kazi Waziri huyo mkuu, baada ya kupitisha agizo la kutokuwa na imani naye.

Hilo limeafikiwa baada ya meli ya Korea Kaskazini kuingia katika bandari ya taifa hilo na kuondoka na mafuta ghafi bila idhini ya serikali.

Makundi ya wapiganaji yamekuwa yakidhibiti baadhi ya bandari ya taifa hilo mashariki mwa taifa, tangu Julai mwaka jana na kuuza mafuta nje ya taifa.

Mwaandishi wa BBC Rana Jawad anatuarifu kutoka Tripoli.

Meli ya Mafuta iliyonaswa na wanajeshi ikisafirisha mafuta ghafi kisiri

Bunge la Libya limekuwa likijadiliana namna ya kumtimua Waziri mkuu Ali Zeidan kwa miezi kadhaa sasa.

Wabunge 200 wa taifa hilo walipiga kura na kupata maoni 124 iliyotosha kumuondoa madarakani.

Serikali ya mpito

Kiwanda cha mafuta nchini Libya

Waziri wa sasa wa ulinzi Abdullah Al-Thani amechukua mahala pake kama kama kaimu waziri mkuu.

Anatarajiwa kuhudumu kwa kipindi cha majuma mawili, kuruhusu bunge kukubaliana kumteuwa mridhi wa wadhifa huo.

Chama cha Libya National Congress, tume ya kwanza ya uchaguzi ndio yenye majukumu ya kumteuwa waziri mkuu mpya.

Lakini shinikizo kali limekuwepo Nchini humo la kutaka Bunge livunjwe.

Bwana Zeidan amekuwa akilaumu baadhi ya wanasiasa katika tume hiyo, hasa kutoka ndani ya vyama vya kiislamu ya kutaka kumtimua toka uongozini.

Hatua hiyo ya hivi punde inatazamiwa kuibua maswala mbalimbali ya udhibiti wa uongozi Nchini Libya, inapojikakamua kutafuta uungwaji mkono kutoka pembe zote za Nchi.

'Oscar Pistorius alipenda sana Bunduki'


Pistorius akiwa mahakamani

Katika ushahidi unaoendelea kutolewa dhidi ya mwanariadha mlemavu wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius, rafiki ya mwanariadha huyo, ameambia mahakama kuwa Pistorius alipenda sana bunduki

Darren Fresco, alisema kuwa alikuwa naye mara mbili alipokuwa na bunduki aliyoiofyatua katika sehemu ya umma.

Bwana Pistorius wakati mmoja alifyatua bunduki yake akiwa ndani ya mkahawa , ingawa yeye ndiye aliyelaumiwa kwa hilo,alisema bwana Fresco said.

Mwanariadha huyo amekanusha madai ya kumuua mpenzi wake kwa maksudi, akisema kuwa alidhania kuwa ni mwizi aliyevamia nyumba yake.

Bwana Fresco alisema kuwa katika tukio lengine, alikuwa anaendeshagari lake wakati ambapo Pistorius alipofyatua tena bunduki yake baada ya polisi kumzuia kuendesha gari lake kwa kasi.

Alisema kuwa Pistorius alikasirika baada ya polisi kuchukua dunduki yake iliyokuwa kwenye kiti cha nyuma ya gari lake na kumwambia: '' hauruhusi kugusa bunduki ya mtu mwingine, ikiwa chochote kitatokea atakuwa wa kulaumiwa.''

Mwandishi wa BBC nchini humo, Pumza Fihlani anasema kuwa Pistotius katika kikao cha Jumanne alikuwa mtulivu ikilinganishwa na Jumatatu.

Aliketi akiwa kimya na kuandika baadhi ya maneno yaliyokuwa yanasemwa.

Ushahidi wa Fresco, ulitoa taswira ya mchezaji huyo alivyopenda maisha ya kifahari akiwa na rafiki zake. Alipenda magari, wanawake warembo , bunduki na kwamba aliwashukia sana polisi.

Aliyekuwa mpenzi wa Oscar pia alitoa ushahidi sawana huo mahakamani, wiki ya kwanza ya kuzikilizwa kwa kesi hiyo.

Maduka yafungwa Dodoma wenyewe wagomea mashine za kieletroniki EFDs za TRA


  
  
 
 Maduka yakiwa yamefungwa katika mitaa mbalimbali ya manispaa ya Dodoma baada ya wafanyabiashara kugoma kuazia jana karibu nchi nzima kwa muda usiyojulikana huku mapendekezo yao kuwa gharama za uendeshaji mashine hizo zifanywe na serekali.
 
 Baadhi ya wafanyabiashara wa maduka wakipiga soga nje ya maduka yao baada ya kuyafunga kwa muda usiyojulikana wakipinga mashine ya kielektroniki EFDs iliyotolewa na TRA na kutakiwa kila mfanyabiashara kuwa nayo.
[PICHA NA JOHN BANDA]

Wajitokeza na kudai watoto wa Mandela


Pretoria. Wanawake wawili wanaodai kuwa watoto wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, wamejitokeza na kutaka watambuliwe kwenye mirathi ya familia yake.

Kwa mujibu wa mwanasheria anayesimamia mirathi hiyo, Michael Katz, wanawake hao wanadai kwamba ni watoto wa Mandela na kwamba wanashangaa kutotajwa katika mirathi yake iliyotangazwa wiki iliyopita.

Wakili Katz alisema wawakilishi wa wanawake hao, Onica Mothoa na Mpho Pule, wamewasiliana naye wakitaka utata uliopo sasa utatuliwe, ili nao waweze kupata haki yao kama watoto wengine wa marehemu.

Katz alisema, Mothoa na Pule wanadaiwa kuzaliwa na Mandela wakati akiwa katika ndoa ya mke wake wa kwanza, Evelyn Mase, aliyeachana naye mwishoni mwa miaka ya 1950.

Taarifa ya kipindi cha televisheni cha Carte Blanche, iliripoti juzi jioni kwamba tayari wanasheria wawili wanaowawakilisha wanawake hao, wameshawasiliana na wasimamizi wa mahakama, kutaka kusitishwa mgawanyo wa mali kama ilivyoelezwa katika wosia wa mirathi wa Mandela, hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.

Naibu Jaji Mkuu, Dikgang Moseneke, aliwaeleza wanahabari Jumatatu wiki iliyopita kwamba mali za Mandela zinafikia Randi 46 milioni (sawa na Sh5.6 bilioni).

“Kiasi hicho hakijumuishi mapato yatokanayo na kazi zake nyingine na uwekezaji aliowahi kuufanya,” alieleza.

Wosia wa mgawanyo wa mali zake uliandikwa mwaka 2004 na kurekebishwa kwa mara ya mwisho mwaka 2008.

Mwanasheria Katz, alisema wanawake hao wanataka kutambuliwa rasmi katika wosia wake na si kwamba wanahitaji kiasi chochote cha fedha.

Alisema anatarajia kukutana na wasimamizi wa wosia wa Mandela kwa ajili ya kujadili kwa kina kuhusu suala hilo.

Katika kipindi cha Carte Blanche, watu wa karibu wa Mothoa na Pule walidai kwamba waliwahi kujaribu kuzungumza na Mandela ili akubali kwamba ni baba halisi wa watoto hao.

Hata hivyo, hakuwahi kujibu au kutoa msimamo wake.

 

Ukumbi bunge la Katiba sasa wakamilika





Spika wa Bunge, Anne Makinda (aliyekaa) akiwa na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge wakati wakikagua Ukumbi wa Bunge, ambao utatumika kwa ajili ya Bunge la Katiba, mjini Dodoma jana. Picha na Ofisi ya Bunge 


Dodoma. Matengenezo yaliyotarajiwa ndani ya ukumbi wa bunge la Muungano ambao ndio utakaotumika kwa bunge la Katiba, yamekamilika na sasa ukumbi huo uko tayari kwa kazi inayotarajia kuanza Februari 18 mwaka huu.

Kukamilika kwa ukumbi huo kunaondoa hofu iliyoanza kutanda kuwa huenda bunge hilo lingesogezwa mbele kwa siku tatu kwani kulikuwa na mashaka kwa kazi hiyo.

Jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alitembelea ukumbi huo kwa mara ya mwisho na kujiridhisha katika maeneo muhimu yaliyokuwa yakifanyiwa marekebisho .

Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ukumbi huo, Lukuvi alisema tayari viti 676 vimeshafungwa pamoja vipaza sauti vyake ambavyo Rais Jakaya Kikwete alionyesha mashaka kama vingekamilika kwa wakati.

Februari Mosi, Rais Kikwete alipita kukagua ukumbi huo wakati akielekea mkoani Mbeya ambapo alionyesha kutokuridhika hasa akatilia mashaka katika eneo la vipaza sauti ambako alisema kuwa bado kulikuwa na kazi kubwa ya kufanya.

Hata hivyo, jana Lukuvi licha ya kushuhudia kuwa vimefungwa katika viti vyote, lakini alipotakiwa na waandishi kuwasha kwa majaribio, wajenzi wa ukumbi walizuia na kusema kitaalamu hakutakiwa kuwasha jana kwani kazi ilikuwa bado inaendelea.

Alisema kuwa Ofisi ya Bunge imeshatafuta kumbi nyingine nje ya bunge kwa ajili ya kufanyika mikutano ambayo itahitaji wajumbe zaidi ya 60.

Mgomo kila kona kuzipinga EFDs


Mikoani. Sakata la matumizi ya Mashine za Elektroniki za Kutolea Risiti (EFD), limechukua sura mpya baada ya wafanyabiashara mikoa mbalimbali kuja juu wakisema matumizi yake yanalenga kuwaangamiza katika biashara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao wameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufikiria upya mfumo wa kuzitumia, vinginenyo watajikuta wanaingia kwenye mgogoro mkubwa baina yao.

Tayari, wafanyabiashara miji ya Iringa, Songea na Mara wametoa msimamo wa kugomea matumizi ya mashine hizo na kuazimia kufunga biashara zao kama njia ya kupinga matumizi yake.

Wafanyabiashara wa Manispaa ya Iringa, jana walitangaza mgomo usio na kikomo kwa sababu mashine hizo zinawasababishia hasara. Wanadai mashine hizo licha ya kununuliwa kwa bei kubwa, inawabidi kuajiri wafanyakazi wenye ujuzi na kodi nyingine wanajikuta wakitumia sehemu za mitaji yao.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma aliwataka wafanyabiashara kuacha migomo isiokuwa na tija wala sababu, badala yake wafikishe malalamiko yao kwa uongozi husika kupitia viongozi wao.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Mara, Baltazar Gibogo alisema mgomo huo ni halali yao, kwani Serikali inawanyanyasa wananchi wake.

Gibogo alikanusha kuwa Serikali imeshindwa kukusanya kodi hadi kubuni kutumia mashine, bali chanzo kikubwa ni kukithiri kwa rushwa baina ya wafanyabiashara wakubwa na wafanyakazi wa TRA.

Mjini Mbeya, wafanyabiashara walishauri Serikali kuzitoa bure mashine za EFD ili kuwasaidia wafanyabiashara kujijenga kibiashara badala ya kufilisika.

“Pamoja na kwamba Mamlaka ya Mapato tanzania (TRA) inasema mfanyabiashara akinunua anaweza kurudisha fedha zake kwa kupunguza zile za kodi, ukweli unabaki palepale kwamba wafanyabiashara hawana fedha taslimu kununua kitu ambacho siyo cha kuuza na kupata fedha kwa wakati huo,’’ alisema Anania Kasisi.

Imeandikwa na Florence Focas , Musoma; Geofrey Nyang’oro na Zainab Maeda, Iringa na Lauden Mwambona, Mbeya

Mwenyekiti wa CCM Dar kizimbani kwa tuhuma za kusambaza ARV feki

 
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI), Ramadhani Madabida (kulia) na Ofisa Ubora wa Bidhaa wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Evance Mwemezi walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana kusomewa mashtaka ya kuuza na kusambaza dawa feki za ARV. Picha na Venance Nestory 


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Ltd cha Dar es Salaam (TPI), Ramadhani Madabida na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kusambaza dawa bandia na kusababisha hasara ya Sh148.3 milioni.

Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi aliwataja washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo kuwa ni Mkurugenzi wa Operesheni wa TPI, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon Msofe, Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango pamoja na wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD), Sadick Materu na Evans Mwemezi.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nyigulile Mwaseba, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro alisema katika shtaka la kwanza, Aprili 5, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango wakiwa na nyadhifa hizo kwenye kiwanda cha TPI walisambaza makopo 7,776 ya dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) aina ya Antirectroviral.

Kimaro alidai kuwa washtakiwa hao, walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 76 (1)(2) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003, wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halali na kwamba zimetengenezwa Machi, 2011 na muda wake wa kutumika unakwisha 2013 wakati wakijua kuwa si kweli.

Katika shtaka la pili, Wakili Kimaro alidai kuwa Aprili 11, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango walisambaza na kuuza makopo 4,476 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral walizokuwa wakijaribu kuonyesha kuwa zilikuwa na viambatanisho vya Starudine 30mg, Nevirapine 200mg, Lamivudine 150mg pamoja na fungu namba OC 01.85.

Alidai kuwa washtakiwa hao waliweka viambatanisho hivyo wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halisi na kwamba zilitengenezwa Machi 2011 na muda wake wa kutumika ulikwisha Februari 2013 huku wakijua kwamba ni uongo.

Katika shtaka la tatu wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kinyume na Kifungu cha 302 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Wakili Kimaro alidai kuwa kati ya Aprili 12 na 29, 2011, washtakiwa hao wakiwa na nia ya kulaghai, walijipatia Dola za Marekani 98,506 sawa na Sh148,350,156.48 wakijaribu kuonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha ni malipo halali ya makopo 12,252 ya dawa aina ya Antirectrovial yaliyokuwa katika fungu (batch) namba OC 1.85.

Alidai pia kuwa washtakiwa hao walikuwa wakionyesha dawa hizo bandia zilikuwa zimetengenezwa Machi, 2011 na kwamba muda wake wa kumalizika kutumika ni Februari, 2013 na wakafanikiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka MSD.

Katika shtaka la nne, Materu na Mwemezi wakiwa ni Meneja wa Udhibiti Viwango na Ofisa Udhibiti Viwango wa MSD, kati ya Aprili 2 na 13, 2011 huku wakijua nia ya kutendeka kwa makosa hayo ya usambazwaji wa dawa bandia, walishindwa kuzuia kinyume na Kifungu cha Sheria namba 383 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Katika shtaka la tano, wakili huyo wa Serikali alidai kuwa kati ya Aprili 5 na 30, 2011, washtakiwa Madabida, Shamte, Msofe, Shango pamoja na Materu na Mwemezi, kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi, walishindwa kutekeleza majukumu yao wakiwa watendaji.

Alidai kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kusambaza makopo 12,252 ya dawa bandia wakijaribu kuonyesha kuwa zilitengenezwa Machi 2011 na kwamba zitakwisha muda wake wa kutumika Februari 2013 na kuisababishia mamlaka hiyo ya Serikali hasara ya Sh148,350,156.48.

Washtakiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili na upande wa mashtaka ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Mwaseba alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao wanafanya kazi kwenye taasisi zinazotambulika kisheria na kwamba kila mdhamini angesaini bondi ya Sh6,181, 256.

Pia alimtaka kila mshtakiwa kutoa kiasi cha Sh12, 362,513 milioni taslimu mahakamani hapo au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Madabida na Materu waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti hayo huku wenzao wakipelekwa mahabusu kusubiri kuyakamilisha.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, mwaka huu itakapotajwa.

MBOWE: ACHENI KUINGILIA TUME YA WARIOBA

MWENYEKITI wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Taifa Freeman Mbowe, amesema Kitendo cha baadhi ya vyama vya siasa kuingilia tume ya jaji Joseph Warioba iliyoteuliwa na rais ili kuleta katiba mpya yenye neema kwa watanzania ni Uoga wa kuondolewa madarakani.
Amesema tume ya jaji Warioba haikujitengenezea maoni yake ili kuwafurahisha wananchi bali maoni yaliyomo kwenye rasmu ya katiba ni maoni ya wananchi ambayo hayatakiwi kuingiliwa na chama chochote.
Mbowe amesema hayo jana jumatatu kwenye uwanja wa Magereza mjini Geita ikiwa ni ziara yake ya vuguvugu la mabadiliko''M4C''Pamoja Daima akitokea wilayani Biharamulo mkoani Kagera.
Amesema kuingilia tume ya mabadiliko ya katiba kuhusu maoni ya wananchi yaliyokusanya na tume unatokana na kubaini mapema kwamba kufikia mwaka 2015 chama kilichoko madarakani ccm itang'oka madarakani.

Mbowe amesema endapo serikali haitalifanyia marekebisho daftari la wapiga kura Chadema kitwahamasisha wananchi nchi nzima wasishiriki kupiga kura za maoni ya katiba.

Aidha ameitaka serikali kurekebisha daftari hilo ili kutoa fursa kwa watanzania wengi kushiriki kuipigia kura maoni ya katiba na chaguzi mbalimbali zijazo ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa,na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Majalada kesi yasombwa na mafuriko Moro

Magole. Wakati Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Magole, Fredy Mbogela akisema kesi zote zilizokuwa zikisikilizwa katika mahakama hiyo ambayo imesombwa na maji pamoja na mafaili yote, zitaanza upya, Mkuu wa Wilaya na Mkoa wa Morogoro wanahaha kukusanya takwimu za waathirika wa mafuriko.

Mafuriko makubwa yalitokea katikati ya wiki iliyopita Kijiji cha Magole, huku yakisababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu. Pia, mafuriko hayo yalisomba majalada ya kesi mbalimbali mahakamani hapo.

Akizungumza jana, Hakimu Mbogela alisema hivi sasa kesi zote za jinai zilizokuwa zikisikilizwa mahakamani hapo zitafunguliwa na kusomwa na kusikilizwa upya.

“Polisi ndiyo watakaofungua na kuzipeleka kesi hizo katika mahakama hiyo, kwa sababu wao wanazo kumbukumbu za kesi hizo kupitia kwa waendesha mashtaka na wapelelezi,” alisema Hakimu Mbogela na kuongeza:

“Hakuna kesi itakayofutwa kutokana kuharibiwa majalada hayo, kama nilivyosema polisi watazileta kesi mahakamani, hata kama kulikuwa na kesi iliyokuwa imekaribia hukumu itaanza upya.” alisema.

Alisema: mahakama itaanza kufanya kazi baada ya kufanyiwa usafi na kuweka samani.

Alisema hatua ya awali ambayo inaendelea kufanywa, ni kusafisha jengo la mahakama hiyo ndani na nje kwa kutoa matope, magogo ya miti na taka nyingine ambazo zilikwama eneo hilo na kwamba, utaratibu wa utendaji unaendelea kufanywa.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Nestory Munjunangoma alisema Idara ya Mahakama kwa kushirikina na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wapo kwenye mchakato wa ukaguzi na tathmini ya uharibifu wa jengo la mahakama hiyo.

Munjunangoma alisema hivi sasa jitihada za kufanya ukaguzi na upembuzi yakinifu zinafanyika kabla ya TBA kutoa ushauri kulingana na uharibifu uliotokea kamajengo hilo linaweza kukarabatiwa ama kujengwa upya.

Alisema hivi sasa shughuli za mahakama hiyo zimesimama, kuruhusu usafi wa mazingira.

Mauaji yazidi kutikisa Tarime

Tarime. Hali ya usalama Tarime imezidi kutoweka baada ya jambazi lisilofahamika likiwa na bunduki ambayo haijafahamika aina yake kuendelea kuua watu kwa risasi hasa wa jinsi ya kiume, ambapo idadi ya waliouawa imefikia saba hadi sasa na inadaiwa huwaua watu na kupotea bila kutambuliwa.

Jambazi hilo lisilofahamika liliua watu hao usiku wa Januari 27, mwaka huu katika maeneo ya Nkende likianza na kumuua Mwendesha Bodaboda, Juma Marwa Mkazi wa Nkende mjini Tarime akiwa anaelekea nyumbani kwake ambaye alikufa akiwa hospitali akipatiwa matibabu.

Mganga wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Marco Nega alisema tangu Januari 27 hadi sasa hospitali imeendelea kupokea watu waliouawa na majeruhi ambao wamefanyiwa uchunguzi na kugundulika wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi katika sehemu mbalimbali za mwili na kwamba watu wapatao 7 wamekwisha kufa mpaka sasa.

“Tumepokea maiti za watu na majeruhi na tumewafanyia uchunguzi wakagundulika wana majeraha ya risasi sehemu mbalimbali za mwili, ambapo tayari watu saba wamekufa wengine wamekufa wakiwa njiani wakienda kwenye matibabu Musoma, marehemu hadi ni saba,” alisema Nega.

Waliojeruhiwa wakosa huduma ya X-ray

Watu waliojeruhiwa wameshindwa kupatiwa huduma ya X-Ray kutokana na Hospitali ya Wilaya kutokuwa na huduma hiyo kwa muda wa zaidi ya miezi 3 na kusababisha wagonjwa kusafirishwa kwenda Musoma na Mwanza kwa matibabu, ambapo Samweli Richard amekufa akiwa njiani kuelekea Musoma kwenye matibabu ikiwamo huduma hiyo ya X-ray.

Hospitali ya Wilaya yashindwa kutoa huduma

Huduma kwa wagonjwa mbalimbali katika Hospitali ya Wilaya imeshindwa kuendela vilivyo baada ya kupatwa na misiba miwili ya watumishi wawili, ni baada ya waume zao kuuawa na jambazi hilo lisilofahamika.

Awali Januari 26 jambazi hilo lilimuuwa Robert Kisiri (45) mkazi wa Mugabiri ambapo Mstaafu wa JWTZ Zacharia Mwita(58) na Erick Makanya (25)wote wakazi wa Kijiji cha Mogabiri Kata ya Kitare Wilayani Tarime walikutwa wakiwa wameuawa na miili yao ikiwa na majeraha ya risasi mbavuni kushoto na mgongoni.

Pia jambazi hilo liliwajeruhi watu watano kwa risasi ambao ni Mgosi Marwa Mkazi wa Mogabiri, Joseph Richard Mkazi wa Rebu, Gastor Richard Mkazi wa Rebu, Juma Mwita Mkazi wa Mogabiri na Mkandarasi Binafsi wa ujenzi, Mwasi Yomami ambao kati ya hao wawili wamefariki wakati wakipatiwa matibabu.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Justus Kamugisha amesema wamemkamata mtu mmoja anayeshukiwa kuwa mhusika wa mauaji ambaye yuko chini ya ulinzi kwa mahojiano na kwamba anazidi kuongeza vikosi vya doria kuimarisha ulinzi na usalama na kuwasaka wahalifu.

Wananchi wacharuka

Wananchi Mjini Tarime waliitaka polisi kuhakikisha jambazi hilo linapatikana vinginevyo walitaka polisi kuwakabidhi bunduki ili waweze kumsaka jambazi huyo.

‘Kamanda kashindwa kazi haiwezekani mtu mmoja aue watu 7 ndani ya siku mbili, huu ni uzembe wa polisi katika kuimarisha ulinzi, tunaomba tukabidhiwe bunduki tulisake jambazi,” alisema mwananchi mmoja.